Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kutembelea Shamba la Migomba

Kutembelea Shamba la Migomba

Kutembelea Shamba la Migomba

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI AFRIKA KUSINI

MIMI hupenda kula ndizi. Nadhani watu wengi pia huzipenda. Ndizi ni tamu na pia zina vitamini, madini, na nyuzi. Je, ungependa kujua mengi zaidi kuhusu tunda hilo tamu? Hivi majuzi mkulima mmoja na mkewe walinionyesha jinsi migomba inavyokua kwa njia ya ajabu.

Tony na Marie (ona picha) ni wakulima katika eneo la Levubu, lililo kwenye Mkoa wa Limpopo huko Afrika Kusini. Wanakuza mimea mbalimbali kwenye shamba lao la ekari 140. Hata hivyo, wao hupanda ndizi kwa wingi. Tony angependa kutuambia mengi zaidi kuhusu tunda hilo linalopendwa sana.

Ukuzaji na Hali za Hewa

Tony asema kwamba “migomba hukua vizuri kwenye udongo wa mfinyanzi usio na mchanga au mawe. Ni lazima uwe na kina kirefu na unaofyonza maji haraka. Migomba ya ndizi husitawi katika maeneo yenye joto yasiyo na baridi kali. Eneo la Levubu lina hali ya joto ya wastani wa nyuzi za Selsiasi 12 hadi 35 kwa mwaka.” Ninapouliza kuhusu mvua, Tony anajibu: “Ndizi huhitaji mvua kila wakati au kunyunyiziwa maji kila juma.”

Ingawa mgomba ni kama mti, kwa kweli una shina lenye majani yaliyosongamana. Mgomba ni gugu kubwa, wala si mti. Shina lake kuu huwa ardhini. Mizizi humea kwenye shina hilo, na hatimaye majani na ua kubwa la zambarau hukua kwenye shina hilo. Machipukizi huota na kuwa migomba.

Migomba ina hatua tatu za ukuzi, ambazo wakulima huiita “nyanya, binti, na mjukuu.” (Ona picha.) “Nyanya” atazaa matunda mwaka huu “binti” mwaka ujao, na “mjukuu” mwaka wa tatu. “Wajukuu” hukua kwa wingi karibu na “mama” yao. “Watoto” hao wanapofikia kimo cha magoti, wote hukatwa isipokuwa wale wenye afya.

Ua kubwa la zambarau, ambalo baadaye huwa mkungu wa ndizi, hukua kutoka kwenye shina. Hatimaye, ua hilo hutokea katikati ya majani mawili ya juu na kuning’inia. Ua linaponyauka, vichala 10 hadi 15 huibuka kwenye mkungu na mtu asiyejua mambo ya ndizi hufikiri kwamba unakua kuelekea chini! Mkungu unaweza kuwa na ndizi 20 au zaidi.

Wakati wa Mavuno

Ndizi huvunwa miezi mitatu hadi sita baada ya ua lake la zambarau kuchanua, ikitegemea wakati wa mwaka. Tunda hilo huvunwa likiwa bichi, lakini baada tu ya ndizi kukomaa. Mkungu wenye uzito wa kadiri una kilogramu 35 hivi. Wakati wa mavuno mkungu huwekwa katika mfuko wa plastiki ili usipondwe unaposafirishwa kwa mkokoteni hadi chumba cha kuhifadhia. Katika chumba hicho mkungu hugawanywa katika vichala vyenye ndizi tatu hadi sita na kisha kutiwa dawa ya kuzuia kuvu.

Nchini Afrika Kusini ndizi hupakiwa katika masanduku yaliyopakwa nta na kutobolewa ili kupitisha hewa, na huwekwa katika chumba cha kuivisha. Gesi iitwayo ethylene huzifanya ziive haraka. * Masanduku huwekwa humo katika hali ya joto inayofaa kwa siku moja au mbili kisha husafirishwa sokoni.

“Labda ninapendelea ndizi zetu,” asema Tony, akitabasamu, “lakini nafikiri ndizi za Levubu ni tamu sana, huenda ni kwa sababu ya udongo wetu. Kwa kusikitisha, hatuwezi kuuza ndizi zetu nje ya nchi yetu kwa hiyo zinaliwa humuhumu tu.”

Nzuri kwa Afya Yako

Ndizi zina madini ya potasiamu. “Uchunguzi mbalimbali unaonyesha kwamba madini hayo yanaweza kuimarisha mifupa na kupunguza uwezekano wa kupata shinikizo la damu na mshtuko wa akili,” yasema makala kuhusu ndizi katika gazeti la Health. Gazeti hilo laongezea kwamba, “ndizi zina madini yanayowalinda watoto wasizaliwe na kasoro, na vitamini B iliyo muhimu kwa wanawake waja-wazito au wenye umri wa kuzaa.” Ndizi zina madini mengine muhimu kama vile magnesi, ambayo husaidia mifupa kufyonza kalisi na kubaki ikiwa yenye nguvu.

Protini iliyo katika ndizi ina asidi-amino 18, kutia ndani zote zilizo muhimu ambazo mwili wako hauwezi kutengeneza za kutosha au hautengenezi hata kidogo. Ndizi zina asilimia 22 ya wanga, ambayo hukupatia nguvu haraka kwa sababu husagwa kwa urahisi tumboni. Marie anaongezea kwamba “Ndizi zina vitamini A, B, na C kwa wingi. Pia, yaelekea hizo hupunguza hamu ya chakula kwa sababu inaonekana watu hawapendi kula ndizi nyingi wakati mmoja.” Kwa hiyo kwa nini usile ndizi moja—ni nzuri kwa afya yako na ni tamu sana pia!

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 12 Ndizi zinapoiva zenyewe hutoa gesi hiyohiyo inayozisaidia kuiva haraka. Kwa hiyo, njia nyingine ya kuivisha ndizi ni kuzichanganya na ndizi chache zilizoiva.

[Mchoro/Picha katika ukurasa wa 16]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

Jani

Ua/ndizi

Shina la majani

Ardhi

Mzizi

Shina kuu

[Hisani]

Sketch: Based on drawing from The Complete Encyclopedia of Illustration/J. G. Heck

[Mchoro/Picha katika ukurasa wa 17]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

Nyanya

Binti

Mjukuu

[Picha katika ukurasa wa 17]

Ua kubwa la zambarau ambalo baadaye huwa mkungu wa ndizi

[Hisani]

Photo by Kazuo Yamasaki ▲

[Picha katika ukurasa wa 18]

Wakati wa mavuno (kushoto); migomba ikikua (juu)