Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Mabingwa wa Kuigiza Sauti

Inasemekana kwamba kwezi wanaweza kuigiza milio ya zaidi ya ndege 40 tofauti-tofauti. Isitoshe, kwezi fulani amesikika akiigiza sauti ya mabasi, mashine ya kukata mbao, ving’ora vya magari, kondoo, na hata mlio wa farasi. Lakini sasa kwezi wameanza kuigiza sauti mpya—mlio wa simu za mkononi. Kwa hiyo, “ukisikia simu ya mkononi ikilia nje, huenda ukashangaa kugundua kwamba ‘simu’ hiyo ina mabawa,” laripoti gazeti National Geographic. ‘Kadiri simu za mkononi zinavyozidi kuongezeka, ndivyo ndege wanaoigiza sauti watakavyokuwa na milio mipya ya kuigiza,’ lasema gazeti hilo.

“Kusema Uwongo Ni Kazi Ngumu kwa Ubongo”

Watafiti katika Chuo Kikuu cha Pennsylvania wamegundua kwamba ubongo hufanya kazi nyingi sana mtu anaposema uwongo kuliko anaposema kweli. Dakt. Daniel Langleben amechunguza jambo hilo akitumia mashine inayopima utendaji wa ubongo ili kutambua sehemu za ubongo zinazofanya kazi wakati mtu anaposema uwongo. Mtu anapoulizwa swali, ubongo hulichanganua swali hilo kwanza. Halafu, “kwa kawaida, mwongo hufikiria jibu la kweli kabla ya kubuni au kusema jibu la uwongo,” laripoti gazeti The News la Mexico City. “Ubongo hauwezi kutoa jibu lolote bila kufikiri kwanza,” Langleben anasema. “Kusema uwongo huhusisha mambo mengi kuliko kusema kweli, hivyo kuna utendaji mwingi zaidi wa ubongo.” Utendaji huo ulioongezeka hutambuliwa na mashine hiyo. “Hata kwa mtu mwenye ufasaha zaidi, kusema uwongo ni kazi ngumu kwa ubongo,” lasema gazeti hilo.

Rundo la Silaha Duniani Lazidi Kuongezeka

Inakadiriwa kwamba katika mwaka wa 2001, polisi, jeshi, wanamgambo, na watu binafsi ulimwenguni pote walikuwa na jumla ya silaha ndogo milioni 639, chasema kichapo Small Arms Survey 2002, kinachoripoti uchunguzi uliodhaminiwa na Umoja wa Mataifa. “Idadi hiyo ilipita idadi iliyokadiriwa kwa asilimia 16,” yasema ripoti hiyo. Isitoshe, kwa sababu ya utengenezaji wa silaha mpya, silaha ndogo zinaongezeka kwa asilimia 1 hivi kila mwaka. Kwa sasa, bastola, bunduki, na bunduki za kurusha makombora hutengenezwa na angalau makampuni 1,000 katika zaidi ya nchi 98 ulimwenguni. Kulingana na ripoti hiyo, “mnamo mwaka wa 2000 thamani ya silaha ndogo [zote] ulimwenguni, kutia ndani risasi, . . . ilikadiriwa kuwa angalau dola bilioni 7 za Marekani.” Asilimia 80 hadi 90 ya biashara ya silaha ndogo ni halali, na idadi kubwa ya silaha hizo (asilimia 59) inamilikiwa na raia.

Moshi Unaoua

“Asilimia 20 ya watu wote wanaokufa kutokana na kansa ya mapafu katika majiji huuawa na vipande vidogo sana vilivyo katika hewa iliyochafuliwa hasa na moshi wa magari,” laripoti gazeti New Scientist. Watafiti huko Marekani na Kanada walichunguza maisha ya Wamarekani nusu milioni kwa miaka 16, wakizingatia mambo ambayo huongeza uwezekano wa kuugua ugonjwa huo, kama umri, jinsia, rangi, uvutaji wa sigara, ulaji, unywaji wa kileo, na kufanya kazi katika mazingira yenye vichafuzi. “Utafiti huo ulichunguza vipande vyenye vipenyo vinavyopungua maikrometa 2.5,” lasema gazeti New Scientist, kwa sababu “inadhaniwa kwamba vipande hivyo vidogo huua vinapoingia katika sehemu za ndani sana za mapafu.” Utafiti huo ulionyesha kwamba hatari ya kuvuta moshi huo katika majiji fulani inaweza “kulinganishwa na hatari ya kuvuta moshi unaotolewa na watu wanaovuta sigara kwa muda mrefu,” lasema gazeti hilo.

