Ugonjwa wa Kisukari “Huua Kimyakimya”
Ugonjwa wa Kisukari “Huua Kimyakimya”
ALIPOKUWA mwenye umri wa miaka 21, Ken alianza kuhisi kiu kisichoisha na ambacho hakikuwa cha kawaida. Pia alihitaji kwenda haja ndogo mara nyingi, na baadaye akahitaji kufanya hivyo kila baada ya dakika 20. Punde si punde, Ken alianza kuhisi uzito miguuni. Alikuwa mchovu kila wakati, na macho yake hayakuweza kuona vizuri.
Mambo yalibadilika wakati Ken alipopata mafua. Daktari alimwambia kwamba hakuwa na mafua tu, bali pia ugonjwa wa kisukari wa Aina ya 1 (Type 1 diabetes mellitus). Ugonjwa huo huathiri uwezo wa mwili wa kutumia virutubisho fulani, hasa aina ya sukari inayoitwa glukosi inayopatikana kwenye damu. Ken alikaa hospitalini kwa majuma sita kabla ya kiwango cha sukari mwilini mwake kurudia hali ya kawaida.
Hilo lilitukia zaidi ya miaka 50 iliyopita, na njia za matibabu zimeboreshwa sana tangu wakati huo. Hata hivyo, Ken bado anaugua ugonjwa wa kisukari, na si yeye tu. Inakisiwa kuwa watu milioni 140 wana ugonjwa wa kisukari ulimwenguni pote, na kulingana na Shirika la Afya Ulimwenguni, idadi hiyo huenda ikaongezeka mara mbili kufikia mwaka wa 2025. Kwa hiyo, wataalamu wana sababu ya kuhangaika. Mkurugenzi mmoja wa kituo kimoja cha tiba nchini Marekani anayeitwa Dakt. Robin S. Goland, anasema: “Kutokana na ongezeko kubwa la idadi ya watu wanaougua ugonjwa wa kisukari, huenda tumeanza kukabili janga kubwa.”
Hebu fikiria takwimu zifuatazo kutoka sehemu mbalimbali duniani.
AUSTRALIA: Kulingana na Taasisi ya Kimataifa ya Ugonjwa wa Kisukari ya Australia, “ugonjwa wa kisukari ni mojawapo ya magonjwa magumu sana kutibu katika karne ya 21.”
INDIA: Angalau watu milioni 30 wanaugua ugonjwa wa kisukari. Daktari mmoja anasema: “Miaka 15 hivi iliyopita, watu wenye umri wa chini ya miaka 40 hawakuwa wakiugua ugonjwa wa kisukari. Hata hivyo, nusu ya watu wanaougua kisukari siku hizi wana umri wa chini ya miaka 40.”
SINGAPORE: Karibu thuluthi moja ya watu walio na umri wa kati ya miaka 30 na 69 wanaugua ugonjwa wa kisukari. Watoto wengi, hata wale walio na umri wa chini ya miaka kumi, wamepimwa na kupatikana na ugonjwa huo.
MAREKANI: Inakadiriwa kuwa watu milioni 16 wana ugonjwa wa kisukari, na kwamba wengine 800,000 wanapatwa na ugonjwa huo kila mwaka. Mamilioni ya watu wana ugonjwa huo lakini hawana habari.
Ni vigumu zaidi kutibu ugonjwa wa kisukari kwa kuwa mtu anaweza kuishi nao kwa muda mrefu kabla haujagunduliwa. Gazeti la Asiaweek linasema: “Kwa kuwa dalili za mapema za ugonjwa wa kisukari hazionekani waziwazi, mara nyingi ugonjwa huo haugunduliwi.” Hiyo ndiyo sababu watu husema kwamba ugonjwa huo huua kimyakimya.
Kwa vile ugonjwa huo umeenea sana, makala zifuatazo zitazungumzia maswali haya:
● Ugonjwa wa kisukari husababishwa na nini?
● Watu wanaougua ugonjwa huo wanawezaje kukabiliana nao?
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 4]
Maana ya Jina Hilo
Jina “diabetes mellitus” linatokana na neno la Kigiriki linalomaanisha “kunyonya” na neno la Kilatini linalomaanisha “tamu kama asali.” Maneno hayo yanafafanua vizuri sana ugonjwa huo, kwani maji hupita mwilini mwa mtu aliye na ugonjwa wa kisukari kana kwamba yananyonywa na mdomo na kupitia kwenye njia ya mkojo kisha kutoka nje ya mwili. Isitoshe, mkojo huwa na ladha tamu kwa kuwa una sukari. Ndiyo sababu kabla ya kuvumbua njia bora za kupima ugonjwa huo, mbinu moja ya kutambua kama mtu ana ugonjwa wa kisukari ilikuwa kumwaga mkojo wa mgonjwa karibu na kichuguu cha sisimizi. Ikiwa sisimizi wangevutiwa na mkojo huo, basi hilo lilimaanisha kwamba mkojo una sukari.