Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Mojawapo ya Matunda Muhimu Zaidi Duniani

Mojawapo ya Matunda Muhimu Zaidi Duniani

Mojawapo ya Matunda Muhimu Zaidi Duniani

KUNA tunda la pekee ambalo limesambaa ulimwenguni pote. Tunda hilo hutumiwa kama chakula na kinywaji. Na umbo la pekee la mti unaozaa tunda hilo ni ishara ya visiwa vyenye joto. Ni tunda gani tunalozungumzia? Ni nazi—mojawapo ya matunda muhimu zaidi duniani.

Mnazi huenda ukawakumbusha watu wa maeneo yasiyo na joto kuhusu likizo kwenye maeneo yenye joto. Lakini mti huo una matumizi mengi kwa wale wanaoishi katika maeneo yenye joto. Waindonesia hudai kwamba tunda lake “lina matumizi mengi kama zilivyo siku za mwaka.” Nchini Ufilipino, kuna msemo usemao: “Apandaye nazi hupanda vyombo na mavazi, chakula na kinywaji, makao, na urithi kwa watoto wake.”

Msemo huo haujatiwa chumvi. Kulingana na kitabu Coconut—Tree of Life, mnazi “hutoa chakula, maji na mafuta ya kupikia, vilevile makuti ya kuezeka, makumbi ya kusokota kamba na kufuma mikeka, vifuu vinavyoweza kutumiwa kama vyombo na virembesho, na maji matamu ambayo hutumiwa kutengeneza sukari na tembo.” Kitabu hicho chaongezea hivi: “Hata mbao zake zinaweza kutumiwa zikikatwa ifaavyo.” Ama kweli, wakazi wa visiwa vya Maldive vilivyo katika Bahari ya Hindi walitumia mbao yake kutengenezea mashua, na yasemekana kwamba walisafiri kwa mashua hizo hadi Uarabuni na Ufilipino. Lakini nazi imeelea baharini na kufika mbali sana kuliko wakulima wake.

Mbegu Inayoelea Baharini

Nazi husitawi sana katika pwani nyingi zenye joto, maadamu tu kuna mvua ya kutosha. Ingawa wenyeji huenda wakapanda mnazi wenye matumizi chungu nzima, nazi imeelea yenyewe na kufika sehemu za mbali sana duniani. Mbegu aina mbalimbali husambazwa kwa njia tofauti-tofauti, lakini nazi husambazwa kupitia bahari. Na ndiyo sababu imefika katika sehemu nyingi za dunia.

Nazi inapoiva, huanguka chini. Nyakati nyingine, nazi iliyoiva hubingirika ufuoni kuelekea baharini. Kisha mawimbi huibeba. Kwa sababu makumbi yake yana hewa nyingi, hiyo huwezesha nazi kuelea kwa urahisi majini. Nazi ikiwa kwenye kisiwa cha matumbawe huko Pasifiki, huenda ikaelekea upande mwingine wa bahari. Lakini ikifika kwenye bahari kuu, nazi inaweza kufika mbali sana.

Maji ya chumvi ambayo huharibu mbegu nyingi, hayapenyi kwa urahisi ganda gumu la nazi lenye makumbi. Nazi zaweza kudumu baharini kwa miezi mitatu, nyakati nyingine zikielea umbali wa maelfu ya kilometa na bado huota vizuri zinapofika katika ufuo wenye hali nzuri. Labda nazi zimeenea katika pwani nyingi za maeneo yenye joto ulimwenguni kwa njia hiyo.

Ladha ya Vyakula vya Maeneo Yenye Joto

Katika maeneo yasiyo na joto, huenda watu wakaona nazi kuwa kiungo cha kuongezea ladha peremende au biskuti tu. Hata hivyo, ukienda Asia ya Kusini-Mashariki utagundua kwamba nazi ni tunda lenye matumizi mengi sana. Kulingana na kitabu Pacific and Southeast Asian Cooking, “nazi ni kiungo muhimu sana katika mapishi ya nchi na visiwa vyote kuanzia Hawaii hadi Bangkok.” Kitabu hicho chasema pia kwamba kwa wakazi wa maeneo hayo “nazi ni lishe muhimu sana maishani . . . katika njia nyingi na hutumiwa sana kutia ladha katika vyakula mbalimbali.”

Sababu inayofanya nazi itumiwe sana katika mapishi ya maeneo hayo ni hii: Huwa na maji, tui, na mafuta ya kupikia. Madafu huwa na maji matamu ya kunywa, na mara nyingi huuzwa katika vibanda vilivyo kandokando ya barabara. Na tui hutengenezwa kwa kuchanganya maji na nazi iliyokunwa kisha kukamuliwa. Tui huongeza ladha na uzito kwenye michuzi na unga uliokandwa.

Wakulima hutengeneza mafuta ya nazi kwa kupasua nazi iliyoiva na kuikausha juani. Inapokauka, nyama ya nazi au mbata, inaweza kutolewa kwenye kifuu, kisha mafuta hutengenezwa. Katika maeneo yenye joto, mafuta ya nazi hutumiwa sana kupikia ilhali katika nchi za Magharibi hutumiwa kupaka mikate, kwenye aiskrimu, na biskuti.

Kuangua nazi si kazi rahisi. Mara nyingi, mkwezi hupanda mnazi na kuangua nazi hizo. Wakwezi wengine hutumia mti mrefu wenye kisu. Huko Indonesia, nyani wamezoezwa kufanya kazi hiyo. Kwa wale ambao wanataka kupata nazi iliyoiva, njia rahisi zaidi ni kungoja ianguke chini yenyewe.

Haidhuru jinsi inavyoanguliwa, nazi imekuwa muhimu kibiashara na chakula cha watu wengi kwa sababu ya matumizi yake mbalimbali. Kwa hiyo ukiona mnazi, iwe ni kwenye picha au mti halisi, kumbuka kwamba si mti maridadi tu unaorembesha pwani za nchi zenye joto. Ni mti unaozaa mojawapo ya matunda muhimu zaidi duniani.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 26]

MAMBO YA PEKEE NA YENYE KUVUTIA KUHUSU NAZI

KAA ALAYE NAZI Si wanadamu tu wanaothamini nazi. Kaa alaye nazi hukaa shimoni mchana, lakini hula nazi usiku. Wanadamu wanahitaji kutumia panga kupasua nazi, lakini kaa huyo mbunifu hufanya kazi ngumu ya kugongesha nazi kwenye mwamba ili ipasuke. Yaonekana kiumbe huyo hufaidika sana kwa kula nazi kwani anaweza kuishi zaidi ya miaka 30!

NAZI KATIKA UREMBO Kwa kuwa mafuta ya nazi yanafaa kwa ngozi, watengenezaji huyatumia kutengenezea rangi ya midomo na mafuta ya kuzuia ngozi isibambuliwe na jua. Na ikiwa unatumia sabuni au shampuu yenye povu jingi inayoweza kuvundishwa na bakteria, huenda imetengenezwa kwa kutumia mafuta ya nazi.

[Picha]

Nazi haiharibiwi na maji ya bahari

Kaa alaye nazi

Mnazi

[Hisani]

Godo-Foto

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 25]

Top right inset: Godo-Foto