Mwanamume Aliyeamua Kumtii Mungu
Mwanamume Aliyeamua Kumtii Mungu
MWAKA wa 1937 ulikuwa wakati wenye kuhuzunisha kwa sababu tofauti za kisiasa zilisababisha migogoro katika nchi nyingi za Ulaya, na Wakristo walikabiliana na maamuzi mazito. Walipaswa kuamua ikiwa wangemtii Mungu au wanadamu. (Matendo 5:29) Vijana waliokuwa wamefikia umri wa kutumikia jeshini walijua kwamba kumtii Mungu kungehatarisha uhai wao.
Mhispania mwenye umri wa miaka 19 aitwaye Antonio Gargallo alihitaji kufanya uamuzi huo. Alipoitwa atumikie katika jeshi la wazalendo la Jenerali Franco, tayari kulikuwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe kwa mwaka mmoja hivi huko Hispania. Mwaka uliotangulia, Antonio alikuwa amebatizwa na kuwa Shahidi wa Yehova, na alikuwa amesoma shauri la Kimaandiko kwamba watumishi wa Mungu hawapaswi kuunga mkono upande wowote wa kisiasa au hata kujifunza vita. (Isaya 2:4; Yohana 17:16) Kwa kuwa hakutaka kuwa mwanajeshi na kuwaua raia wenzake, Antonio alijaribu kukimbilia Ufaransa. Lakini alikamatwa na kupelekwa kwenye kambi ya wanajeshi huko Jaca, Huesca, karibu na mpaka wa Hispania na Ufaransa.
Mahakama moja ya kijeshi ilimwambia waziwazi achague kati ya mambo haya: Aende vitani au auawe. Antonio aliamua kumtii Mungu. Muda mfupi kabla ya kuuawa, aliandika barua hii kwa mamake na dadake, ambao hawakuwa Mashahidi wa Yehova:
“Nimekamatwa na kuhukumiwa kifo hata kabla ya kesi yangu kusikizwa. Nitakufa usiku wa leo. Msihuzunike wala msilie . . . , kwa kuwa nimemtii Mungu. Vyovyote iwavyo, sitapata hasara yoyote, kwa kuwa Mungu akipenda, nitakuwa na maisha mapya na yaliyo bora. . . . Najihisi mtulivu muda wangu wa kufa unapowadia. Tafadhali pokeeni kumbatio la mwisho kutoka kwangu, mwana na ndugu yenu anayewapenda sana.” *
Wanajeshi watatu walisema kwamba Antonio aliimba nyimbo za kumsifu Yehova alipokuwa akienda kuuawa. Bila shaka, Mungu na Mwana wake wanathamini watumishi kama hao wanaoamua kumtii hadi kifo. Tuna uhakika kwamba Wakristo waaminifu kama Antonio watapata thawabu yao katika ufufuo.—Yohana 5:28, 29.
[Maelezo ya Chini]
^ fu. 5 Barua ya Antonio haikumfikia mamake kamwe, bali iliwekwa kwa miaka mingi katika hifadhi ya nyaraka za jeshi la Hispania.