Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kutoka kwa Wasomaji Wetu

Kutoka kwa Wasomaji Wetu

Kutoka kwa Wasomaji Wetu

Polisi Ningependa kuwashukuru kwa mfululizo wa makala “Kwa Nini Tunahitaji Polisi?” (Julai 8, 2002) Baba yangu alikufa katika msiba wa barabarani miaka mitatu iliyopita. Maafisa wawili wa polisi katika eneo letu walituletea habari hiyo na wakatusaidia na kutufariji. Mmoja wao hata alimtuliza mama yangu alipolia. Nina hakika kazi ya maafisa hao si rahisi, na tulithamini sana kazi yao.

D. E., Marekani

Baada ya kusoma mfululizo huo, nina swali. Je, Shahidi wa Yehova anaweza kuwa polisi? Vita ikitokea, huenda akaitumia bunduki na kumuua mtu.

J. S., Australia

“Amkeni!” lajibu: Kusudi la mfululizo wetu wa makala ni kuonyesha umuhimu wa kazi ya polisi katika kudumisha amani na kutoa huduma nyingine. Mashahidi wengi wa Yehova huepuka kufanya kazi inayowataka wachukue silaha kwa sababu hawataki kuwa na hatia ya damu kwa kumwua mtu. (Kutoka 20:13; Mathayo 26:51, 52) Hata hivyo, ni lazima ikumbukwe kwamba kuna watu wengi walioajiriwa kulinda usalama ambao hawabebi silaha, na katika nchi fulani polisi wengi hawabebi bunduki.

Nimemaliza kusoma makala kuhusu umuhimu wa kuwa na polisi. Hizo ni makala nzuri na zinaonyesha uthamini kwa kazi ngumu ambayo polisi hufanya ili kudumisha kiasi fulani cha amani katika ulimwengu huu wenye misukosuko. Katika miaka ya 1970, mimi na mke wangu tulikuwa wahudumu waliosafiri na tuliishi katika orofa ya chini katika Jumba la Ufalme zee. Tulikuwa tukitembelea kutaniko moja katikati ya jiji. Kwa sababu kulikuwa na joto jingi, tulifungua dirisha kidogo ili tupate hewa. Saa nane usiku, mke wangu alisikia wanaume wawili wakizungumza karibu na dirisha na akaniamsha. Niliwasikiliza. Mmoja alisema kwamba mara nyingi dirisha hilo huwa limefungwa. Yule mwingine alisema kwamba huenda kulikuwa na watu humo kwa sababu kulikuwa na gari lililoegeshwa nje. Walikuwa maafisa wa polisi, na inaonekana kwamba mara nyingi walikuwa wakilinda Jumba la Ufalme. Baada ya tukio hilo, tulilala fofofo!

P. S., Marekani

Makala hizo kuhusu polisi zilikuja kwa wakati unaofaa, hasa baada ya mashambulizi ya kigaidi dhidi ya World Trade Center na makao makuu ya kijeshi ya Pentagon, nchini Marekani. Natumaini tumeongeza uthamini wetu kwa polisi, wazima-moto, na watumishi wengine wa umma walio na daraka la kulinda raia na mali dhidi ya ugaidi na uhalifu kwa ujumla.

H. B., Marekani

Kuishi Pamoja Kwa muda mrefu nimetamani kupata makala inayozungumza kuhusu kuishi pamoja. Niliposoma makala “Vijana Huuliza . . . Ninawezaje Kupata Mtu Mzuri wa kuishi Naye?” (Mei 22, 2002), nilishangaa kutambua kwamba kuna watu ambao hawapendi kuwa marafiki wa karibu sana na watu wanaoishi pamoja nao au hata kutembea nao. Hilo ni jambo la kawaida. Hata hivyo, watu wanaoishi pamoja husaidiana kulipia gharama na kufanya kazi za nyumbani. Asanteni kwa kunisaidia niwe na maoni yanayofaa.

S. M., Japan

Baada ya majuma mawili nitaanza kuishi pamoja na Shahidi mwenzangu huko Dresden. Makala zinazozungumza kuhusu kuishi pamoja katika matoleo ya Aprili 22, Mei 22, na Juni 22, zina ushauri mzuri sana na zilikuja kwa wakati unaofaa. Endeleeni kuandika makala nzuri kama hizo!

R. P., Ujerumani