Maisha ya Utotoni Yanapoharakishwa
Maisha ya Utotoni Yanapoharakishwa
NDEGE ndogo yenye injini moja ilipita kasi kwenye barabara ya uwanja wa ndege na kuanza kupaa chini ya anga lenye mawingu meusi. Waandishi wa habari walikuwepo kunasa tukio hilo na kupiga picha, huku wakiuliza maswali na kustaajabu sana. Kwa nini wakastaajabu? Si kwa sababu ya rubani aliyekuwa ndani ya ndege hiyo wala abiria mwanamume aliyekuwepo, bali ni kwa sababu ya binti ya abiria huyo. Msichana huyo alikuwa na umri wa miaka saba.
Msichana huyo alikuwa aendeshe ndege hiyo. Angekuwa mtu mwenye umri mdogo zaidi kuwahi kuendesha ndege nchini Marekani. Waandishi wa habari walikuwa na shughuli nyingi kwani wangeisubiri ndege hiyo mahali ambapo ingetua. Ijapokuwa kulikuwa na mawingu meusi, watu hao watatu waliipanda ndege hiyo. Msichana huyo alikalia mto ili aweze kuona mbele na aliwekewa vifaa vya kukanyagia vilivyomsaidia kufikia pedali.
Kwa kusikitisha, safari yao ilikuwa fupi sana. Kwa ghafula, ndege hiyo ikaanza kuyumbayumba, ikashindwa kusonga mbele na ikaanguka kwa sababu ya dhoruba kali, na wote watatu wakafa. Waandishi wa habari waliripoti kisa hicho upesi. Badala ya kutangaza habari njema zilizokuwa zikitarajiwa, waliripoti habari zenye kuhuzunisha. Hata waandishi wachache wa habari waliona ni kana kwamba waandishi wenzao wamechangia mkasa huo. Watu wengi walianza kusema kwamba watoto hawapaswi kuruhusiwa kuendesha ndege. Nchini Marekani, sheria zilitungwa ili kutekeleza jambo hilo. Ijapokuwa watu walikuwa na huzuni nyingi na walitoa masuluhisho ya muda mfupi, bado masuala makubwa yalihusika.
Tukio hilo liliwafanya wengi wafikirie mwelekeo ambao watu wanao siku hizi. Watoto wachanga sana wanapewa madaraka ya watu wazima. Huenda matokeo yasije ghafula sikuzote au yawe mabaya sana. Hata hivyo, huenda yakawa mazito na yakadumu kwa muda mrefu. Hebu tuchunguze mambo machache yanayoonyesha jinsi ambavyo maisha ya utotoni yanaweza kuharakishwa.
Wanaelimishwa Haraka-Haraka
Ni kawaida kwa wazazi kutamani watoto wao wafanikiwe maishani. Lakini wanapohangaikia jambo hilo kupita kiasi, huenda wakawalemea watoto wao wachanga mno. Hata wanaweza kuwa na nia nzuri wanapofanya hivyo. Kwa mfano, siku hizi wazazi wengi wanawaandikisha watoto wao kwenye shughuli za baada ya shule, kama vile michezo, muziki, au kucheza dansi. Wengi wanawapeleka watoto wao kwenye mafunzo ya ziada.
Bila shaka si vibaya kuwatia moyo watoto wakuze uwezo au mapendezi yao. Hata hivyo, hatari hutokea mambo hayo yanapofanywa kupita kiasi, hasa watoto wanapokuwa na mahangaiko mengi kama watu wazima. Gazeti Time lasema hivi: “Ingawa zamani watoto walifurahia maisha yao ya utotoni, siku hizi wanalemewa na masomo; watoto ambao wanapaswa kutumia nguvu zao za ujana kwa uhuru, sasa wanafanya kazi kama siafu.”
Wazazi wengine hutarajia watoto wao wawe mabingwa wa riadha, muziki, au wa sarakasi. Hata kabla watoto wao hawajazaliwa, wazazi wanawaandikisha katika shule, ili wafanikiwe wakati ujao. Isitoshe, akina mama wengine hujiandikisha kwenye “vyuo vikuu vya wanawake wajawazito” ili vijusi visomeshwe muziki vikiwa vingali tumboni. Wanafanya hivyo ili kuchemsha bongo za watoto wao zinazokua.
Katika nchi fulani, watoto wanapewa mitihani ya kusoma na ya hesabu kabla hawajafikisha umri wa miaka sita. Mambo hayo yamezusha maswali fulani kuhusu afya ya kihisia ya mtoto. Kwa mfano, vipi mtoto akianguka mtihani akiwa kwenye shule ya watoto wadogo? David Elkind, mwandishi wa kitabu The Hurried Child, asema kwamba shule zinaamua mapema mno jinsi maisha ya watoto yatakavyokuwa. Elkind anasema wao hufanya hivyo kwa sababu wanataka shule zao zionekane kuwa bora badala ya kuwaelimisha watoto hao vizuri.
