Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kundi Kubwa Lahama

Kundi Kubwa Lahama

Kundi Kubwa Lahama

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI KENYA

ARDHI yatetemeshwa na milio ya kwato milioni moja. Kundi kubwa la wanyama linasonga mbele, huku likitifua vumbi jekundu. Wanyama hao wenye miguu mirefu myembamba wanapiga hatua kati ya mabonde na vilima, na kuvuka nyanda za mbuga, mito na vijito. Wanasonga mbele wakiwa kundi kubwa, huku waking’oa nyasi nyingi kabisa. Uhamaji huo wa kundi kubwa la nyumbu wanaolia kama ng’ombe ni mojawapo ya matukio ya porini yenye kustaajabisha zaidi.

Bustani ya Edeni ya Afrika

Eneo la Serengeti ni nyika. Ni mbuga kubwa yenye miinuko-inuko midogo inayopatikana nchini Tanzania na Kenya, na ina ukubwa wa kilometa 30,000 hivi za mraba. Udongo wa mbuga hiyo una rutuba, na hilo linawezesha nyasi nyingi ziote kila mahali. Sehemu fulani zina migunga na vichaka vyenye miti yenye miiba, na makundi ya tembo hula majani yake. Makundi ya twiga hutembea kwa madaha kati ya vichaka hivyo huku yakipiga hatua ndefu polepole.

Katika sehemu fulani, kuna majabali ya matale, ambayo yamelainishwa na pepo na mvua, ambapo simba na chui huwaotea wanyama. Mito inayoenda kasi na inayojipinda-pinda ina viboko na mamba wengi. Unaweza kuona makundi ya nyumbu, kongoni, nyamera, na paa wa aina nyinginezo wakilisha kwenye nyanda hizo. Pundamilia wenye kiu hukusanyika kwenye vidimbwi na kuvizunguka kama mikufu yenye shanga nyeupe na nyeusi. Swala na swalapala wanarukaruka hapa na pale katika nyanda hizo. Makundi makubwa ya nyati wenye pembe kubwa zilizojipinda na misuli mikubwa, wanalisha taratibu huku wakivuta nyasi kwa midomo yao mipana.

Kuna makundi mengi ya simba katika mbuga ya Serengeti. Wakati wa joto kali la mchana, simba hao hupumzika chini ya vivuli vya miti na vichaka wakisubiri usiku ufike ili waende kuwinda. Huwezi kuwaona chui wenye madoadoa kwa urahisi wanapolala kwani huwa wamejinyoosha kwa starehe juu ya matawi ya miti huku wakiwa wamefunikwa na mwangaza hafifu unaopenyeza majani ya miti hiyo. Duma hukimbia kama mshale katika nyanda za mbuga hiyo. Yeye ana mwili mwembamba, naye hutimua kwelikweli anapokimbiza windo lake.

Ama kweli, Serengeti ni mbuga iliyojaa wanyama wenye kupendeza. Lakini yale makundi mengi ya nyumbu hufanya mojawapo ya mambo ya kustaajabisha zaidi kati ya mambo yote yanayotukia porini.

Mcheshi wa Nyanda

Kuna karibu nyumbu milioni moja na nusu huko Serengeti. Nyumbu ana sura ya kiajabu, kwani ana kichwa kirefu na macho yanayong’aa ambayo yameachana sana na ambayo yako karibu na kipaji cha uso wake. Ana pembe kama za ng’ombe ambazo hujipindapinda. Mgongo wake huinama chini hadi kwenye miguu ya nyuma, ambayo inaonekana kuwa dhaifu na myembamba inapolinganishwa na mabega yake na shingo yake yenye nguvu. Miguu yake myembamba hutegemeza mwili wake mzito. Ama kwa hakika, nyumbu anafanana na wanyama kadhaa kwani ana ndevu nyeupe, ana nywele nyeusi shingoni, na mkia kama wa farasi.

Nyumbu wana tabia zenye kuchekesha. Wanapokusanyika pamoja katika makundi makubwa, wao hutoa mlio unaofanana na mikoromo ya maelfu ya vyura. Wanaposimama kwenye nyanda, wao huzubaa kana kwamba wanashangazwa na mazingira yao.

