Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kwa Nini Yamerudi?

Kwa Nini Yamerudi?

Kwa Nini Yamerudi?

MIAKA 40 hivi iliyopita, ilidhaniwa kwamba magonjwa yanayoenezwa na wadudu kama vile malaria, homa ya manjano, na kidingapopo yalikuwa yamekomeshwa katika sehemu nyingi za ulimwengu. Lakini pasipo kutarajiwa, magonjwa hayo yakaanza kurudi tena.

Kwa nini? Sababu moja ni kwamba wadudu fulani na viini vilivyo mwilini mwao vimekuwa sugu hivi kwamba haviwezi kufa kwa dawa. Jambo hilo limetokea kwa sababu watu wanatumia dawa za kuua wadudu kupita kiasi na wanatumia vibaya dawa za matibabu. Kitabu Mosquito kinasema: “Katika familia nyingi maskini, watu hununua dawa halafu wanazitumia kidogo tu kutuliza maumivu yao, kisha wanahifadhi dawa zilizobaki ili wazitumie watakapougua tena.” Kwa kuwa hawaponi kabisa, viini vyenye nguvu vinaweza kuendelea kuishi miilini mwao na kutokeza viini vingine sugu.

Kubadilika kwa Hali ya Hewa

Jambo moja kuu ambalo limesababisha magonjwa yanayoenezwa na wadudu kurudi tena ni mabadiliko ya kimazingira na ya kijamii. Kwa mfano, hali ya hewa ulimwenguni pote inabadilika. Wanasayansi fulani wanatarajia kwamba wadudu wanaoeneza magonjwa watahamia katika maeneo ya baridi kwa kuwa joto linaongezeka ulimwenguni pote. Kuna uthibitisho kwamba huenda jambo hilo linatukia. Dakt. Paul R. Epstein wa Kituo cha Afya na Mazingira ya Ulimwenguni Pote cha Chuo cha Kitiba cha Harvard anasema hivi: “Inasemekana kwamba wadudu na magonjwa yanayoenezwa na wadudu (kutia ndani malaria na kidingapopo) yanarudi katika maeneo ya milimani huko Afrika, Asia, na Amerika Kusini.” Huko Costa Rica, kufikia hivi majuzi ugonjwa wa kidingapopo ulikuwa unapatikana tu katika Pwani ya Pasifiki ya nchi hiyo, lakini sasa umeenea katika maeneo ya milimani na katika nchi yote.

Lakini joto linaweza pia kusababisha hali nyinginezo. Katika maeneo fulani yenye joto, mito hukauka na kuwa vidimbwi, na katika maeneo mengine joto husababisha mvua na mafuriko ambayo hutokeza vidimbwi vyenye maji yaliyotuama. Mbu huzaana katika maji hayo. Joto hufanya mbu wazaane haraka, na kuwafanya wadumu kwa muda mrefu. Mbu huwa watendaji sana kunapokuwa na joto. Joto hilo huingia katika utumbo wao na kufanya viini vilivyomo vizaane haraka. Hivyo, mbu akimuuma mtu mara moja wakati wa joto, kuna uwezekano mkubwa kwamba mtu huyo ataambukizwa ugonjwa. Lakini, kuna mambo mengine ambayo yamesababisha magonjwa yazuke tena.

Mfano Unaoonyesha Jinsi Wadudu Wanavyoeneza Magonjwa

Mabadiliko ya kijamii yanaweza kusababisha magonjwa yanayoenezwa na wadudu. Ili kuelewa jambo hilo, tunahitaji kuchunguza jinsi wadudu wanavyohusika. Unapochunguza magonjwa mengi, utaona kwamba si wadudu tu ambao huchangia kuyaeneza. Mnyama au ndege anaweza kubeba viini vya ugonjwa nje ya mwili wake au ndani ya mwili wake. Mnyama huyo au ndege huyo anaweza kuendelea kuishi na viini hivyo bila kuathiriwa.

