Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Viumbe Wana Hisi za Ajabu

Viumbe Wana Hisi za Ajabu

Viumbe Wana Hisi za Ajabu

PANYA anazunguka-zunguka gizani akitafuta chakula huku akihisi yu salama. Lakini hana habari kwamba nyoka aina ya kipiri anaweza kutambua joto linalomtoka mwilini. Ole wake! Samaki aina ya wayo amejificha kabisa mchangani katika kidimbwi chenye papa. Papa mwenye njaa anamwelekea samaki huyo. Ingawa papa hamwoni, kufumba na kufumbua anamrukia yule wayo na kumnyafua papo hapo.

Kipiri na papa ni baadhi ya wanyama wenye hisi za kipekee ambazo wanadamu hawana. Kwa upande mwingine, viumbe wengi wana hisi kama zetu lakini zenye nguvu zaidi au zinazowawezesha kutambua mambo mengi zaidi. Uwezo wa kuona ni mojawapo ya hisi hizo.

Macho Yanayoona Vitu Ambavyo Hatuwezi Kuona

Macho yetu huona rangi chache sana kati ya rangi zote zilizopo. Kwa mfano, macho yetu hayawezi kuona miale inayoitwa infrared. Miale hiyo ni mirefu zaidi kuliko miale ya rangi nyekundu. Lakini aina fulani ya kipiri anaweza kutambua miale hiyo akitumia matundu mawili madogo yaliyo katikati ya macho na pua yake. * Kwa hiyo, anaweza kumshambulia mnyama mwenye damu moto hata akiwa gizani.

Ingawa wanadamu hawawezi kuona miale ya urujuanimno, viumbe wengi kutia ndani ndege na wadudu wanaweza kuiona. Kwa mfano, nyuki huongozwa na jua kutambua mahali wanapoelekea. Hata jua linapofunikwa kidogo na mawingu, wao hutambua mahali lilipo kwa kutafuta anga lililo wazi na kutazama mpangilio wa miale ya urujuanimno. Jua linapoangaza, mimea mingi inayochanua maua hurudisha miale ambayo wanadamu hawawezi kuiona, na mingine hurudisha miale ya urujuanimno kwa njia inayowawezesha wadudu kutambua mahali hususa penye umajimaji mtamu. Vilevile ndege hutambua matunda na mbegu fulani kwa njia hiyo.

Kwa kuwa ndege wanaweza kuona miale ya urujuanimno na kwa sababu miale hiyo hufanya manyoya yao yang’ae zaidi, huenda wao huwaona ndege wenzao wakiwa maridadi zaidi kuliko tunavyowaona. Mtaalamu mmoja anayechunguza ndege alisema kwamba ndege wanaweza kuona “rangi vizuri sana kuliko tunavyoweza kuwazia.” Mwewe na kozi fulani wanaweza kutumia uwezo huo wa kuona miale ya urujuanimno kuwakamata panyabuku. Kwa njia gani? Gazeti BioScience linasema kwamba “mkojo na kinyesi cha panyabuku wa kiume una kemikali ambazo hufyonza miale ya urujuanimno, na panya hao hutia alama kwenye njia wanayopitia kwa mkojo huo.” Hiyo ndiyo sababu ndege wanaweza “kutambua maeneo yenye panyabuku wengi” na kuwinda huko.

Kwa Nini Ndege Huona Vizuri Sana?

Ndege ana uwezo wenye kustaajabisha sana wa kuona. Kitabu All the Birds of the Bible kinasema kwamba “uwezo huo unatokana hasa na utando ulio ndani ya jicho lake unaomfanya aone vizuri. Utando huo una chembe nyingi za kuona kuliko utando wa viumbe wengine. Chembe za kuona zikiwa nyingi, jicho huona vitu vidogo kutoka mbali. Utando wa jicho la mwanadamu una chembe za kuona zipatazo 200,000 kwa kila milimeta ya mraba, ilhali chembe zilizo katika macho ya ndege wengi ni mara tatu ya idadi hiyo. Mwewe, tumbusi, na tai wana chembe milioni moja au zaidi kwa kila milimeta ya mraba.” Isitoshe, ndege fulani wana matundu mawili kwenye utando wa kila jicho ambayo huwawezesha kutambua vizuri umbali na mwendo wa vitu. Vilevile, ndege ambao hunasa wadudu wanaoruka wana uwezo kama huo.