Nyakati nyingine, nyumbu-dume hukimbia akiruka huku na huku na kuzunguka-zunguka. Yeye hurukaruka akiwa amenyoosha miguu yake na kutikisa-tikisa kichwa chake, huku akitifua vumbi kwa njia yenye kuchekesha. Watu fulani wanasema kwamba nyumbu hufanya hivyo ili kuwafurahisha nyumbu-jike au kuwaonya madume wengine. Hata hivyo, yaonekana nyakati nyingine nyumbu-dume hufanya hivyo anapoona raha.

Wanazaliwa Katika Mazingira Hatari

Nyumbu huanza kuzaa kwa wakati barabara. Nyumbu wana uwezo wa kipekee, kwani nyumbu wengi wanaweza kuzaa watoto wakati uleule. Asilimia 80 hadi 90 ya watoto wao huzaliwa katika kipindi cha majuma matatu. Wakati huo, kundi lao huwa na maelfu ya nyumbu wachanga wanaolialia. Kila mama anahitaji kuharakisha awe karibu na mtoto wake. Hiyo ni kwa sababu endapo kundi litaanza kukimbia haraka, mama anaweza kutenganishwa na mtoto wake, na haitakuwa rahisi kwa mtoto kuendelea kuishi akiwa peke yake.

Watoto wa nyumbu huzaliwa katika mazingira hatari kwani kuna wanyama wengi wawindaji ambao wanawaotea. Nyumbu-jike husubiri mambo yawe shwari ili wazae. Hata hivyo, adui akijitokeza ghafula, nyumbu-jike wana uwezo wa ajabu wa kuacha kuzaa na kukimbia. Kisha, mambo yanapokuwa shwari, wanaweza kuendelea kuzaa.

Ni kana kwamba nyumbu wachanga huzaliwa wakijua kuwa wamo hatarini, kwani wao huanza kusimama dakika chache tu baada ya kuzaliwa. Baada ya juma moja, nyumbu wachanga huweza kukimbia kilometa 50 kwa saa.

Wakati wa Kuhama

Nyumbu huhamahama wakiwa makundi makubwa katika mbuga ya Serengeti. Wao huhama hasa kwa sababu ya mvua. Mvua hunyesha kwa kutegemea hali ya hewa ambayo hubadilika-badilika kila mwaka. Mvua hunyesha katika sehemu tofauti-tofauti za mbuga hiyo kubwa siku zote za mwaka.

Nyumbu huhitaji maji kila siku na nyasi ya kutosha. Maadamu kuna chakula na maji, hawahami. Lakini majira ya kiangazi yanapoendelea, nyasi na vidimbwi vya maji hukauka. Nyumbu hawawezi kuendelea kujikalia kitako wakisubiri mvua inyeshe. Inawabidi waende mahali penye mvua.

Mvua inaponyesha, nyanda hizo kavu hubadilika. Baada ya siku chache, nyasi huanza kuchipuka ghafula kutoka kwenye udongo wenye rutuba na kufanya eneo hilo liwe na rangi ya kijani. Nyasi hizo zina virutubisho vingi na unyevunyevu mwingi—na nyumbu wanapenda sana nyasi za aina hiyo.

Viumbe hao wanaweza kujua mahali ambapo mvua inanyesha hata wakiwa mbali sana. Haijulikani jinsi ambavyo wao hutambua kwamba kuna mvua katika sehemu nyingine ya Serengeti—labda ni kwa kutazama mawingu ya mvua kutoka mbali au kwa kunusa unyevunyevu ulio katika hewa kavu. Kwa vyovyote vile, ili kuendelea kuishi, makundi ya nyumbu hulazimika kuhama. Na hivyo ndivyo wanavyofanya!

