Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kula kwa Mikono

Kula kwa Mikono

Kula kwa Mikono

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI GHANA

WATU wengi hula kwa kutumia uma, kisu, na kijiko. Wengine, kama wale wanaoishi Asia, hula kwa kutumia vijiti viwili. Hata hivyo, wengine husema kwamba vyakula fulani huwa vitamu zaidi vinapoliwa kwa mikono kama nyama choma, nyama ya kuku, ugali, mkate, au chapati.

Lakini vipi unapokula mchuzi? Je, unaweza kuula kwa mikono? Huenda ukasema, ‘Haiwezekani! Mchuzi huwa moto na haushikiki.’ Katika nchi nyingi za Afrika, watu wamezoea kula mchuzi kwa mikono sawa na vile watu kutoka Asia wamezoea kula kwa vijiti. Hebu tukueleze kuhusu chakula fulani cha Waghana na jinsi unavyoweza kufurahia kukila kwa mikono.

Fufu na Mchuzi wa Njugu

Fufu hupikwa kwa kutumia ndizi aina ya mzuzu zilizochemshwa na mhogo, ambao hupatikana kotekote katika maeneo ya kitropiki. Ndizi na mihogo huambuliwa ngozi, huoshwa, na kuchemshwa ili ziwe laini. Maji yakiisha kumwagwa, chakula hicho hutwangwa-twangwa katika kinu kwa kutumia mchi ili kufanyiza mchanganyiko ulio laini. Mchanganyiko huo unaposhikamana kabisa hugawanywa katika vibonge vya mviringo.

Mchuzi wa njugu hutengenezwa kutokana na mchanganyiko wa njugu zilizopondwa, nyama au samaki, nyanya, vitunguu, pilipili, na vikolezo vingine. Nyama au samaki hupikwa kwa kutumia mvuke na kutiwa vikolezo, kisha maji na mchanganyiko wa njugu zilizopondwa huongezwa. Kisha mboga huchanganywa pamoja na kuongezwa ndani ya mchuzi. Halafu vitu hivyo vyote vinakorogwa pamoja na kupikwa vizuri. Fufu huandaliwa katika bakuli, huku mchuzi moto wa njugu ukiwa umewekwa juu yake.

Ustadi wa Kula kwa Mikono

Chakula hicho kitamu kikiisha kutayarishwa, utakilaje kwa mikono? Unahitaji ustadi wa kula kwa mikono.

Kwanza, nawa mikono yako vizuri. Halafu tumbukiza vidole vyako vya mkono wa kulia kwenye mchuzi. Lakini uwe mwangalifu! Ikiwa hujazoea, vidole vyako vinaweza kuungua!

Sasa mega tonge la fufu ukitumia kidole gumba, shahada, cha kati, na cha pete. Tia tonge hilo ndani ya mchuzi na ulibonyeze kwa kidole gumba ili ufanyize shimo litakalofyonza mchuzi.

Nyanyua tonge hilo. Halafu peleka mkono wako mdomoni bila kuinua vidole sana ili mchuzi usitiririke hadi kwenye kiwiko.

Inamisha kichwa chako kidogo na utumie kidole cha kati na cha pete kuingiza fufu na mchuzi mdomoni. Furahia kutafuna mlo wako, na bado, uwe mwangalifu kwani kwa kawaida Waghana hutia pilipili katika vyakula!

Utahitaji kurudia hatua hizo mpaka uimalize fufu yako. Ule vyakula vile vingine pia, kama vile vipande vya nyama, ukiendelea kula fufu yako. Na unaweza kumaliza kula mchuzi uliobaki kwa kutumia mkono.

Kula kwa Mikono

Waghana wengine husema kwamba wanapenda kutumia zile hisi tano za msingi wanapokula. Mtu husikia na kunusa chakula kinapopikwa. Unapokula unakiona na kuonja ladha yake. Lakini ili utumie ile hisi ya tano, ni lazima ukiguse.

Haidhuru umetoka wapi, uwe na hakika kwamba Muumba wetu, Yehova Mungu, anawapenda “watu wa namna zote.” (1 Timotheo 2:4) Hilo linawawezesha wanadamu kuwa na desturi mbalimbali zenye kupendeza. Na hata ikiwa hujazoea kula mchuzi kwa mikono, unaweza kufurahia kufanya hivyo.