Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Fumbo la Cahokia

Fumbo la Cahokia

Fumbo la Cahokia

NI MAJIJI yapi ya kihistoria unayokumbuka? Rome, London, Paris? Vipi Cahokia? ‘Ati Cahokia?’ huenda ukauliza. Naam, jiji la Cahokia lililo katika jimbo la Illinois, kilometa 13 mashariki ya St. Louis, Missouri, Marekani. * Lilikuwa jiji kubwa lenye mpangilio mzuri, ambalo lilionwa kuwa jiji muhimu la Wahindi Wamarekani kwa miaka 500. Ustaarabu wa Cahokia ulipofikia upeo wake yapata mwaka wa 1150 W.K., jiji hilo lilikuwa kubwa kuliko jiji la London au Rome wakati huo.

Kichapo kimoja kinasema kwamba Cahokia “lilikuwa jiji kubwa zaidi la kale upande wa kaskazini wa Mexico, likiwa na ukubwa wa kilometa 13 za mraba.” (Encyclopedia of North American Indians) Zaidi ya hayo, vilima vya udongo vimebaki katika bonde la Mto Mississippi, vikionyesha kwamba eneo hilo lilikuwa na ustaarabu wenye ufanisi hapo awali. Isitoshe, jiji la St. Louis liliitwa Jiji la Vilima kabla ya vilima 26 vya udongo kuondolewa, wakati jiji lilipokuwa likipanuka.

Eneo la Kihistoria Linalolindwa

Baadhi ya Wahindi Wamarekani huliona jiji la Cahokia kuwa mahali ambapo makabila mengi yalianzia. Kitabu cha The Native Americans kinasema kwamba “wazao wa wajenzi wa vilima wa Mississippi wanatia ndani makabila ya Chickasaw, Seminole, na Choctaw.” Kitabu kingine kinasema kwamba wao ni babu za makabila ya Creek, Cherokee, Natchez na makabila mengine.

Mwanzoni, jiji la Cahokia lilikuwa na vilima 120 vya udongo. Lakini sasa, ni vilima 80 tu vinavyosalia baada ya watu kulima na kupanua jiji hilo kwa miaka mingi. Vilima 68 kati ya vilima hivyo viko kwenye eneo hilo lenye ukubwa wa ekari 2,200.

Tangu mwaka wa 1925, Cahokia limekuwa likilindwa likiwa Eneo la Kihistoria katika jimbo la Illinois. Na katika mwaka wa 1982, Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa lilitangaza Vilima vya Cahokia kuwa Mahali Muhimu pa Kitamaduni Ulimwenguni, kwa sababu ya umuhimu wake katika historia ya kale ya Amerika Kaskazini.

Kwa Nini Lilijengwa Hapo?

Zamani sana katika mwaka wa 700 W.K., eneo la Cahokia lilikaliwa na Wahindi waliotegemea misitu. Hata hivyo, vilima vilijengwa miaka 200 hivi baadaye. Kwa nini Cahokia lilijengwa hapo? Kwa sababu zilezile zilizofanya jiji jirani la St. Louis lijengwe. Jiji hilo liko karibu na makutano ya mito mitatu mikubwa—Mto Mississippi, Mto Missouri, na Mto Illinois—katika bonde lenye rutuba ambalo wataalamu wa ardhi huita Ncha ya Kusini ya Amerika.

Mito hiyo na vijito vyake vilikuwa na samaki wengi na ndege wengi wahamaji wanaopenda maji. Wakazi walipata mbao za ujenzi na nyama kwa kuwinda wanyama hasa kulungu wenye mkia mweupe walioishi katika misitu iliyozunguka eneo hilo. Rasilimali nyingine kama vile mawe ya volkeno, ngegu, galina, na matale yalipatikana katika Uwanda wa Ozark ulio karibu. Wakazi karibu 20,000 au zaidi wa jiji hilo walikusanya nyasi nyingi ndefu walizotumia kwa ujenzi wa nyumba zao na majengo mengineyo kutoka kwenye mbuga zilizo karibu. Mimea mingi sana ilikuzwa kwenye bonde hilo, kutia ndani mahindi, amaranth, maboga, matunda yanayofanana na mung’unye, na alizeti. Wakazi wa Cahokia waliweza pia kukusanya pecan, beri nyeusi, kokwa za hickory, na plamu za mwituni. Isitoshe, mito hiyo iliwawezesha kufanya biashara kotekote. Makombe ya baharini kutoka Ghuba ya Mexico, shaba kutoka eneo la Maziwa Makuu huko Amerika Kaskazini, na ulanga kutoka Milima ya Appalachia vimepatikana Cahokia.

