Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Unachunguzwa?

Unachunguzwa?

Unachunguzwa?

ELIZABETH huchunguzwa kwa kamera kila siku anapokuwa kazini. Kamera moja humtazama moja kwa moja usoni, na kamera nyingine nyingi huchunguza kila jambo analofanya. Uchunguzi huo wa hali ya juu ni wa kawaida katika kampuni hiyo kwa sababu inashughulikia mamilioni ya pesa taslimu kila siku.

Elizabeth anajua kwamba atachunguzwa kwa makini kazini kwa sababu alipoajiriwa alielezwa waziwazi jambo hilo. Hata hivyo, mamilioni ya watu wengine hawajui ni kwa kadiri gani wanachunguzwa kila siku.

Kuishi Katika Ulimwengu Ambamo Watu Wanachunguzwa

Je, wewe huchunguzwa kazini? Mamilioni ya wafanyakazi ulimwenguni pote huchunguzwa daima wanapotumia Internet na kuandika Barua-pepe. Uchunguzi wa kila mwaka wa Shirika la Usimamizi la Marekani wa mwaka wa 2001 uligundua kwamba “karibu robo tatu (asilimia 73.5) ya makampuni makubwa ya Marekani . . . hurekodi na kuchunguza mawasiliano ya wafanyakazi wake wakati wa kazi, kama vile mawasiliano ya simu, barua-pepe, matumizi ya Internet na faili wanazohifadhi kwenye kompyuta.”

Serikali hutumia pesa nyingi kununua vifaa vya kuchunguza utendaji wa watu. Ripoti moja iliyokabidhiwa Bunge la Ulaya mnamo Julai 11, 2001, ilisema kwamba “kuna mfumo wa kunasa mawasiliano kati ya watu ulimwenguni pote unaotumiwa kwa ushirikiano nchini Marekani, Muungano wa Uingereza, Kanada, Australia na New Zealand.” Inaripotiwa kwamba serikali hizo zinaweza kutumia mfumo unaoitwa ECHELON wenye vituo vya setilaiti ulimwenguni pote, kunasa na kukagua ujumbe wa setilaiti unaotumwa kupitia simu, faksi, Internet, na Barua-pepe. Gazeti Australian linadai kwamba kwa kutumia mfumo huo, serikali zinaweza “kunasa faksi na barua-pepe za watu fulani, na kuna programu inayoweza kutambua sauti fulani, na hivyo simu zinazopigwa na watu hao zinaweza kusikilizwa.”

Mamlaka zinazotekeleza sheria hutegemea pia mbinu za kisasa za kupeleleza. Nchini Marekani, gazeti la BusinessWeek linaripoti kwamba Shirika la Upelelezi la Marekani (FBI) hutumia mfumo unaoitwa Carnivore “kukagua barua-pepe, ujumbe unaotumwa haraka kwa kompyuta, na simu zinazopigwa kwa njia ya kielektroni.” Kwa sasa, sheria mpya imetungwa nchini Uingereza ili kuruhusu mamlaka zinazotekeleza sheria ‘kupeleleza kisiri maelfu ya watu wanaotumia simu, faksi na Internet,’ laripoti Shirika la Utangazaji la Uingereza.

Kamera Zilizofichwa na Hifadhi za Habari Nyingi Katika Kompyuta

Huenda mtu akawa anachunguzwa hata asipotumia simu, faksi, au Barua-pepe. Katika jimbo la New South Wales nchini Australia, watu wanaosafiri kwa gari-moshi huchunguzwa na zaidi ya kamera 5,500. Katika jimbo hilohilo, mabasi 1,900 ya serikali yana kamera za kuwachunguza abiria.

Inaripotiwa kwamba Uingereza ina kamera nyingi zaidi ulimwenguni zinazowachunguza watu ikilinganishwa na idadi ya watu—uchunguzi mmoja unaonyesha kwamba kuna kamera 1 kwa kila watu 55. Mnamo mwaka wa 1996, kulikuwa na kamera kwenye sehemu za umma za miji au majiji 74 tu katika Muungano wa Uingereza. Kufikia mwaka wa 1999, kamera hizo zilikuwa katika miji na majiji 500. Programu mpya za kompyuta zinaunganishwa na kamera ambazo zinaweza kumtambua mtu fulani hususa, hata akiwa katikati ya umati kwenye eneo la umma au katika uwanja wa ndege.

Sasa kuliko wakati mwingine wowote, maisha yako ya faraghani yanaweza kuchunguzwa bila hata wewe kujua. Simon Davies, mkurugenzi wa kikundi cha kutetea haki za binadamu cha Privacy International, anasema: “Habari kuhusu umma zimekusanywa kwa wingi sana sasa kuliko wakati mwingine wowote katika historia. Habari nyingi kuhusu mfanyakazi wa kawaida katika nchi zilizositawi zimehifadhiwa katika vituo vikuu 400 vya kompyuta—habari hizo ni nyingi sana hivi kwamba kila mtu anaweza kuwa na kitabu kikubwa chenye habari zake.”

Ni hatua gani unazoweza kuchukua ili kulinda faragha yako?