Pia, ndege wana lenzi nyororo sana inayowawezesha kuona vizuri. Ikiwa ndege hawangeweza kuona vizuri, wangekabili hatari nyingi sana hasa wanaporuka msituni au kichakani. Ama kweli, jicho la ndege limebuniwa kwa hekima nyingi sana! *

Uwezo wa Kuhisi Umeme

Kisa kilichotajwa mwanzoni kuhusu samaki aina ya wayo na papa kilitukia wakati wa uchunguzi wa kisayansi kuhusu papa. Watafiti walitaka kujua iwapo papa na samaki aina ya taa wanaweza kuhisi nguvu kidogo za umeme zinazotokezwa na samaki aliye hai. * Walipitisha kiasi kinachofaa cha umeme kwenye mabamba yaliyowekwa mchangani katika kidimbwi chenye papa. Ikawaje? Mara tu papa alipoyakaribia mabamba hayo, aliyashambulia vikali.

Papa wanaweza kuhisi nguvu za umeme kama vile sikio linavyoweza kusikia sauti mbalimbali. Lakini, samaki wengine hutokeza nguvu za umeme. Kama vile popo anavyotoa mlio na kusikiliza mwangwi wake, samaki hao hutokeza mawimbi ya umeme, kisha wakitumia vipokezi maalumu wanaweza kutambua jinsi mawimbi hayo yanavyobadilika yanapogonga kitu fulani. * Kwa kutumia njia hiyo, samaki hao wanaweza kujua mahali penye vizuizi, windo, au hata mwenzi.

Uwezo wa Kujua Njia

Hebu wazia jinsi maisha yangekuwa iwapo ungekuwa na dira mwilini mwako. Hungepotea njia. Wanasayansi wamegundua kwamba viumbe fulani kama vile nyuki na samaki aina ya trauti wana chembe zenye sumaku ndogondogo mwilini mwao. Chembe hizo zimeunganishwa na mfumo wao wa neva. Hiyo inaonyesha kwamba nyuki na trauti wanaweza kuhisi nguvu za sumaku. Nyuki hutumia nguvu za sumaku kutengeneza sega na kujua wanakoelekea.

Watafiti pia wamegundua sumaku katika bakteria fulani zinazoishi kwenye mchanga unaopatikana chini ya bahari. Mchanga huo unapotibuliwa, sumaku zilizo katika bakteria hizo huvutwa na sumaku za dunia ili kusaidia bakteria hizo kurejea kwenye makao yake chini ya bahari. Zisipofanya hivyo, zitakufa.

Huenda wanyama wengi wanaohamahama kama vile ndege, kasa, samaki aina ya salmoni, na nyangumi wanaweza kuhisi nguvu za sumaku. Hata hivyo, inaonekana wanyama hao hawategemei hisi hiyo peke yake, bali wao hutegemea hisi mbalimbali wanapohama. Kwa mfano, huenda salmoni hutumia uwezo wao wa kunusa wenye nguvu ili wafike mahali walipozaliwa. Kwezi fulani huongozwa na jua ili wafike mahali wanapoenda na ndege wengine huongozwa na nyota. Lakini kama alivyosema profesa wa saikolojia Howard C. Hughes katika kitabu chake Sensory Exotica—A World Beyond Human Experience, “ni wazi kwamba itachukua muda mrefu kuelewa mambo hayo na mambo mengine tata kuhusu viumbe.”

Uwezo wa Ajabu wa Kusikia

Wanyama wengi wana uwezo wa ajabu wa kusikia ambao ni bora kuliko wa wanadamu. Ingawa tunaweza kusikia sauti zenye frikwensi ya hezi 20 hadi 20,000 (hezi ni idadi ya mizunguko ya wimbi la sauti kwa sekunde moja), mbwa wanaweza kusikia sauti zenye frikwensi ya hezi 40 hadi 46,000 na farasi hezi 31 hadi 40,000. Tembo na ng’ombe hata wanaweza kusikia sauti za chini zenye frikwensi ya hezi 16 ambazo wanadamu hawawezi kusikia. Kwa kuwa sauti zenye frikwensi ya chini husafiri mbali zaidi, tembo wanaweza kuwasiliana wakiwa umbali wa kilometa nne au zaidi. Watafiti fulani hata wanasema kwamba tunaweza kuwatumia wanyama hao kutambua mapema ishara za matetemeko ya ardhi na hali mbaya ya hewa, kwani matukio hayo huanza kwa sauti zenye frikwensi za chini sana.

