Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

“Mama wa Simu” Hupika Chakula Bora

Vijana waseja wenye shughuli nyingi ambao wanapenda kula chakula kitamu na chenye afya lakini hawana nafasi au hawapendi kupika wamepata suluhisho jipya la tatizo lao. Wao huwaajiri “mama wa simu” kupitia Internet, lasema gazeti la Hispania El País. Mara mbili kwa juma, mama huyo huwapelekea chakula kizuri, kilichopikwa nyumbani, ambacho watakila kwa siku kadhaa. Chakula hicho hutia ndani samaki, tambi, mboga, maharagwe, nyama, matunda, na vitu vingine vinavyotengenezwa kutokana na maziwa. “Mama wa simu” huendelea kuwasiliana kwa simu na wateja wapya ili kujua kiasi cha chakula kilichomo kwenye friji zao, mapendezi yao, na mahitaji yao. Mtu anaweza kuagiza chakula cha watu wanne au zaidi kiletwe ofisini, na kuna chakula cha mwisho-juma pia.

Kivuko cha Vyura

Wahandisi waliotengeneza Barabara Kuu katika Kisiwa cha Vancouver nchini Kanada walishangaa kugundua kwamba barabara waliyokuwa wakiunda ilivuka njia nyingine muhimu—“njia ya vyura.” Kulingana na gazeti Beautiful British Columbia, “maelfu ya vyura wenye urefu wa sentimeta tatu” walivuka barabara hiyo iliyokuwa haijakamilika wakielekea kwenye makao yao katika eneo lililoinuka kutoka eneo la majimaji ambapo walianguliwa. “Wahandisi hao waliwaza na kuwazua kuhusu jinsi ambavyo wangetatua tatizo hilo” walipotambua madhara ambayo barabara hiyo ingewaletea vyura hao. Wangetatuaje tatizo hilo? Craig Barlow, msimamizi wa mambo ya mazingira ya mradi huo asema kwamba wahandisi waliunda “ukuta ulioelekeza vyura hao kwenye mtaro uliotengenezwa chini ya barabara hiyo.” Gazeti hilo lasema kwamba vyura hao “huathiriwa sana na maji machafu, kupoteza makao, na badiliko la hali ya hewa.”

Walaghai Wafaidika na Shambulizi la Septemba 11

Kabla hata siku moja kupita baada ya mashambulizi ya kigaidi mnamo Septemba 11, 2001, wezi na walaghai walianza kujifaidi kutokana na huzuni ya watu na matendo ya ukarimu yaliyoonyeshwa. Watu fulani walijifanya kuwa waokoaji na wakaiba. Usiku mmoja, mashine kubwa ya kuondoa vifusi iliibwa. Kulikuwa na walaghai wengi. Watu wengine waliuza vifaa bandia vya kujikinga na silaha za kibiolojia na dawa za ugonjwa wa kimeta. Wengine waliuza mchanga bandia wa eneo ambapo majengo ya World Trade Center yalikuwa kama kumbukumbu. Watu fulani walitoa hati za uwongo za kudai malipo ya bima ya maisha na ya uharibifu wa mali. Wenzi fulani wa ndoa walijaribu kukusanya pesa za bima, wakidai eti nyumba yao iliyoko kilometa 6 kutoka hapo, ilikuwa imeharibiwa katika mashambulizi hayo. Wengi walipokea malipo kwa ajili ya watu wa ukoo “waliokufa,” ambao bado walikuwa hai au waliobuniwa. Walaghai waliuza vitu kama bendera na beji fulani, wakisema kwamba faida ya mauzo hayo ingesaidia mashirika ya kutoa misaada, lakini hawakutoa pesa zozote kwa mashirika hayo. Walaghai walianzisha vituo vya Internet vya kuchangisha pesa ambazo walisema zingetumiwa kusaidia watu walioathiriwa. Wengine walitumia orodha ya majina ya watu ambao hawakupatikana kuomba habari zaidi kuwahusu kutoka kwa familia zao, halafu wakatumia majina ya watu hao kuiba au kulaghai. Uchunguzi bado unaendelea.

Ugonjwa wa Kifua Kikuu Unazidi Kuenea

Bado ugonjwa wa kifua kikuu haujakomeshwa, laripoti gazeti Clarín la Buenos Aires. Hiyo ni kweli hasa katika nchi ambazo zina umaskini mwingi. Huko Argentina, “watu 14,000 huambukizwa kila mwaka,” makala hiyo ilisema. “Kulingana na ripoti moja ya Shirika la Afya Ulimwenguni . . . , ugonjwa huo huua watu milioni mbili hivi kila mwaka.” Ingawa ugonjwa huo huhusianishwa sana na utapiamlo na umaskini, unaambukizwa kwa urahisi na hivyo kila mtu anakabili hatari ya kuupata. “Ugonjwa wa kifua kikuu huambukiza kwa urahisi sana, na huwapata watu wa jamii zote,” asema Dakt. Julio González Montaner, mmoja wa wavumbuzi wa dawa za ugonjwa wa kifua kikuu. Alieleza kwamba mtu anaweza kuambukizwa anaposafiri kwa ndege, kwenye ujirani wake, au mahali anapofanya kazi.

