Ndege Wenye Rangi ya Waridi
Ndege Wenye Rangi ya Waridi
NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI KENYA
KELELE ya maelfu ya ndege wanaolia inaendelea bila kukoma kwenye ziwa la mbali. Maelfu ya ndege wenye rangi ya waridi wanatembea-tembea katika maji ya kijani yanayometameta. Ndege wengine wanaruka angani kwa madaha sana. Wengine wanazunguka-zunguka juu ya uso wa maji wakionyesha wazi manyoya mekundu ya mabawa yao marefu membamba. Ndege hao wenye rangi nyangavu wanavutia sana! Yamkini mandhari hiyo ya maelfu ya ndege ndiyo mandhari ya ndege inayostaajabisha zaidi duniani. Hao ndio flamingo wenye rangi ya waridi wa Bonde Kuu la Ufa la Afrika Mashariki.
Ndege Maridadi Wenye Miguu Mirefu
Flamingo amependwa tangu zamani kwa sababu ya umbo lake jembamba lenye kuvutia. Wamisri wa kale walichonga picha za ndege huyo mwenye shingo ndefu katika maandishi yao. Ndege huyo alikuwa wa kipekee sana na alipendwa hivi kwamba Wamisri walimwona kuwa mfano wa mungu wao aliyeitwa Ra. Watu wa kale walichora picha za ndege huyo
mwenye shingo iliyojipinda na miguu myembamba kwenye kuta za mapango.Leo kuna aina nne za flamingo katika maeneo ya Afrika, Amerika Kusini, Eurasia, na Karibea. Flamingo mdogo kuliko wote ana rangi maridadi sana, manyoya yenye rangi ya waridi na miguu myekundu miangavu. Flamingo mkubwa (mweupe) ana urefu wa sentimeta 140. Urefu huo ni mara mbili ya urefu wa flamingo mdogo (mwekundu). Flamingo wote wana mdomo uliojipinda kuanzia katikati na kuelekea chini. Umbo hilo linapendeza sana.
Anapotaka kuruka, yeye hupigapiga mabawa yake kwa madaha na kukimbia majini ili apate mbio ya kutosha kupaa angani. Anaruka kwa madaha sana huku akinyoosha shingo yake kuelekea mbele na miguu yake kuelekea nyuma. Yakadiriwa kwamba flamingo milioni nne wanaishi katika Bonde Kuu la Ufa la Afrika.
Ndege Dhaifu, Mazingira Magumu
Flamingo wengi wanaoishi katika Bonde Kuu la Ufa hupenda sana maziwa kadhaa ya kipekee yenye magadi. Maji ya maziwa hayo yana magadi nyingi sana hivi kwamba ngozi huwasha unapoyagusa, na ni kana kwamba yana mafuta. Halijoto katika maeneo ya maziwa hayo ya Bonde la Ufa inaweza kufikia nyuzi Selsiasi 65. Hewa ya joto imejaa harufu kali ya chumvi na magadi. Chumvi na kemikali nyingine majini ni nyingi hivi kwamba kandokando ya ziwa kuna matabaka meupe ya kemikali hizo zilizoganda.
Ni wanyama wachache tu wanaoweza kuishi katika maji hayo. Hata hivyo vijiumbe fulani husitawi humo, yaani, mwani mdogo wa samawati-kijani. Jua kali la eneo hilo linafanya maji hayo yenye magadi yawe vuguvugu, hali inayofaa kabisa kwa mwani ambao husitawi sana
humo. Mwani ni mwingi sana hivi kwamba maji ya maziwa yaonekana kuwa ya kijani. Maziwa hayo ni kama vito vya kijani vinavyopamba mabonde na milima ya Bonde Kuu la Ufa.Ni jambo la ajabu kwamba ndege huyo dhaifu anaweza kuishi katika mazingira hayo magumu yenye joto. Hata hivyo flamingo hustarehe huko. Miguu yao myembamba haiathiriwi na maji yenye magadi, na ngozi iliyo katikati ya vidole vyao inawazuia wasizame katika matope. Mazingira hayo magumu yanamfaa kabisa flamingo mdogo. Mdomo wake una nyuzi ndogo sana zinazomwezesha kuvuta na kuchuja vijiumbe vinavyopatikana kwa wingi katika tabaka la juu la maji. Anapokula, flamingo huweka mdomo wake juu chini majini, chini tu ya uso wa maji, naye hutumia ulimi wake kuvuta maji na kuyapitisha kati ya nyuzi zile ndogo zinazochuja na kunasa vijiumbe vile vidogo.
