Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Maajabu ya Mchanga

Maajabu ya Mchanga

Maajabu ya Mchanga

Inapendeza kama nini kutembea kwenye mchanga, lakini unahisi uchungu ulioje unapokuingia machoni! Kuna mchanga tele baharini, na vilevile katika majangwa makavu. Viumbe wengi hukimbia majangwa yenye mchanga, lakini wengine huishi humo. Mara nyingi mchanga huudhi, lakini maisha yangekuwa magumu sana leo bila mchanga.

Kulingana na maelezo yaliyo juu, yaonekana kwamba mchanga ni kitu chenye kushangaza. Lakini mchanga ni nini, na unatoka wapi?

Hutokana na Miamba

Mchanga huwa na visehemu vya madini, miamba, au udongo na kiasi kikubwa cha kwazi. Vilele vya miamba vimemomonyoka vikawa mchanga. Mmomonyoko huo hutokeaje?

Mchanga husababishwa na msukosuko wa bahari. Mawimbi hupiga majabali ya pwani, kisha huyalegeza na kupasua vipande vya miamba. Vipande vikubwa huangushwa na nguvu nyingi ya bahari, na husukumwa na mawimbi yenye povu hadi ufuoni. Bahari inayosukasuka husugua ncha zilizochongoka na kuacha majabali. Msukosuko huo huvunjavunja majabali hayo na kuyafanya kokoto, ambazo huvunjwa vipande-vipande na kuwa mchanga. Nyakati nyingine bahari husomba mchanga huo, lakini katika sehemu nyingi, mawimbi hurudisha mchanga huo ufuoni, yakiacha fuo safi kabisa.

Bahari inaposukasuka wakati wa baridi kali, maji ya barafu hukwama katikati ya miamba na kuipasua. Miamba mikubwa huendelea kupasuka hadi inapokuwa vipande vidogo zaidi, ambavyo hatimaye huwa mchanga.

Pia upepo hupeperusha chembechembe za mchanga na kuzivurumisha kwenye miamba. Vipande hivyo hukwaruza miamba na kufanyiza mchanga zaidi. Matabaka ya miamba yenye ukubwa wa mamia ya kilometa humomonyolewa na upepo na kuwa mchanga laini. Kisha upepo husambaza mchanga huo kama zulia jangwani.

Kwa maelfu ya miaka, tani nyingi za mchanga zimetengenezwa kwa njia hiyo. Watu wengi wangefurahi ikiwa ungetumiwa tu kutengeneza fuo za kupumzikia zenye mchanga laini. Lakini kama tutakavyoona, mchanga ni muhimu katika mambo mengine mbali na kuboresha fuo.

Chembechembe Zenye Faida Kubwa

Chakula na maji tunayokunywa hutegemea sana mchanga. Jinsi gani? Kwa njia moja au nyingine, vyakula vyetu vyote hutokana na mimea inayokua ardhini. Mchanga, tope na udongo wa mfinyanzi huwa na madini muhimu kwa mimea. Isitoshe, mchanga huruhusu hewa na maji kupenya ardhini. Kwa hiyo, mizizi ya mimea hufyonza virutubishi kwa urahisi. Lakini mchanga unasaidiaje kukata kiu yetu?

Ukijaza mchanga mkavu kwenye mtungi wa lita moja, unaweza kuongeza milimeta 300 za maji kwenye mtungi huohuo na yasimwagike. Sababu ni kuwa, mchanga huruhusu maji kupenya, yaani, mna nafasi nyingi kati ya chembechembe zake. Kwa kweli, kuna ‘mitungi mikubwa ya maji’ mchangani inayoweza kuandalia miji mikubwa maji ya kutosha. Ni mitungi ipi hiyo?

Kuna miamba yenye maji chini ya ardhi. Miamba hiyo ina matabaka mengi ya mchanga na madini mengineyo ambamo maji yamekuwa yakichuruzika kwa maelfu ya miaka. Wanasayansi wanakadiria kwamba kiasi cha maji katika hiyo “mitungi” isiyoonekana kinazidi kiasi cha maji katika maziwa na mito yote duniani kwa zaidi ya mara 40. Maji ya visima yanayotegemewa na mamilioni ya watu hutoka kwenye miamba hiyo.

Mchanga Uko Mbele Yako

Huenda ukawa unatembea juu ya mchanga kila siku bila kwenda ufuoni. Je, barabara za kwenu zimetengenezwa kwa zege? Nyakati nyingine, zege inayotumiwa kwa kawaida katika ujenzi huwa na asilimia 25 ya mchanga. Mamia ya mamilioni ya tani za mchanga hutumiwa kila mwaka katika ujenzi hivi kwamba kuna upungufu wa mchanga katika maeneo fulani.

Ingawa kwa kawaida sisi hutembea juu ya mchanga, huenda ukawa mbele yako kwa namna tofauti. Yaelekea kiwambo cha kompyuta yako kimetengenezwa kwa mchanga, kutia ndani lenzi za darubini na hadubini. Pia vyombo vya kuwekea maua na vioo vya kujiangalia. Vitu vyote hivyo vimetengenezwa kwa glasi, na zaidi ya nusu ya mali-ghafi inayotumiwa kutengeneza glasi ni mchanga. Mchanga hutumiwaje kutengeneza glasi?

