Methali za Waakan Zinaonyesha Maadili ya Kijamii
Methali za Waakan Zinaonyesha Maadili ya Kijamii
NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI GHANA
METHALI ni nini? Kamusi moja inasema methali ni “kifungu cha maneno kinachonukuliwa na watu mara nyingi, ambacho hushauri au kuelezea jambo fulani maishani.” Wayoruba wa Nigeria hufafanua methali kwa njia ya kupendeza zaidi, wakiiita “farasi anayeweza kukupeleka kwa urahisi kuvumbua mambo mapya.”
Umuhimu wa methali au misemo, unaelezwa na methali hii inayojulikana sana na Waakan wa Ghana: “Mtu mwenye hekima huzungumziwa kwa methali, si kwa maneno ya kawaida.” Maana yake ni kwamba, mtu mwenye hekima hahitaji kuambiwa mengi sikuzote ili asadikishwe kuhusu jambo linalofaa. Methali inayofaa huchochea kufikiri, huelewesha, na kumsukuma mtu afanye lililo sawa.
Nchini Ghana, methali hutumiwa sana wakati wa harusi na mazishi na hutajwa kwenye nyimbo za kitamaduni. Pia ni muhimu sana katika mazungumzo ya kirafiki. Mara nyingi msemaji au mjumbe hutumia methali kwa ustadi.
Katika jamii ya Waakan, kutumia methali kwa ustadi ni ishara ya hekima. Kwa kupendeza, Biblia inasema kwamba mfalme Sulemani—mwanamume aliyejulikana kwa hekima, elimu, na busara—alijua methali 3,000. Bila shaka, methali za Biblia ziliongozwa na Mungu na ni za kweli sikuzote, tofauti na methali zinazotegemea ujuzi na ufahamu wa wanadamu. Hata methali za wanadamu ziwe zenye hekima jinsi gani, hazipasi kamwe kulinganishwa na methali za Biblia. Lakini hebu tuchunguze baadhi ya methali za Waakan.
Imani Kuhusu Mungu
Huko Ghana, mara nyingi methali huonyesha kuwapo kwa Mungu, na ndivyo ilivyo na methali nyingi za Waakan. Waakan wanaamini Mungu yupo. Kwa mfano methali moja yasema: “Mtoto hafundishwi kumhusu Mungu.” Hata mtoto anajua kwamba Mungu yupo. Mara nyingi methali hiyo hutumiwa kuonyesha jambo ambalo mtoto atajifunza bila kufundishwa.
Methali nyingine ya Waakan inasema: “Ukimkimbia Mungu, bado uko chini yake.” Kwa hiyo, mtu yeyote anayempuuza Mungu anajidanganya. Zamani za kale, Biblia ilisema vivyo hivyo, kwamba macho ya Mungu “yako kila mahali; yakimchunguza mbaya na mwema.” (Mithali 15:3) Sisi sote tunawajibika kwa Mwenyezi Mungu.
Maadili na Kanuni za Kijamii
Kama ilivyo katika jamii nyingine, methali za Waakan huhifadhi maadili na kanuni za kijamii. Kwa mfano, umuhimu wa maneno unakaziwa katika mfano huu: “Ni heri kujikwaa dole kuliko kujikwaa ulimi.” Mtu anayeongea ovyoovyo anaweza kuleta madhara makubwa na hata kusababisha kifo.—Mithali 18:21.
Hata hivyo, mtu anapokuwa mwangalifu kuhusu maneno anayosema, anaweza kuleta amani, kama inavyoonyeshwa na msemo huu, “Meno hayashindani penye ulimi.” Yaani, matatizo yanaweza kusuluhishwa kwa amani—kama vile kati ya mume na mkewe—kupitia mazungumzo yenye utulivu. Hata wasipofaulu, kutumia ulimi kwa
ustadi kunaweza kupunguza migogoro na kufanya mapatano.Hekima Yenye Manufaa
Umuhimu wa kutumia utambuzi na busara unaonyeshwa waziwazi na methali kadhaa zinazokazia hekima yenye manufaa. Mpumbavu anayetenda bila kufikiria matokeo ya matendo yake anaweza kufaidika na methali isemayo, “Usimchokoze fira kama huna pa kukimbilia.”
Mzazi mwenye mtoto mtundu angetaka kutii methali hii, “Ukiona kijiti kinachoweza kukudunga jicho, king’oe, usikinoe.” Aha, tabia mbovu inapaswa kung’olewa ama kukatwa mapema, kabla haijazua matatizo.
Mila na Desturi
Nyakati nyingine ni muhimu kuelewa utamaduni wa jamii fulani ili uelewe methali zake. Kwa mfano, Waakan huona kutoa ishara kwa mkono wa kushoto hadharani kuwa tabia mbaya, hasa mbele ya wazee. Kanuni hiyo inaelezwa na methali, “Usitumie mkono wako wa kushoto kuonyesha njia ya kwenda kwenu.” Yaani, mtu anapaswa kuthamini kile alicho nacho, hata kwao.
Methali inayoeleza kuhusu mazoea ya ulaji ya Waakan inasema: “Mtoto anayejifunza kunawa mikono hula pamoja na wazee.” Wakati wa chakula, washiriki wa familia hupangwa kulingana na umri wao. Hata hivyo, mtoto mwenye tabia njema, hasa anayezingatia usafi na tabia njema, anaweza kuruhusiwa kula pamoja na baba yake na watu wengine wazima. Methali hiyo huonyesha kwamba mtu huheshimiwa kwa sababu ya mwenendo na si umri wake.