Safari Ngumu

Wao huanza kuhama polepole. Nyumbu ni wanyama wanaopenda kufanya mambo kwa ushirikiano. Hivyo, nyumbu mmoja akianza kutembea kuelekea upande fulani, nyumbu wengine walio karibu naye huacha kula na kumfuata. Punde si punde, kundi lote huanza kuhama. Kwa sababu ya kiu na njaa, wao huzidi kusonga mbele. Nyakati nyingine wao hukimbia. Nyakati nyingine wao hutembea polepole wakifuatana katika mistari mirefu na kufanyiza vijia mavumbini.

Safari yao imejaa hatari nyingi. Wanyama wanaowinda hufuata makundi hayo ya nyumbu na huwa macho kuona wanyama wowote wanaotembea polepole, walio vilema, au wagonjwa. Nyumbu wanaposonga mbele, wao huingia katika maeneo yenye makundi ya simba wanaootea. Simba hujificha katika nyasi ndefu, kisha wao hukimbia kati ya makundi ya nyumbu wanaolisha na kuwafanya watawanyike kwa hofu. Chui, duma, mbwa-mwitu, na fisi huwaotea wanyama wanaobaki nyuma au wanaojitenga na kundi. Nyumbu anapouawa, tai-mzoga hujitokeza. Tai hao hung’ang’ania na kupigania mabaki ya mzoga huo na kuacha mifupa tu. Kisha mifupa hiyo huchomwa na jua na kuwa myeupe.

Inabidi makundi ya nyumbu yavuke mito inayoenda kasi. Inavutia sana kuona nyumbu wakivuka mito, kwani maelfu ya wanyama hao husimama kwenye kingo za mito zilizoinuka na kuruka ndani ya maji. Wengi wao hufaulu kuvuka salama salimini hadi upande wa pili wa mto. Wengine hubebwa na maji au hutafunwa na mamba ambao wanaotea chini ya maji. Nyumbu hufunga safari hiyo ngumu kila mwaka. Wao husafiri umbali wa kilometa 3,000 hivi.

Mwanadamu Ndiye Adui Mkubwa Zaidi

Kwa karne na miaka, mwanadamu hakuingilia uhamaji wa nyumbu. Sasa, mwanadamu ndiye anayeathiri sana uhamaji huo. Katika miaka ya majuzi, serikali za Tanzania na Kenya zimejitahidi kuwalinda wanyama wa Serengeti. Hata hivyo, ijapokuwa uhamaji huo wa nyumbu hutukia hasa katika mbuga za wanyama, maelfu ya wanyama hao hunaswa kinyume cha sheria na kuuawa na wawindaji haramu. Wao hutumia mitego iliyotengenezwa kwa nyaya, mishale yenye sumu, na bunduki kuwawinda wanyama hao ili kuwauzia wateja walio tayari kununua nyama yao na sehemu nyingine zinazotumiwa kama mapambo. Walinzi wa hifadhi za wanyama wa pori huzunguka maeneo yanayohifadhiwa, lakini mbuga ya Serengeti ni kubwa sana hivi kwamba si rahisi kulinda sehemu zake zote. Idadi ya watu inapozidi kuongezeka, inawabidi watu wengi zaidi wahamie kwenye mbuga hizo zenye rutuba. Bado kuna mjadala mkali kuhusu uhitaji wa kutenga maeneo makubwa kwa ajili ya wanyama wa pori.

Wakati mmoja mamilioni ya nyati walikuwapo katika nyanda za Amerika Kaskazini. Sasa wametoweka. Watu fulani wana wasiwasi kwamba jambo hilohilo litayakumba yale makundi makubwa ya nyumbu wa Afrika Mashariki. Hapana shaka kwamba tutahuzunika sana endapo wanyama hao wenye kustaajabisha watatoweka. Tunatazamia kwa hamu wakati ambapo wanadamu na wanyama wataishi kwa amani na upatano kabisa chini ya utawala mwadilifu wa Mungu. (Isaya 11:6-9) Kwa sasa, tutaendelea kustaajabishwa na ule uhamaji wa makundi makubwa ya nyumbu.

[Picha katika ukurasa wa 18]

Makundi ya nyumbu hulazimika kuvuka mito inayoenda kasi