Sheria ya Kwanza Kudhibiti Matumizi ya Mwangaza

Jamhuri ya Cheki ndio nchi ya kwanza kutunga sheria inayoagiza mwangaza uelekezwe mahali unapokusudiwa, lasema gazeti Berliner Morgenpost. Sheria hiyo ilianza kutumika mnamo Juni 1, 2002 na imeungwa mkono na wataalamu wa anga na watu kwa ujumla. Inasema kwamba “mwangaza haupaswi kumulika mahali ambapo haukukusudiwa, hasa angani.” Raia na mashirika mbalimbali yanapaswa kutumia taa zenye vifaa vya kudhibiti mwangaza kuzuia mwangaza usienee angani, na kuwafanya watu wasione anga lenye nyota usiku. Hata kabla ya Juni 1, vifaa vya kudhibiti mwangaza vilivyotumiwa jijini Brno vilipunguza mwangaza kwa kadiri kubwa. “Hayo ni maendeleo makubwa,” asema mtaalamu wa anga kutoka Cheki, Jan Hollan.

Tatizo la Kutojua Kusoma na Kuandika Ulimwenguni Pote

Je, wanafunzi wanaelimishwa vizuri siku hizi? Shirika la Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo lilifanya uchunguzi mmoja uliohusisha wanafunzi 265,000 wa shule za upili wenye umri wa miaka 15 katika nchi 32 ili kujua “ikiwa wanafunzi wanaokaribia kumaliza elimu yao ya msingi wana ujuzi na ustadi wa kutosha ili wafanikiwe maishani.” Uchunguzi huo unaonyesha kwamba asilimia 6 ya wanafunzi “wana ufasaha mdogo sana wa kusoma.” Asilimia 12 wana “uwezo wa kusoma tu habari rahisi au kichwa kikuu cha habari.” Kwa wastani, katika nchi zote, wasichana wanasoma vizuri kushinda wavulana. Wanafunzi kutoka Finland wanajua kusoma vizuri zaidi, wanafunzi Wajapan na Wakorea wanafanya vyema zaidi katika masomo ya sayansi na hesabu. Uchunguzi huo wasema “katika nchi 20 kati ya nchi 28, zaidi ya asilimia 25 ya wanafunzi hawapendi kwenda shuleni.”

Habari Ambazo Hazikuchapishwa

“Ni habari zipi ambazo hazikuchapishwa na magazeti kwa sababu ya ‘Maafa makubwa’ [ya Septemba 11, 2001]?” liliuliza gazeti la Ufaransa Médias. Vichwa vya habari vya ukurasa wa mbele ambavyo havikuchapishwa katika magazeti 12 ya kitaifa na ya mikoa nchini Ufaransa vilitia ndani habari kuhusu ndege ya kijeshi ya Marekani iliyoangushwa huko Iraki, tetemeko la ardhi nchini Taiwan, kimbunga kilichowaua watu watano nchini Japan, na mgogoro wa kidini uliosababisha vifo vya angalau watu 165 huko Nigeria. Habari nyingine ambazo hazikuandikwa kwa sababu ya maafa ya World Trade Centre zilihusu kashfa katika michezo fulani na habari kuhusu msichana wa miaka 15 aliyemdunga kisu na kumwua mvulana mwenye umri wa miaka 14. Ni gazeti moja tu la habari za michezo nchini Ufaransa ambalo lilichapisha habari zilizokuwa zimepangwa kuchapwa. Lakini kulingana na gazeti Médias, gazeti hilo liliandika habari hiyo kwa sababu picha iliyoonyesha wachezaji wakitoa heshima yao kwa wale waliokufa katika msiba huo kabla ya mechi kuanza haikufika kwa wakati ili kuwekwa katika ukurasa wa mbele.

Matokeo ya Miaka 40 ya Uvutaji wa Sigara

Kulingana na gazeti The Independent la London, mnamo mwaka wa 1962, Chuo cha Royal College of Physicians cha Uingereza kilikuwa ‘shirika rasmi la kwanza la Uingereza kuchapisha onyo la wazi kuhusu hatari za kuvuta sigara.’ Onyo hilo lilichapishwa katika kichapo Smoking and Health. Wakati huo, asilimia 70 ya wanaume na asilimia 43 ya wanawake walivuta sigara. Zaidi ya miaka 40 baadaye, “watu milioni tano huko Uingereza wamekufa kutokana na uvutaji wa sigara. Idadi hiyo ni mara 12 zaidi ya wale waliokufa katika Vita ya Pili ya Ulimwengu.” Ingawa leo ni asilimia 29 ya wanaume na asilimia 25 ya wanawake pekee wanaovuta sigara, bado sigara “zinatangazwa, kusifiwa na kuuziwa vijana,” lasema gazeti The Independent. Kulingana na ripoti ya hivi majuzi ya Chuo cha Royal, utumizi wa tumbaku unaongezeka na bado ndio kisababishi kikuu cha kuzorota kwa afya ya watu. Richard Doll, ambaye katika mwaka wa 1950 alifanya uchunguzi wa kwanza ulioonyesha kwamba uvutaji wa sigara husababisha kansa ya mapafu, anasema kwamba kuna manufaa ya kuacha kuvuta sigara hata kama mtu amevuta kwa muda mrefu au ni mzee. Anaongeza hivi: “Ujumbe wangu ni huu, acha kuvuta sigara, furahia maisha na uishi kwa muda mrefu.”