Maisha na Imani za Wakazi wa Cahokia

Kituo cha wageni kina sanamu kubwa zinazoonyesha shughuli za kila siku za watu wa Cahokia, kama vile kumchuna kulungu ngozi na kusaga mahindi. Elimu kuhusu ukuzaji wa mahindi, pamoja na matumizi ya rasilimali nyingine za asili yalikuwa mambo ya msingi katika ustaarabu wa Cahokia.

Mtaalamu mmoja wa vitu vya kale aliliita jiji la Cahokia “Yerusalemu la Amerika Kaskazini,” kwa sababu yaonekana dini iliathiri kila sehemu ya maisha ya wakazi wa jiji hilo. Chanzo kingine cha habari kinasema kwamba “Cahokia ilipofikia upeo wake (A.D. 1000-1150) ilikuwa na serikali iliyoongozwa na watawala wa kidini.” Vitu vya kale vilivyopatikana vinaonyesha kwamba watu wa Cahokia waliiona dini kuwa muhimu sana katika jamii. Kitabu cha Cahokia—City of the Sun kinasema kwamba “maisha yao yalikuwa na dhana zenye kupingana, kama vile giza na nuru, utaratibu na mchafuko, wema ambao ulithawabishwa na uovu ambao uliadhibiwa.”

Wakazi wa Cahokia waliamini kwamba kuna uhai baada ya kifo. Kwa hiyo, wafu walizikwa kwa heshima na mara nyingi kulikuwa na sherehe za mazishi zilizohusisha mambo mengi, hasa mazishi ya watu mashuhuri. Vilima fulani vilikuwa makaburi na huenda vilitumiwa kama piramidi za Mafarao wa Misri.

Kutembelea Vilima

Hebu tuchunguze vilima hivyo kwa makini. Vilima hivyo vina ukubwa na maumbo mbalimbali, lakini vyote ni vya udongo. Udongo huo uliletwa kwa vikapu hadi kwenye maeneo ya ujenzi wa vilima. Inakadiriwa kwamba, kwa ujumla, kiasi cha udongo cha meta milioni 1.5 za mchemraba kilisafirishwa kwa vikapu!

Kuna vilima vya aina tatu: vilima vyenye umbo la hema, ambavyo huenda vilitumiwa kuweka mipaka, lakini baadhi yake vina makaburi; vilima vyenye umbo la pia, ambavyo huenda pia vilitumiwa kama makaburi; vilima vyenye umbo la jukwaa, vyenye kimo cha meta moja hadi meta 30 hivi, na majengo yalijengwa juu yake. Mara nyingi mahekalu, majengo ya baraza la mji, au nyumba za watu mashuhuri zilijengwa juu ya vilima hivyo vya majukwaa.

Kwanza tunafika kwenye Kilima Namba 72, kilichojengwa juu ya vilima viwili vidogo vyenye makaburi. Kina urefu wa meta 43, upana wa meta 22, na kimo kisichozidi meta 2. Ijapokuwa ni kilima kidogo kikilinganishwa na vingine, Kilima Namba 72 kina hazina ya vitu muhimu sana vya kale vinavyoeleza mengi kuhusu Cahokia. Inaonekana kwamba kilima hicho kilikuwa na kaburi la mtu mmoja ambaye huenda alikuwa kiongozi maarufu, kwa sababu kuna shanga zipatazo 20, 000 za makombe ya Ghuba ya Pwani. Isitoshe, ncha 800 za mishale, mawe 15 yaliyobonyea ambayo yalitumiwa kwenye michezo ya Wahindi, rundo la ulanga, na shaba nyekundu iliyokunjwa vilitiwa kaburini vikiwa matoleo. Pia, watu 300 hivi, hasa wasichana walizikwa humo—yaelekea wengi wao walitolewa dhabihu.

Kwa Nini Kilima cha Watawa Ni cha Kipekee?

Sasa na tuelekee kaskazini kwenye jumba la kati la Cahokia hadi Kilima cha Watawa, kilichopewa jina la watawa wa Trappist ambao waliishi karibu hapo mwanzoni mwa miaka ya 1800. Walikuwa wakilima kwenye kilima hicho. Hicho ndicho kilima kikubwa zaidi katika Cahokia chenye umbo la piramidi iliyo bapa yenye vidato vinne. Kilijengwa katika hatua 14, na inaaminika kwamba kilijengwa kati ya mwaka wa 900 na 1200 W.K. Sehemu ya chini ya kilima hicho ina ukubwa wa ekari 14, “na ni kubwa kuliko piramidi yoyote ya Misri au Mexico.” Kilima hicho chenye kimo cha meta 30 na urefu wa zaidi ya meta 300, ndilo jengo kubwa zaidi la udongo lililojengwa katika Amerika Kaskazini na Kusini kabla ya mwaka wa 1492. Kuna kijia kirefu kinachopanda hadi kwenye vidato vilivyo upande wa kusini wa Kilima cha Watawa. Vitu vilivyochimbuliwa vinadokeza kwamba kijia hicho kilikuwa na ngazi.

