Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Tunda la Manjano Lenye Historia ya Kupendeza

Tunda la Manjano Lenye Historia ya Kupendeza

Tunda la Manjano Lenye Historia ya Kupendeza

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI FIJI

NI MWAKA wa 1789. Mashua isiyo na tanga yenye urefu wa meta saba iliyojaa wanaume, inaonekana ikiwa ndogo sana inapokuwa katika bahari kubwa. Wanaume hao ni dhaifu sana kwa sababu ya kukosa chakula na uchovu wa safari ambayo imechukua siku nyingi. Pia wamekabili mawimbi yenye nguvu na upepo mkali. Bado wanahitaji kusafiri kilometa 5,000 katika bahari wasiyoifahamu, na kuna hatari ya miamba ya tumbawe. Chakula ni haba na kila mwanamume anaruhusiwa kula gramu 30 za mkate (biskuti ya melini) kwa siku na kunywa maji kidogo. Hakuna tumaini la kuokoka.

Juma moja hivi mapema, abiria wa meli hiyo walikuwa wameasi na kutoroka wakitumia mashua za kuokolea na mmoja wao aliuawa wakati wenyeji wa huko walipowavamia. Pia walikabili dhoruba kali ya radi na mvua na kuokoka shambulizi la wenyeji waliowafukuza kwa mashua karibu na visiwa vilivyoitwa Visiwa vya Cannibal.

Kwa nini watu hao walisafiri hadi eneo hatari la Pasifiki Kusini, mbali sana na Uingereza, nchi ya kwao yenye mashamba mazuri ya matunda na mabustani? Walikuwa wakitafuta miti maridadi ya mishelisheli. Hebu tuone jinsi miti hiyo yenye kuvutia na matunda yake yenye matumizi mengi ilivyokuwa muhimu katika hadithi hiyo na katika safari maarufu za kale zaidi za uvumbuzi.

Huenda umetambua kwamba wanaume waliotajwa awali walikuwa waokokaji wa uasi unaojulikana sana wa meli ya Bounty. Meli hiyo ya jeshi la wanamaji la Uingereza yenye uzito wa tani 215, iliyoongozwa na Nahodha William Bligh, ilikuwa ikisafiri kutoka Uingereza hadi Tahiti. Ilipowasili Tahiti, meli hiyo ilibeba “abiria” wasio wa kawaida—karibu miche 1,000 ya mshelisheli. Miche hiyo iliyokuwa imepandwa ingeweza kuleta faida baadaye kwa kuzaa matunda ya rangi ya manjano ilipopandwa shambani na kunawiri katika makoloni ya Uingereza huko Karibea.

Mradi huo ulitokana na ushauri aliotoa Bwana Joseph Banks kwa serikali ya Uingereza. Wakati huo, Uingereza ilikuwa ikitafuta njia nyingine ya kuandaa chakula kwa ajili ya watumwa wake waliofanya kazi katika mashamba ya miwa. Hapo awali Banks, ambaye wakati huo alikuwa mshauri wa Bustani ya Kew karibu na London, Uingereza, alikuwa amesafiri pamoja na Nahodha James Cook katika safari yake ya uvumbuzi huko Pasifiki. * Yeye na Cook walikuwa wametambua umuhimu wa mshelisheli.

Ingawa yeye mwenyewe hangeandamana na Bligh, Banks alipanga jinsi ambavyo miche hiyo ingetunzwa wakati wa safari hiyo ndefu, akifikiria hasa uhitaji wa kuitilia maji yasiyo na chumvi. Waandishi fulani wanaamini kwamba uangalifu mkubwa uliopewa miche hiyo na maji mengi ambayo yalimwagwa—huku mahitaji ya wasafiri yakipuuzwa—ndio uliowachochea wasafiri hao waliokuwa wanalalamika waasi. Mnamo Aprili 28, 1789, Bligh na wanaume 18 walilazimishwa kung’oa nanga asubuhi na mapema karibu na pwani ya Tonga walipotishwa kuuawa. Huenda miche ya mshelisheli ilitupwa baharini na waasi wenye furaha wakati wa uasi.

