Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Ua Unaoathiri Hali ya Hewa

Ua Unaoathiri Hali ya Hewa

Ua Unaoathiri Hali ya Hewa

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI AUSTRALIA

WAKATI mmoja huo uligawanya jimbo la Australia Magharibi toka kaskazini hadi kusini. Ulipokamilika katika mwaka wa 1907, ukuta huo wenye urefu wa kilometa 1,830 ulioundwa kwa mbao na waya ukawa ua mrefu zaidi wa aina yake ulimwenguni. Jina lake rasmi lilikuwa Ua Na. 1 wa Kuzuia Sungura.

Kama jina hilo linavyodokeza, ua huo uliundwa kuzuia sungura waliovamia eneo la magharibi mwa Australia mwishoni mwa karne ya 19. Ijapokuwa miaka mia moja imepita tangu uundwe, sehemu kubwa ya ua huo ingalipo. Hata hivyo, katika miaka ya majuzi ua huo umewavutia wanasayansi kwa sababu tofauti. Inaonekana ua huo unaathiri hali ya hewa ya eneo hilo kwa njia isiyo ya moja kwa moja.

Kabla ya kujua jinsi ua huo wenye urefu wa meta moja hivi unavyoathiri hali ya hewa, hebu kwanza tujifunze historia ya ujenzi wake yenye kupendeza.

Jitihada Isiyofanikiwa

Ua Na. 1 wa Kuzuia Sungura ulijengwa na watu 400 waliofanya kazi ya jasho kutoka mwaka wa 1901 hadi mwaka wa 1907 ili kuzuia uvamizi wa sungura. Kulingana na Idara ya Kilimo ya Australia Magharibi, “tani zipatazo 8,000 za vifaa zilisafirishwa kwa meli na kupelekwa kwa gari-moshi hadi kwenye depo ambapo vilichukuliwa kwa vikundi vya farasi, ngamia na punda hadi katika maeneo ya mbali ya ujenzi.”

Wafanyakazi walifyeka eneo lenye upana wa meta tatu kila upande wa ua. Miti iliyokatwa ilitumiwa kama vigingi vya kutengenezea ua, na mahali ambapo hapakuwa na miti, vigingi vya chuma viliagizwa kutoka nchi za nje. Ulipokamilika, ua huo haukutumiwa tu kuzuia sungura, bali pia ukawa barabara ya kupitia bara hilo.

Ua huo ulikuwa kama wavu mkubwa wa kuelekeza sungura kwenye vyumba ambapo walinaswa na kufa. Hata hivyo, sungura waliruka sehemu fulani za ua. Vipi? Walipoelekea upande wa magharibi, sungura walipanda juu ya mizoga ya sungura wenzao waliorundamana uani na hivyo wengi wakaruka hadi upande wa pili. Nyua nyingine mbili zilijengwa na zikashikana na ua wa kwanza. Kwa ujumla, ua wote ulikuwa na urefu wa kilometa 3,256.

Walivumilia Sana

Wapanda-farasi kadhaa walifanya kazi ya kulinda doria wakizunguka ua wote. Mmoja wao alikuwa F. H. Broomhall. Katika kitabu chake The Longest Fence in the World, Broomhall anasema: “Kazi ya mlinda-doria . . . ilikuwa kutunza Ua na njia iliyokuwa kando yake . . . , kupunguza ukubwa wa miti pande zote za Ua, kutunza milango iliyokuwa imeundwa kila baada ya kilometa 32 kwenye Ua, na kutoa sungura waliokufa vyumbani.”

Mlinda-doria wa mpakani alikuwa mpweke sana. Akiwa na ngamia wake tu, kila mmoja alihitajika kutunza kilometa nyingi za ua huo mrefu sana. Wengine hawakuweza hata kutumia ngamia kwa sababu walihitajika kusafiri kwa baiskeli kwenye barabara mbovu. Leo magari makubwa yenye starehe hutumiwa kulinda doria katika sehemu inayobaki ya ua huo.

Haikuwa Kazi Bure

Ingawa huenda ua huo ulishindwa kuzuia uvamizi wa sungura, umesaidia kuzuia tatizo jingine—ndege wa Australia, aitwaye emu. Mnamo mwaka wa 1976, zaidi ya ndege hao wakubwa 100,000 wasioruka waliamua kusafiri kuelekea kwenye mashamba yenye rutuba magharibi mwa ua huo. Ingawa ndege 90,000 waliuawa, ua huo ulizuia uvamizi huo na sehemu kubwa ya mavuno ya mwaka huo iliokolewa kutokana na janga ambalo lingetokea.

Tangu wakati wa janga hilo, sehemu ya ua huo yenye urefu wa kilometa 1,170 imeimarishwa au kusongezwa ili kulinda mashamba ya Australia Magharibi kutokana na ndege hao wahamaji na kutokana na mbwa-mwitu. * Sasa ua huo umegawanya maeneo mawili. Upande wa mashariki una nyika ambayo iko katikati ya Australia. Upande wa magharibi una mashamba yanayotunzwa vizuri.

Ukuta Unaoathiri Hali ya Hewa

Huenda tofauti hiyo kubwa kati ya eneo la magharibi na mashariki ikaeleza kwa nini ua huo unaathiri hali ya hewa. Gazeti la kisayansi The Helix lasema: “Amini usiamini, mvua imeongezeka upande wa mashariki wa ua na kupungua upande wa magharibi wa ua.” Kwa hiyo, kichaka kilichoko upande wa mashariki hupata mvua kwa ukawaida, huku wakulima upande wa magharibi wakilazimika kunyunyizia maji mashamba. Likitoa sababu moja ambayo huenda inaleta tofauti hiyo, gazeti hilo linasema: “Mimea inayokuzwa ina mizizi mifupi ambayo haipeleki maji mengi hewani kama mimea ya kiasili yenye mizizi mirefu.”

Akitoa sababu nyingine, Tom Lyons, profesa wa sayansi ya anga-hewa, asema: “Tunafikiri kwamba kwa kuwa mimea ya kiasili ni yenye rangi nzito ya kijani kuliko ile inayokuzwa, hiyo hupeleka joto jingi kwenye anga-hewa na kusababisha . . . upepo ambao husaidia kufanyiza mawingu.”

Huenda Ua wa Kuzuia Sungura haukuzuia sungura wasivamie mashamba ya wakulima wa Australia Magharibi. Hata hivyo, huenda umeleta manufaa kutokana na jinsi ambavyo umeathiri hali ya hewa, na kuonyesha umuhimu wa kupanga shughuli za kilimo tukizingatia wakati ujao.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 15 Sasa ua huo unaitwa Ua wa Kugawanya Jimbo.

[Ramani katika ukurasa wa 14, 15]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

Ua Na. 1 wa Kuzuia Sungura

[Picha katika ukurasa wa 15]

Sungura

[Picha katika ukurasa wa 15]

Kulinda doria kuzunguka ua, mapema katika karne ya 20

[Picha katika ukurasa wa 15]

“Emu”

[Picha katika ukurasa wa 15]

Ua Na. 1 wa Kuzuia Sungura ulikuwa ua mrefu ulimwenguni wa kilometa 1,833. Ua huo unatenganisha kichaka na mashamba, hivyo kugawanya hali tofauti za hewa

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 15]

All color pictures: Department of Agriculture, Western Australia; top center: Courtesy of Battye Library Image number 003582D