Wadudu pia wanaweza kusikia sauti zenye frikwensi tofauti-tofauti, nyingine zenye frikwensi ya juu sana ambazo wanadamu hawawezi kusikia na nyingine zenye frikwensi ya chini sana. Wadudu wachache husikia kupitia viungo vyembamba vilivyo katika sehemu zote za mwili isipokuwa kichwani. Wengine wana nywele nyembamba zinazowasaidia kusikia sauti na vilevile vitu vinavyosonga polepole sana hewani kama vile wakati mkono wa mwanadamu unaposonga. Hiyo ndiyo sababu ni vigumu sana kumgonga nzi.

Wazia ukiwa na uwezo wa kusikia mdudu akitembea! Popo—mnyama pekee anayeweza kuruka kama ndege—ana uwezo huo. Bila shaka, popo wanahitaji uwezo wa kipekee wa kusikia ili kusafiri gizani na kukamata wadudu kwa kusikiliza mwangwi wa sauti yao wenyewe. * Profesa Hughes anasema hivi: “Hebu wazia mfumo wa kupokea mwangwi ulio tata kuliko ule wa nyambizi ya hali ya juu zaidi. Sasa wazia mfumo huo ukitumiwa na popo mdogo sana anayeweza kutoshea katika kiganja cha mkono wako. Ubongo wake ambao ni mdogo kuliko ukucha wa kidole gumba humwezesha kutambua umbali, mwendo, na hata aina ya wadudu anaonuia kukamata!”

Ili popo watambue mahali vitu vilipo kwa usahihi, wanahitaji kutoa sauti nzuri. Wao hufanya hivyo kwa kutumia “uwezo wao wa ajabu wa kuinua na kushusha sauti ambao unapita ule wa mwimbaji bora,” chasema kitabu kimoja. * Inaonekana jamii fulani ya popo hutumia viungo fulani vilivyo juu ya pua zao kuelekeza sauti mahali fulani. Kwa kutumia uwezo huo, popo wanaweza kutambua hata vitu vidogo sana kama unywele wa mwanadamu!

Mbali na popo, kuna angalau aina mbili za ndege wanaotumia mwangwi kutambua mahali vitu vilipo. Ndege hao ni mbayuwayu fulani wa Asia na Australia na ndege aina ya oilbird wa Amerika Kusini. Hata hivyo, inaonekana ndege hao hutumia uwezo huo kuwasaidia tu kusafiri katika mapango yao yenye giza.

Kutumia Mwangwi Baharini

Nyangumi wa aina fulani pia hutumia mwangwi kutambua mahali vitu vilipo baharini, hata ingawa wanasayansi hawana uhakika jinsi wanavyotumia uwezo huo. Pomboo hutoa milio tofauti-tofauti ambayo inadhaniwa kuwa hutoka puani wala si kooni. Kiungo fulani chenye mafuta kilicho kwenye kipaji cha uso wa pomboo huelekeza milio hiyo ili kumwezesha kutambua vitu vilivyo mbele yake. Pomboo husikiaje mwangwi wa sauti yao? Inaonekana hawatumii masikio yao moja kwa moja, bali wao hutumia utaya wao wa chini na viungo vingine vilivyounganishwa na sehemu ya ndani ya sikio. Sehemu hiyo ya sikio ina mafuta kama yale yanayopatikana kwenye kipaji cha uso wa pomboo.

Mawimbi ya milio ya pomboo yanafanana sana na wimbi linaloitwa Gabor linalotumiwa katika hesabu. Kulingana na Hughes, wimbi hilo linathibitisha kwamba pomboo hutoa milio “inayokaribia kufanana sana na ile inayotolewa na mifumo ya kupokea mwangwi.”

Pomboo wanaweza kutoa milio ya chini sana au milio ya juu sana yenye kipimo cha desibeli 220. Milio hiyo ni ya juu sana kiasi gani? Muziki wa roki wenye sauti ya juu unaweza kufikia kipimo cha desibeli 120, na mlio wa bunduki desibeli 130. Pomboo wanaweza kutumia mlio mkubwa zaidi kuliko huo kutambua vitu vidogo sana kama mpira wa sentimeta nane ulio umbali wa meta 120. Wanaweza kutambua vitu vilivyo mbali hata zaidi maji yanapokuwa matulivu.