Uchumba Unaovutia
Jua linapochomoza juu ya maji ya kijani ya ziwa ni kana kwamba mchezo fulani wa kuigiza unataka kuanza. Katika mwangaza wa jua la alfajiri lile kundi kubwa la flamingo ambao wamesongamana sana linaonekana kama miale ya moto kwenye uso wa maji.
Ndege hao walio tayari kujamiiana hutembea-tembea katika makundi wakinyoosha shingo zao na kutikisa midomo.Rangi nyingi mbalimbali za waridi na nyekundu zinaonekana jua linapoangazia manyoya mororo ya ndege wanaotembea-tembea, kundi moja kuelekea upande mmoja huku lingine likielekea upande ule mwingine. Ndege wanaruka-ruka na kucheza huku wakitandaza mabawa yao ili kuonyesha manyoya yao mekundu. Wakijivunia rangi nyangavu ya mabawa yao, wao hukimbia majini na kupaa, kisha wanatua na kupaa tena. Ndege hao wamesongamana sana hivi kwamba walio katikati hawawezi kupaa hadi wale walio ukingoni mwa kundi wapae kwanza. Ndege hao waliosisimuka wanalia na kupiga kelele sana.
Kisha, ghafula usiku mmoja, ndege hao wote wanapaa na kuhama ziwa hilo. Wakiwa hewani, wanasafiri katika mpangilio unaofanana na herufi ya V. Wanasafiri mamia ya kilometa hadi ziwa jingine la magadi linalofaa kwa kutaga mayai na kuwatunza vifaranga. Jambo la ajabu ni kwamba flamingo wote wa maziwa yote ya Bonde Kuu la Ufa huhama wakati mmoja.
Sura Mbaya Hubadilika Kuwa Nzuri
Flamingo hupenda kujenga viota vyao kandokando ya maziwa ya mbali ambayo hayawezi kufikiwa kwa urahisi. Jambo hilo ni muhimu kwa maana ndege hao hawapaswi kusumbuliwa wanapojenga viota na wanapolalia mayai. Wakisumbuliwa, ndege hao wanaweza kuondoka na kuacha mayai yao kabisa.
Ndege wanaojenga viota wana shughuli nyingi, nao wanafurahia sana kazi hiyo. Wanatumia mdomo wao kuokota matope, samadi ya ndege, na manyoya machache ili kutengeneza tuta dogo lenye urefu wa sentimeta 40 hivi. Kisha flamingo huchimba shimo dogo juu ya tuta na kutaga yai lake humo, ambamo maji yenye magadi hayawezi kuingia. Punde mamia ya maelfu ya vifaranga huanguliwa. Ndege wazazi wengi huruka huku na huku wakiwa na kazi nyingi za kuwalisha na kuwatunza vifaranga wao wanaolilia chakula.
Kisha vifaranga wanapoweza kutembea, ndege wazazi huondoka ghafula na kuwaacha vifaranga wao. Wao husafiri hadi sehemu nyingine ya ziwa ambako kuna mwani mwingi wa samawati-kijani. Huko, ndege wazazi wanaweza kula na kupumzika wakiwa mbali na vifaranga wao wanaolilia chakula sikuzote. Baadaye ndege wachache wakubwa waliobaki hukusanya vifaranga wote pamoja ili kuwatunza. Kisha vifaranga hao wanaopiga kelele huongozwa na ndege wale wanaowatunza kuvuka matabaka ya chumvi yaliyo kandokando ya ziwa ili waungane tena na wazazi wao. Jambo la kushangaza ni kwamba katika vurugu hiyo yote, ndege wazazi wanaweza kuwatambua vifaranga wao na kuendelea kuwatunza.
Vifaranga wachanga hawana sura nzuri kama wazazi wao wanaopendeza sana. Vifaranga wana shingo na miguu mifupi, midomo iliyonyooka, na manyoya meupe. Muda si muda, miguu na shingo huanza kurefuka, na midomo na shingo huanza kupindika na kuwa kama za wazazi wao. Baada ya miaka miwili au mitatu, manyoya ya vifaranga hao yatakuwa yamebadilika kuwa yenye rangi maridadi ya waridi. Ndipo watakapotafuta wenzi na kujiunga na makundi makubwa ya flamingo wanaopamba maziwa ya magadi katika Bonde Kuu la Ufa.
Flamingo anayependeza na kustaajabisha ameumbwa kwa akili sana. Tunapowaona ndege hao porini sisi hufurahishwa na sura na sauti yao. Lakini zaidi ya hayo, uthamini na upendo wetu kwa Muumba, Yehova Mungu, unaongezeka.
[Picha katika ukurasa wa 17]
Flamingo mweupe
[Picha katika ukurasa wa 17]
Flamingo mwekundu
[Picha katika ukurasa wa 18]
Vifaranga hawana sura nzuri kama wazazi wao