Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

‘Barabara Iliyoinuka Zaidi’?

‘Barabara Iliyoinuka Zaidi’?

‘Barabara Iliyoinuka Zaidi’?

▪ Kwa nini Barabara ya Baldwin, huko Dunedin, New Zealand ni ya kipekee? Kwa muda mrefu, watu wa mji wa Dunedin wamedai kwamba barabara hiyo ndiyo ina mwinuko mkali zaidi ulimwenguni. Ijapokuwa wengine wamepinga dai hilo, jambo moja ni hakika: Barabara ya Baldwin ina mwinuko mkali sana.

Barabara hiyo inayojulikana sana imewavutia watalii wengi kutoka sehemu zote za ulimwengu. Huhitaji kuwa mpandaji wa milima ili uipande hadi kileleni. Unaweza kuipanda barabara hiyo yenye umbali wa meta 359 kwa miguu, lakini haipendekezwi waendeshaji wa magari waitumie.

Njoo Tupande Pamoja

Siku moja wakati ambapo jua lilikuwa limechomoza, mimi na wenzangu wawili tulitazama mwinuko mkali wa barabara hiyo iliyokuwa mbele yetu. Tulipoanza kupanda, tulianza kuhema huku tukiinama mbele ili tuweze kujisawazisha. Mmoja wetu alisema hivi akivuta pumzi: “Lo, ni kama kupanda ukuta.” Kisha tukaona benchi kando yetu na tukatamani sana kupumzika.

Baadaye, tuliendelea kupanda, na punde si punde tukafika kileleni na tukatazama mandhari nzuri huku tukihema. Tuliona nyumba na bustani maridadi sana. Kwenye upeo wa macho yetu tuliona anga la bluu, na chini yake kulikuwa na kichaka chenye rangi ya kijani nzito kilichozunguka malisho yenye nyasi nzuri.

Tulichukua muda mrefu kupanda barabara hiyo. Baada ya kushuka, tukasimama ili kupiga picha ya kusherehekea ushindi wetu na tukadai Cheti cha Mafanikio cha jiji hilo kinachoonyesha “Barabara Yenye Mwinuko Mkali Zaidi Duniani.” —Tulitumiwa makala hii.