Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Utapiamlo Utakoma Karibuni!

Utapiamlo Utakoma Karibuni!

Utapiamlo Utakoma Karibuni!

‘LEO kuna chakula tele ulimwenguni kuliko miaka michache iliyopita. . . . Kuna chakula kinachoweza kuwatosha watu wote na cha ziada.’ Ndivyo unavyosema uchunguzi mmoja wa Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO). Kama kuna chakula tele, mbona kuna utapiamlo?

Shirika la WHO linasema “tatizo ni kwamba chakula hakizalishwi wala kugawanywa kwa usawa. Mara nyingi wakazi maskini, wenye njaa wanaoishi katika maeneo yenye rutuba katika nchi zinazoendelea hujionea mazao mengi mno yakiuzwa nchi za nje ili kuleta pesa. Watu wachache hupata faida kubwa ya kifedha kwa muda mfupi huku wengi wakiumia kwa muda mrefu.” Uchunguzi uliofanywa hivi majuzi na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) unaonyesha kwamba ‘asilimia 20 ya watu matajiri ulimwenguni hula asilimia 45 ya nyama na samaki huku asilimia 20 ya watu maskini wakila asilimia 5 tu.’

Kwa upande mwingine, “utapiamlo husababishwa pia na kutokuwa na elimu nzuri na habari sahihi,” lasema Shirika la Hazina ya Watoto ya Umoja wa Mataifa, kisha laongezea hivi: “Bila mipango thabiti ya kuwafundisha na kuwaelimisha watu wote, hawatakuwa na ujuzi, ustadi na mazoea yanayohitajiwa ili kukabiliana na utapiamlo.” Utapiamlo hudhoofisha afya ya mtu na uwezo wake wa kupata elimu bora zaidi—na hilo huendeleza ugonjwa huo.

Haki na Kuwapenda Wengine Bila Ubinafsi

Licha ya vizuizi hivyo vyenye kuvunja moyo, baadhi ya wataalamu wanaoshughulikia tatizo hilo bado wana matumaini. Kwa mfano, mkurugenzi mkuu wa shirika la FAO, Jacques Diouf, alieleza mambo anayotumaini kuona: “Ninatumaini kuona ulimwengu ambamo kila mwanamume, mwanamke na mtoto atakuwa na chakula salama cha kutosha kila siku. Ninatumaini kwamba pengo lenye kushtua kati ya matajiri na maskini litapungua. Ninatarajia wakati ambapo watu watavumiliana badala ya kubaguana; kutakuwa na amani badala ya vita; rasilimali zitatumiwa bila mazingira kuharibiwa; watu wote watakuwa na ufanisi wala hawatavunjika moyo.”

Hata hivyo, kama tulivyoona matumaini hayo hayategemei kuwa tu na chakula cha kutosha na kukigawanya vizuri. Ni lazima tuwatendee wote kwa haki na kuwapenda bila ubinafsi. Lakini sifa hizo bora sana hazipatikani katika ulimwengu wa kisasa wa kibiashara.

Je, vizuizi vikubwa sana kama pupa, umaskini, vita, na ubinafsi vinaweza kukomeshwa ili kusiwe na utapiamlo ulimwenguni? Au hiyo ni ndoto tu?

Suluhisho Pekee la Kweli

Biblia yaonyesha kwamba hatupaswi kushangazwa na mambo yanayosababisha utapiamlo. Neno la Mungu linasema: “Katika siku za mwisho nyakati za hatari zilizo ngumu kushughulika nazo zitakuwa hapa. Kwa maana watu watakuwa wenye kujipenda wenyewe, wapenda-fedha, . . . wasio na shauku ya kiasili, wasiotaka upatano wowote, . . . wasio na upendo wa wema, . . . wakiwa na namna ya ujitoaji-kimungu lakini wakithibitika kuwa si kweli kwa nguvu ya hiyo.”—2 Timotheo 3:1-5.

Je, wanadamu wanaweza kukomesha tabia hizo zilizokita mizizi bila msaada wa Mungu? Yaonekana hawawezi, sivyo? Labda umegundua kwamba watu fulani wenye mamlaka huwa na nia nzuri ya kukomesha matatizo ya kijamii yanayokumba wanadamu, lakini ubinafsi, kupenda pesa, na kutokamilika kwa wengine huvuruga na hata kuharibu jitihada hizo nzuri.—Yeremia 10:23.

Hata hivyo, tatizo hilo litasuluhishwa kikweli. Biblia inaahidi kwamba Ufalme wa Mungu utakomesha tatizo la ukosefu wa haki na matatizo mengine yanayowakumba wanadamu leo.

Andiko la Isaya 9:6-7 hutupatia tumaini hili zuri ajabu: “Maana kwa ajili yetu mtoto amezaliwa, tumepewa mtoto mwanamume; na uweza wa kifalme utakuwa begani mwake; naye ataitwa jina lake, Mshauri wa ajabu, Mungu mwenye nguvu, Baba wa milele, Mfalme wa amani. Maongeo ya enzi yake na amani hayatakuwa na mwisho kamwe, katika kiti cha enzi cha Daudi na ufalme wake; kuuthibitisha na kuutegemeza kwa hukumu na kwa haki, tangu sasa na hata milele. Wivu wa BWANA wa majeshi ndio utakaotenda hayo.”

Ni Ufalme huohuo ambao watu husali juu yake wanapokariri ile Sala ya Bwana na kumwambia Mungu hivi: “Acha ufalme wako uje.” (Mathayo 6:9, 10) Ona kwamba Isaya anasema kwamba “wivu wa BWANA wa majeshi ndio utakaotenda hayo.” Naam, Yehova Mungu hutaka daima kutimiza mahitaji ya wanadamu. Ameiumba dunia hii ili izae chakula cha kuwatosha watu wote.

Zaburi 65:9-13 yasema hivi kumhusu: “Umeijilia nchi na kuisitawisha, umeitajirisha sana. Mto wa Mungu umejaa maji; wawaruzuku watu nafaka maana ndiwe uitengenezaye ardhi. Matuta yake wayajaza maji; wapasawazisha palipoinuka, wailainisha nchi kwa manyunyu; waibariki mimea yake. . . . Na malisho yamevikwa kondoo, na mabonde yamepambwa nafaka.”

Naam, Yehova Muumba, ndiye mtimizaji bora wa mahitaji ya wanadamu. Ndiye ‘anayekipa kila chenye mwili chakula chake; kwa maana fadhili zake ni za milele.’—Zaburi 136:25.

Tunaweza kuwa na hakika kwamba Ufalme wa Mungu chini ya Kristo utawatunza watu wote. Biblia yasema kwamba ‘kutakuwepo wingi wa nafaka katika ardhi juu ya milima.’ Pia watu wote watapata chakula cha kutosha, kwa kuwa “[Yesu Kristo] atamkomboa mhitaji aliapo, na mtu aliyeonewa iwapo hana msaidizi. . . . Nafsi za wahitaji ataziokoa.” (Zaburi 72:12, 13, 16) Kwa hiyo jipe moyo! Hatari hiyo iliyofichika itakomeshwa kabisa hivi karibuni.

[Blabu katika ukurasa wa 11]

“Kukomesha njaa na utapiamlo ni jambo linalowezekana. Njia zipo. Tatizo ni . . . kuchukua hatua madhubuti kitaifa na kimataifa.”—Shirika la Afya Ulimwenguni

[Picha ya ukurasa mzima katika ukurasa wa 10]