Hata hivyo, Bligh hakukata tamaa. Alifunga safari nyingine iliyotajwa kuwa “safari maarufu zaidi kati ya safari zote za baharini zilizofungwa kwa kutumia mashua isiyo na tanga.” Kwa majuma saba yenye matatizo mengi, aliendesha meli hiyo ndogo umbali wa zaidi ya kilometa 5,800 kaskazini-magharibi kupitia visiwa vya sasa vya Fiji, kuelekea pwani ya mashariki ya New Holland (Australia), hadi eneo salama katika kisiwa cha Timor.

Aliporudi Uingereza, Bligh alipewa meli mbili zaidi ili aende Tahiti kuchukua miche ya mshelisheli. Mnamo mwaka wa 1792, alisafirisha miche 700 hadi kisiwa cha St. Vincent na Jamaika huko West Indies. Mishelisheli inapatikana huko hata leo na inazaa matunda yenye manufaa nyingi katikati ya matawi yake mapana.

Ingawa safari ya Bligh ina visa vingi vya hatari na uvumbuzi, hiyo ni sehemu tu ya historia ndefu ya tunda la shelisheli. Iwapo mshelisheli ungeweza kujisemea, ungeeleza historia ndefu ya maelfu ya miaka wakati ulipoandamana na wasafiri wa zamani katika safari za uvumbuzi!

Historia ya Mapema ya Mshelisheli

Wataalamu ambao huchunguza vitu vya kale wanaamini kwamba safari nyingi zilifanywa huko Pasifiki magharibi, na safari za hivi karibuni zaidi zilianza katika mwaka wa 1500 K.W.K. * Watu wa kabila la Lapita walitumia mitumbwi mikubwa yenye viunzi viwili kusafiri kutoka Kusini-Mashariki mwa Asia hadi nchi ambazo leo zinaitwa Indonesia, New Guinea, New Caledonia, Vanuatu, na Fiji na kufika katikati ya Pasifiki. Hayo yalikuwa mafanikio makubwa, kwa sababu safari nyingine zilihusisha kuvuka mamia ya kilometa kupitia bahari kuu.

Mitumbwi ya watu wa kabila la Lapita yenye viunzi viwili ilikuwa na uwezo wa kubeba watu wengi na mifugo, chakula, na mbegu aina mbalimbali, vipandikizi, na miche iliyopandwa. Watu wa kabila la Lapita walipoenea katika eneo lote la Pasifiki, walihamia katika visiwa ambavyo waligundua vya Melanesia, Polynesia, na Micronesia upande wa kaskazini, na New Zealand upande wa kusini. Walienea sana hata hatimaye wakafika mbali sana katika Kisiwa cha Easter na Hawaii. * Mahali popote walipoenda, walikuwa na miche sugu ya mshelisheli.

Tunda Bora Lenye Matumizi Mengi

Leo nchini Fiji, na katika sehemu nyingine za ulimwengu, tunda la shelisheli huonwa kuwa chakula bora na cha bei nafuu. Mishelisheli fulani huhimili hali ngumu na kunawiri vizuri, nayo huzaa matunda mara tatu kwa mwaka kwa miaka 50 hata wakati hali ya hewa ni mbaya. Tunda la shelisheli linafanana na mkate na kila aina ya shelisheli ina ladha tofauti ambayo inakaribia ladha ya mkate au viazi. Tunda hilo linaweza kuchemshwa, kuokwa, au kukaangwa, na kuliwa baada ya mlo. Linaweza kukaushwa na kutwangwa liwe unga, na sehemu yake ya ndani inaweza kuhifadhiwa na kutumiwa kwa miaka mingi.

Majani yake yanaweza kutumiwa kufunika vyakula kama samaki au nyama ya kuku, ili kuhifadhi umajimaji na kuongeza ladha ya vyakula hivyo vinapopikwa. Mbegu ya shelisheli yenye ladha ya njugu hutolewa maganda na kuliwa pia. Wakati mwingine watoto hupenda kukusanya utomvu wake na kuutafuna kama chingamu. Tunda hilo lina matumizi mengi kama nini! Sasa unaweza kuelewa kwa nini wakazi wengine wa visiwa vya Pasifiki wanapenda mshelisheli sana.

