Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Jihadhari na Wadudu Hatari Wanaouma!

Jihadhari na Wadudu Hatari Wanaouma!

Jihadhari na Wadudu Hatari Wanaouma!

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI AUSTRALIA

ILIKUWA asubuhi yenye kupendeza ya kiangazi huko kaskazini mwa Queensland, Australia. Hiyo ilikuwa siku nzuri sana ya kuogelea katika maji matulivu ya eneo hilo ili kuepuka joto kali. Hata hivyo, asubuhi hiyo kulikuwa na tangazo moja lililorudiwa-rudiwa kwenye redio ya eneo hilo la Townsville. Lilisema kwamba viwavi hatari wa baharini walikuwa wameonekana majini na liliwatahadharisha wote ambao wangependa kuogelea.

Kijana mmoja na mke wake hawakusikia tangazo hilo. Walikuwa wameketi karibu na ufuo wa bahari, sentimeta 50 hivi kutoka kwenye maji ya buluu ya Pasifiki. Kufumba na kufumbua, mke wake aliyekuwa na mimba ya majuma 34 akapiga kelele na kuruka huku akijaribu kuvuta minyiri kadhaa kutoka kwenye paja na tumbo lake. Mumewe pia alikuwa ameumwa lakini alimsaidia kutoka ufuoni na akakimbia kupata msaada. Aliporudi dakika chache baadaye, mke wake alikuwa ameacha kupumua na uso wake, mikono yake, na miguu yake ilikuwa myeusi. Hata hivyo, mwanamke huyo alipuliziwa pumzi mara moja ili kumhuisha na gari la wagonjwa likaja bila kukawia. Basi, akaokoka na kujifungua majuma kadhaa baadaye.

Kila mwaka, mamia ya waogeleaji huumwa na viwavi wa baharini. Baadhi yao wamekufa dakika moja tu baada ya kuumwa. Basi, si ajabu kwamba watu huondoka ufuoni haraka wanaposikia kwamba viwavi wa baharini wameonekana! Viwavi hao huwa na minyiri 40 hadi 60, nayo huwa mirefu sana na hatari.

Je, Kuna Njia Zozote za Kuepuka Hatari Hiyo?

Watu wengine huamua kutoogelea baharini viwavi hao wanapokuwapo. Lakini wale wanaojasiria kuogelea baharini wakati wa miezi yenye joto wanahitaji kuvaa vazi la kuogelea linalofunika mwili mzima ili kuepuka kuumwa.

Fuo nyingi za Australia kaskazini huchunguzwa kwa ukawaida, na viwavi hao wanapoonekana, wengi wao hukamatwa. Pia, matangazo hutolewa mara nyingi kwenye redio ili kuwaonya watu kuhusu viwavi hao. Licha ya tahadhari hizo, hatari huendelea kuwapo kwani viwavi hao huenea. Yaonekana wao huzaana katika mikono ya bahari na mitoni. Wanapokomaa, wao huhamia ufuoni.

Hata hivyo, si rahisi kusikia mtu amekufa baada ya kuumwa na kiwavi wa baharini. Madhara ambayo mtu hupata anapoumwa yanategemea hasa kiasi cha mnyiri na sumu kilichoingia mwilini, umri wa kiwavi, na umri na afya ya mtu aliyeumwa. Lakini mtu asipotibiwa mara moja anaweza kufa kutokana na mshtuko wa moyo dakika moja tu baada ya kuumwa. Hiyo ni kwa sababu minyiri ya viwavi hao ina chembe nyingi kali ambazo hutoka kama mishale wanapowagusa viumbe wengine. Viwavi hao hutumia njia hiyo kuwanasa viumbe kama kamba kwa ajili ya chakula.

Viwavi wengine wa baharini wana macho manane ambayo huwawezesha kuona viumbe wengine kama wanadamu au wanyama wawindaji. Wanaweza kuona hata wanapojipinda na kuangalia vitu kupitia mwili wao ambao hupitisha mwangaza. Hiyo haimaanishi kwamba viwavi hao huwashambulia watu kimakusudi kwani wao hujaribu kuzunguka kitu wanachokutana nacho ikiwa wana muda wa kutosha. Wao hutumia mwili wao wenye umbo la sanduku, ambao hufyonza maji na kuyatoa ili waweze kusonga mbele.

Kwa kuwa wanadamu hukimbia au kuruka majini, viwavi wa baharini hawawezi kuepuka kugongana nao. Basi, minyiri yao inapogusa ngozi ya mwanadamu, hiyo hukwama ngozini na kutoa sumu. Mtu aliyeumwa huhisi maumivu makali. Chembe nyingi zilizo kwenye minyiri hutoa sumu ambayo huingia mwilini haraka. Mtu huyo anapokimbia au kurusharusha miguu yake, sumu huingia haraka zaidi mwilini. Tatizo jingine kubwa ni kwamba ijapokuwa minyiri huvunjika, hiyo hukwama mwilini mwa mtu aliyeumwa, na sumu zaidi hutokezwa mtu anapojaribu kuivuta.

Je, Kuna Dawa?

Ndiyo, dawa ipo. Watu wengi wameokoka baada ya kutumia dawa inayofaa haraka. Kwa miaka mingi watu walidhani kwamba njia bora na ya haraka ya kuzuia sumu isisambae ni kutia spiriti kwenye minyiri iliyokwama mwilini. Hata hivyo, utafiti uliofanywa hivi karibuni umebainisha kwamba spiriti hufanya sumu ienee zaidi.

Sasa inaaminika kwamba siki ndiyo dawa inayofaa zaidi kutiwa mahali mtu alipoumwa, nayo inapatikana kwa urahisi na kwa bei nafuu. Siki hukomesha nguvu za chembe zenye sumu na kuzizuia zisitoe sumu zaidi. Kwa hiyo, wawakilishi wa serikali katika maeneo yenye viwavi hao huweka chupa zenye siki mahali ambapo zinaweza kuonekana kwa urahisi, na vilevile ishara kubwa za kuonya.

Kwa hiyo, ingawa kuogelea kwenye maji yenye joto ya Australia kwaweza kuburudisha, acha mwogeleaji ajihadhari kunapokuwa na viwavi wa baharini!

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 27]

MAMBO YA KUFANYA ILI KUJILINDA NA VIWAVI WA BAHARINI

• Ogelea tu kwenye fuo zinazochunguzwa

• Vaa vazi la kuogelea linalofunika mwili mzima kunapokuwa na viwavi wa baharini

• Beba vifaa vya huduma ya kwanza pamoja na siki

• Usijaribu kuvuta minyiri unapoumwa

• Moyo wa mtu aliyeumwa unapoacha kupiga au anapoacha kupumua, mhuishe haraka kwa kumpulizia pumzi

[Picha katika ukurasa wa 26]

Picha kubwa ya minyiri ya kiwavi wa baharini

[Hisani]

Courtesy of Surf Life Saving Queensland