Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Visababishi Vilivyotia Mizizi, Athari Mbaya za Utapiamlo

Visababishi Vilivyotia Mizizi, Athari Mbaya za Utapiamlo

Visababishi Vilivyotia Mizizi, Athari Mbaya za Utapiamlo

“Nilipohisi njaa, mlianzisha tume ya kuchunguza chanzo cha tatizo langu. Nilipokosa makao, mlitangaza magazetini. Nilipokuwa mgonjwa, mlifanya mkutano wa kujadili watu wa hali ya chini katika jamii. Mlichunguza matatizo yangu yote kinaganaga lakini ningali mgonjwa, nina njaa na sina makao.”—Mwandishi hajulikani.

MASHIRIKA ya ulimwengu yameshindwa kabisa kukomesha utapiamlo licha ya jitihada nyingi ambazo zimefanywa. Kwa mfano, mnamo mwaka wa 1996, Mkutano wa Chakula Ulimwenguni uliopangwa na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) uliazimia kupunguza idadi ya watu wenye utapiamlo kwa asilimia 50—karibu watu milioni 400—kufikia mwaka wa 2015. *

Maendeleo fulani yamefanywa. Lakini kwa kusikitisha, ripoti ya hivi karibuni ya shirika la FAO, The State of Food Insecurity in the World 2001, inakiri hivi: “Ni wazi kwamba jitihada ya kupunguza idadi ya watu wasiopata chakula cha kutosha ulimwenguni imepungua.” Kwa hiyo inaonekana kwamba azimio la mkutano huo bado haliwezi kutimizwa. Zaidi ya hayo, ripoti hiyo inakiri kwamba “idadi ya watu wasio na chakula cha kutosha imeongezeka sana katika nchi nyingi zinazoendelea.”

Kwa nini ni vigumu sana kushinda tatizo hilo? Ili kupata jibu, ni vyema kuujua kwanza ugonjwa wa utapiamlo, na kuchunguza athari na visababishi vilivyotia mizizi vya ugonjwa huo.

Utapiamlo Husababishwa na Nini?

Utapiamlo husababishwa na ukosefu wa vitamini na madini ya kutosha katika chembe za mwili, na kwa kawaida husababishwa na mambo mawili: (1) ukosefu wa protini, nishati, vitamini, na madini na (2) maambukizo ya mara kwa mara.

Magonjwa kama vile kuharisha, surua, malaria, na magonjwa ya kupumua hudhoofisha mwili sana na kupunguza vitamini na madini. Magonjwa hayo humfanya mgonjwa apoteze hamu ya kula naye hula chakula kidogo sana, na hivyo anapata utapiamlo. Kwa upande mwingine, mtoto asiyepata chakula cha kutosha anaweza kuambukizwa magonjwa kwa urahisi. Jambo hilo huongeza idadi ya watoto wanaokufa kwa sababu ya kukosa vyakula vinavyojenga mwili.

Kwa nini utapiamlo unawashambulia hasa watoto? Watoto wanakua haraka na hivyo wanahitaji nishati na protini nyingi zaidi. Vivyo hivyo, akina mama wajawazito na wanaonyonyesha wanaweza kupata utapiamlo.

Mara nyingi, mtoto mchanga huanza kuathiriwa akiwa tumboni. Ikiwa mama hapati chakula cha kutosha au hali chakula bora kabla na wakati wa mimba, basi atajifungua mtoto mwenye uzito kidogo. Mtoto huyo akiachishwa kunyonya mapema, asipolishwa vizuri, au usafi usipozingatiwa, anaweza kuugua utapiamlo.

Mtoto hawezi kukua au kusitawi vizuri asipopata vitamini na madini muhimu. Yeye hulia bila sababu yoyote na kuwa mgonjwa-mgonjwa. Kadiri hali yake inavyozorota ndivyo anavyozidi kukonda, macho na utosi wa kichwa hubonyea, ngozi na tishu za mwili hukauka, na uwezo wa kudhibiti joto la mwili hupungua.