Ledua, anayeishi nchini Fiji, anatueleza kwamba tunda la shelisheli humfanya akumbuke siku za utotoni. Kulikuwa na mishelisheli mitano nyumbani kwao. Kazi ya Ledua ilikuwa kufagia majani ya mishelisheli yaliyoanguka uani, na alichukia kazi hiyo sana. Kwa upande mwingine, mara nyingi baada ya shule, yeye pamoja na ndugu na dada zake walichuma shelisheli na kuziuza nyumba kwa nyumba. Kisha wazazi wao walitumia pesa walizopata kufanya matayarisho kwa ajili ya makusanyiko ya Kikristo, kama vile kununua chakula, kulipia nauli, au kununua viatu.

Huenda unaishi katika eneo lenye mti huo wenye historia ndefu, ambao una jina la kifahari Artocarpus altilis. Labda hujawahi kufikiria uumbaji huo wa ajabu kuwa wenye thamani au kuwa kitu muhimu au maridadi. Hata hivyo, tunda la shelisheli huwakumbusha wengi wanaoishi katika eneo la Pasifiki mafanikio mengi ya baharini, safari za uvumbuzi, watu wa Lapita, na Nahodha Bligh.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 7 Ona makala yenye kichwa “Kuhifadhi Mbegu Haraka,” katika gazeti la Amkeni! la Aprili 8, 2002.

^ fu. 13 Tarehe hii inategemea rekodi za wataalamu wa kuchimbua vitu vya kale pekee na haizingatii nyakati za Biblia.

^ fu. 14 Wanahistoria fulani wanaamini kwamba baadhi ya wasafiri hao wa kale wa Pasifiki walisafiri hadi pwani ya Peru huko Amerika Kusini na kwamba walirudi na viazi vitamu. Ikiwa ni hivyo, inamaanisha kwamba viazi vitamu vilielekea upande tofauti na tunda la shelisheli, kwani hatimaye vilifika Kusini-Mashariki mwa Asia, ambapo miche ya mshelisheli ilitoka.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 25]

Mti Unaotoa Zawadi Nyingi

Mshelisheli uliokomaa huvutia sana kwani una rangi ya kijani wakati wote wa mwaka. Mti huo ulitolewa katika misitu ya Malaysia. Huo ni sehemu ya jamii ya miti ya Moraceae, inayotia ndani mtini, mforosadi, na mfenesi. Mshelisheli uliokomaa unaweza kufikia urefu wa meta 12, na hutoa machipukizi ambayo yanaweza kukatwa na kupandwa. Mshelisheli huchanua maua ya kike na ya kiume katika vichala tofauti. Maua hayo huchavuliwa na kutawanywa na popo wadogo walao matunda yanapokuwa msituni. Mti huo huzaa matunda makubwa ya mviringo au yenye umbo la yai. Matunda hayo huwa na ukubwa wa tikiti-maji dogo na ganda lake huwa na rangi ya kijani, lakini ndani huwa na rangi ya malai au ya manjano.

Mshelisheli pia hutoa majani makubwa maangavu yenye rangi nzito ya kijani, ambayo hutokeza kivuli kizuri cha kujikinga kutokana na jua kali. Mbao zake nyepesi hutumiwa kutengenezea fanicha na mitumbwi, na nyakati nyingine sehemu ya ndani ya ganda lake hutumiwa kutengeneza vazi linaloitwa tapa huko Pasifiki. Utomvu wake ulio kama maziwa hutumiwa kuziba nyufa, na katika maeneo mengine umetumiwa kuweka plasta kwenye mifupa iliyovunjika na kama gundi ya kunasa ndege.

[Picha katika ukurasa wa 24]

Mchoro wa Robert Dodd unaoonyesha uasi uliotokea katika meli ya “Bounty”

[Hisani]

National Library of Australia, Canberra, Australia/Bridgeman Art Library

[Picha katika ukurasa wa 26]

Tunda la shelisheli linaweza kupikwa kwa njia mbalimbali