Tuna Hisi Ngapi?
Tuna Hisi Ngapi?
“Sisi hufanya mambo mengi vizuri na kwa urahisi katika mazingira yetu. Ni vigumu kuelewa ile mifumo tata inayotuwezesha hata kuhisi vitu vidogo sana.”—SENSORY EXOTICA—A WORLD BEYOND HUMAN EXPERIENCE.
WAZIA ukiendesha baiskeli katika barabara tulivu ya mashambani. Unaposonga mbele, vipokezi vya hisi kwenye miguu yako vinakuwezesha kukanyaga pedali ipasavyo ili uende kwa mwendo unaotaka. Viungo fulani mwilini vinakusaidia udumishe usawaziko; pua yako inanusa harufu nzuri; macho yako yanatazama mandhari; na masikio yako yanasikia nyimbo za ndege. Unapokuwa na kiu, vipokezi vya hisi katika vidole vyako vinakuwezesha kushika chupa ya kinywaji. Vionjio vilivyo kwenye ulimi wako vinakuwezesha kuhisi ladha ya kinywaji hicho na vipokezi vingine vya hisi vinakusaidia kutambua ikiwa kinywaji hicho ni baridi au moto. Vipokezi vya hisi katika ngozi na nywele vinakuwezesha kufahamu upepo ni wenye nguvu kadiri gani. Vipokezi hivyo pamoja na macho yako vinakuwezesha kutambua unaenda kasi kadiri gani. Ngozi yako pia inakuwezesha kujua hali ya hewa, na uwezo wako wa kutambua wakati unakusaidia kukadiria muda ambao umekuwa ukiendesha baiskeli. Mwishowe, hisi zako za ndani zinakulazimisha upumzike na ule. Ama kweli, uhai unategemea hisi zinazotenda kazi kwa upatano kabisa!
Je, Tuna Hisi Tano Tu?
Ulitumia hisi ngapi ulipokuwa ukiendesha baiskeli? Je, ulitumia zile tano tu za kawaida: kuona, kusikia, kunusa, kuonja, na kugusa? Kulingana na kitabu Encyclopædia Britannica, ile dhana kuhusu hisi tano ilitokana na yule mwanafalsafa wa zamani Aristotle. “Maoni yake yamedumu kwa muda mrefu hivi kwamba mpaka leo watu wengi bado wanafikiri kuna hisi tano tu.”
Hata hivyo, kulingana na kitabu hicho, uchunguzi uliofanywa kuhusu hisi zinazopatikana kwenye ngozi “unadokeza kwamba wanadamu wana zaidi ya hisi tano.” Kwa nini tunasema hivyo? Hapo awali hisi fulani zilidhaniwa kuwa sehemu ya hisi ya kugusa, lakini sasa zinaonwa kuwa hisi tofauti. Kwa mfano, hisi za uchungu zinaweza kutambua na kutofautisha kati ya uchungu unaosikia unapogongwa na kitu na ule unaosikia unapoungua kwa moto au kemikali. Pia kuna hisi zinazotambua mwasho.
Uchunguzi unaonyesha kwamba tuna angalau hisi mbili zinazotambua wakati mwili unapofinywa—moja hutuwezesha kutambua tunapofinywa kidogo na nyingine tunapofinywa sana. Miili yetu pia ina hisi nyingi za ndani. Hisi za ndani zinafanya kazi gani?Hisi za Ndani
Hisi za ndani hutambua mabadiliko yanayotokea mwilini mwetu. Hizo hutusaidia tujue tunapokuwa na njaa, kiu, uchovu, maumivu ndani ya mwili, na tunapohitaji kupumua au kwenda msalani. Hisi hizo hufanya kazi pamoja na uwezo wa mwili wa kutambua wakati. Hivyo, tunahisi uchovu wakati wa jioni au baada ya kusafiri kwa ndege kwa saa nyingi. Watu wengine wamesema kwamba uwezo wa mwili wa kutambua wakati ni mojawapo ya hisi za mwili kwa sababu tunaweza “kuhisi” wakati ukipita.
Tuna hisi nyingine ndani ya sikio inayotusaidia tutembee kwa usawaziko. Hiyo hutufanya tuhisi nguvu ya uvutano, tuhisi tunapoenda kasi, na tunapozunguka. Mwishowe, tuna hisi inayotuwezesha tujue misuli yetu inapokazika. Hisi hiyo hutuwezesha pia kutambua miguu na mikono yetu inaposonga, na mahali ilipo, hata tukiwa tumefunga macho.
Bila shaka, si wanadamu pekee walio na hisi. Wanyama pia wana hisi nyingi tofauti-tofauti, na nyingine zenye kustaajabisha sana ambazo wanadamu hawana. Tutachunguza baadhi ya hisi hizo katika makala inayofuata. Pia tutajichunguza kwa undani tuone sifa zinazotufanya tuwe viumbe wa kipekee.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 4]
Wanadamu Wana Hisi ya Kugusa Inayostaajabisha
Mkono wa mwanadamu una hisi ya kugusa yenye nguvu sana. Kulingana na gazeti Smithsonian, watafiti waligundua kwamba mkono wa mwanadamu unaweza kuhisi alama ndogo sana ya kituo yenye ukubwa wa mikroni tatu. (Unywele wa mwanadamu una kipenyo cha mikroni 50 hadi 100.) Hata hivyo, “watafiti hao walipofanya uchunguzi kwa kugusa mkwaruzo badala ya alama ya kituo, waligundua kwamba mkono wa mwanadamu unaweza kuhisi mkwaruzo wenye ukubwa wa nanometa 75”—mikroni moja ina ukubwa wa nanometa elfu moja! Uwezo huo wa ajabu unatokana na vipokezi 2,000 vya hisi vilivyo katika ncha za vidole.
Hisi ya kugusa hutusaidia pia kuwa na afya bora na furaha. Gazeti U.S. News & World Report lasema kwamba “mtu anapopapaswa, mwili wake hutokeza homoni ambazo zinaweza kupunguza maumivu na kutuliza akili.” Watu wengine wanaamini kwamba mtoto asipopapaswa kwa upendo, ukuzi wake huathiriwa.
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 3]
Eye: The Complete Encyclopedia of Illustration/J. G. Heck; ear and inner ear: © 1997 Visual Language; hand: The Anatomy of Humane Bodies, with figures drawn after the life by some of the best masters in Europe . . . Oxford, 1698, William Cowper