Manufaa ya Tabasamu
Manufaa ya Tabasamu
NI TENDO linaloweza kutokezwa kwa muda mfupi tu lakini likakumbukwa milele. Ni lenye thamani sana, lakini hakuna mtu aliye maskini sana asiyeweza kulitoa wala tajiri sana ambaye halihitaji. Tunazungumzia nini? Tabasamu.
Mtu anapotabasamu, msuli fulani hujikunja na kufanya macho yang’ae na mdomo kupinda kidogo pembeni kuelekea juu kuonyesha hali ya kuridhika. Kwenye majuma ya kwanza-kwanza baada ya kuzaliwa, wazazi hufurahi sana mtoto wao anapoanza kutabasamu. Hiyo si tabasamu ya hiari. Wataalamu wanaeleza kwamba aina hiyo ya tabasamu mara nyingi hutokea wakati mtoto anapoota na yaelekea inatokana na hisia zake na utendaji katika ubongo na uti wa mgongo. Hata tukiwa watu wazima, aina hii ya tabasamu inaweza kutokea baada ya kula au wakati tunaposikiliza muziki.
Hata hivyo, kuanzia juma la sita, mtoto hutabasamu anapoona uso au kusikia sauti. Aina hiyo ya tabasamu—inayofanywa kwa hiari na inayoonyesha hisia—hutuburudisha, tuwe watoto au watu wazima. Inasemekana kwamba aina hiyo ya tabasamu hutufaidi kiafya pia. Kulingana na wataalamu wa usemi Mirtha Manno na Rubén Delauro, ambao ni wasimamizi wa kituo kiitwacho Tabasamu na Afya, tabasamu hutokeza mawimbi ya umeme mwilini ambayo huchochea tezi inayoitwa pituitari. Kisha tezi hiyo hutoa kemikali fulani zinazoitwa endorphin katika ubongo, ambazo hutufanya tufurahi.
Sababu nyingine ambayo hutufanya tutabasamu ni kwamba tabasamu huwavutia wengine. Hata bila kutamka neno lolote, tabasamu ya kweli huonyesha hisia zetu, iwe ni tabasamu ya salamu, ya kumsikitikia mtu, au ya kutia moyo. Wakati mwingine sisi hutabasamu tunapotazama picha ya mtoto akitabasamu.
Tabasamu changamfu ya mtu mwingine hutuliwaza na kutusaidia tukabiliane na hali ngumu au matatizo. Biblia hutuambia hivi: “Usiwanyime watu mema yaliyo haki yao, ikiwa katika uwezo wa mkono wako kuyatenda.” (Mithali 3:27) Naam, kwa tendo hilo sahili tunaweza kujifaidi na kuwanufaisha wengine. Kwa nini usijitahidi kuwagawia wengine zawadi hiyo yenye thamani sana—tabasamu changamfu?