Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Ugumu wa Kulinda Faragha

Ugumu wa Kulinda Faragha

Ugumu wa Kulinda Faragha

MTU ALIYE MASKINI HOHEHAHE ANAWEZA KUKINZA MAMLAKA YA MFALME WA UINGEREZA AKIWA NYUMBANI MWAKE.”WILLIAM PITT, MWANASIASA MWINGEREZA, MWAKA WA 1759-1806.

MANENO hayo ya Pitt yanadokeza kwamba kila mtu ana haki ya kuwa na faragha, kuwa na mambo ya siri maishani mwake bila kuingiliwa na mtu yeyote yule.

Watu wa tamaduni mbalimbali huwa na maoni tofauti-tofauti kuhusu faragha. Kwa mfano, kwenye kisiwa cha Samoa katika Pasifiki, kwa kawaida nyumba hazina kuta, na wapita-njia wanaweza kuona kwa urahisi mambo mengi yanayotendeka humo. Hata hivyo, kuingia katika nyumba bila kukaribishwa huonwa kuwa utovu wa adabu.

Kwa muda mrefu watu wametambua uhitaji wa kuwa na kiasi fulani cha faragha. Maelfu ya miaka kabla ya William Pitt kusema maneno hayo yanayojulikana sana, Biblia ilionyesha uhitaji wa kuheshimu faragha ya wengine. Mfalme Sulemani aliandika hivi: “Mguu wako usiingie katika nyumba ya jirani yako ila kwa kiasi; asije akakukinai na kukuchukia.” (Mithali 25:17) Mtume Paulo alishauri hivi: ‘Fanyeni iwe shabaha yenu kushughulika na mambo yenu wenyewe.’—1 Wathesalonike 4:11.

Likionyesha umuhimu wa kuwa na faragha, gazeti la The UNESCO Courier linasema kwamba faragha “ndiyo msingi wa haki zote za raia.” Pia, mwanasiasa maarufu wa Amerika ya Latini alisema hivi: “Kwa njia fulani, haki zote za binadamu zinahusiana na haki ya kuwa na faragha.”

Hata hivyo, uhalifu na ugaidi unapozidi kuongezeka ulimwenguni, serikali na mamlaka zinazotekeleza sheria zinahisi kwamba ni lazima ziingilie mambo ya watu ya faraghani ili kuwalinda raia. Kwa nini? Kwa sababu wahalifu katika jamii hutumia haki ya kuwa na faragha kuwa udhuru wa kutenda uovu. Kwa hiyo, tatizo lililopo ni kusawazisha jukumu la serikali la kuwalinda raia na haki ya kila mtu kuwa na faragha.

Faragha na Usalama

Mashambulizi ya kigaidi yaliyoshtua ulimwengu mnamo Septemba 11, 2001, yalibadili maoni ya watu kuhusu haki ya serikali ya kuingilia mambo fulani ya siri katika maisha ya watu. Mtu mmoja aliyekuwa mshiriki wa tume ya biashara ya Marekani aliliambia gazeti la BusinessWeek kwamba “Septemba 11 ilibadili mambo.” Alisema hivi: “Magaidi husitawi katika jamii ambayo inalinda faragha yao. Ikiwa ni lazima maisha yao ya faragha yaingiliwe kwa kiasi fulani ili kuwafichua, watu wengi watasema ‘ni sawa, fanyeni hivyo.’” Gazeti hilo linaripoti hivi: “Maoni yaliyokusanywa tangu Septemba 11 yanaonyesha kwamba asilimia 86 ya Wamarekani wanaunga mkono matumizi ya mifumo inayotambua nyuso za watu; asilimia 81 wanataka shughuli za benki na matumizi ya kadi za mikopo yachunguzwe kwa makini; na asilimia 68 wanaunga mkono matumizi ya kitambulisho cha kitaifa.”

