Kuutazama Ulimwengu
Kuutazama Ulimwengu
Wanaogopa Watu Wasiowajua
“Zaidi ya asilimia 80 ya madereva wanawake wangependelea kulala ndani ya magari yao yaliyoharibika badala ya kukubali kusaidiwa na watu wasiowajua,” laripoti gazeti The Independent la London. Uchunguzi mmoja uliofanywa na shirika fulani kuhusu madereva 2,000, ulionyesha kwamba asilimia 83 ya wanawake na asilimia 47 ya wanaume hawawezi kukubali kusaidiwa magari yao yanapoharibika. Vivyo hivyo, madereva wengi walisema kwamba hawawezi kusimamisha gari ili kumsaidia dereva mwenye shida. Wanawake hasa huogopa kusaidia kwani wao hudhani kwamba watu hao wanasingizia kuwa magari yao yameharibika. Msemaji Nick Cole alisema: “Inahuzunisha kwamba leo madereva wengi hupendelea kuketi ndani ya magari yao usiku kucha kuliko kusaidiwa na watu wasiowajua.”
Makasisi Wasio na Imani
Makasisi wanawake katika Kanisa la Uingereza “hawaamini . . . mafundisho ya msingi ya Kikristo kwa kulinganisha na makasisi wanaume,” laripoti gazeti The Times la London. Uchunguzi uliofanywa kuhusu makasisi wapatao 2,000 wa kanisa hilo ulionyesha kwamba “asilimia 80 ya makasisi wanaume wanaamini kwamba Yesu alikufa ili kuondoa dhambi ulimwenguni,” ilhali asilimia 60 tu ya makasisi wanawake ndio wanaoamini jambo hilo. Na ijapokuwa asilimia 70 ya makasisi wanaume huamini kwamba Yesu Kristo alifufuka, asilimia 50 tu ya wanawake ndio wanaoamini jambo hilo. Robbie Low, msemaji wa shirika linaloitwa Cost of Conscience, ambalo lilidhamini uchunguzi huo, alisema: “Kanisa la Uingereza limegawanyika katika makundi mawili: Kanisa linaloamini na Kanisa lisiloamini, na hiyo ni aibu kubwa. Imani ya watu wengi wanaopewa nyadhifa za uongozi inazidi kudhoofika. Haivumiliki kuona kwamba makasisi wengi zaidi ni watu wasio na imani.”
Hawana Tumaini Licha ya Kuwa na Mali na Afya Bora
Ijapokuwa ripoti moja ilionyesha kwamba katika mwaka wa 2001 “hali za kiuchumi na za kijamii ziliboreka kwa miaka mitatu mfululizo,” bado Wakanada hawana tumaini la wakati ujao, lasema gazeti The Toronto Star. Watafiti katika taasisi moja ya maendeleo ya kijamii huko Kanada waligundua kwamba “Wakanada wana wasiwasi licha ya kuwa na mali, wanapata mfadhaiko kazini, hawana uhakika kwamba watapata huduma za kijamii wanapohitaji msaada, na wanaathiriwa zaidi na uhalifu.” Mahangaiko hayo yanatokana na “mshahara usioweza kukimu mahitaji, ongezeko la madeni, . . . foleni ndefu hospitalini, kuongezeka kwa bei za dawa, watu wengi zaidi wanajeruhiwa na misiba ya barabarani, na wanakuwa na wasiwasi mwingi kupita kiasi kwa sababu ya ongezeko la uhalifu.” Waandishi wa ripoti hiyo wanasema: “Ikiwa usalama ni kuwa na amani ya akili tu, basi hakuna maendeleo yoyote ambayo tumefanya.”
Je, Idadi ya Vifo Imepungua?
Nchini Marekani, “maendeleo ambayo yamefanywa katika utunzaji wa dharura katika miaka 40 iliyopita yamepunguza idadi ya vifo vya watu wanaoshambuliwa,” yasema ripoti moja ya shirika la Associated Press. Watafiti waligundua kwamba kati ya mwaka wa 1960 na 1999, idadi ya vifo vya watu walioshambuliwa na wahalifu nchini humo vilipungua kwa asilimia 70 hivi, hata ingawa visa vya uhalifu viliongezeka mara sita zaidi katika kipindi hichohicho. Uchunguzi huo pia ulionyesha kwamba mnamo mwaka wa 1960, asilimia 5.6 ya watu walioshambuliwa walikufa, lakini katika mwaka wa 1999 ni asilimia 1.7 tu waliokufa. Watafiti wanasema kwamba maendeleo ya kitiba ambayo yamepunguza idadi ya vifo yanatia ndani “maendeleo katika huduma za dharura, kuwasaidia na kuwasafirisha haraka watu waliopatwa na tukio la kutisha, mafunzo bora yanayotolewa kwa watu wanaotoa huduma za dharura, na kuongezeka kwa hospitali na vituo vinavyowasaidia watu hao,” yasema ripoti hiyo. Profesa Anthony Harris, wa Chuo Kikuu cha Massachusetts huko Amherst, alisema: “Leo watu wanatibiwa na kuruhusiwa kuenda nyumbani baada ya siku chache tu, lakini miaka 20 iliyopita watu wenye matatizo hayohayo walikuwa wakifa tu.”
