Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Njugu Ni Mbegu Ndogo Inayopendwa Ulimwenguni Pote

Njugu Ni Mbegu Ndogo Inayopendwa Ulimwenguni Pote

Njugu Ni Mbegu Ndogo Inayopendwa Ulimwenguni Pote

Je, unapenda njugu? Ikiwa ndivyo, si wewe peke yako unayezipenda. Njugu zinapendwa na watu wengi. China na India, mataifa yenye watu wengi zaidi duniani, huzalisha zaidi ya nusu ya njugu zinazozalishwa ulimwenguni.

Marekani huvuna zaidi ya kilogramu bilioni moja za njugu kila mwaka. Hivyo, nchi hiyo huzalisha asilimia 10 hivi ya njugu zote zinazozalishwa ulimwenguni. Nchi nyingine zinazozalisha njugu kwa wingi ni Afrika Kusini, Argentina, Brazili, Malawi, Nigeria, Senegal, na Sudan. Njugu ilipataje kuwa maarufu? Je, nyakati nyingine inafaa kuepuka kula njugu?

Historia Ndefu ya Njugu

Inadhaniwa kwamba njugu zilitoka Amerika Kusini. Uthibitisho mmoja wa kale zaidi ambao unaonyesha kwamba watu wanapenda njugu uligunduliwa huko Peru. Chombo cha kuwekea maua kilichoundwa kabla ya kipindi cha Columbus kiligunduliwa huko. Chombo hicho kina umbo la njugu na kimepambwa kwa maumbo ya njugu. Wavumbuzi Wahispania ambao waliona njugu kwa mara ya kwanza huko Amerika Kusini, waliona zinafaa sana kuwa chakula bora kwa ajili ya safari zao. Walirudi Ulaya na njugu kadhaa. Wazungu walitumia njugu kwa njia nyingine, hata wakazitumia badala ya mbegu za kahawa.

Baadaye, Wareno walileta njugu huku Afrika. Wenyeji wa Afrika walitambua upesi kwamba njugu ni zao bora la chakula ambalo lingesitawi katika udongo usio na rutuba. Isitoshe, mmea wa njugu ulirutubisha udongo kwa nitrojeni. Hatimaye, njugu ilisafirishwa kutoka Afrika hadi Amerika Kaskazini wakati wa biashara ya watumwa.

Katika miaka ya 1530, Wareno walipeleka njugu huko India na Macao, na Wahispania wakaipeleka Ufilipino. Kisha, wafanyabiashara waliinunua kutoka katika nchi hizo na kuipeleka China. Ilidhaniwa kwamba zao la njugu lingeisaidia nchi ya China kukabiliana na baa la njaa.

Wataalamu wa mimea katika miaka ya 1700 walifanya utafiti kuhusu njugu, ambazo waliziita choroko za ardhini, na wakaona kwamba zingekuwa chakula kizuri cha nguruwe. Kufikia mwanzoni mwa miaka ya 1800, kilimo cha njugu kilikuwa kikiendelea huko South Carolina, Marekani. Njugu zilitumiwa kuwalisha maaskari waliokuwa wakipigana wakati wa Vita ya Wenyewe kwa Wenyewe ya Marekani, ambayo ilianza mwaka wa 1861.

Hata hivyo, watu wengi wakati huo waliona njugu kuwa chakula cha maskini. Huenda hiyo ndiyo sababu wakulima Wamarekani wa wakati huo hawakuzalisha njugu kwa wingi. Zaidi ya hayo, kabla ya mwaka wa 1900, wakati ambapo mashine za kilimo zilianza kuvumbuliwa, ilikuwa kazi ngumu sana kusitawisha njugu.

