Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Mnara wa Bosporus

Mnara wa Bosporus

Mnara wa Bosporus

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI UTURUKI

MNARA huo unafanana na mama anayesimama mlangoni pa nyumba yake akisubiri wapendwa wake warudi. Amesimama akiwa mpweke na mwenye huzuni kwa mamia ya miaka mahali ambapo Mlango-Bahari wa Bosporus unaingia kwenye Bahari ya Marmara. (Ona ramani.) Maji yanayoenda kasi hufanya mawimbi yenye nguvu yanayogonga mawe ya ufuo yaonekane kama mshono wa chini wa rinda la mwanamke kuzunguka mnara huo. Mambo mengi ya kihistoria yametukia katika mnara huo.

Kwa mamia ya miaka meli zimezamishwa, majeshi yenye pupa yalipora mali, kulikuwa na mapigano makali, na anasa katika makao ya kifalme. Ama kweli, jiji la Istanbul linapotajwa, watu wengi hukumbuka mnara huo unaowakilisha jiji hilo la kale.

Mnara huo huwavutia watu wengi isivyoelezeka. Kila jioni wakati wa machweo, watu huenda kwenye ufuo huo wa Asia kutazama mnara huo na jiji la Istanbul linaloonekana nyuma yake. Si ajabu kumwona mzee amesimama hapo akifikiria mambo yaliyotukia maishani mwake au kijana mwenye matarajio mengi akifikiria maisha yake ya usoni. Au labda ni mwanamke aliyefiwa na wapendwa wake akiwazia kwamba mnara huo ni mpweke kama yeye. Wakati mmoja, mtungaji wa mashairi Mturuki Sunay Akin, ambaye hutaja mnara huo tena na tena katika mashairi yake alisema hivi: ‘Jiji la Istanbul halipendezi hata kidogo bila mnara huo maridadi kuonekana.’

Si rahisi kujua historia ya mnara huo. Kadiri unavyochunguza historia yake ndivyo inavyoonekana kuwa imefichwa na desturi na hekaya.

Historia ya Mapema ya Kisiwa Hicho

Mambo ya kale zaidi yanayojulikana yanahusu miamba iliyo chini ya mnara, wala si mnara wenyewe. Katika mwaka wa 411 K.W.K., wakazi wa Sparta waliunga mkono Byzantium (leo Istanbul) ilipokuwa ikipigana na Athens. Kwa hiyo, Sparta ilinyakua sehemu ya Ulaya ya Bosporus, na Athens ikachukua upande wa Asia. Hatimaye, Sparta ilishindwa na Athens, lakini Athens haikushambulia Byzantium kwa muda, ikipendelea kusimamia Mlango-Bahari wa Bosporus na kufaidika na kodi zilizotozwa meli zilizopita hapo. Inaaminika kwamba jenerali na mwanasiasa wa Athens Alcibiades alijenga kituo cha kutoza kodi kwenye miamba hiyo. Hata hivyo, hakuna jambo lolote linalodokeza kwamba hapo palikuwa na mnara wakati huo.

Miaka kadhaa baadaye, jiji la Byzantium lilianza kutawaliwa na Athens. Athens ilituma meli 40 za kivita ili kulinda miliki yake huko Byzantium kwa kuhofia vitisho vya Mfalme Philip wa Pili wa Macedonia. Hares, kamanda mkuu wa jeshi hilo la wanamaji, aliandamana na mkewe, ambaye aliugua na baadaye kufa huko Chrysopolis (Üsküdar). Kamanda Hares alimjengea mkewe nguzo ya ukumbusho, na inasemekana aliijenga kwenye kisiwa kidogo chenye miamba ambapo Mnara wa Bosporus ulijengwa.

Mnara Huo Umewezaje Kudumu?

Kulingana na kitabu The Book of the Maiden’s Tower, jengo la kwanza lililofanana na mnara lilijengwa kwenye miamba hiyo wakati wa utawala wa Manuel I Comnenus (1143-1180). Jengo hilo lilifanana na ngome ndogo na lilikuwa na mizinga.

Baada ya Istanbul kushindwa katika mwaka wa 1453, ngome hiyo ndogo ilihifadhiwa na kuendelea kutumiwa na wanajeshi. Baadaye, mnara wa mbao wa kuongozea meli ulijengwa kuelekeana na Bahari ya Marmara. Kufuatia kushindwa kwa Istanbul, mnara huo uliendelea kuwapo huku wanadamu wakiendelea kuangamizana—wakitumia meli za kivita na mapanga. Meli za mizigo zilizojaa baruti na vitu vingine vinavyoshika moto zilitumiwa katika vita.

Kadiri miaka ilivyopita, mnara huo uliathiriwa na matetemeko ya ardhi na mioto, na hatimaye katika mwaka wa 1720 uliharibiwa vibaya sana na moto. Kisha Damat Ibrahim Pasha aliujenga upya mnara huo kwa mawe, na kuongeza mnara mwingine mdogo wenye madirisha yaliyofunikwa kwa madini ya risasi. Mnamo mwaka wa 1829 wakati wa mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu, mnara huo ulitumiwa kuwahudumia wagonjwa. Muda mfupi baadaye, marekebisho makubwa yalifanywa wakati wa utawala wa Mahmud wa Pili katika mwaka wa 1832. Mnamo mwaka wa 1857, Kamati ya Usimamizi wa Minara ya Taa za Kuongozea Meli ilianza kusimamia mnara huo. Katika mwaka wa 1920, kampuni ya Ufaransa ilipewa kazi ya kuurekebisha ili uweze kutumiwa na ukatiwa mashine zinazofanya kazi zenyewe. Mnara huo wa taa uliendelea kutumiwa kwa miaka mia moja hivi baadaye.