Utapiamlo humwathiri mtoto kwa njia nyingine ambazo pia zinaweza kuathiri ukuzi wake. Kwa mfano, kutopata madini ya kutosha—hasa chuma, iodini, na zinki—na vitamini—hasa vitamini A—kunaweza kusababisha madhara hayo. Shirika la Hazina ya Watoto ya Umoja wa Mataifa (UNICEF) linasema kwamba ukosefu wa vitamini A huathiri watoto wachanga milioni 100 hivi ulimwenguni na husababisha upofu. Vilevile unadhoofisha mfumo wa kinga, na hivyo kupunguza uwezo wa mtoto wa kukinza maambukizo.

Madhara Mabaya Zaidi

Utapiamlo hudhuru kabisa mwili, hasa mwili wa mtoto. Unaweza kudhuru viungo na mifumo yote mwilini kutia ndani moyo, mafigo, tumbo, matumbo, mapafu, na ubongo.

Uchunguzi mbalimbali umeonyesha kwamba ukuzi wa polepole wa mtoto hudhoofisha maendeleo yake ya kiakili na uwezo wa kufikiri na kufanya vyema shuleni. Ripoti moja ya Umoja wa Mataifa inasema hizo ndizo athari mbaya zaidi na za kudumu za utapiamlo.

Mtoto anaweza kuendelea kuathiriwa na matokeo ya utapiamlo hata anapokuwa mtu mzima. Ndiyo sababu shirika la UNICEF lililalamika hivi: “Kudhoofisha uwezo wa akili wa binadamu kwa kadiri kubwa hivyo—kwa sababu ambazo zinaweza kuzuiwa—ni kosa kubwa sana la kimaadili na hasara kubwa.” Kwa hiyo matokeo ya kudumu ya utapiamlo ni mabaya sana. Uchunguzi wa hivi majuzi unaonyesha kwamba kutokula chakula cha kutosha wakati wa utotoni kunaweza kusababisha magonjwa hatari kama vile ugonjwa wa moyo, kisukari, na shinikizo la juu la damu mtu anapokuwa mtu mzima.

Hata hivyo, watu wengi hawaugui utapiamlo hatari, kama shirika la UNICEF linavyokiri: “Zaidi ya robo tatu ya watu wanaokufa kutokana na magonjwa yanayohusiana na ukosefu wa chakula, hufa kwa sababu ya utapiamlo mdogo au wa wastani.” (Italiki ni zetu.) Watoto wanaopatwa na utapiamlo mdogo au wa wastani wanaweza kupata matatizo ya kudumu ya afya. Kwa hiyo ni muhimu kugundua watoto wenye dalili za utapiamlo ili waweze kupata matibabu yanayofaa.—Ona sanduku kwenye ukurasa wa 7.

Visababishi Vilivyotia Mizizi

Kama ilivyotajwa awali, utapiamlo husababishwa na ukosefu wa chakula. Lakini, unasababishwa pia na mambo mengine mazito zaidi ya kijamii, kiuchumi, kitamaduni, na ya kimazingira. Kisababishi kikuu ni umaskini, ambao huathiri mamilioni ya watu, hasa katika nchi zinazoendelea. Hata hivyo, mbali na kuwa kisababishi, umaskini pia husababishwa na utapiamlo. Ukosefu wa chakula cha kutosha hupunguza uwezo wa kufanya kazi, na hilo huzidisha umaskini.

Kuna mambo mengine yanayochangia utapiamlo. Watu huwa na mazoea mabaya ya kula kwa sababu ya kukosa elimu. Kama tulivyoona, maambukizo huchangia pia. Vilevile kuna sababu za kijamii na za kitamaduni, kama vile ugawaji usiofaa wa chakula na kuwabagua wanawake. Mara nyingi wanawake hula chakula kichache kilichosalia baada ya wanaume kula. Wanawake hunyimwa pia fursa za kupata elimu ambayo ingewasaidia kuwatunza watoto wao vyema.