Je, watoto wanaathiriwa kwa njia yoyote wanapolazimishwa kufanya mambo ya watu wazima wakiwa bado wachanga mno? Elkind analalamika kwamba jamii inawaona watoto kuwa watu wazima wanaoweza kubeba majukumu mazito. Anasema: “Inaonyesha tunaona kwamba
mwelekeo wa kuwalemea vijana na mambo mengi ni jambo la ‘kawaida.’” Kwa kweli, maoni ya watu kuhusu mambo yaliyo ya kawaida kwa watoto yanabadilika.Wanaharakisha Kuwa Mabingwa
Yaelekea wazazi wengi wanaona kuwa ni jambo la kawaida, ama hata linalofaa, kuwafundisha watoto kwamba kuwa bingwa ndilo jambo la maana zaidi, hasa michezoni. Leo watoto wengi wanawekewa miradi ya kushinda medali katika michezo ya Olimpiki. Ili wapate sifa ya kuwa mabingwa kwa muda mfupi na kuhakikisha kwamba watachuma mapato mazuri wanapokuwa watu wazima, watoto fulani hulazimishwa kufanya mambo ambayo huwazuia kufurahia maisha yao ya utotoni.
Kwa mfano, wanasarakasi wa kike huanza kufanya mazoezi mapema sana. Mazoezi hayo ya kuendelea huwa mazito sana na hufanya miili yao michanga iwe na mkazo mwingi sana. Kwa muda wa miaka mingi, wao hujitayarisha kiakili na kimwili kwa ajili ya michezo ya Olimpiki. Ukweli wa mambo ni kwamba ni wachache tu ndio hushinda. Je, kweli wale walioshindwa watahisi kwamba ilifaa wajinyime maisha yao ya utotoni? Baada ya muda fulani, hata washindi hujiuliza kama kweli walistahili kufanya jitihada hizo zote ili washinde tu.
Hisia za wasichana hao wachanga huathiriwa pia kwani maisha yao ya utotoni huharakishwa wanapochochewa sana kuwa mabingwa. Mazoezi hayo mazito huenda yakaathiri ukuzi wao wa kimwili. Mifupa ya wengine hukosa kukua vizuri. Wengine hupata matatizo ya ulaji. Baadhi yao huchelewa kubalehe, hata kwa miaka kadhaa. Hata hivyo, wasichana wengi leo huwa na tatizo tofauti kabisa: kubalehe mapema.—Ona sanduku lililo juu.
Ni Matajiri Lakini Hawafurahii Maisha ya Utotoni
Ni kana kwamba vyombo vya habari vinataka tuamini kwamba ili mtu afurahie maisha yake ya utotoni, ni lazima aishi maisha ya starehe. Wazazi wengine hufanya kazi kwa bidii sana ili waweze kuwanunulia watoto wao vitu vya kuwastarehesha, kama nyumba nzuri, kuwaandalia burudani za kila aina, na mavazi ya bei ghali.
Hata hivyo, watoto wengi waliolelewa kwa njia hiyo, hujiingiza katika unywaji wa kupindukia, hutumia dawa za kulevya, na huwa waasi na hukosa furaha. Kwa nini? Wengi huwa na hasira mno kwa kuwa wanahisi wamepuuzwa. Watoto wanahitaji wazazi wanaowapenda na kuwatunza. Wazazi wenye shughuli nyingi ambao hawana nafasi ya kuwapenda na kuwatunza watoto huamini kwamba wakifanya kazi kwa bidii watawafanya watoto
wao wafurahi, lakini matokeo huwa kinyume kabisa.Dakt. Judith Paphazy anasema kuhusu “wazazi wanaofanya kazi, na walio matajiri,” ambao mara nyingi “huwapa watoto wao vitu vingi kwa kuwa wanatambua kwamba familia zao zinaathiriwa kwa sababu wanatumia wakati mwingi sana kazini.” Anaonelea kwamba wazazi hao “wanaepa daraka lao kwa kuwanunulia vitu.”