Lakini kufikia mwaka wa 1903, Mmarekani George Washington Carver, mmojawapo wa wanakemia wa kwanza wa kilimo, alikuwa ameanza kufanya utafiti kuhusu matumizi mapya ya mmea wa njugu. Muda si muda akatengeneza zaidi ya bidhaa 300 kutokana na njugu. Bidhaa hizo zilitia ndani vinywaji, vipodozi, rangi, dawa, sabuni, dawa za kuua wadudu, na wino wa kuchapia. Carver aliwatia moyo wakulima wa nchi hiyo waache zoea la kupanda pamba tu na badala yake wapande mimea ya njugu pia katikati ya mimea ya pamba ili udongo usidhoofike. Wakati huo, mdudu fulani wa jamii ya fukusi alikuwa akiharibu mimea ya pamba, na wakulima wengi walilazimika kufuata mashauri ya Carver. Ikawaje? Mimea ya njugu ilinawiri sana hivi kwamba ikawa zao kuu kusini mwa Marekani. Hivi leo kuna mnara wa ukumbusho kwa ajili ya Carver huko Dothan, Alabama. Na mnara wa ukumbusho wa mdudu huyo mharibifu umechongwa katika mji wa Enterprise, Alabama, kwani uvamizi wake ndio uliowachochea wakulima wapande njugu.

Kilimo cha Njugu

Njugu ni mbegu za mmea wa njugu. Mmea huo unapoendelea kusitawi huwa unachanua maua ya manjano ambayo hujichavusha yenyewe.

Ovari iliyotiwa mbegu ya kiume ambayo iko kwenye ncha ya shina ya mmea huo huanza kuingia udongoni. Ovari hiyo huwa na mbegu. Mbegu hiyo inapoingia udongoni, hukua sambamba na udongo wa juu, halafu inakomaa ikielekea chini. Kisha mbegu hiyo inakuwa njugu. Mmea mmoja unaweza kuwa na njugu 40.

Njugu husitawi vizuri katika maeneo yenye joto na mvua ya wastani. Kuna kipindi cha siku 120 au 160 kati ya wakati wa kupanda na kuvuna, ikitegemea aina ya njugu na hali ya hewa. Wakati wa kuvuna, ni lazima wakulima wa njugu wachimbue mimea hiyo na kuipindua, halafu wanaiacha ikauke ili isioze wakati inapohifadhiwa. Siku hizi, wakulima wengi hutumia mashine za kilimo za kisasa zinazowawezesha kuchimbua mimea hiyo, kuikung’uta, na kuipindua kwa wakati mmoja.

Matumizi Mengi ya Njugu

Njugu ni chakula chenye virutubisho vingi sana. Njugu husaidia sana umeng’enyaji wa chakula, na zina vitamini 13 na madini 26. Vingi kati ya virutubisho hivyo havipatikani katika vyakula vya kisasa. Kitabu The Encyclopædia Britannica kinasema: “Njugu zina protini nyingi zaidi, madini mengi zaidi, na vitamini nyingi kuliko maini ya ng’ombe.” Lakini watu wanaotaka kupunguza uzito wao wanapaswa kutahadhari! Njugu zina “mafuta mengi kuliko malai nzito” na “kalori nyingi kuliko sukari.”

Njugu hutumiwa katika vyakula vingi vinavyopikwa katika nchi nyingi na ni rahisi sana kutambua ladha yake. Anya von Bremzen, mwandishi katika fani ya upishi, anasema: “Ladha ya njugu ni tamu sana na haina kifani, kwa hiyo chakula chochote kilichotiwa njugu kitakuwa na ladha kama ya njugu. Kwa hiyo, uwe ni mchuzi wa njugu wa Indonesia, supu ya Afrika Magharibi, spageti za Kichina, kitoweo cha Peru, au mkate uliopakwa siagi ya njugu, ladha ni ileile.”

Vilevile, njugu ni kitafuno kinachopendwa na wengi kotekote ulimwenguni. Kwa mfano, huko India njugu huchanganywa na maharagwe makavu na kuuzwa barabarani. Kulingana na kitabu The Great American Peanut, inasemekana kwamba siagi ya njugu, ambayo hupakwa kwenye mkate katika nchi kadhaa, “ilivumbuliwa na daktari mmoja kutoka St. Louis [Marekani] wapata mwaka wa 1890 kwa madhumuni ya kutunza afya ya watu wazee.”

