Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Minyoo wa Ajabu

Minyoo wa Ajabu

Minyoo wa Ajabu

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI AUSTRALIA

MALKIA CLEOPATRA wa Misri alisema kwamba ni watakatifu. Aristotle aliwaita matumbo ya dunia. Charles Darwin alifikiri kwamba wao ni muhimu sana katika historia ya ulimwengu. Ni viumbe gani waliowastaajabisha watu hao mashuhuri? Ni minyoo wa kawaida tu wa ardhini.

Kama utakavyoona, minyoo wanastahili kuthaminiwa. Ni kweli kwamba minyoo huwa na miili yenye utelezi inayojipindapinda. Lakini hata sifa hizo ambazo huenda zisituvutie, zinaweza kukustaajabisha unapowajua minyoo vizuri zaidi. Wewe inama tu chini na kupindua bonge la udongo au uondoe majani yaliyo ardhini, utaona minyoo wenye kustaajabisha.

Ubongo Mdogo, Lakini Uwezo Wenye Kustaajabisha

Unapomtazama kwa makini mnyoo wa ardhini, utagundua kwamba mwili wake una pingili za mviringo ambazo zinafanana na donati ndogo zilizoshikana. Kila pingili ina mafungu mawili ya misuli. Fungu la kwanza huwa chini tu ya ngozi na huwa na umbo la mviringo. Fungu la pili huwa sambamba na mwili wa mnyoo. Mnyoo hutembea kwa kupanua na kukunja misuli hiyo, na kupinda pingili baada ya pingili kama mawimbi.

Ukimchukua mnyoo mkononi mwako, bila shaka atajinyonga-nyonga na kujipindapinda. Mnyoo hufanya hivyo kwa sababu mwili wake umejaa viungo vya hisi—viungo 1,900 kwenye pingili moja tu. Viungo hivyo humsaidia mnyoo kugusa, kuonja, na kutambua nuru.

Mnyoo hushika udongo kwa kutumia miguu midogo inayofanana na nywele. Kila pingili huwa na miguu kadhaa inayosonga kama makasia ya mashua. Mnyoo huitumbukiza ardhini halafu hujivuta na kuiachilia. Mnyoo anaweza kwenda upande wowote kwa kutumia miguu ya pingili moja kwa wakati au, akitishwa anaweza kusonga kwa kujishikilia upande mmoja na kurudi nyuma haraka-haraka kwa kutumia upande wa pili. Ustadi wa kupiga “makasia” hayo kwa wakati barabara unaweza kuwatia wivu wapiga-makasia wa timu ya Olimpiki.

Pingili za mkiani za minyoo fulani humea tena baada ya kutafunwa na ndege—lakini idadi hubaki ileile. Yaonekana kwamba kila pingili hutokeza kiasi kidogo cha nguvu za umeme na pingili zilizokatika hukua tena hadi nguvu hizo zinapofikia kiasi fulani hususa.

Maelfu ya viungo vya hisi na misuli tata huungana katika kiini cha ubongo, nyuma ya mdomo wa mnyoo. Uchunguzi umeonyesha kwamba mbali na uwezo wao mbalimbali, minyoo wana kumbukumbu ndogo na hata wanaweza kujifunza kuepuka hatari.

Kwa Nini Miili Yao Ina Utelezi?

Ngozi yenye utelezi ya mnyoo ambayo huwachukiza watu wengi, humwezesha kiumbe huyo mdogo apumue. Ngozi ya mnyoo ina matundu-matundu na mishipa ya damu iliyo chini yake hufyonza oksijeni iliyo hewani au kwenye maji na kutoa kaboni dioksaidi. Lakini gesi hizo zinaweza kutoka na kuingia ikiwa tu ngozi ina unyevunyevu. Ngozi ya mnyoo ikikauka, muda si muda atakufa.

Kwa upande mwingine, mnyoo akikwama shimoni wakati wa mvua kubwa, atatumia na kumaliza haraka oksijeni iliyo kwenye maji yaliyo shimoni. Hiyo ni moja ya sababu zinazowafanya minyoo waje juu ya ardhi wakati wa mafuriko. Watakosa hewa wasipotoka shimoni.

Dunia Imejaa Walimaji Stadi

Kuna zaidi ya aina 1,800 za minyoo katika dunia yetu. Wanapatikana kila mahali isipokuwa katika sehemu kame na zenye baridi sana duniani. Katika mbuga za savanna huko Afrika Kusini, huenda kukawa na minyoo wasiozidi 7 katika kila eneo la meta moja ya mraba, ilhali kwaweza kuwa na minyoo zaidi ya 70 katika eneo la meta moja za mraba katika msitu nchini Kanada.