Zaidi ya hayo, hali za kimazingira kama vile misiba ya kiasili na vita hupunguza uzalishaji wa chakula. Ripoti ya The State of Food Insecurity in the World 2001, ilisema kwamba kati ya Oktoba 1999 na Juni 2001, nchi 22 ziliathiriwa na ukame, nchi 17 na vimbunga au mafuriko, nchi 14 na vita vya wenyewe kwa wenyewe au migogoro, nchi 3 na baridi kali kupita kiasi, na nchi 2 na matetemeko ya ardhi.

Kutibu na Kuzuia

Mtoto mwenye utapiamlo anaweza kutibiwaje? Ikiwa mtoto huyo amedhoofika kabisa huenda ikafaa alazwe hospitalini kwanza. Kichapo kimoja cha madaktari kilichochapishwa na Shirika la Afya Ulimwenguni kinasema kwamba madaktari wanapaswa kumchunguza mtoto huyo na kutibu maambukizo yoyote au upungufu wa maji mwilini. Anaweza kuanza kulishwa hatua kwa hatua, labda kupitia mrija kwa muda wa juma moja hivi.

Katika hatua ya pili, mtoto hunyonyeshwa na kusaidiwa ale chakula kingi iwezekanavyo. Ni muhimu kuboresha tena hali yake ya kihisia na ya kimwili wakati huo. Mtoto huyo anaweza kukua vyema akitunzwa kwa uangalifu na kuonyeshwa upendo. Wakati huo huenda ikafaa kumfundisha mama kumtunza mtoto wake kwa kumlisha chakula kinachofaa na kutunza afya yake ili asipate tena utapiamlo. Kisha mtoto hurudishwa nyumbani. Ni muhimu mtoto apelekwe hospitalini au kwenye kliniki ili maendeleo yake yachunguzwe.

Hata hivyo, kuuzuia utapiamlo ndilo jambo la maana zaidi. Ndiyo sababu serikali na mashirika yasiyo ya kiserikali katika nchi nyingi yameanzisha miradi ya kuboresha chakula kinacholiwa na umma. Jamii pia hujitahidi kuzuia utapiamlo kwa njia nyingi, kama vile kuanzisha mipango ya kuwaelimisha watu kuhusu chakula, kuwa na maji safi ya kunywa, kujenga vyoo, kudumisha usafi wa mazingira, kutoa michango kwa ajili ya kampeni za chanjo, na kusimamia ukuzi na maendeleo ya watoto.

Lakini mtu mmoja-mmoja anaweza kufanya nini ili kuzuia utapiamlo? Sanduku lililo kwenye ukurasa wa 8 lina madokezo kadhaa yenye faida. Pamoja na hayo, mtaalamu wa magonjwa ya watoto yanayosababishwa na lishe, Georgina Toussaint anapendekeza kwamba, mama anapaswa kumwona tena daktari wa watoto au kurudi hospitalini siku saba baada ya kujifungua, mtoto anapokuwa na umri wa mwezi mmoja, na kila mwezi baada ya hapo. Mama anapaswa pia kumwona daktari mtoto anapokuwa na dalili za kupungukiwa na maji mwilini, anaharisha sana, au akiwa na dalili za homa.

Ijapokuwa mapendekezo hayo yanasaidia kuboresha chakula cha watoto, hatuna budi kukubali kwamba utapiamlo ni tatizo kubwa sana lisiloweza kutatuliwa na wanadamu. Kitabu Encyclopædia Britannica kinakiri: “Kuwapa watu wote chakula cha kutosha na kuwaelimisha kuhusu lishe bora bado ni tatizo kubwa sana.” Basi je, kuna tumaini kwamba hatari hiyo iliyofichika itakoma?

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 3 Kwa habari zaidi kuhusu Mkutano huo wa Chakula Ulimwenguni, soma gazeti la Amkeni! la Agosti 8, 1997, ukurasa wa 12-14.

