Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Mtazame Kiboko Mwenye Nguvu Ajabu!

Mtazame Kiboko Mwenye Nguvu Ajabu!

Mtazame Kiboko Mwenye Nguvu Ajabu!

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI KENYA

KWENYE Hifadhi kubwa ya Wanyama-pori ya Masai Mara nchini Kenya mna dimbwi kubwa la maji linalong’aa katika umaridadi wenye utulivu wa jua la jioni. Jua linapoendelea kuzama wakati wa machweo, maji yanakuwa na rangi maridadi sana ya dhahabu-kahawia. Hatua chache kutoka hapo, makundi ya pundamilia na nyumbu yanakaribia dimbwi hilo taratibu. Ghafula, na kwa wasiwasi mwingi, wanyama hao wasimama tuli na kukazia macho kitu kinachofanana na jabali kinachoelea karibu na kingo za dimbwi hilo. Baada ya kutibua maji, “jabali” hilo latokomea majini. Wanyama hao wamemwona mnyama mkali sana wa majini anayeitwa kiboko.

Kiboko anayeishi kwenye vidimbwi, mito na maziwa ya Afrika Mashariki ni mkubwa kuliko wanyama wote isipokuwa ndovu. Kiboko aliyekomaa anaweza kuwa na urefu wa zaidi ya meta 4 na kimo cha meta 1.5. Ana uzito wa tani nne hivi. Neno “Behemothi” linalotajwa katika kitabu cha Biblia cha Ayubu huonwa kuwa jina jingine la kiboko. Si ajabu kwamba Biblia husema kuwa mnyama huyo mkubwa ana mifupa inayofanana na “mirija ya shaba,” na huilinganisha na “vipande vya chuma.”—Ayubu 40:15-18.

Kiboko mwenye ngozi nene isiyo na manyoya ambaye ni mzito hufanana na pipa na havutii hata kidogo. Miguu ya kiboko ni mifupi, na inashangaza jinsi inavyoweza kuutegemeza mwili wake mkubwa. Lakini usiidharau miguu hiyo mifupi minene. Kiboko anaweza kukimbia kasi kumshinda mwanadamu kwenye nchi kavu. Imedaiwa kwamba kiboko husonga kasi majini kuliko mashua inayoendeshwa kwa makasia au hata mashua yenye injini.

Maisha Yake Majini

Viboko huishi pamoja kwa vikundi vyenye viboko 10 hadi 15 wakiongozwa na dume, lakini vikundi vyenye viboko 150 hivi vimewahi kuonekana. Viboko huishi majini na vilevile kwenye nchi kavu nao hutoka majini hasa usiku ili kula majani laini yaliyo kwenye kingo za maji. Kwa kawaida, hawapendi kwenda mbali na maji. Hata hivyo, viboko fulani wameonekana wakitembea umbali wa kilometa 10 kutafuta chakula wakati wa kiangazi.

Haijulikani kabisa jinsi viboko wanavyoitia alama mipaka ya maeneo yao. Watu fulani wanaamini kwamba tabia yao ya kushangaza ya kusambaza kinyesi chao kwa kutumia mikia yao ni mbinu ya kuvutia viboko wa kike au kuwafukuza adui. Wanaposhambuliwa wao hulia kama farasi, na hutoa sauti kubwa nzito au kunguruma wanapopigana. Mikoromo ya juu husikika hata wakiwa ndani ya maji. Kiboko-dume aliye kiongozi hujitangaza kwa sauti ya MO-Mo-mo.

Kwa siku nzima kiboko hushinda majini mwili wake ukiwa umefunikwa na maji kabisa au kwa sehemu, na mwili wake mkubwa humwezesha kufanya hivyo. Ingawa huenda asiwe mwogeleaji stadi kama wanyama wengine wanaoishi kwenye maji na nchi kavu, kiboko anaweza kuzama majini kwa dakika 15! Pua, macho, na masikio yake yako katika mstari mmoja, ili kumwezesha kuficha sehemu iliyobaki ya mwili wake ndani ya maji. Kiboko hufanyia shughuli zake kadhaa humo majini, kutia ndani uchumba na kujamiiana.