Lakini mbali na kutumiwa kama chakula, njugu zina matumizi mengineyo. Katika bara lote la Asia, njugu hutumiwa kutengeneza mafuta ya kupikia. Mafuta ya njugu yanaweza kutumiwa pia kupikia vyakula vinavyohitaji kupikwa kwa moto mkali, na hayapati harufu ya vyakula vinavyopikwa.

Huko Brazili, masalio ya njugu zilizotumiwa kutengeneza mafuta ya kupikia hutumiwa kutengeneza chakula cha mifugo. Na bidhaa nyingi hutengenezwa kutokana na njugu.—Ona maelezo yaliyo juu.

Jihadhari na Mizio ya Njugu!

Njugu zinaweza kukaa kwa muda mrefu bila kuhifadhiwa kwenye friji. Hata hivyo, tunapaswa kutahadhari. Njugu ambazo zimeanza kupata kuvu zina kemikali hatari inayoitwa aflatoxin ambayo ina uwezo mkubwa wa kusababisha kansa. Isitoshe, watu wengine wana mizio ya njugu. Wanapokula njugu ‘wanaweza kutokwa na kamasi puani na kupata vipele au kuathiriwa mwili mzima (anaphylactic shock),’ lasema gazeti Prevention. Uchunguzi mbalimbali umeonyesha kwamba siku hizi watoto wengi zaidi wanapata mizio ya njugu.

Gazeti Prevention linaripoti kwamba ikiwa wazazi wote wawili wana ugonjwa wa pumu, mzio wa kupata uvimbe puani, au ukurutu, kuna uwezekano mkubwa kwamba mtoto wao atapata mzio wa njugu.

Jambo hilo pia linawahusu watoto ambao mama zao wana mizio na pia watoto wanaopata mzio wa maziwa kabla ya kufikia umri wa mwaka mmoja. Dakt. Hugh Sampson, profesa wa magonjwa ya watoto kwenye Kituo cha Kitiba cha Chuo Kikuu cha Johns Hopkins huko Marekani, anasema: “Ni afadhali wazazi wasiwape watoto wao siagi ya njugu hadi wanapofikia umri wa miaka mitatu.”

Iwe unapenda njugu au la, huenda mazungumzo haya kuhusu matumizi yake mengi yamekufanya uthamini mbegu hiyo ndogo inayopendwa na wengi.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 24]

Njugu Hutumiwa Kutengeneza Bidhaa Nyingi

• Ubao unaotumiwa kujenga ukuta

• Makaa ya kuwashia moto wa kuota

• Matandiko ya paka

• Karatasi

• Sabuni ya kufulia nguo

• Marhamu

• Dawa ya kung’arisha chuma

• Dawa ya kuondoa madoa

• Wino

• Mafuta ya ekseli

• Krimu ya kunyolea

• Krimu ya kupaka usoni

 

• Mazulia ya plastiki

• Mpira

• Vipodozi

• Rangi

• Vilipukaji

• Sabuni ya nywele

• Dawa za tiba

[Hisani]

Source: The Great American Peanut

[Mchoro/Picha katika ukurasa wa 22]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

Majani

Shina

Ardhi

Mizizi Njugu

[Hisani]

Gazeti The Peanut Farmer

[Picha katika ukurasa wa 22]

Mnara wa ukumbusho wa George Washington Carver

[Picha katika ukurasa wa 23]

Marekani

[Picha katika ukurasa wa 23]

Afrika

[Picha katika ukurasa wa 23]

Asia

[Hisani]

FAO photo/R. Faidutti

[Picha katika ukurasa wa 23]

Baadhi ya vitafuno vinavyotayarishwa kwa njugu

[Picha katika ukurasa wa 24]

Siagi ya njugu ni chakula kinachopendwa sana katika nchi kadhaa