Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuonyesha Upendo Nyakati za Taabu

Kuonyesha Upendo Nyakati za Taabu

Kuonyesha Upendo Nyakati za Taabu

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI NIGERIA

JUMAPILI ya Januari 27, 2002, iliitwa Jumapili Mbaya Sana huko Lagos, Nigeria. Wakati wa jioni, mlipuko ulitokea katika hifadhi ya silaha iliyokuwa chini ya ardhi na kusababisha moto mkubwa na mitikisiko yenye nguvu kotekote katika jiji hilo. Kwa muda wa saa kadhaa, makombora na vifusi vilitupwa umbali wa kilometa tatu na kusababisha wasiwasi jijini.

Uvumi ulisambaa na kuongeza hofu. Halaiki ya watu waliojawa na hofu walikimbia barabarani, bila kujua wanakimbia nini au wanaenda wapi. Kwa kuwa kulikuwa na giza, mamia ya watu, kutia ndani watoto wengi wenye wasiwasi, walitumbukia na kuzama ndani ya mitaro yenye maji machafu. Nyumba, shule, na majengo ya biashara yalibomolewa au kuharibiwa sana, hivyo maelfu ya watu wakapoteza makao yao na kazi. Inakadiriwa kwamba watu 1,000 walikufa katika msiba huo. Makadirio ya baadaye yalionyesha idadi kubwa zaidi.

Mabomu 1,350 hivi ambayo hayakulipuka, mizinga, na mabomu ya kutupwa kwa mkono yalipatikana baadaye kwenye makao ya watu wanaoishi karibu na hifadhi hiyo ya kijeshi ambako kulitokea mlipuko. Mtu mmoja alipata chuma fulani sebuleni mwake. Bila kutambua kwamba chuma hicho kilikuwa bomu, alikiokota, akakiweka nyuma ya gari lake, na kukirudisha kwa wenye mamlaka.

Baada ya kupokea habari hizo za mlipuko, ofisi ya tawi ya Mashahidi wa Yehova huko Nigeria iliwasiliana mara moja na mzee mmoja huko Lagos na ikawaagiza waangalizi wasafirio 16 wa eneo hilo wachunguze hali ya Mashahidi 36,000 wanaoishi Lagos. Ofisi ya tawi ilituma naira milioni moja (dola 10,000 hivi za Marekani) na ikawaagiza waanzishe halmashauri ya kutoa msaada.

Mwanamume mmoja Shahidi aliumizwa sana na mabaki ya bomu; wasichana wawili Mashahidi wakafa; na Majumba mawili ya Ufalme na nyumba za familia 45 zikaharibiwa.

Mnamo Februari 2, 2002, siku sita baada ya mlipuko huo, vita vya kikabila vilizuka katika eneo jingine la jiji hilo. Kulingana na Shirika la Msalaba Mwekundu, vita hivyo vilisababisha vifo vya watu 100, watu 430 wakajeruhiwa, watu 3,000 wakalazimika kuhama makwao, na nyumba 50 zikateketezwa. Ndugu wa halmashauri ya kutoa msaada waliokuwa wameshughulikia mahitaji ya wale walioathiriwa na mlipuko wa bomu waliwatafuta ndugu zao Wakristo katika eneo hilo haraka.

Hakuna Shahidi yeyote aliyekufa katika kisa hiki, kwani wengi wao walikuwa wanahudhuria kusanyiko la mzunguko vita hivyo vilipozuka. Hata hivyo, washiriki wengi wa makutaniko matano yaliyo katika eneo hilo walipoteza makao yao. Ndugu zao Wakristo waliwakaribisha nyumbani mwao kwa hiari. Daktari mmoja Shahidi na mke wake waliwapa makao watu 27 waliolazimika kuhama makwao.

Mashahidi huko Lagos ambao hawakuathiriwa na ule mlipuko wala vita walitoa chakula, mavazi, na vyombo vya nyumbani kwa hiari. Mwangalizi wa jiji aliripoti hivi: “Michango ya ndugu zetu wa Lagos ni mingi sana kuliko mahitaji ya wale walioathiriwa.” Ilibidi ofisi ya tawi iyaandikie makutaniko barua ili kuyaomba yasitoe michango zaidi. Vitu vilivyochangwa na kubaki vilipakiwa katika malori matatu na kupelekwa kwenye ofisi ya tawi ili vihifadhiwe huko.

Wazee wa makutaniko walitembelea watu wengi walioathiriwa na vilevile familia zilizofiwa. Waliwafariji kwa Maandiko. Halmashauri ya kutoa msaada ilifanya mipango ili nyumba zilizoharibiwa zirekebishwe. Halmashauri hiyo iliwapa wale walioathiriwa na misiba hiyo miwili vyombo vya nyumbani, mavazi, na chakula. Iliwasaidia wale waliolazimika kuhama wapate mahali pa kulala. Halmashauri hiyo ilisaidia familia 90 na watu wengine mmoja-mmoja.

Watu wengi walioathiriwa na misiba hiyo walifurahia sana msaada waliopokea. Shahidi mmoja aliiambia hivi halmashauri ya kutoa msaada: “Maadamu niko hai, nitamfanya Yehova kuwa ‘kimbilio na nguvu’ zangu!”—Zaburi 46:1, 2.

Watu ambao si Mashahidi waliona jinsi Mashahidi wa Yehova walivyotunzana nyakati hizo za taabu. Mjomba wa Shahidi mmoja aliyekufa, aliwaeleza hivi wazee wa kutaniko la Shahidi huyo: “Nitarudi kuwashukuru kwa dhati na kujifunza mengi zaidi.” Naye akawaambia hivi watu wa jamaa yake: “Nilifurahia sana yale niliyoona huko Lagos. Hata watu wa jamaa moja hawakusaidiana kama vile watu hawa walivyofanya.”

[Picha katika ukurasa wa 13]

Lori lenye misaada

[Picha katika ukurasa wa 13]

Baadhi ya wale waliosaidiwa

[Picha katika ukurasa wa 14]

Wenzi hawa waliwapa makao watu 27 waliolazimika kuhama makwao

[Picha katika ukurasa wa 14]

Mashahidi wanarekebisha nyumba iliyoharibiwa

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 13]

Top: Sam Olusegun - The Guardian