Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Paniolo Wachungaji wa Ng’ombe wa Hawaii

Paniolo Wachungaji wa Ng’ombe wa Hawaii

Paniolo Wachungaji wa Ng’ombe wa Hawaii

Na mwandishi wa Amkeni! nchini Hawaii

WAGENI wengi wanaotembelea Visiwa vya Hawaii hushangaa wanapogundua kwamba watu hufuga ng’ombe huku, hasa katika Kisiwa Kikubwa kinachoitwa Hawaii. Ingawa wageni wanajua kwamba kulikuwa na mashamba ya miwa, mananasi, na kahawa kutoka Kona, wao hushangaa sana wanapowaona wachungaji wa ng’ombe wanaoitwa paniolo. Wao huuliza, “Wachungaji hao na ng’ombe hao walifikaje huku Hawaii?”

Jinsi Ng’ombe Walivyofika Huku

Ng’ombe waliletwa huku Hawaii mnamo mwaka wa 1793 na George Vancouver, nahodha Mwingereza aliyekuwa pia mvumbuzi, wakiwa zawadi kwa Mfalme Kamehameha wa Kwanza. Hiyo haikuwa mara ya kwanza kwa Nahodha Vancouver kufika kwenye Visiwa vya Hawaii, kwani hapo awali yeye na Nahodha James Cook, aliyekuwa mvumbuzi mashuhuri wa Uingereza, walikuwa Wazungu wa kwanza kutembelea visiwa hivyo.

Mfalme alikubali zawadi hiyo na alifurahi sana Vancouver aliporudi mwaka uliofuata, akiwa na ng’ombe na kondoo zaidi. Vancouver alitarajia ng’ombe hao wangezaana na kuongezeka na kuongeza mapato ya wenyeji wa visiwa hivyo, vilivyoitwa Visiwa vya Sandwich wakati huo. Ili waongezeke haraka, alimshauri Mfalme Kamehameha atunge sheria ambayo ingewazuia wenyeji kuwachinja wanyama hao. Mfalme alitambua umuhimu wa kufanya hivyo, na akatunga sheria ambayo ilidumu kwa muda wa miaka kumi.

Ng’ombe Wawa Wasumbufu

Vancouver alileta ng’ombe wenye pembe ndefu kutoka California. (Ona picha kwenye ukurasa wa 18.) Ng’ombe hao walikuwa wakubwa na wenye kutisha na kulikuwa na nafasi kubwa sana katikati ya pembe zao mbili. Wahawaii waliwaita ng’ombe hao nguruwe na hawakuwadhuru kwa sababu ya sheria iliyokuwepo. Ng’ombe hao waliachiliwa wakazurura kila mahali na kuongezeka sana.

Punde si punde ng’ombe hao wakawa wasumbufu! Kwa kuwa walitangatanga huku na huku na hawakuwindwa, walianza kuharibu misitu ya maeneo ya milimani, na walilisha kwenye mashamba yaliyokuwa karibu na bahari, ambako wenyeji walipanda viazi vitamu, viazi vikuu, miyugwa, na mimea mingine. Viumbe hao wenye nguvu, wakali, na wakakamavu hawangezuiwa na nyua za mawe wala za mipungate.

Mnamo mwaka wa 1815, John Palmer Parker, mwanamume mjasiri kutoka New England, aliruhusiwa na Mfalme Kamehameha wa Kwanza kutumia bunduki yake mpya iliyoundwa nchini Marekani kuwaua baadhi ya ng’ombe hao waliokuwa wameongezeka na kuwa wasumbufu kwenye Kisiwa Kikubwa. Mfalme huyo mwenye busara alitambua umuhimu wa nyama, mafuta, na ngozi ya ng’ombe hao. Hivyo, nyama ya ng’ombe iliyotiwa chumvi ikawa bidhaa muhimu ya kibiashara katika Kisiwa Kikubwa, na muda si muda ilileta mapato mengi kuliko mbao za msandali ambazo hapo awali zilikuwa zinaingiza mapato mengi zaidi.

Zamani Paniolo Waliitwa Vaquero

Mapema katika miaka ya 1830, ng’ombe hao walikuwa wameongezeka sana na walikuwa hatari, hivyo ilibidi hatua fulani ichukuliwe. Mfalme Kamehameha wa Tatu aliona uhitaji wa kuwadhibiti wanyama hao. Kwa hiyo, alimtuma chifu mkuu huko California, ambayo ilikuwa chini ya Mexico wakati huo, ili awatafute watu wenye ustadi wa kuchunga ng’ombe. Kazi yao ingekuwa kuwakusanya ng’ombe hao na kuwazoeza Wahawaii kufanya kazi hiyo. Kufikia wakati huo, wanyama hao walikuwa wamesambaa hadi nje ya Kisiwa Kikubwa na kufika Oahu, Maui, na Kauai.

Mnamo mwaka wa 1832, wachungaji Wahispania, Wameksiko, na Wahindi waliwasili Hawaii. Walikuwa wenye kuvutia, stadi, na walikuwa wamezoezwa katika mashamba makubwa huko Mexico. Walikuwa na kofia kubwa, matandiko ya farasi, kamba, na vichokoo na walibandikwa jina paniolo kwa sababu walitoka Hispania, yaani kutoka utamaduni wa español. Jina hilo linaendelea kutumiwa hadi leo.