Baada ya kubeba mimba kwa miezi minane hivi, kiboko huzaa ndama mmoja tu katika maji yasiyo na kina kirefu. Ndama wake hunyonya akiwa ndani ya maji au katika maji yanayofika kwenye kiwiko. Ajapokuwa mwenye nguvu, kiboko huchukua daraka lake la kuwa mzazi kwa uzito sana, humtunza ndama wake kwa upendo wa ajabu. Kiboko-jike anayeelea akiwa amembeba ndama mgongoni anavutia sana. Bila shaka, mnyama huyo anayeonekana mtulivu hupigana kufa na kupona ili kumlinda ndama wake!

Ngozi ya kiboko inafaana sana na mazingira ya maji. Ngozi yake hubadilika sana anapotoka majini. Tezi zilizo chini ya ngozi yake hutoa ute mwekundu-mwekundu wenye chumvi nyingi. Akiwa mbali, mnyama huyo huonekana kana kwamba anatokwa na jasho la damu. Hata hivyo, ute huo huilinda ngozi yake akiwa ndani ya maji na kwenye nchi kavu. Jamii za kale za Kiafrika zilikata vipande virefu vya ngozi ya kiboko na kuvitumbukiza kwenye mafuta. Kisha vipande hivyo vilipindwa na kukaushwa ili kutengeneza kiboko kilichotumiwa na watu walipopigania mashamba. * Kitabu Grzimek’s Animal Life Encyclopedia kinasema kwamba utaratibu wa kubadili ngozi ya kiboko ili iwe “ngumu kama jiwe na yenye unene wa sentimeta nne na nusu hivi” ulichukua muda wa miaka sita hivi.

Miayo Yenye Kuvutia Inayotisha

Bila shaka mdomo wa kiboko ndiyo sehemu yenye kutokeza zaidi. Akiwa kwenye nchi kavu, mnyama huyo hutumia midomo yake yenye upana wa futi moja na nusu ili kula majani karibu na maji. Hata hivyo, mdomo wake hautumiwi tu wakati wa kula. Kiboko anapofunua mataya yake kufikia ukubwa wa nyuzi 150, hafanyi hivyo ili kupiga miayo tu lakini hutaka kuwatisha adui kwa hasira. Viboko hupigana vikali ili kulinda maeneo yao yanayoendelea kupungua. Meno makubwa huonekana kwenye sehemu ya chini anapofunua mdomo wake. Meno hayo makali ya kujilinda yanaweza kuwa na urefu wa sentimeta 30.

Mdomo wa kiboko ni hatari kwa viboko wenzao na pia wanadamu. Wanadamu wameshindwa kuishi pamoja na viboko kwa amani. Kiboko humshambulia mtu yeyote anayejaribu kuingia katika eneo lake. Isitoshe, kiboko huwa na hasira kali zaidi anapojeruhiwa na hivyo anaweza kumjeruhi vibaya sana yeyote anayemkaribia. Viboko wenye hasira hata wamezamisha mashua kwa mataya yao makubwa.

Kiboko ni hatari sana kwenye nchi kavu kama tu alivyo kwenye maji. Kwa mfano, ni hatari sana kuwa kati ya maji na kiboko anayelisha. Katika sehemu fulani za Afrika, wanakijiji wasio na habari wameshambuliwa na viboko walipopita kati ya viboko hao na maji. Mnyama huyo huwaogofya sana wanadamu na pia wanyama wengine na ni lazima kujihadhari kabisa naye.

Je, Kiboko Ataokoka?

Kiboko aliye peke yake anaweza kushambuliwa na simba anapokula majani kwenye nchi kavu. Hata hivyo, yaelekea adui mkubwa zaidi wa kiboko ni mwanadamu. Kitabu World Book Encyclopedia kinasema kwamba “watu wamepunguza sana idadi ya viboko na makao yao. Wawindaji wamewaua viboko wengi sana na wakulima wamefanya makao ya viboko kuwa mashamba yao.”

Naam, viboko wamelazimika kuishi katika sehemu ndogo na hivyo hawawezi kutembea kwa uhuru na kuzaana kwa sababu wanadamu wameingilia makao yao. Inapendeza kujua kwamba chini ya utawala wa Ufalme wa Mungu, Muumba ameahidi kurudisha uhusiano kati ya wanadamu na wanyama, na hakuna yeyote ‘atakayedhuru wala kuharibu’ katika Paradiso itakayorudishwa duniani.—Isaya 11:9.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 11 Kiboko ni jina la kiswahili linalomaanisha mjeledi.

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 25]

◀ Elizabeth DeLaney/Index Stock Photography