Wakati wa utawala wa Uturuki mnara huo ulitumiwa hasa kuongozea meli usiku; na pia ulitumiwa wakati wa mchana kulipokuwa na ukungu. Bahari ilipochafuka, mashua ndogo zilifungiliwa kwenye mnara huo ili zisipeperushwe na mawimbi. Mizinga ililipuliwa kutoka mnara huo wakati wa sherehe za kiserikali.

Mara kwa mara, wafalme wa Uturuki waliutumia mnara huo kwa njia mbalimbali. Maofisa wa serikali waliokuwa wakipelekwa uhamishoni au kuhukumiwa kifo walifungiwa humo kwa muda kabla ya kusafirishwa mbali au kwenda kuuawa.

Umetumiwa kwa Njia Mbalimbali

Baada ya mwaka wa 1923, mnara huo haukutumiwa tena na serikali bali ulitumiwa tu kuongozea meli. Vita vya Pili vya Ulimwengu vilipokuwa vimepamba moto, mnara huo ulirekebishwa na sehemu zake za ndani zikaimarishwa kwa saruji. Baada ya kutwaliwa na jeshi la wanamaji katika mwaka wa 1965, mnara huo ulitumiwa kwa muda fulani kama kituo cha kijeshi cha mawasiliano. Kisha, mwishoni mwa karne ya 20, meli kubwa za kimataifa zilizotumia Mlango-Bahari wa Bosporus ziliongezeka. Meli hizo zilivuruga utulivu kwenye mnara huo. Baada ya mwaka wa 1983, mnara huo ulitumiwa na Shirika Linalosimamia Usafiri wa Meli Nchini Uturuki kama kituo cha kuelekeza meli katika Mlango-Bahari huo.

Kabla tu ya mwaka wa 1989 kuanza, habari ya pekee kuhusu mnara huo ilivutia uangalifu wa watu kwa mara nyingine tena. Kichwa kikuu cha gazeti moja kilisema hivi: “Sumu Imetiwa Kwenye Mnara wa Bosporus.” Gazeti hilo lilidai kwamba sumu ya cyanide iliyotumiwa kuangamiza wadudu hatari waliojaa kwenye meli, ilikuwa imehifadhiwa ndani ya mnara huo. Sumu hiyo hatari ilikuwa imehifadhiwa katika bohari lililokuwa bandarini ambalo lilibomolewa baadaye na sumu ikahamishwa hadi kwenye mnara huo “kwa sababu hakukuwa na mahali pengine pa kuiweka.” Kwa hiyo, mnara huo ukatiwa sumu. Isitoshe, ripoti hiyo ilisema kwamba kama gesi hiyo ingelipuka, jiji la Istanbul lingehatarishwa. Baada ya habari hizo kutangazwa kotekote magazetini na katika televisheni, hatimaye tatizo hilo lilisuluhishwa gesi hiyo ilipohamishwa hadi mahali pengine.

Si ajabu kwamba mnamo Mei 1992, kikundi cha washairi vijana, wakiungwa mkono na meya, walienda kwenye mnara huo uliokuwa umeachwa na kutangaza kwamba walitaka ufanywe kuwa kituo cha kitamaduni. Ama kweli, kwa mamia ya miaka mnara huo uliwachochea washairi wengi na waandishi wa vitabu. Muda mfupi baadaye, kulikuwa na maonyesho mengi ya picha na sanaa, na tamasha kadhaa zilifanyiwa humo. Kwa kipindi hicho kifupi, mnara huo ulitangazwa kuwa “jamhuri ya ushairi.”

Mnara Huo Leo

Katika mwaka wa 1999, marekebisho makubwa yalifanywa kwenye mnara huo ili wageni waweze kuutembelea. Baadaye, ilitangazwa kwamba mwaka uliofuata mnara huo ungekuwa na mkahawa na kituo cha kitamaduni ili kuendeleza utalii. Leo, kuna mikahawa, baa, mahali pa kutazama mandhari, na duka la vitu vya kale kwa ajili ya wageni na watalii. Mashua ndogo huwasafirisha watu hadi sehemu mbalimbali za Istanbul.

Ni wazi kwamba watu wengi hawafurahii kuanzishwa kwa biashara hizo. Hata hivyo, mnara huo bado ni maridadi. Ukipata nafasi ya kufika Istanbul, usikose kutembelea Mnara wa Bosporus. Huenda ukafurahia kuzuru mojawapo ya mikahawa mingi yenye bustani iliyo upande wa Asia wa Istanbul, huku ukinywa chai, na kutazama mandhari isiyo na kifani ya Kisiwa cha Bosporus pamoja na Mnara wake. Na kwa muda mfupi, labda utakumbuka historia ndefu ya Mnara wa Bosporus.

[Ramani katika ukurasa wa 25]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

UTURUKI

ISTANBUL

BAHARI YA MARMARA

Mlango-Bahari wa Bosporus

BAHARI NYEUSI

[Picha katika ukurasa wa 25]

Picha ya mnara huo katika karne ya 19

[Picha katika ukurasa wa 26]

Mkahawa

[Picha katika ukurasa wa 26]

Mahali pa kutazama mandhari