[Sanduku katika ukurasa wa 7]

JE, MTOTO WAKO ANA UTAPIAMLO?

Wataalamu wa afya wanawezaje kujua kama mtoto ana utapiamlo? Huenda wakachunguza dalili fulani-fulani, wakauliza maswali kuhusu mazoea yake ya kula, na kuomba apimwe kwenye maabara. Hata hivyo, mara nyingi wao humpima mtoto moja kwa moja. Wao hupima mwili wa mtoto na kulinganisha vipimo hivyo na vipimo vya kawaida. Na hivyo wanajua mtoto anakosa chakula gani na athari za ugonjwa huo.

Vitu muhimu sana wanavyopima ni uzito, kimo, na unene wa mkono. Wanaweza kujua athari za utapiamlo kwa kulinganisha uzito wa mwili na umri wake; mtoto aliyeathiriwa sana huwa amedhoofika na kukonda. Mtoto huonwa kuwa ameathiriwa sana na utapiamlo iwapo uzito wake umepungua kwa asilimia 40, na ameathiriwa kwa kadiri ikiwa uzito wake umepungua kwa asilimia 25 hadi 40, na ameathiriwa kidogo iwapo uzito wake umepungua kwa asilimia 10 hadi 25. Ikiwa mtoto ana uzito mdogo sana na umri wake ni mkubwa, hiyo ni ishara ya kwamba ni mgonjwa sana—na hakui kamwe.

Ugonjwa wa marasmus, ugonjwa wa kwashiorkor, na mchanganyiko wa magonjwa hayo mawili husababishwa na aina ya utapiamlo ulio hatari sana wa kukosa vyakula vinavyojenga mwili. Ugonjwa wa marasmus huwapata watoto wanaonyonya wenye umri wa kati ya miezi 6 na miezi 18. Huanza polepole kwa upungufu mkubwa wa nishati, vitamini na madini na husababishwa na kutonyonya vya kutosha au kula vyakula vya badala visivyo na virutubisho vya kutosha. Mtoto mwenye ugonjwa huo hukonda sana, misuli yake hunyauka kiasi cha kubaki mifupa na ngozi, naye hakui. Uso wake huwa kama wa mtu aliyezeeka, anakasirika haraka na kulia sana.

Neno la Kiafrika kwashiorkor linamaanisha “mtoto aliyeachishwa.” Linawahusu hasa watoto ambao wanaachishwa kunyonya ili ndugu au dada zao wachanga zaidi wanyonye. Ugonjwa huo huanza baada ya mtoto kuachishwa kunyonya. Unasababishwa na ukosefu mkubwa sana wa protini na upungufu wa kalori mwilini. Maji hurundamana mwilini na kumfanya mtoto avimbe tumbo, mikono na miguu. Nyakati nyingine uso wake huvimba na kuwa na umbo la mwezi mpevu. Vidonda hutokea kwenye ngozi na nywele hubadilika rangi na kukauka. Watoto wenye ugonjwa huu huvimba ini, hukosa uchangamfu na furaha. Ndivyo alivyokuwa Erik, aliyetajwa awali, ambaye alinyonyeshwa na mamaye kwa mwezi mmoja tu; kisha akaanza kunyweshwa maziwa ya ng’ombe yaliyotiwa maji. Alianza kunyweshwa mchuzi wa mboga na maji yenye sukari akiwa na umri wa miezi mitatu na kuachiwa jirani amtunze.

Aina ya tatu ya utapiamlo huwa ni mchanganyiko wa ugonjwa wa marasmus na kwashiorkor. Magonjwa hayo yanaweza kuua yasipotibiwa haraka.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 8]

MLINDE MTOTO WAKO ASIPATE UTAPIAMLO!

▪ Ni muhimu mama ale chakula bora. Akina mama wajawazito na wanaonyonyesha wanahitaji nishati na protini zaidi. Protini hasa humsaidia mama kuongeza maziwa. Kwa hiyo kunapokuwa na uhaba wa chakula, walisheni kwanza akina mama wenye umri wa kupata watoto na watoto wachanga.