Watu wa kawaida hawakuruhusiwa kupanda ngazi hizo. Kulikuwa na jengo kubwa kileleni ambamo mtawala mkuu wa Cahokia aliyeitwa Jua Kuu aliishi. Kitabu cha Cahokia—City of the Sun kinasema kwamba “huenda mtawala mkuu na makuhani wake walitumia jengo hilo kufanyia desturi za kidini, kutekeleza majukumu yao ya utawala, kusimamia milki yao, na kuwakaribisha wajumbe kutoka maeneo ya mbali.” Akiwa humo, mtawala angeweza pia kuangalia majengo mbalimbali ya umma, kama vile majengo ya baraza la mji, maghala, majengo ya starehe, nyumba za kuhifadhia maiti au mifupa, na nyumba za raia.

Mkuu huyo angeweza pia kuona ukuta uliozingira jiji, pamoja na minara mingi ya walinzi iliyokuwepo. Ukuta huo wenye urefu wa kilometa 3 ulijengwa upya mara tatu, kila mara walitumia miti 20,000 katika ujenzi. Wataalamu fulani wa vitu vya kale wanaamini kwamba ukuta huo ulitenganisha watu wa matabaka mbalimbali. Lakini yaelekea kwamba ulijengwa ili kuandaa ulinzi pia. Hata hivyo, wale waliokuwa maadui wa Cahokia hawajulikani.

Wakazi wa Cahokia Walienda Wapi?

Bado kuna fumbo lingine ambalo halijafumbuliwa. Kufikia mwaka wa 1500 W.K., Cahokia lilibaki ukiwa. Ni nini kilichotukia? Kuna maelezo chungu nzima kuhusu jambo hilo. Vitu vilivyochimbuliwa havionyeshi kwamba ufanisi wa Cahokia ulitokomea kwa sababu ya ugonjwa, uvamizi au msiba wa kiasili. Labda walitoweka kwa sababu ya mambo mbalimbali, kama vile mabadiliko ya hali ya hewa na ukataji wa miti uliosababisha ukame, njaa, na migogoro ya kijamii.

Wanasayansi fulani wanaamini kwamba huenda Cahokia lilikuwa na matatizo mengi ya kijamii yanayokumba majiji ya leo kama uchafuzi, kuzidi mno kwa idadi ya watu, kurundamana kwa taka, na labda hata vita vya wenyewe kwa wenyewe. Lakini sasa hatuwezi kufumbua mafumbo hayo mengi kwa sababu wakazi wa Cahokia hawapo ili waeleze jinsi walivyoishi.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 2 Jina Cahokia lilibuniwa katika miaka ya 1800. Watu fulani wanaamini kwamba jina hilo linamaanisha “jiji la jua.” Baadhi ya wataalamu wanaamini kwamba linamaanisha “bata-bukini wa mwituni.” Hakuna maandishi yoyote yanayoonyesha jinsi wenyeji walivyojiita au kuita jiji lao.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 14, 15]

JIJI LA CAHOKIA LILIANZAJE?

Kuna makisio mengi kuhusu mwanzo wa ustaarabu wa Cahokia, na wataalamu wana maoni yanayotofautiana juu ya hilo. Francis Jennings, mkurugenzi-mstaafu wa Maktaba ya Newberry Yenye Historia ya Wahindi Wamarekani, anasadiki kwamba wakoloni wa kale kutoka Amerika ya Kati walianzisha ukuzaji wa mahindi na mbinu zao za ujenzi katika Bonde la Mississippi. Anaandika hivi: “Wakoloni hao walileta ufanisi mkubwa wa kibiashara kuliko wenyeji wa Bonde la Mississippi na kulifanya eneo hilo liwe kama milki. Walianzisha ujenzi wa piramidi zenye pembe fupi kama zile za Amerika ya Kati na walijenga pia mahekalu na majengo ya kiserikali kwenye majukwaa ya juu ya piramidi.”

Hata hivyo, Jennings anakiri kwamba kuna ma-mbo mengi yasiyojulikana kwa uhakika. “Wataa-lamu wa vitu vya kale wanabishana iwapo watu wa Mississippi walikuwa wakoloni kutoka Mexico. Hawajui ukweli na wala hawatoi mwelekezo mwingine unaosadikisha.”

