Kuutazama Ulimwengu
Kuutazama Ulimwengu
Kupokea Ujumbe Wenye Vitisho
“Kijana mmoja kati ya vijana wanne ametishwa kupitia kompyuta au simu ya mkononi,” lasema gazeti la The Guardian la London. Ripoti iliyotolewa na Shirika la Kitaifa la Ufadhili wa Watoto nchini Uingereza lilifunua kwamba asilimia 16 ya vijana wenye umri wa kati ya miaka 11 na 19 “walipokea ujumbe wenye vitisho kupitia simu zao za mkononi,” ilhali asilimia 11 ya vijana walitishwa kupitia vituo vya maongezi kwenye Internet au Barua-pepe. Shirika hilo lilisema kwamba watoto hao “hawamwambii mtu yeyote na hivyo huteseka kimya-kimya, au huwaambia watu ambao hawawezi kuwasaidia.” Shirika hilo linawashauri vijana wasinyamaze wanapotishwa lakini wamjulishe mtu mwenye kutumainika anayeweza kuwasaidia; wawe waangalifu sana wanapopeana nambari za simu na anwani za Barua-pepe; na wazibadilishe ikiwezekana. Shirika hilo linashauri kwamba “ukipokea ujumbe unaoudhi, andika wakati na tarehe ambayo umeupokea na uwajulishe polisi,” lasema gazeti la The Guardian.
Mimea “Huongea”
Watafiti kwenye Taasisi ya Fizikia ya Kuboresha Bidhaa katika Chuo Kikuu cha Bonn, Ujerumani, wamebuni vikuza-sauti vinavyotumia miale ya leza ambavyo vinaweza “kusikiliza” mimea. Vikuza-sauti hivyo hupokea mawimbi ya sauti yanayotokezwa na gesi ya ethylene, kutoka kwenye mimea yenye ugonjwa. Mwanasayansi wa Chuo Kikuu cha Bonn, Dakt. Frank Kühnemann anasema: “Kadiri mmea unavyopatwa na ugonjwa, ndivyo tunavyosikia sauti kubwa zaidi kwenye kikuza-sauti chetu.” Vipimo vilionyesha kwamba tango moja lililoonekana lenye afya “lilikuwa linatoa sauti kubwa.” “Lilipochunguzwa kwa makini liligunduliwa kuwa na kuvu, lakini dalili hazikuwa zikionekana.” Madoa ya kuvu huonekana baada ya siku nane au tisa, ndipo wakulima wawezapo kugundua ugonjwa huo. Gazeti The Times la London linasema kwamba “mfumo wa kugundua mapema wadudu na magonjwa unaweza kubuniwa kwa kusikiliza sauti za mimea. Kujua kiwango cha ugonjwa wa matunda na mboga kunaweza pia kusaidia katika kuzihifadhi na kuzisafirisha.”
Nikotini Husababisha Kifo cha Ghafula cha Watoto
Huenda watafiti nchini Ufaransa na Sweden wamegundua kwa nini kuvuta sigara huzidisha hatari ya kifo cha ghafula cha watoto, laripoti gazeti la Kifaransa la kila siku la Le Figaro. Uchunguzi wa wanyama umeonyesha kwamba nikotini inaweza kuathiri mfumo wa kupumua wakati wa usingizi. “Kukosa oksijeni (hypoxia) wakati wa usingizi, ambako kunaweza kutukia katika vipindi vifupi vya kutopumua (apnea), kwa kawaida huushtua moyo na mfumo wa kupumua na kumfanya mtu aamke. Lakini utaratibu huo unaomlinda mtu ukiathiriwa, matatizo ya kukosa oksijeni na kutopumua huwa mabaya zaidi na hata mtu anaweza kushindwa kabisa kupumua anapolala,” yasema ripoti hiyo. Watafiti wanasema kwamba utaratibu huo wa ulinzi unaweza kudhoofika ikiwa mtoto aliye tumboni anaendelea kupata nikotini kutoka kwenye damu ya mama yake anayevuta sigara akiwa mjamzito. Hilo laweza “kudhoofisha uwezo wa kukabiliana na matatizo ya kupumua wakati wa usingizi, na hivyo kuzidisha hatari ya kifo cha ghafula cha mtoto.” Gazeti la Le Figaro linasema kwamba hicho “bado ni kisababishi kikuu cha vifo vya watoto katika mwaka wa kwanza wa maisha” nchini Ufaransa.
“Ashiki” Inapendwa Sana
Mitindo, matangazo ya kibiashara, vyombo vya habari, na burudani, “zinachochea sana ashiki leo kwa kutumia vibaya tamaa ya wanadamu ya ngono,” lasema gazeti Polityka linalochapishwa kila juma huko Poland. Wabuni wa mitindo wanasema kwamba “mitindo huchochea ashiki, na ashiki huendeleza mitindo.” Jambo kuu ni, ‘kadiri unavyoonyesha mwili wako, ndivyo unavyozidi kutambuliwa.’ Vivyo hivyo, ngono na ashiki “hufanya matangazo ya kibiashara yakumbukwe zaidi” na kuwavutia wateja, asema Dakt. Ewa Szczęsna, mtaalamu wa ishara katika Chuo Kikuu cha Warsaw. Aongezea hivi: “Mipaka ya mambo yanayoonwa kuwa yanachochea ashiki imebadilika sana.” Gazeti Polityka lasema kwamba watangazaji wa bidhaa wako tayari kuvunja kanuni zozote za maadili mradi wapate pesa.