Serikali fulani za Ulaya na Amerika zinafikiria kutumia vitambulisho ambavyo vinaweza kuhifadhi alama za vidole na picha ya retina ya jicho la mwenye kitambulisho hicho na vitatumiwa kuchunguza hali yake ya kifedha na iwapo amewahi kuhusika katika uhalifu wowote. Kwa kutumia tekinolojia fulani, inawezekana kulinganisha habari iliyo kwenye kitambulisho na habari iliyo kwenye kadi ya mkopo na kuutambua uso wa mtumiaji kwa kamera maalumu. Hivyo wahalifu wanaweza kukamatwa wanapotaka kununua vitu wanavyonuia kutumia katika uhalifu.

Wahalifu wakijaribu kuficha mabomu, bunduki, au visu ndani ya nguo, au hata kuvificha ndani ya nyumba, bado wanaweza kukamatwa. Mashine zinazotumiwa na mashirika fulani ya usalama zinaweza kutambua kitu chochote kilicho nguoni mwako. Vifaa vipya vya rada vinawawezesha polisi kutambua watu wanaotembea au hata kupumua katika chumba kilicho karibu. Lakini je, mbinu za kisasa zaidi za uchunguzi zinapunguza uhalifu?

Je, Kamera Zinawazuia Wahalifu?

Uhalifu ulipoanza kuongezeka huko Bourke, mji ulio mashambani mwa Australia, kamera nne zilizounganishwa na televisheni ziliwekwa. Kamera hizo zilisaidia kupunguza uhalifu kwa kiasi kikubwa. Lakini matokeo hayo hayako kila mahali. Katika jitihada za kupunguza uhalifu huko Glasgow, Scotland, kamera 32 za aina hiyo ziliwekwa mnamo mwaka wa 1994. Uchunguzi uliofanywa na Kituo Kikuu cha Utafiti cha Scotland ulionyesha kwamba mwaka uliofuata, visa fulani vya uhalifu vilipungua. Hata hivyo, ripoti hiyo inasema hivi: “Idadi ya visa vya uhalifu unaohusiana na ukosefu wa maadili, kutia ndani ukahaba, iliongezeka hadi 120; ulaghai uliongezeka hadi 2185; na makosa mengine (pamoja na makosa yanayohusu dawa za kulevya) yaliongezeka hadi 464.”

Mifumo hiyo ya uchunguzi inaweza kupunguza uhalifu katika maeneo fulani tu lakini huenda isipunguze uhalifu kwa ujumla. Gazeti la The Sydney Morning Herald lilitaja kwamba polisi na wachunguzi wa uhalifu walisema kuwa ongezeko la uhalifu husababishwa na ‘kuhama.’ Gazeti hilo lilisema: “Wahalifu wanapogundua kwamba wanaweza kunaswa kwa kamera au na polisi wa doria katika eneo fulani, wanahamia eneo jingine ili kufanya uhalifu.” Huenda jambo hilo likakukumbusha maneno yaliyoandikwa kwenye Biblia miaka mingi iliyopita: “Yeye ambaye huzoea kufanya mambo maovu huchukia nuru na haji kwenye nuru, ili kazi zake zisipate kukaripiwa.”—Yohana 3:20.

Tatizo linalokabili mamlaka zinazotekeleza sheria ni kwamba hata mfumo wa kisasa zaidi wa rada au unaotumia eksirei hauwezi kutambua mambo yaliyo akilini na moyoni mwa mtu, na humohumo ndimo mapambano ya kukomesha uhalifu, chuki na jeuri yanapaswa kuanzia.

Hata hivyo, kuna namna fulani ya uchunguzi ambao ni bora kuliko tekinolojia yoyote iliyovumbuliwa na mwanadamu. Makala inayofuata itazungumzia uchunguzi huo na jinsi unavyoweza kubadili kabisa tabia ya wanadamu.

[Blabu katika ukurasa wa 6]

“Magaidi husitawi katika jamii ambayo inalinda faragha yao”

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 7]

Je, Rekodi Zako za Tiba Ni Siri?

