Kutoka kwa Wasomaji Wetu
Kutoka kwa Wasomaji Wetu
Upimaji-Ramani Nilifurahia kusoma makala “Upimaji-Ramani Ni Nini?” (Juni 8, 2002) Mimi na mume wangu ni wakaguzi wa ujenzi wa barabara katika jimbo la Florida. Upimaji-ramani ni sehemu ya kazi yetu ya kawaida. Nilipendezwa na historia ya upimaji-ramani, na utumizi wa andiko la Mithali 22:28 ulifanya historia hiyo iwe ya pekee zaidi. Ingawa naelewa kwamba picha zilitumiwa kama mfano tu, ningependa kutaja kwamba sisi huwasizitizia
wapimaji-ramani wote wavalie vesti za usalama na watumie vifaa vya usalama. Kuvaa hivyo huwafanya waonekane kwa urahisi, kwa sababu wao hufanya kazi kando ya barabara migongo yao ikielekea magari. Asanteni kwa makala hiyo yenye kuarifu sana!
C. S., Marekani
Vita Nilihisi vizuri sana niliposoma makala “Maoni ya Biblia: Je, Mungu Huunga Mkono Vita?” (Mei 8, 2002) Habari hiyo ilinipendeza kwa sababu mimi ni Shahidi wa Yehova na watu wengi ninaokuta katika huduma huniuliza kwa nini taifa la Israeli la kale lilipigana vita nyingi sana. Nimejaribu kuwajibu, lakini sikuwa na habari za kutosha. Makala hiyo ni rahisi na yenye kusadikisha! Nimeandika mambo makuu ili niyatumie wakati wowote. Tunahitaji sana makala kama hizo!
V. S., Urusi
Nilikuwa dereva wa kifaru kikubwa katika Vita ya Pili ya Ulimwengu. Baada ya kuteka mlima mmoja muhimu, madhabahu ilijengwa uwanjani asubuhi iliyofuata. Nakumbuka wanajeshi watatu wa vifaru wakipiga magoti mbele ya madhabahu hiyo na kubarikiwa na kasisi wa jeshi. Muda mfupi baadaye, tulishambuliwa na wale wanajeshi watatu waliuawa. Mwaka wa 1957 mimi na mke wangu tukawa Mashahidi wa Yehova, na tukafahamu kwamba Mungu hakuunga mkono upande wowote wa vita hiyo. Tangu wakati huo, tumekuwa tukipigana vita ya kiroho, na tunajua kwa hakika Mungu anaunga mkono upande gani.
F. S., New Zealand
Mama Asanteni kwa mfululizo wa makala “Je, Mama Wana Kazi Nyingi Mno?” (Aprili 8, 2002) Nina umri wa miaka 13 tu, lakini makala hizi zilinifundisha mambo ambayo mama yangu hukabili na yale atakayokabili katika miezi michache ijayo—ana mimba ya miezi mitano na nusu. Kwa sababu nimesoma gazeti hilo, ninajitahidi sana kumheshimu na kumstahi.
N. B., Marekani
Shinikizo la Damu Asanteni sana kwa makala yenu nzuri “Kuzuia na Kudhibiti Kupanda kwa Shinikizo la Damu.” (Aprili 8, 2002) Nililazwa hospitalini kwa sababu moyo wangu ulishindwa kufanya kazi ghafula. Baadaye nilisoma makala hiyo, na ilieleza mambo mengi sana kuhusu jinsi ya kukabiliana na kupanda kwa shinikizo la damu. Nilipokea ushauri mwingi pia kutoka kwa daktari wangu na mtaalamu wa chakula. Hata hivyo, makala hiyo imeandikwa kwa njia ninayoweza kuelewa. Kuanzia sasa, ninataka kutunza sana uhai ambao Yehova amenipa!
N. I., Japan
Nina shinikizo la juu la damu, na nimeshauriwa na wataalamu wa afya nipunguze kiasi cha chumvi ninachotumia hadi gramu mbili kwa siku. Yaelekea kwamba kiasi cha gramu sita kwa siku kilichotajwa kwenye ukurasa wa 22, kulingana na Mwafikiano wa Tatu wa Brazili Kuhusu Kupanda kwa Shinikizo la Damu, ni cha juu sana. Je, hilo ni kosa la uchapishaji?
F. S., Marekani
“Amkeni!” lajibu: Chanzo cha habari hiyo chapendekeza kiasi kisichozidi gramu 5.85 kwa siku. Kijiko cha chai, ambacho huenda kikawa rahisi kukadiria, kinaweza kuchukua gramu 5.18 za chumvi. Hata hivyo, kama inavyoonyeshwa katika kielezi cha chini, mtu aliye na shinikizo la juu la damu au magonjwa mengine anapaswa kumwona daktari. Huenda ikambidi apunguze kiasi cha chumvi hata zaidi.