Kutoka kwa Wasomaji Wetu
Kutoka kwa Wasomaji Wetu
Kucheza Kamari Nimetoka tu kusoma mfululizo wa makala “Je, Kucheza Kamari Ni Tafrija Isiyodhuru?” (Julai 22, 2002) Namshukuru Yehova kwa kuwa anawatumia nyinyi kutupatia habari hii ya wakati unaofaa. Sikuamini niliposoma kuhusu tabia za wale walio na tatizo la kucheza kamari. Ni kama mlieleza kuhusu mume wangu! Jambo la kusikitisha ni kwamba tabia hiyo ilifanya atende dhambi nyingine nzito. Kucheza kamari ni tabia mbaya sana. Natumaini wote watakumbuka kwamba kucheza kamari si raha tu.
M. G., Marekani
Vipepeo Nina umri wa miaka kumi na nilifurahi sana kusoma makala “Kufuga Vipepeo.” (Julai 22, 2002) Tulikuwa na mradi wa kuchunguza vipepeo shuleni mwaka uliopita. Kila mtoto alipata kiwavi wa kutunza. Ilitubidi kumlisha kiwavi kila siku na kusafisha chombo chake. Hata niliwaona viwavi wanne wakiambua ngozi yao. Walipogeuka kuwa vifukofuko, tuliwarudisha kwenye kituo cha uchunguzi. Kisha tukaenda kuwaona vipepeo miezi sita hivi baadaye. Tafadhali endeleeni kuandika makala nzuri kama hizo.
B. P., Ujerumani
Nilikulia katika nyumba iliyokuwa karibu na uwanja fulani, na mara nyingi niliona vipepeo wengi nje ya nyumba yetu. Nilivutiwa na umaridadi wao. Kwa kuwa sasa mimi ni mtu mzima, viumbe hao wenye kupendeza hunisaidia kuona sifa za Yehova. (Waroma 1:20) Wazia furaha yangu nilipoona picha za vipepeo wenye rangi mbalimbali katika Amkeni! Asanteni kwa kazi yenu nzuri sana.
D. G., Slovakia
Kushuka Moyo Habari katika makala “Nilipambana na Ugonjwa wa Kushuka Moyo Baada ya Kujifungua” (Julai 22, 2002) zinaweza kutumiwa kuhusu magonjwa yote ya kushuka moyo. Mimi hupambana na ugonjwa wa kushuka moyo sikuzote. Inatia moyo sana kujua kwamba siko peke yangu, na kwamba ugonjwa huo, na magonjwa mengine yote yatakomeshwa na Ufalme wa Mungu.
C. H., Marekani
Miezi kumi iliyopita, baada ya kujifungua mtoto msichana, nilianza kuugua ugonjwa wa akili uliosababishwa na kujifungua. Nilimkataa mtoto wangu kabisa. Matibabu yalinisaidia sana na vilevile familia yangu na kutaniko. Natumaini kwamba makala hii itawasaidia wanawake wengine na familia zao kuelewa ugonjwa huo. Nimepanga kumpatia daktari wangu gazeti moja.
S. Z., Afrika Kusini
Baada ya kuzaa mtoto wangu wa pili, nilishuka moyo sana. Familia yangu na marafiki walinitia moyo kutafuta matibabu. Nashukuru tengenezo la Yehova kwa kuandaa chakula cha kiroho kwa wakati unaofaa kupitia vichapo kama Amkeni!
C. O., Marekani
Nywele Ninashukuru sana kwa makala “Je, Nywele Zako Zinakuhangaisha?” (Agosti 8, 2002) Nina umri wa miaka 36, na nimehangaika kwa muda mrefu kwa sababu nywele zangu hukatika na kupunguka. Makala hiyo ilinisaidia kuelewa kwamba nywele chache hukatika kwa ukawaida. Sasa sina wasiwasi tena. Msiache kuchapisha makala kama hizo!
V. G., Slovakia
Nilipata makala hiyo kwa wakati unaofaa kabisa. Nilikuwa na wasiwasi sana kwa sababu nywele zangu zilikuwa zikikatika. Makala hii ilinituliza hasa iliposema kwamba “kwa kawaida wengine hawaangalii nywele zako kama wewe.” Pia ilisema kwamba nywele 70 hadi 100 hukatika kila siku hata kama mtu hana tatizo la nywele!
E. L., Marekani