Watu wengi hufikiri kwamba rekodi zao za tiba na mazungumzo yao pamoja na daktari na mamlaka za hospitali ni siri kabisa. Hata hivyo, shirika la Privacy Rights Clearinghouse linalolinda faragha ya watu linaonya kwamba “huenda ukawa umedanganyika kuwa u usalama.” Simson Garfinkel anasema hivi katika kitabu chake, Database Nation—The Death of Privacy in the 21st Century: “Leo, rekodi za tiba zinatumiwa kwa makusudi mbalimbali . . . Zinatumiwa na waajiri wanapowatafuta wafanyakazi na makampuni ya bima kutafuta wanunuzi wa bima. Zinatumiwa na hospitali na mashirika ya kidini kuomba michango. Hata wafanyabiashara wananunua rekodi chungu nzima za tiba ili wajue watu wanaoweza kununua bidhaa zao.”

Garfinkel aongezea hivi: “Ni vigumu sana kuweka habari hizo zikiwa siri kwa sababu kila mara mgonjwa anapoenda hospitalini, rekodi yake ya tiba husomwa na watu 50 hadi 75.” Katika sehemu nyingine, huenda wagonjwa wenyewe wakafunua mambo yao ya siri kwa kutia sahihi bila kujua hati zinazohusu mambo mbalimbali au fomu za idhini wanapoenda hospitalini. Unapotia sahihi fomu hizo, “unamruhusu daktari atoe habari zako za tiba kwa makampuni ya bima, mashirika ya kiserikali na mashirika mengineyo,” lasema shirika la Privacy Rights Clearinghouse.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 8]

Faragha Katika Biashara

Faragha ya watu wanaotumia Internet inaweza kuingiliwa na mtu yeyote yule. Shirika la Privacy Rights Clearinghouse linasema hivi: “Hakuna huduma zozote za Internet zinazoweza kutuhakikishia haki ya faragha. . . . Watumiaji wa Internet wanaweza kupata habari kwenye vituo mbalimbali . . . , au watumiaji wanaweza tu ‘kusoma’ habari hizo bila kuzibadili. Watumiaji wengi hufikiri kwamba hawawezi kujulikana wanapofanya hivyo. Hiyo si kweli. Unaweza kujua mambo yaliyofanywa na mtu kwenye Internet, kutia ndani mashirika ya habari au faili na vituo vilivyotazamwa na mteja. . . . Rekodi zinazoonyesha ‘mazoea ya mteja ya kutumia Internet’ . . . zinaweza kutumiwa kuchuma pesa nyingi sana . . . Habari hiyo huwasaidia sana wafanyabiashara kupata orodha ya watumiaji wa Internet ambao wanapenda bidhaa au huduma fulani hususa.”

Jina lako linawezaje kuingia kwenye orodha ya wafanyabiashara wanaotafuta wateja moja kwa moja kwenye Internet? Jina lako linaweza kuingizwa kwenye orodha yao ukifanya mojawapo ya mambo yafuatayo:

▪ Ukijaza fomu ya dhamana ya bidhaa kutoka kwa watengenezaji au kadi za kukubali bidhaa fulani.

▪ Ukijiunga au kutoa michango kwa klabu, mashirika, au vyama vya kutoa misaada.

▪ Ukiandikisha magazeti, vitabu, kanda au CD za muziki.

▪ Ukiandikisha jina na anwani yako kwenye kitabu cha orodha ya namba za simu.

▪ Ukishiriki mashindano ya bahati nasibu au mashindano mengineyo.

Zaidi ya hayo, unapotumia kadi ya kutoa pesa, kadi ya mkopo, au unaponunua vitu kwa kadi ya malipo, kampuni hiyo inaweza kuandika jina na anwani yako pamoja na vitu unavyonunua wakati mashine inaposoma bei yake. Na hivyo habari nyingi kuhusu bidhaa unazopenda kununua zinaweza kukusanywa na labda kutumiwa kwa makusudi ya kibiashara. *

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 32 Habari hii imetolewa kwenye Kituo cha Internet cha shirika la Privacy Rights Clearinghouse.

[Picha katika kurasa za 6, 7]

Je, kamera za kuchunguza watu hupunguza uhalifu?