Kuna aina tatu za minyoo wa ardhini huko New Zealand. Aina ya kwanza huzaana haraka, hutembea haraka-haraka na huishi katikati ya mimea inayooza kwenye ardhi. Minyoo wa aina ya pili hupatikana katika sehemu nyingi na huchimba mashimo yanayopita katika matabaka ya juu ya udongo. Minyoo wa aina ya tatu huchimba mashimo kuelekea chini na wanaweza kuishi katika shimo moja kwa miaka kadhaa, yaani, maisha yao yote. Hao ndio minyoo wenye nguvu zaidi ulimwenguni. Wana misuli ya mviringo yenye nguvu kichwani ambayo inawasaidia kupenya ardhini. Mnyoo mkubwa zaidi duniani anapatikana kusini mwa Australia. Mnyoo huyo anaweza kuwa na urefu wa zaidi ya meta 1.5 na uzito wa nusu kilo.

Minyoo wanapopita ardhini huwa kama walimaji wadogo. Wanapokula mbolea, udongo, na mimea inayooza, wanakunya kinyesi kingi sana. Imekadiriwa kwamba minyoo walio katika mashamba ya Uingereza hunya tani nane hivi za kinyesi kwenye eneo la ekari moja. Minyoo wenye kustaajabisha zaidi ni wale walio katika Bonde la Nile. Minyoo hao wanaweza kunya tani 1,000 hivi za kinyesi kwa kila ekari moja. Minyoo wanapogeuza-geuza udongo, hewa na maji yanapenya kwa urahisi zaidi na rutuba inaongezeka.

Wanasayansi wamegundua kwamba mfumo unaosaga chakula katika mnyoo hubadili virutubishi ili viweze kutumiwa na mimea, kwa hiyo kinyesi cha mnyoo kimejaa chakula cha mimea. Isitoshe, vijidudu vingi hatari vinavyopatikana katika mbolea na mimea inayooza hufa vinapopitia kwenye tumbo la mnyoo. Kwa hiyo, minyoo wanasafisha udongo wanapokula. Hutengeneza chakula cha mimea chenye virutubishi kwa kula takataka.

Kutumia Uwezo wa Minyoo

Makampuni yanayokusanya takataka yanategemea uwezo wa kustaajabisha wa minyoo ili kutengeneza bidhaa muhimu kutokana na takataka. Kampuni moja nchini Australia hutumia minyoo milioni 500 katika mitambo kadhaa ya kusafisha maji machafu. Minyoo hao huhifadhiwa katika sehemu maalumu na hulishwa kinyesi cha nguruwe au cha wanadamu kilichochanganywa na mimea mingine na makaratasi yaliyochanwa-chanwa. Kila siku minyoo hao hula chakula kinachopita uzito wa miili yao kwa kati ya asilimia 50 na 100 na hutokeza chakula cha mimea kilichojaa virutubishi kinachouzwa kotekote.

Uchunguzi umeonyesha kwamba minyoo wanaweza pia kutumiwa kama chakula. Minyoo wana asidi-amino muhimu kama zile za nyama ya ng’ombe. Wao hukaushwa na kupakiwa wakiwa na asilimia 60 ya protini, asilimia 10 ya mafuta, kalisi na fosforasi. Minyoo waliookwa ndani ya mikate wanaliwa katika nchi fulani. Katika sehemu nyingine za ulimwengu, watu hukaanga minyoo wa ardhini na hata huwala wakiwa wabichi.

Bila shaka ulimwengu ungekuwa tofauti sana bila minyoo licha ya kwamba huenda wasipendwe na watu wengi. Kwa hiyo, unapofurahia mandhari maridadi ya mashambani, hebu tua na uwafikirie minyoo wengi walio ardhini, ambao wanajitahidi kulima, kurutubisha, na hata kudumisha umaridadi huo.

[Mchoro/Picha katika ukurasa wa 22]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

Mwili wa Mnyoo wa Ardhini

Gamba

Misuli iliyo sambamba na mwili

Misuli ya miguu

Miguu midogo

Msuli wa duara

Kibofu cha mkojo

Utumbo

Mshipa wa neva

[Hisani]

Lydekker

J. Soucie © BIODIDAC

[Picha katika ukurasa wa 20]

Minyoo “hupiga makasia” ardhini kwa miguu yao midogo

[Picha katika ukurasa wa 21]

Minyoo hugeuza-geuza udongo na kuongeza rutuba

[Picha katika ukurasa wa 21]

Mnyoo mkubwa aina ya Gippsland aliye Australia ambaye anakabili hatari ya kutoweka, anaweza kuwa na urefu wa zaidi ya meta 1.5

[Hisani]

Courtesy Dr A. L. Yen

[Picha katika ukurasa wa 22]

Minyoo hugeuza takataka kuwa chakula cha mimea kilichojaa virutubishi