Je, unapanga kufunga ndoa? Basi fikiria methali hii ya Waakan, “Ndoa si tembo la mnazi linaloonjwa.” Wauzaji wa tembo hilo, linalogemwa kutoka kwenye mnazi, huwaruhusu wanunuzi walionje kabla ya kuamua kiasi watakachonunua au hata kuamua kutonunua. Lakini ndoa haiwezi kuonjwa. Methali hiyo yakazia kwamba kifungo cha ndoa chapaswa kudumu na ndoa za njoo tuishi hazikubaliwi.
Kuchunguza Mambo kwa Makini
Methali nyingi za Waakan zaonyesha kwamba mababu zao walichunguza watu na wanyama kwa makini. Kwa mfano, walitunga methali hii baada ya kumchunguza kuku na vifaranga wake kwa makini: “Kifaranga anayesimama karibu na mamaye hula paja la panzi.” Maana yake? Mtu akijitenga, anaweza kusahaulika wengine wanapopata vitu vizuri.
Mtu anayetazama chura aliyekufa hakosi kuelewa ukweli wa msemo huu, “Ukubwa wa chura huonekana afapo.” Methali hii hutumiwa mara nyingi mtu anapodharauliwa. Mtu huyo hujifariji kwamba anaweza kuthaminiwa zaidi asipokuwapo.
Methali Zilizofupishwa
Ingawa methali za Waakan zimepitishwa kizazi hadi kizazi kwa mdomo, nyingi zimehifadhiwa katika sanaa. Sanaa hizo huonekana katika michongo ya mbao, bakora, mawe ya dhahabu, mavazi ya kitamaduni na vitambaa vya kisasa. Wageni wanaotembelea majengo ya sanaa ya Ghana wanaweza kuona michoro ya mtu akipanda juu ya mti huku mtu mwingine akimsaidia. Picha hiyo yawakilisha methali
isemayo, “Ukipanda juu ya mti mzuri, unaweza kusaidiwa.” Maana ya methali hiyo ni wazi—ukifuatia miradi ya maana, unaweza kuungwa mkono.Wakati wa mazishi huwa fursa ya kuonyesha yale yaliyoitwa na mwandishi mmoja, ‘maandishi ya kanga.’ Huzuni ya pindi hiyo huwafanya watu watafakari sana kuhusu maisha. Kwa hiyo, michoro inayoonyeshwa katika mavazi yanayotumiwa kwenye mazishi huwa na ujumbe muhimu kuhusu maisha. Kwa mfano, kanga inayoonyesha ngazi humkumbusha mtu methali hii, “Mtu hawezi kupanda ngazi ya kifo akiwa peke yake.” * Methali hiyo huwatahadharisha watu wote wawe wanyenyekevu na wasiishi kana kwamba hawawezi kufa.—Mhubiri 7:2.
Katika jamii ya Waakan, wajumbe au wasemaji wa watawala wa kitamaduni ni stadi sana wa kutumia methali, na pia hubeba bakora zenye picha zinazoonyesha kanuni zinazopendwa. Kwa mfano, picha inayoonyesha ndege akimshika nyoka kichwa ni ufupi wa msemo, “Ukimshika nyoka kichwani, sehemu inayobaki ni kama kamba tu.” Inamaanisha nini? Pambana na kiini cha tatizo.
Matumizi Yanayofaa ya Methali
Kama mfano mwingine wowote, matumizi ya methali hutegemea hoja na watu wanaohusika. Huenda maana ikapotea methali isipotumiwa inavyofaa. Kwa kuwa katika tamaduni fulani matumizi ya methali ni muhimu katika mawasiliano, zikitumiwa isivyofaa zinaweza kuathiri maoni ya watu kuhusu anayezitumia.
Huko Ghana, wazee wa jamii huonwa kuwa watungaji na wahifadhi wa methali. Kwa hiyo, methali huanza kwa kusema, “Wahenga husema . . .” Na msemaji anapozungumza na watu wenye umri mkubwa zaidi, ni adabu kusema hivi kabla ya kutaja methali fulani, “Nyinyi wahenga husema . . .” Kwa sababu ya heshima, kijana hapendi kuonekana kana kwamba anawafundisha wazee maneno ya hekima yaliyo katika methali.
Baadhi ya Semi Muhimu
Methali zaweza kusemwa kabla ya hoja au baada ya hoja. Pia, nyakati nyingine zinaweza kutumiwa katika hoja ambayo huenda mtu akahitaji ufahamu ili kuelewa maana yake. Kwa mfano, Mwakan anaweza kusema hivi kuhusu mtu mnyenyekevu na mwenye kupenda amani: “Kama kungekuwa na fulani peke yake kijijini, hakungekuwa na mlio wa bunduki.” Hiyo yahusiana na methali hii, “Kama kungekuwa na konokono na kobe tu, hakungekuwa na mlio wa bunduki msituni.” Viumbe hao ni wapole na si rahisi kupigana. Watu wenye sifa hizo hudumisha amani.
Hata hivyo, ukitaka Mwakan akwambie methali nyingi, huenda akataja methali hii, “Mtu hawezi kuota pasipo usingizi.” Yaani, mtu hawezi kusema methali bila sababu kama tu isivyowezekana kuota ndoto bila usingizi. Methali hutumiwa kulingana na hali fulani.
[Maelezo ya Chini]
^ fu. 25 Inafaa tutaje kwamba picha hizo huchorwa kwenye nguo za rangi mbalimbali na wala si nguo nyeusi tu zinazotumiwa kwa kawaida katika mazishi.