Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kutoka kwa Wasomaji Wetu

Kutoka kwa Wasomaji Wetu

Kutoka kwa Wasomaji Wetu

Vijana Huuliza Asanteni sana kwa makala “Vijana Huuliza . . . Mbona Mzazi Wangu Hanipendi?” (Septemba 22, 2002) Nina umri wa miaka 16 na sijamwona baba yangu tangu nilipokuwa na umri wa miaka 4. Makala hiyo ilielezea hisia zangu vizuri sana. Ilisema kweli kwamba kutopendwa na wazazi ni mojawapo ya mambo ambayo huumiza sana. Asanteni kwa chakula hicho cha wakati unaofaa.

J. J., Marekani

Wazazi wangu waliamua kutalikiana baada ya kutengana kwa muda wa miaka 13. Sijukua kwa nini nilikuwa nikiteseka hivyo, kwa kuwa nilidhani nilikuwa nimeshinda tatizo hilo muda mrefu uliopita. Kuelewa sababu ya huzuni yangu hunisaidia nitaje mambo waziwazi ninaposali na hata kumtupia Yehova mzigo huo.

M. D., Italia

Baba yangu alituacha nilipokuwa na umri wa miaka sita. Tangu wakati huo tumewasiliana mara chache sana. Kwa muda wa miaka mingi nimejihisi nina hatia. Kwa hiyo, mimi hushindwa kuwaeleza watu wengine jinsi ninavyohisi. Mambo yaliyoonwa katika makala hiyo yalinisaidia kuona kwamba si mimi tu niliye na tatizo hilo. Sisi wasomaji tunafaidika sana kutokana na makala hizo na tunawashukuru sana!

A. H., Uingereza

Nina umri wa miaka 16. Baba yangu alimtaliki mama yangu hivi majuzi tu. Mimi, ndugu yangu mdogo, na dada yangu tumevunjika moyo kabisa. Makala hiyo ilikuwa nzuri ajabu. Mara tu nilipoanza kuisoma, niliangua kilio. Imeeleza hisia nilizokuwa nazo moyoni. Maneno yake yalikuwa yenye fadhili na yenye upendo. Nilipoendelea kuisoma, niliguswa moyo zaidi. Mara nyingi nimeshindwa kuelewa kama nilistahili kupendwa na baba yangu. Ndiyo sababu makala hiyo ilinifariji sana. Ni vizuri kujua kwamba hata baba yangu mzazi akikosa kunipenda, Yehova atanipenda milele. Sihitaji kubabaika nikidhani eti kwamba siku moja atabadili nia yake na kuniacha.

A. M., Marekani

Baba yangu alikuwa mlevi wa kupindukia tulipokuwa watoto, na mama yangu aliteseka sana. Sisi watoto hatukutunzwa hata kidogo. Nilijihisi kuwa sifai kitu na hata niliona afadhali nife. Nilisali ili nipate msaada. Makala hiyo ilipokuja nilifurahi sana. Nilifarijika kutambua kwamba hata watu walio na tatizo kama langu wanaweza kufanikiwa kwa kutumia kanuni za Biblia. Nilitambua kuwa hata mimi ninaweza kupata shangwe!

A. I., Japan

Vanila Nina wasiwasi kidogo kuhusu makala inayosema “Vanila—Kiungo cha Tangu Zamani za Kale.” (Septemba 22, 2002) Miaka mingi iliyopita, nilisoma makala kuhusu vanila yenye sumu kutoka Mexico. Watu wengi huinunua lakini huwa hawana habari kwamba inaweza kuwa na sumu.

P. D., Marekani

“Amkeni!” linajibu: Vanila nyingine kutoka Mexico, na vilevile kutoka nchi nyingine, hutiwa kiasi kidogo cha mbegu zinazoitwa “tonka,” ambazo zina kemikali iitwayo “coumarin.” Idara ya Marekani ya Chakula na Dawa imepiga kemikali hiyo marufuku kwa sababu ina sumu. Kwa kuwa haiwezekani kutambua kama vanila imetiwa “coumarin” kwa kuangalia au kunusa, wanunuzi hushauriwa wanunue vanila kutoka kwa maduka yanayotambuliwa pekee. Isitoshe, kwa sababu vanila isiyochanganywa na bidhaa nyingine hugharimu pesa nyingi kwa sababu ya gharama za uzalishaji, ni vizuri kuwa mwangalifu sana unapoona ikiuzwa kwa bei ya chini isivyo kawaida.