Watoto Ambao Hawaandikishwi Wanapozaliwa

“Kila mwaka zaidi ya watoto milioni 50 hukosa kuandikishwa wanapozaliwa, na hiyo ni zaidi ya asilimia 40 ya watoto wanaozaliwa ulimwenguni pote,” laripoti Shirika la Umoja wa Mataifa la Hazina ya Watoto (UNICEF). Shirika hilo laongeza kusema: “Katika nchi 39, angalau asilimia 30 ya watoto wote hawakuandikishwa walipozaliwa na katika nchi 19 asilimia 60 hawakuandikishwa.” Tokeo ni nini? Hawatambuliwi kisheria na hilo linaweza kuwanyima huduma za msingi. “Kuandikishwa baada ya kuzaliwa ni mojawapo ya haki za msingi za binadamu, nayo humwezesha mtu kupata haki nyingine kama elimu, matibabu, . . . na kumlinda asibaguliwe, asitendewe vibaya na kutumiwa vibaya,” lasema shirika hilo. Na matatizo yanayotokana na kutoandikishwa huendelea hata anapokuwa mtu mzima. “Baadaye, huenda asiweze . . . kuandikisha ndoa yake kisheria,” yasema ripoti hiyo.

Dunia “Itafilisika Kimazingira”

Wanasayansi wanasema kwamba iwapo mali ya asili itaendelea kutumiwa kama inavyotumiwa sasa, “dunia itafilisika kimazingira,” laripoti gazeti la Kanada Globe and Mail. Kulingana na uchunguzi uliochapishwa kwanza katika gazeti Proceedings of the National Academy of Sciences, imekadiriwa kwamba mnamo mwaka wa 1961, “wanadamu walitumia asilimia 70 ya mali ya asili. Mnamo mwaka wa 1999, wanadamu walitumia asilimia 120 ya mali hiyo, na leo wanatumia asilimia 125.” Hiyo inamaanisha kwamba inachukua miezi 15 ili dunia iweze “kufanyiza tena mali ya asili ambayo wanadamu wametumia” kwa mwaka mmoja, katika shughuli za uvuvi, kilimo, uchimbaji wa madini, na vilevile matumizi ya mafuta na makaa ya mawe. “Jambo moja linalofanya tatizo hilo lizidi kuwa baya haraka ni kwamba uwezo wa dunia wa uzalishaji umepungua kwa sababu maeneo fulani yameharibika hivi kwamba hayawezi kuzalisha mimea. Isitoshe, gazeti hilo linasema kwamba ni lazima dunia iongeze mazao kadiri idadi ya watu inavyozidi kuongezeka.”

Kugeuza Makanisa

“Wakati Mark Twain alipotembelea Montreal katika mwaka wa 1881, alisema kwamba ‘haingewezekana kutupa tofali bila kuvunja kioo cha dirisha la kanisa fulani.’ Leo, huenda ukavunja vioo vya madirisha ya nyumba za watu wanaoishi katika makanisa ya zamani,” lasema gazeti The Gazette la Montreal. Ingawa bado kuna majengo 600 hivi ya kuabudia, gazeti hilo linasema kwamba majengo 100 hivi kati ya hayo, mengi yakiwa ya Kanisa Katoliki, huenda yakauzwa katika miaka kumi ijayo. “Kulingana na Dayosisi Kuu ya Montreal, parokia 25 za Kanisa Katoliki zimefungwa tangu mwaka wa 1960.” Ingawa idadi ya Wakatoliki nchini Kanada iliongezeka kutoka milioni moja na nusu hivi katika mwaka wa 1871 hadi karibu milioni 10 katika mwaka wa 1971; “wahudhuriaji wa kanisa walipungua sana, hasa katika wilaya ya Quebec,” lasema gazeti The Gazette. Bernard Fortin, anayeshughulikia mambo ya ibada katika Dayosisi Kuu ya Montreal, alimwambia mwandishi wa gazeti hilo kuwa hudhurio la makanisa ya eneo hilo limepungua kutoka asilimia 75 katika mwaka wa 1970 hadi asilimia 8 leo.

Kutazama Televisheni Husababisha Matatizo ya Kula

Kulingana na ripoti katika gazeti The Independent la London, “wasichana wadogo wanaotazama televisheni hupata matatizo ya kula.” Dakt. Anne Becker wa Chuo cha Tiba cha Harvard, nchini Marekani, aliwahoji wasichana wanaobalehe nchini Fiji muda mfupi baada ya televisheni kuanza kutumiwa huko katika mwaka wa 1995. Aligundua kwamba televisheni “inafanya watu wasipendezwe na maumbile yao ya mwili na kunasababisha matatizo ya kula.” Vipi? Utamaduni wa Wafiji huwatia moyo watu wale chakula kingi na wawe wanene. Lakini baada ya kutazama watu wembamba katika televisheni, wasichana wengi wa shule walitaka kuwaiga. Kwa mfano, kabla ya televisheni kuingia nchini Fiji, hakuna msichana aliyekuwa amewahi kujitapisha ili apunguze uzito. Hata hivyo, miaka mitatu baadaye, asilimia 11.3 ya wasichana waliohojiwa walisema kwamba walikuwa wamejitapisha ili wapunguze uzito. Watafiti waligundua pia kwamba asilimia 69 ya wasichana wa shule walijinyima chakula ili wapunguze uzito, na karibu asilimia 75 walisema kwamba walijiona wakiwa na “miili mikubwa sana au wanene.”