Je, hustaajabishwi na hisi hizo za ajabu za viumbe? Watu wanyenyekevu wenye ujuzi hustaajabishwa nazo. Hilo latufanya tufikirie jinsi tulivyoumbwa. Ni kweli kwamba hisi zetu ni duni sana zinapolinganishwa na zile za wanyama na wadudu fulani. Hata hivyo, ni sisi tu tunaosisimuliwa na maumbile. Kwa nini? Kwa nini tunajitahidi kujifunza kuhusu viumbe na kusudi la kuwapo kwa viumbe hao, na vilevile kujua kusudi letu maishani?

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 5 Kuna aina 100 hivi za vipiri.

^ fu. 10 Wasomaji wanaotaka kujua tofauti iliyopo kati ya dhana ya mageuzi na ubuni wenye hekima wanaweza kusoma kitabu Je, Kuna Muumba Anayekujali?, kilichochapishwa na Mashahidi wa Yehova.

^ fu. 12 Viumbe wote walio hai, kutia ndani wanadamu, hutokeza kiasi kidogo cha umeme kinachoweza kutambuliwa wanapokuwa ndani ya maji.

^ fu. 13 Samaki tunaozungumzia hapa hutokeza nguvu kidogo sana za umeme. Wao ni tofauti na samaki wengine kama vile taa na mkunga, ambao hutokeza nguvu nyingi za umeme ili kushtua adui au kunasa windo. Mkunga hutokeza nguvu nyingi sana za umeme zinazoweza kumuua farasi!

^ fu. 21 Kuna aina 1,000 hivi za popo. Tofauti na maoni ya watu wengi, popo wote wanaweza kuona vizuri, lakini si wote wanaoweza kutumia mwangwi wa sauti zao. Baadhi yao, kama wale popo wanaokula matunda, hutumia uwezo wao wa kuona vizuri gizani kupata chakula.

^ fu. 22 Popo hutoa mlio wenye frikwensi tofauti-tofauti kuanzia hezi 20,000 hadi hezi 120,000 au zaidi.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 9]

Enyi Wadudu, Jihadharini!

“Kila siku, wakati wa jioni, jambo la kushangaza sana hutukia chini ya vilima vilivyo karibu na San Antonio, Texas [Marekani],” chasema kitabu Sensory Exotica—A World Beyond Human Experience. “Ukiwa mbali, unaweza kufikiri umeona wingu kubwa la moshi mweusi likipaa kutoka chini ya ardhi. Hata hivyo, si moshi unaofanya anga kuwa jeusi, bali ni popo milioni 20 wenye mikia mirefu ambao wanatoka katika Pango la Bracken.”

Makadirio yaliyofanywa hivi karibuni yanaonyesha kwamba kuna popo milioni 60 katika Pango la Bracken. Popo hao hupaa kufikia meta 3,000 angani ili kutafuta wadudu, kwani hicho ndicho chakula wanachokipenda sana. Ijapokuwa sauti nyingi sana za popo zinasambaa angani wakati wa usiku, hakuna mvurugo wowote unaotokea kwani kila mmoja wa popo hao ana mfumo tata sana unaomsaidia kutambua mwangwi wake.

[Picha]

Pango la Bracken

[Hisani]

Courtesy Lise Hogan

[Picha]

Popo wenye mikia mirefu—husikia mwangwi

[Hisani]

© Merlin D. Tuttle, Bat Conservation International, Inc.

[Picha katika ukurasa wa 7]

Nyuki—huona na hutambua nguvu za sumaku

[Picha katika ukurasa wa 7]

Tai—huona

[Picha katika ukurasa wa 7]

Taa—hutambua nguvu za umeme

[Picha katika ukurasa wa 7]

Kwezi—huona

[Picha katika ukurasa wa 7]

Salmoni—hunusa

[Hisani]

U.S. Fish & Wildlife Service, Washington, D.C.

[Picha katika ukurasa wa 7]

Kasa—pengine anaweza kutambua nguvu za sumaku

[Picha katika ukurasa wa 7]

Papa—hutambua nguvu za umeme

[Picha katika ukurasa wa 8]

Tembo—husikia sauti za chini sana

[Picha katika ukurasa wa 8]

Mbwa—husikia sauti za juu sana

[Picha katika ukurasa wa 9]

Pomboo—husikia mwangwi