Mchanga huchanganywa na vitu vingine kisha huyeyushwa kwa joto linalozidi nyuzi 1,400 za Selsiasi. Umajimaji huo mzito unaweza kuviringwa, kupulizwa, kukunjwa, kuvutwa, na kupindwa kwa umbo lolote. Nyuzi za glasi hufumwa na kuwa nguo. Lakini haidhuru inatumiwa vipi, iwe ni katika mapambo au viwandani, iwe inaakisi au kupinda nuru, glasi laini isiyo na rangi hutokana na chembechembe za mchanga zisizopitisha nuru.

Mchanga Hupeperuka

Wazia kilima chenye urefu wa meta 75 kinachopeperuka. Jambo hilo hutokea wakati marundo ya mchanga yanapopeperushwa na upepo. Katika sehemu fulani za Jangwa la Sahara, pembe za vilima vya mchanga huonekana zikipinda bila mwisho.

Vilima vya mchanga vinaweza kuwatatiza wanadamu wanaoishi karibu navyo. Ni kawaida kwa mchanga unaopeperushwa kuziba njia, kufunika nyumba, na hata kuzika miji mizima.

Ni Makao ya Viumbe Wengi

Huenda mchanga ukaonekana kama hauna viumbe, lakini viumbe wengi huishi humo. Mbweha, nyoka, na nge hujificha katika mchanga wa jangwani wakati wa mchana. Wao hulala humo wakati wa joto, na kutoka nje usiku kuwinda. Katika Skeleton Coast huko Namibia, kusini-magharibi mwa Afrika, ndovu hurandaranda kwenye vilima vingi vya mchanga. Yaonekana wao hupenda kuteleza kwa miguu yao ya nyuma kwenye miteremko mikali ya vilima hivyo. Ngamia ambao pia huitwa “meli za jangwani,” husafiri mwendo mrefu kwenye majangwa ya Asia na Afrika.

Wanyama fulani hutoka baharini na kuja kwenye mchanga ufuoni. Majira yafaayo yanapowadia, kaa aina ya horseshoe, kasa wa baharini, na samaki wadogo wanaoitwa grunion huelea mawimbini na kuja ufuoni. Hutaga mayai ufuoni ili yaatamie kwenye mchanga huo laini.

Maua fulani hunawiri sana kwenye vilima vya mchanga kana kwamba yamepandwa bustanini. Maua aina ya Sea rocket, beach peas, na morning glory ya ufuoni hunawiri na kuibuka hata yanapozikwa na mchanga. Mizizi yake mirefu huvuta maji na virutubishi ili kulisha maua yake yanayoanza kuchanua—na hivyo huremba jangwa lote lenye mchanga.

Ni kweli kwamba mchanga waweza kuudhi ukiingia ndani ya viatu unapotembea karibu na ufuo. Hata hivyo, usiudhike. Ukweli ni kwamba tunategemea chembechembe hizo za mchanga ambazo ni za kawaida tu! Mchanga hudhihirisha pia hekima ya Muumba, Yehova Mungu.—Zaburi 104:24.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 18, 19]

Mambo ya Ajabu Kuhusu Mchanga

Mchanga huwa na rangi mbalimbali. Katika nchi tofauti-tofauti unaweza kupata mchanga mweusi tititi, mweupe pepepe, wa rangi ya zambarau, ya kijivu, nyekundu, rangi ya machungwa, ya manjano, na mchanganyiko wa rangi mbalimbali. Mwingine huwa na mchanganyiko wa makombe yaliyovunjika-vunjika. Rangi na ukubwa mbalimbali wa chembe za mchanga huwastaajabisha watu wengine hivi kwamba wameanza kukusanya mchanga. Wengi huuza mchanga, husafiri kuutafuta, huinama na kukusanya aina mbalimbali kwenye chupa ndogo na kuongezea aina mpya-mpya. Wao hujiita “wapenda-mchanga.”

[Hisani]

Courtesy Serge tkint

[Picha katika ukurasa wa 16]

Jangwa la Namib, nchini Namibia

[Picha katika ukurasa wa 16]

Vitu ambavyo huvunjavunja miamba na kufanyiza mchanga hutia ndani mawimbi yenye nguvu, mawimbi yenye povu, na upepo

[Picha katika ukurasa wa 17]

Wadudu, maua, mbweha, na ngamia huishi mchangani

[Hisani]

Foxes: Hai-Bar, Yotvata, Israel

[Picha katika ukurasa wa 18]

Mchanga ni kiungo muhimu cha kutengenezea glasi na zege

[Picha katika ukurasa wa 18]

Vilima vya mchanga vinaweza kuwa na kimo cha mamia ya meta

[Hisani]

▼ Glassmakers: Provided by The Corning Museum of Glass