Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Unahitaji Usingizi!

Unahitaji Usingizi!

Unahitaji Usingizi!

Je, ni kweli kwamba kupata usingizi wa kutosha usiku ni muhimu ili kudumisha afya bora? Labda unajibu ndiyo. Hata hivyo, watu wengi hawaoni usingizi kuwa muhimu. “Lakini wao huumia siku ifuatayo,” asema Shawn Currie, mtaalamu wa tabia na profesa msaidizi katika Chuo Kikuu cha Calgary, nchini Kanada. Kukosa usingizi wa kutosha kwaweza kumfanya mtu awe mwenye kuudhika upesi na hata mara nyingine ashuke moyo.

“Wanasayansi husema kwamba usingizi unaweza kuboresha utendaji wa ubongo, na mtu huendelea kujifunza akiwa usingizini,” lasema gazeti Calgary Herald. Profesa Currie anasema: “Mtu huboresha kumbukumbu lake anapolala na mambo ambayo alijifunza mchana huhifadhiwa vizuri. Akikosa pindi hiyo ya pumziko, kujifunza huathiriwa.” Anaongeza kusema kwamba “huenda kulala vya kutosha husaidia kutuliza akili zetu kwa njia fulani.”

Basi mtu anapaswa kulala kwa saa ngapi? Ingawa wataalamu wengi hupendekeza saa nane, Currie asema hivi: “Mahitaji ya kulala hutofautiana.” Kwa hiyo anadokeza kwamba mtu ajitahidi kulala usingizi mzito na mtulivu. Lakini hilo lawezekanaje, hasa mtu akiwa na matatizo ya kukosa usingizi? Yafuatayo ni madokezo machache:

▪ Oga kwa maji ya moto kabla ya kulala.

▪ Fanya mazoezi ya kutosha mara kadhaa kila juma; lakini usifanye mazoezi yenye kuchosha kabla ya kulala.

▪ Weka chumba chako cha kulala kikiwa kitulivu, chenye giza, na kikiwa na baridi kidogo.

▪ Jaribu kuamka saa zilezile kila asubuhi ili mwili wako uzoee kuamka saa hizo.

Kwa kuwa kulala usingizi mzuri huleta faida za kiafya, uwe mwenye busara na kuuona kuwa muhimu sana.