Paniolo walifanya kazi kwa bidii, walipenda raha, na hawakufurahishwa na kazi yao tu, bali pia walipenda kuimba na kucheza ala za muziki. Walikuwa stadi wa kazi, wajasiri, wakakamavu, wenye nguvu, na waliionea fahari kazi yao. Paniolo mmoja ambaye amefanya kazi hiyo kwa muda mrefu alisema hivi: “Ukifanya kazi kwa bidii, utaishi kwa muda mrefu.” Ama kweli, paniolo walifanya kazi kwa bidii! Kila siku walifanya kazi kwa saa nyingi kuanzia mapambazuko hadi giza lilipoingia. Walikusanya ng’ombe, wakawatenganisha katika makundi mbalimbali, wakawafunga kwa kamba, na kuwatia alama kwenye ngozi. Pia, walitengeneza nyua na kuzitunza kwa kuwa sasa ng’ombe walikuwa wamefugwa.

Hata hivyo, wachungaji hao hawangeweza kufanya kazi vizuri bila farasi. Mnamo mwaka wa 1803, Richard J. Cleveland alileta farasi kwa mara ya kwanza huku Hawaii kwa meli iliyoitwa Lelia Byrd. Farasi hao walikuwa wametoka Uarabuni, na Mfalme Kamehameha wa Kwanza ndiye aliyekuwa Mhawaii wa kwanza kupanda farasi katika visiwa hivyo!

Farasi hao walikuwa wepesi, walienda kasi, na walizoea haraka eneo hilo lenye mabonde na milima. Wachungaji hao walitumia farasi sana katika kazi yao ngumu ya kutunza na kufuga ng’ombe.

Mwanzoni, farasi wengine walizurura-zurura kama wale ng’ombe, na baada ya muda, walijamiiana na farasi wengine kutoka Uingereza, Marekani, na Uarabuni. Walitokeza farasi wa aina mbalimbali wenye kupendeza, ambao walitumiwa na paniolo. Ukimwuliza paniolo wa kisasa ni farasi yupi anayependelea kwa ajili ya mashindano, huenda atakuambia anapendelea farasi aina ya quarter. Kwa nini? Kwa sababu farasi huyo hutii maagizo haraka wakati wa kuanza na kumaliza mashindano, na hivyo hawezi kushindwa kamwe.

Mashindano ya Farasi ya Ulimwengu

Paniolo wa Hawaii ni stadi kama wachungaji wengine kwa kuendesha farasi, kuwafunga ng’ombe kamba, na kushindana. Wao ni mashuhuri hivi kwamba katika mwaka wa 1908 baadhi yao, kutia ndani Ikua (Ike) Purdy na Archie Ka‘au‘a, walishiriki mashindano makubwa zaidi ya farasi nchini Marekani. Hayo yalikuwa mashindano yenye fahari sana ya Frontier Days yaliyofanyika huko Cheyenne, Wyoming.

Paniolo hao waliwavutia mashabiki wa mashindano hayo huko Ulaya na Marekani kwa sababu ya mavazi yao maridadi, umachachari wao, na mashada yao. Walivutia kwelikweli! Ike Purdy akawa bingwa wa ulimwengu wa mashindano ya farasi na Archie pia akafanya vyema kwenye mashindano hayo. Watu wote ulimwenguni walistaajabishwa na paniolo hao wenye kuvutia ambao walifanya visiwa vya Hawaii viwe maarufu. Baadaye, katika mwaka wa 1996, Ike Purdy alikuwa miongoni mwa watu waliotunukiwa heshima ya mabingwa wa mashindano ya farasi.

Maisha ya Paniolo Leo

Paniolo huishije leo? Ingawa huenda maisha yao si magumu sana kama zamani, bado wana kazi nyingi ya kufanya katika mashamba ya kisasa ya ng’ombe. Mfano mmoja wa mashamba hayo ni Shamba la Parker huko Waimea katika Kisiwa Kikubwa. Shamba hilo ni kubwa sana, limezungushiwa ua wenye urefu wa kilometa nyingi na lina maelfu ya ng’ombe. Paniolo hufanya kazi nyingi mbalimbali leo. Wakiwa na farasi wao, wao hupeleka ng’ombe kulisha katika maeneo mbalimbali.

Leo unapoenda huko Waimea, utawakuta paniolo wakipumzika kwenye mkahawa, wakiwa wamevalia jinzi za buluu, buti za wapanda-farasi, kofia kubwa, na huenda pia kofia hiyo ikawa na shada linaloizunguka. Pia, wao husikiliza muziki maarufu unaochezwa kwa gita au huimba mojawapo ya nyimbo za zamani za Kihawaii!

[Picha katika ukurasa wa 17]

Mfalme Kamehameha wa Kwanza

[Picha katika ukurasa wa 18]

Kutia ng’ombe alama

[Picha katika ukurasa wa 18]

Ng’ombe mwenye pembe kubwa

[Picha katika ukurasa wa 18]

Kushoto hadi kulia: Archie Ka‘au‘a, Eben Low, na Ike Purdy

[Hisani]

Paniolo Preservation Society/Dr. Billy Bergin

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 16]

Hawaiian Islands: Mountain High Maps® Copyright © 1997 Digital Wisdom, Inc.

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 17]

Parker Ranch/John Russell

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 18]

Parker Ranch/John Russell ▼