George E. Stuart anasema hivi katika kitabu chake Ancient Pioneers—The First Americans: “Kwa wataalamu wengi wa vitu vya kale na wanahistoria wa sanaa, vilima vyenye majukwaa vilivyopangwa kwa utaratibu kuzunguka masoko,” na pia vyombo fulani vya udongo “huonyesha wazi athari ya Amerika ya Kati, labda kwa njia isiyo ya moja kwa moja. Aina mbalimbali za mahindi na maharagwe yaliyo kwenye maeneo hayo yanaonyesha hivyo pia.” Hata hivyo, alisema maneno yafuatayo yanayozusha shaka: “Hakuna kitu hata kimoja cha kale ambacho kimetengenezewa Amerika ya Kati kimewahi kupatikana Kusini-Mashariki.” Kwa hiyo, fumbo hili halijafumbuliwa bado—wakazi wa Cahokia waliathiriwa na nani? Je, ni wakoloni kutoka Amerika ya Kati? Huenda tukapata jibu kadiri wakati unavyopita na vitu zaidi vya kale kuchimbuliwa.

[Picha]

Vichwa vya mishale na mawe kutoka kwenye Kilima Na. 72

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 16, 17]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

KITUO CHA CAHOKIA CHA KUANGALIA ANGANI

Kuna jambo jingine la pekee sana huko Cahokia: “Kuna duara kamili zinazofuatana. Wakati mmoja milingoti mikubwa iliyotengwa kwa umbali sawa ilisimama kwenye duara hizo katika sehemu tambarare za vilima.” (Gazeti la National Geographic, Desemba 1972) Milingoti hiyo imeitwa woodhenge kwa sababu inafanana na miamba ya kale iliyotumika kama kalenda huko Stonehenge, Uingereza.

Duara moja ya milingoti imerekebishwa. Ni duara yenye kipenyo cha meta 125 ambayo ina milingoti mikubwa 48 ya mti mwekundu wa mkangazi. Watu fulani wanaamini kwamba duara hiyo ilitumiwa kama kituo cha kuangalia jua. Milingoti hiyo “imepangwa kulingana na ncha za dira. Kulingana na mpangilio huo, mtu angeweza kusimama kwenye mlingoti wa 49 ulio nje ya duara na kuona mapambazuko wakati jua linapovuka mstari wa ikweta na linapokuwa mbali na mstari huo katika A.D. 1000.”

Wataalamu wa vitu vya kale wametambua kusudi la milingoti mitatu peke yake. Mlingoti mmoja huonyesha wakati jua linapovuka mstari wa ikweta, siku ya kwanza ya majira ya kuchipua na ya majani kupukutika, wakati jua linapoibuka mahali palepale. Milingoti mingine miwili huonyesha jua linapoonekana kwa mara ya kwanza baada ya majira ya baridi kali na ya kiangazi. Kusudi la milingoti mingineyo bado halijulikani.

[Picha]

Duara ya milingoti

[Hisani]

Cahokia Mounds State Historic Site

[Picha]

Kulisalimu jua linaloibuka

Soko la Cahokia

Shughuli za kijamii

[Hisani]

Middle three paintings: Cahokia Mounds State Historic Site/Michael Hampshire

[Picha]

Mchoro wa msanii unaoonyesha jinsi ambavyo huenda Cahokia lilikuwa mwaka wa 1200 W.K. hivi. Wakati wa upeo wake, jiji hilo lilikuwa na wakazi wapatao 20,000

1. Kilima cha Watawa

2. Jumba la Kati

3. Vilima Pacha

4. Ukuta unaozingira jiji

[Hisani]

Cahokia Mounds State Historic Site/William R. Iseminger

[Ramani katika ukurasa wa 14]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

Ukubwa wa Eneo Umeongezwa

Mto Mississippi

Mto Illinois 

Mto Missouri

St. Louis

Vilima vya Cahokia

[Hisani]

Mountain High Maps® Copyright © 1997 Digital Wisdom, Inc.

[Picha katika ukurasa wa 15]

Bamba la Birdman kutoka Cahokia

[Picha katika ukurasa wa 17]

Kilima chenye umbo la hema

[Picha katika ukurasa wa 17]

Kilima chenye umbo la pia

[Picha katika ukurasa wa 17]

Kilima chenye umbo la jukwaa

[Picha katika ukurasa wa 18]

Kituo cha Wageni Wanaozuru Vilima vya Cahokia

Kilima cha Watawa

[Hisani]

Pictures above and below: Cahokia Mounds State Historic Site

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 15]

All photos: Cahokia Mounds State Historic Site