Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Msiba Mkubwa Sana

Msiba Mkubwa Sana

Msiba Mkubwa Sana

Erik * ana umri wa miezi sita. Lakini uzito na kimo chake ni kama cha mtoto mwenye umri wa mwezi mmoja au miwili. Amekonda sana lakini miguu, tumbo na uso wake umevimba. Ngozi yake imekuwa nyeusi, nywele zake zimechakaa na zinakatika kwa urahisi, na ana vidonda mwilini. Anaonekana mwenye kukasirika haraka. Ni lazima daktari awe mwangalifu anapoyachunguza macho ya Erik kwa sababu ngozi ya macho inaweza kubambuka kwa urahisi sana. Inaelekea ukuzi wake wa kiakili umeathiriwa. Inahuzunisha kwamba watoto wengi wanaugua ugonjwa huo.

“ZAIDI ya nusu ya watoto wanaokufa ulimwenguni pote hufa kutokana na ugonjwa huo. Tangu ile tauni kubwa iliyotukia katika karne ya 14, hakuna ugonjwa mwingine wa kuambukiza ambao umewaangamiza watu wengi kama ugonjwa huu. Lakini ugonjwa huu hauwezi kuambukizwa. Unawalemaza mamilioni ya watu na kudhoofisha mfumo wao wa kinga na uwezo wao wa kiakili. Unahatarisha uhai wa wanawake, familia, na jamii nzima.”—The State of the World’s Children, Shirika la Hazina ya Watoto la Umoja wa Mataifa.

Ni ugonjwa gani huo? Ni utapiamlo—ukosefu wa chakula bora hasa chakula kinachojenga mwili. Ugonjwa huo umetajwa na Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) kuwa hatari iliyofichika. Ugonjwa huo umeenea kadiri gani? Shirika la WHO linasema kwamba “unaua angalau nusu ya watoto milioni 10.4 wanaokufa kila mwaka.”

Utapiamlo unahusisha magonjwa mengine mengi, kutia ndani magonjwa ya kukosa kirutubisho kimoja au kadhaa mwilini—kama vile vitamini au madini—na kunenepa kupita kiasi na magonjwa mengine sugu yanayohusiana na vyakula. Hata hivyo, shirika la WHO linasema kwamba “ukosefu wa protini mwilini ndio ugonjwa hatari zaidi kati ya aina zote za utapiamlo.” Ugonjwa huo huwapata hasa watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano.

Hebu tua kidogo na umfikirie Erik, aliyetajwa mwanzoni, na mamilioni ya watoto walio na ugonjwa huo. Hawakujiletea ugonjwa huo, wala hawawezi kujinasua. Mtaalamu wa magonjwa ya watoto yanayosababishwa na ukosefu wa lishe Georgina Toussaint alimwambia hivi mwandishi wa Amkeni!: “Wale wanaoteseka na kuumia hawana hatia wala uwezo wa kujikinga.”

Huenda wengine wakadhani kwamba tatizo hilo haliwezi kuepukwa—eti hakuna chakula cha kuwatosha watu wote. Jambo hilo linashangaza kwa sababu kulingana na shirika la WHO “kuna chakula tele ulimwenguni leo.” Kuna chakula cha kuwatosha wanadamu wote duniani—na cha ziada. Isitoshe, hakuna ugonjwa unaoweza kuzuiwa kwa urahisi na kutibiwa kwa gharama ndogo kama utapiamlo. Je, husumbuliwi na habari hizo?

Ni Nani Wanaopatwa na Ugonjwa Huo?

Utapiamlo hauwapati watoto peke yao. Ripoti ya shirika la WHO ya mwezi wa Julai 2001 inasema kwamba “utapiamlo unasambaa sana, unawaathiri watu wapatao milioni 800—asilimia 20 ya watu wanaoishi katika nchi zinazoendelea.” Hiyo yamaanisha kwamba mtu 1 kati ya kila watu 8 ulimwenguni ana utapiamlo.

Ingawa idadi kubwa ya watu wasiopata chakula cha kutosha wako Asia—hasa kwenye maeneo ya kusini na ya kati—bara la Afrika lina idadi kubwa zaidi ya watu wasiopata chakula cha kutosha ukilinganisha na idadi ya watu wanaoishi humo. Kisha inafuatwa na nchi kadhaa zinazoendelea za Amerika ya Latini na Karibea.

Je, nchi zilizoendelea zinakumbwa na ugonjwa huo? Ndiyo. Kichapo The State of Food Insecurity in the World 2001 kinasema kwamba watu milioni 11 wanaoishi katika nchi zilizoendelea wana utapiamlo. Na watu wengine milioni 27 walio na utapiamlo wanaishi katika nchi zinazoendelea kusitawi kiviwanda, hasa nchi zilizo Mashariki mwa Ulaya na jamhuri za ule uliokuwa Muungano wa Sovieti.

Kwa nini utapiamlo umekuwa tatizo kubwa sana? Je, kuna jambo lolote linaloweza kuboresha hali ya watu wasiopata chakula cha kutosha hivi sasa? Je, tatizo hilo litawahi kutoweka duniani? Makala zifuatazo zitajibu maswali hayo.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 2 Si jina lake halisi.

[Chati/Ramani katika ukurasa wa 4]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

NCHI ZINAZOKABILI UHABA WA CHAKULA BORA

UHABA MKUBWA

UHABA WA WASTANI

UHABA MDOGO

HAKUNA UHABA AU TAKWIMU KAMILI HAZIPATIKANI

[Picha katika ukurasa wa 3]

Wasubiri misaada ya chakula nchini Sudan

[Hisani]

UN/DPI Photo by Eskinder Debebe