Hekaya Iliyotia Mizizi
Hekaya Iliyotia Mizizi
NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI UFARANSA
WATOTO ulimwenguni pote wanampenda sana. Katika mwaka wa majuzi alipokea barua zipatazo 800,000 kupitia shirika la posta la Ufaransa, hasa kutoka kwa watoto wenye umri wa kati ya miaka mitatu na minane. Inaonekana sanamu ya Baba Krismasi yenye ndevu nyingi nyeupe na joho jekundu lenye mapindo ya manyoya meupe, ni mojawapo ya vitu vinavyopendwa sana katika shamrashamra za sikukuu. Basi, je, unaweza kuwazia sanamu hiyo ikiteketezwa? Ndivyo ilivyotukia miaka 50 na kitu iliyopita huko Dijon, Ufaransa. Mnamo Desemba 23, 1951, Baba Krismasi “aliuawa” mbele ya watoto 250 hivi.
Alifanya kosa gani? Gazeti France-Soir lilisema kwamba aliteketezwa “baada ya makasisi kukubaliana kwamba alikuwa amenyakua cheo cha Kristo na alikuwa mwasi” na walimshutumu kwa “kufanya sherehe za Krismasi ziwe za kipagani.” Tangazo moja lilisema kwamba tendo hilo lilikuwa na maana fulani. “Uwongo hauwezi kuwafanya watoto wavutiwe na dini na si njia ya kuelimisha kamwe.”
Viongozi fulani wa dini walisema kuwa desturi zinazohusiana na Baba Krismasi zinawapotosha watu kutoka kwa “maana halisi ya Kikristo” ya kuzaliwa kwa Yesu. Na hata mtaalamu wa utamaduni, Claude Lévi-Strauss, alisema katika gazeti la Les Temps Modernes (Nyakati za Kisasa) kwamba imani ya Baba Krismasi ni “mojawapo ya mambo yanayofanya watu wengi wapende upagani leo.” Alisema pia kwamba dini ilikuwa na haki ya kuishutumu imani hiyo. Lévi-Strauss pia alionelea kuwa huenda imani ya Baba Krismasi ilianza zamani za kale wakati wa mfalme wa mungu-jua. Sikukuu ya mungu-jua ilisherehekewa katika Roma ya kale kuanzia Desemba 17 hadi 24. Wakati huo majengo yalipambwa kwa majani mabichi na watu walipeana zawadi. Sikukuu ya mungu-jua ilikuwa na shamrashamra kama za Krismasi.
Leo, zaidi ya miaka 50 tangu sanamu ya Baba Krismasi ilipoteketezwa, Wakatoliki nchini Ufaransa wana maoni gani kuhusu Baba Krismasi? Imani hiyo iliyoanza wakati wa sikukuu ya Roma ya Mungu-jua bado inatumiwa sana wakati wa Krismasi kama sanamu ya Yesu akiwa katika hori la ng’ombe. Pindi kwa pindi, makasisi hudai kwamba Baba Krismasi huwakilisha shughuli ya kibiashara ambayo huwafanya watu wamsahau Kristo wakati wa Krismasi. Hata hivyo, watu wanampenda sana Baba Krismasi hivi kwamba wamepuuza chanzo chake cha kipagani.
[Picha katika ukurasa wa 13]
DR/© Cliché Bibliothèque nationale de France, Paris