▪ Mara nyingi, chakula bora zaidi kwa mtoto mchanga ni maziwa ya mama. Wanahitaji kunyonya hasa siku za kwanza-kwanza baada ya kuzaliwa kwa sababu maziwa ya mama yana kingamwili zinazomlinda mtoto asiambukizwe magonjwa. Katika miezi minne hivi ya kwanza, maziwa ya mama huwa na madini na vitamini zote ambazo mtoto anahitaji ili kukua ifaavyo.

▪ Ijapokuwa mtoto hutegemea sana maziwa ya mama, anaweza kulishwa vyakula vingine kati ya mwezi wa nne na wa sita. Mlishe hatua kwa hatua matunda na mboga zilizopondwa-pondwa. Kila mara mlishe mtoto chakula kipya. Siku mbili au tatu baadaye, akisha zoea chakula hicho, mlishe kingine tofauti. Bila shaka, unahitaji kuwa na subira na kumzoeza mara nyingi ili mtoto akubali chakula kipya. Unapotayarisha chakula hicho, kumbuka kwamba kila kitu chapaswa kuwa safi kabisa. Osha vyakula na vyombo vizuri!

▪ Kati ya mwezi wa tano na wa tisa, kwa kawaida watoto huhitaji nishati na protini zaidi kuliko zinazopatikana kwenye maziwa. Endelea kuwalisha vyakula vingine vipya bila kuacha. Anza kwa kuwalisha nafaka na vyakula vyenye mboga zinazoweza kuliwa na watoto, kisha uwalishe nyama na vyakula vilivyotengenezwa kutokana na maziwa. Ingawa mwanzoni vyakula vinavyoliwa na watoto huchujwa sana, baadaye vinaweza kukatwa-katwa vipande vidogo kuanzia mwezi wa sita na kuendelea. Hakuna haja wala haipendekezwi uongeze chumvi au sukari kwenye vyakula hivyo.

▪ Baada ya miezi minane, mtoto hategemei sana maziwa ya mama, bali hayo ni nyongeza tu. Yeye huanza kula vyakula vinavyoliwa na wengine katika familia. Vyakula vinapasa kuwa safi kabisa, na vinapasa kukatwa-katwa vipande vidogo ili mtoto avitafune kwa urahisi. Mlo unaofaa unatia ndani matunda na mboga, nafaka na kunde, nyama na vyakula vilivyotengenezwa kutokana na maziwa. * Watoto wanahitaji hasa vyakula vyenye vitamini A. Kwa mfano, maziwa ya mama, mboga za kijani, matunda na mboga zenye rangi ya machungwa kama vile maembe, mapapai, na karoti. Watoto wenye umri wa chini ya miaka mitatu wanahitaji kula mara tano au sita kwa siku.

▪ Vyakula mbalimbali vilivyochanganywa kwa njia mbalimbali huwa na vitamini na madini yanayomlinda mtoto wako. Mama anapaswa kujitahidi kumlisha mtoto chakula bora, bila kumlazimisha ale wakati ameshiba wala kumnyima anapotaka kula zaidi.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 43 Utapata habari zaidi katika makala “Vyakula Bora Unavyoweza Kupata,” katika Amkeni! ya Mei 8, 2002.

[Picha katika ukurasa wa 8]

Wataalamu wanakubali kwamba maziwa ya mama ni chakula bora kabisa kwa mtoto aliyezaliwa karibuni

[Hisani]

© Caroline Penn/Panos Pictures

[Picha katika ukurasa wa 7]

Watoto wakila ngano ya ‘bulgur’ na mboga shuleni huko Bhutan

[Hisani]

FAO photo/WFP Photo: F. Mattioli

[Picha katika ukurasa wa 9]

Unaweza kuboresha chakula cha mtoto wako

[Hisani]

FAO photo