Kuendesha Mitambo Kutoka Mbali na Ongezeko la Joto
Australia ndiyo nchi inayotokeza gesi nyingi zaidi zinazoongeza joto la dunia kwa kulinganisha na idadi ya watu, laripoti gazeti The Sydney Morning Herald. Tatizo hilo linasababishwa hasa na “utumizi wenye kupita kiasi wa vifaa vya kuendesha mitambo kutoka mbali nchini Australia.” Vifaa hivyo vinachangiaje ongezeko la gesi hizo? Ili vifaa hivyo vifanye kazi inabidi televisheni, mashine za kucheza video, na mitambo mingine ya elektroni isizimwe kabisa. Hivyo, kila mwaka tani milioni tano zaidi za gesi ya kaboni dioksidi hutolewa na mitambo ya kutokeza nguvu za umeme. Hiyo inamaanisha kwamba nguvu za umeme zinazohitajiwa nchini Australia ili kuendesha vifaa vya umeme wakati ambapo havijazimwa kabisa hutokeza kiwango kilekile cha gesi kinachotolewa na magari milioni moja. Gazeti hilo lilieleza hivi kuhusu gharama ya matumizi hayo: “Mnamo mwaka wa 2000, vifaa vya elektroni ambavyo havikuzimwa kabisa vilitumia asilimia 11.6 ya nguvu zote za umeme zilizotumiwa nyumbani, na hilo lilisababisha gharama ya dola milioni 500 za Marekani.”
Je, Hii Ni “Enzi ya Titani”?
Titani ni chuma chepesi, chenye nguvu, na hakishiki kutu kwa urahisi. Wanasayansi waliyeyusha chuma hicho kwa mara ya kwanza mnamo mwaka wa 1910. Kwa kuwa titani inadumu kwa muda mrefu inatumiwa kuunda ndege na katika tiba. Titani inaweza kutumiwa kutengeneza mifupa bandia mwilini mwa mwanadamu kwani mara nyingi haisababishi uvimbe. Mwakilishi wa Chama cha Titani cha Japan alisema: “Kwa kuwa titani haishiki kutu kwa urahisi, vifaa vilivyotengenezwa kwa titani havihitaji kusafishwa mara nyingi, na chuma hicho kinaweza kutumiwa zaidi ya mara moja. Kulingana na wanamazingira, titani ndicho chuma kitakachotumiwa sana katika karne ya 21.” Tatizo moja tu ni kwamba bei ya chuma hicho ni mara kumi zaidi ya chuma cha pua. Lakini, inatarajiwa kwamba bei ya titani itashuka kadiri inavyotumiwa zaidi. Kulingana na gazeti Daily Yomiuri la Japan, “zamani watu walitumia shaba-nyekundu, halafu wakatumia chuma, kisha wakatumia alumini. Yaonekana karne ya 21 itakuwa enzi ya titani.”
Hawajatayarishwa Vizuri kwa Ajili ya Ndoa
Gazeti Daily News la New York linaripoti kwamba zaidi ya asilimia 40 ya wenzi walioishi pamoja kabla ya kufunga ndoa hutalikiana kabla hawajamaliza miaka kumi ya ndoa. Takwimu zilizokusanywa na kituo fulani pia zinaonyesha kwamba kuna uwezekano maradufu kwamba wenzi walioishi pamoja kabla ya ndoa na ambao huendelea kuishi pamoja kwa zaidi ya miaka kumi baada ya kufunga ndoa watatalikiana. Matthew Bramlett, aliyeongoza utafiti huo anasema hivi: “Ikiwa watu wawili wanaopanga kufunga ndoa wanaonelea kwamba haifai kuishi pamoja kabla ya ndoa, basi kuna uwezekano mkubwa kuwa hawatatalikiana.” Isitoshe, watu wanaoishi pamoja kabla ya ndoa “huelekea zaidi kutovumilia magumu ya ndoa,” asema mshauri wa ndoa Alice Stephens.
Kutafuta Dini
“Zamani ilisemwa kwamba Mmethodisti habadili dini yake kamwe. Lakini mambo yamebadilika,” kulingana na gazeti The Sacramento Bee. Dexter McNamara, mkurugenzi wa shirika fulani la kidini huko Sacramento, anasema kwamba “siku hizi watu hawashikilii sana dini zao . . . Watu wanataka kujaribu dini mbalimbali.” Watu wanapotafuta dini, wao hufikiria mambo kama muziki, namna ya kuabudu, urefu wa vipindi vya ibada, vyama vya vijana, idadi ya waumini, na umbali kutoka wanapoishi. Allan Carlson, mkurugenzi wa Kituo cha Howard cha Familia, Dini na Jamii anasema: ‘Dini ni kama biashara. Katika mwaka wa 1950, asilimia 85 ya watu wazima walikuwa katika dini ya wazazi wao,’ lakini leo ‘wako katika dini tofauti-tofauti.’