Vyombo vya Habari Vyaongezeka India
Uchunguzi uliofanywa na National Readership Studies Council unaonyesha kwamba wasomaji wa magazeti nchini India wameongezeka kutoka milioni 131 hadi milioni 155 katika muda wa miaka mitatu kuanzia 1999 hadi 2002. Wasomaji wa magazeti na majarida mengine nchini humo ni milioni 180. Hata hivyo, kuna uwezekano mkubwa wa idadi ya wasomaji kuongezeka kwa sababu zaidi ya asilimia 65 ya wakazi wanaozidi bilioni moja nchini India wanajua kusoma. Watazamaji wa televisheni ni milioni 383.6 na wasikilizaji wa redio ni milioni 680.6. Watu milioni 6 hivi kwa sasa wanatumia Internet wakilinganishwa na milioni 1.4 mwaka wa 1999. Karibu nusu ya nyumba zenye televisheni nchini India zimejiandikisha kwenye vituo vinavyotumia kebo na setilaiti, ongezeko la asilimia 31 katika muda wa miaka mitatu.
Utekaji-Nyara Umezidi
Gazeti The News la Mexico City linaripoti kwamba “miaka 15 iliyopita hakukuwa na visa vya utekaji-nyara [nchini Mexico.]” “Lakini uhalifu ulianza kuongezeka katika miaka ya 1980, na yaonekana kwamba kuzorota kwa uchumi kati ya 1994-1995 kulileta mabadiliko makubwa nchini Mexico, na kufanya utekaji-nyara na uhalifu uongezeke sana.” Yaonekana kwamba mtu yeyote anaweza kutekwa nyara. “Watekaji hudai fidia ya dola 500 wanapomteka nyara mfanyakazi wa nyumbani. Msichana mwenye umri wa miaka 12 kutoka Tijuana alitekwa nyara . . . na wanafunzi wa chuo waliokuwa wakijaribu kukusanya ada ya chuo, na watu wengine hata wamejisingizia kuwa wametekwa nyara ili wakusanye pesa za fidia kutoka kwa familia zao au makampuni,” lasema gazeti The News. “[Utekaji-nyara umekuwa] jambo la kawaida siku hizi. Wakazi wa Mexico wamekuwa na zoea la kulipa fidia haraka bila kuwajulisha polisi.” Isitoshe, watu waliotekwa nyara, maafisa wa usalama, na hata rekodi za mahakama zinaonyesha kwamba “mara nyingi polisi hujihusisha katika utekaji-nyara, na kwa kawaida hawakamatwi kwa sababu mahakama hazina uwezo na zimejaa ufisadi.”
Ufasaha wa Lugha Unadidimia
Gazeti la Kijapani The Yomiuri Shimbun linasema kwamba “karibu asilimia 20 ya wanafunzi wa shule za msingi na za sekondari hawasomi kwa ukawaida vitabu vya hadithi na karibu asilimia 80 ya walimu wa shule za sekondari wanasema kwamba ufasaha wa wanafunzi katika lugha ya Kijapani umedidimia.” Watafiti katika Taasisi ya Kitaifa ya Utafiti wa Sera ya Elimu waliwachunguza “wanafunzi 2,120 wa darasa la nne na wanafunzi wa sekondari wa kidato cha pili, na walimu 259 wa shule za msingi na wa sekondari,” yasema ripoti hiyo. Waligundua kwamba “ustadi wa [wanafunzi] wa kufahamu, kuelewa misamiati na kuandika umeshuka sana kwa sababu hawasomi sana.” Idadi kubwa ya walimu waliochunguzwa wanafikiri kwamba tabia hiyo inasababishwa na watu wazima, pamoja na walimu waliokuwa wakiwafundisha wanafunzi hao. Walitaja pia “matokeo mabaya ya michezo ya kompyuta.”
Uchafuzi wa Hewa Husababisha Vifo Vingi Kuliko Aksidenti za Magari
“Shirika la Afya Ulimwenguni linaripoti kwamba watu milioni tatu leo hufa kila mwaka kwa sababu ya uchafuzi wa hewa. Idadi hiyo ni mara tatu zaidi ya watu milioni moja wanaokufa katika aksidenti za magari kila mwaka,” yasema ripoti iliyochapishwa na taasisi ya Earth Policy Institute. Serikali hujitahidi sana kupunguza idadi ya watu wanaokufa katika aksidenti za magari, lakini “hawatilii maanani watu wanaokufa kwa sababu ya kusafiri tu kwa magari. Bado watu wanakufa kutokana na magonjwa ya moyo na yale yanayosababishwa na kupumua hewa chafu licha ya kwamba habari hizo hazisambazwi kotekote na huwa hakuna milio ya ving’ora kama inavyokuwa wakati wa aksidenti,” yasema ripoti hiyo. “Gesi zinazochafua hewa zatia ndani kaboni monoksaidi, ozoni, salfa dioksaidi, nitrojeni oksaidi, na visehemu vingine vya gesi.” Gesi hizo zote hutokana na vitu vya asili kama vile makaa ya mawe na petroli.