Watoto ndio huathiriwa zaidi. Ingawa wana vitu vingi vya starehe, wanakosa mambo muhimu ambayo yangefanya maisha yao ya utotoni yafurahishe: kupendwa na wazazi na kutumia wakati pamoja nao. Kwa sababu ya kukosa mwongozo, nidhamu, na mwelekezo, wao hukabili masuala magumu ya watu wazima mapema mno, kabla hawajawa tayari kama vile, ‘Je, nitumie dawa za kulevya? Nifanye ngono? Niwe mjeuri ninapokasirika?’ Huenda wakatafuta majibu yao wenyewe kutoka kwa marafiki, kwenye televisheni, au katika sinema. Mara nyingi matokeo huwa ni maisha mafupi ya utotoni, labda hata yenye kuhuzunisha.
Mtoto Anapolazimika Kuwa Yule Mzazi Mwingine
Familia yenye wazazi wote wawili inapobadilika ghafula na kuwa familia ya mzazi mmoja kwa sababu ya kifo, kutengana, au talaka, mara nyingi hisia za watoto huumia. Bila shaka, familia nyingi za mzazi mmoja hufaulu sana. Lakini katika familia nyingine, maisha ya utotoni huharakishwa.
Mara kwa mara, huenda mzazi aliye peke yake akahisi upweke. Hata hivyo, wazazi wengine humfanya mtoto, hasa yule mkubwa, achukue daraka la yule mzazi mwingine. Labda akihisi mambo yamemlemea, mzazi anaweza kumwambia mwanawe au binti yake kuhusu matatizo ambayo mtoto huyo mchanga hayawezi. Wazazi wengine huenda wakawalemea watoto kihisia.
Wazazi wengine huachilia madaraka yao, huku wakimlazimisha mtoto achukue daraka la yule mzazi mwingine kabisa. Carmen na dada yake, waliotajwa awali, walipatwa na jambo hilo walipoamua kuishi barabarani. Wakiwa wangali watoto, walipewa daraka la kuwatunza wale watoto wengine wadogo. Huo ulikuwa mzigo mkubwa sana.
Ama kwa hakika, kuharakisha maisha ya watoto ni hatari, na ni jambo linalopaswa kuepukwa ikiwezekana. Lakini, kuna habari njema: Wazazi wanaweza kuchukua hatua zinazofaa ili kuhakikisha kwamba watoto wao wanafurahia maisha yao ya utotoni. Ni hatua gani hizo? Acheni tuchunguze baadhi ya hatua ambazo zimethibitika kuwa na matokeo.
[Sanduku katika ukurasa wa 6]
Matatizo ya Kubalehe Mapema
Je, wasichana wanabalehe mapema siku hizi? Wanasayansi wanatofautiana kuhusu jambo hilo. Wengine wanasema kwamba katikati ya karne ya 19, kwa wastani, wasichana walibalehe kuanzia umri wa miaka 17, ilihali leo wanabalehe kabla hawajafikisha miaka 13. Uchunguzi uliofanywa katika mwaka wa 1997 wa wasichana 17,000, ulionyesha kwamba karibu asilimia 15 ya wasichana Wazungu na asilimia 50 ya wasichana Wamarekani wenye asili ya Kiafrika nchini Marekani huonyesha dalili za kubalehe mapema wakiwa na umri wa miaka minane! Hata hivyo, baadhi ya madaktari wanapinga matokeo hayo na kuwaonya wazazi wasione dalili za mapema sana za kubalehe kuwa jambo la “kawaida.”
Vyovyote vile, hali hiyo inatokeza magumu kwa wazazi na watoto. Gazeti la Time linasema: “Mbali na mabadiliko ya kimwili, tatizo kubwa zaidi ni madhara ya kiakili yanayowapata watoto wadogo sana wanaobalehe mapema, ambao husumbuliwa na wanaume. . . . Wakati wao wa utotoni ni mfupi mno.” Makala hiyo inazusha swali hili tata: “Wasichana wadogo wanapokuwa na miili kama ya watu wazima kabla hawajakomaa kihisia na kiakili, watapatwa na nini?”
Mara nyingi wao husumbuliwa kingono. Mama mmoja anasema hivi waziwazi: “Wasichana wenye miili mikubwa kwa sababu ya kubalehe mapema ni kama asali [kwa nyuki]. Wao huwavutia wavulana wenye umri mkubwa zaidi.” Mtoto mdogo anapochochewa kufanya ngono, matokeo huwa mabaya. Msichana mdogo anaweza kujihisi hafai kitu. Anaweza kuwa na dhamiri mbaya na afya yake ya kimwili na ya kihisia kuathiriwa.
[Picha katika ukurasa wa 5]
Kumpangia mtoto shughuli nyingi kwaweza kusababisha matatizo
[Picha katika ukurasa wa 7]
Kuwachochea watoto wawe washindani sana huwafanya wasifurahie michezo
[Picha katika ukurasa wa 7]
Vitu vya kimwili haviwezi kuchukua nafasi ya malezi mazuri