Mfano mmoja ni ugonjwa wa Lyme, ambao uligunduliwa mwaka wa 1975. Ugonjwa huo ulionekana kwanza huko Lyme, Connecticut, Marekani, na ndiyo sababu ulipewa jina hilo. Huenda bakteria inayosababisha ugonjwa huo iliingia Amerika Kaskazini miaka mia moja iliyopita kupitia kwa panya au mifugo waliokuwa ndani ya meli zilizotoka Ulaya. Kupe mdogo anayeitwa Ixodes anaponyonya damu ya mnyama mwenye ugonjwa huo, bakteria hudumu katika utumbo wa kupe huyo hadi anapokufa. Kupe huyo anaweza kueneza bakteria hizo anapomuuma mnyama mwingine au mwanadamu.

Kwa muda mrefu, ugonjwa wa Lyme umekuwa ukiwakumba hasa watu wanaoishi katika eneo lililo kaskazini-mashariki mwa Marekani. Katika eneo hilo, panya wenye miguu myeupe ndio huwa hasa na bakteria za ugonjwa wa Lyme. Panya hao pia hubeba kupe, hasa wale kupe wanaoendelea kukomaa. Kupe hao wakiisha kukomaa, wao huhamia kwenye miili ya mbawala. Kisha wao hujamiiana na kuwanyonya mbawala. Kupe wa kike akiisha kushiba damu, yeye huanguka chini ili kutaga mayai, kisha kupe wanaongezeka.

Hali Zinapobadilika

Wanyama na wadudu wamebeba viini kwa miaka mingi bila kuwaathiri wanadamu. Lakini hali zinapobadilika, ugonjwa ambao haukuwa ukienea unaweza kuenea kwa watu wengi wanaoishi katika eneo moja. Ni hali zipi zilizosababisha ugonjwa wa Lyme uenee?

Hapo zamani, mbawala hawakuwa wengi kwani wanyama fulani waliwawinda. Hivyo, wanadamu hawakuwa wakivamiwa sana na wale kupe wanaoishi kwenye miili ya mbawala. Wakati walowezi Wazungu walipokata misitu ili walime, mbawala na wanyama waliowawinda walihamia katika maeneo mengine. Lakini katikati ya miaka ya 1800, wakulima walihamia katika maeneo ya magharibi mwa Marekani. Basi, mashamba yakaachwa ukiwa, na msitu ukatokea tena. Mbawala wakarudi, lakini wale wanyama waliokuwa wanawawinda hawakurudi. Kwa hiyo, mbawala wakaongezeka sana, na kupe pia.

Muda fulani baadaye, bakteria ya ugonjwa wa Lyme ikaibuka, na ikadumu mwilini mwa wanyama kwa makumi ya miaka kabla ya wanadamu kuambukizwa. Hata hivyo, watu walianza kujenga nyumba karibu na msitu huo, na watoto na watu wazima wengi wakahamia katika eneo hilo lenye kupe. Kupe wakaanza kuwanyonya wanadamu, na wanadamu wakapata ugonjwa wa Lyme.

Magonjwa Katika Ulimwengu Wenye Msukosuko

Matukio hayo yanaonyesha njia moja tu ambayo magonjwa hutokea na kuenea na ni mfano mmoja tu unaoonyesha jinsi shughuli za wanadamu zinavyochangia kuzuka kwa magonjwa. Mwanamazingira Eugene Linden anasema hivi katika kitabu chake The Future in Plain Sight: “Magonjwa mengi sugu yamezuka tena kwa sababu ya shughuli za wanadamu.” Kuna mambo mengine pia yanayoonyesha jinsi wanadamu wanavyochangia kuenea kwa magonjwa. Kwa mfano, kwa kuwa watu wengi siku hizi wanaweza kusafiri haraka, viini vya magonjwa vinaweza kuenezwa ulimwenguni pote. Uharibifu wa makao ya viumbe wakubwa na wadogo unaangamiza jamii mbalimbali za mimea na wanyama. Linden anasema hivi: “Uchafuzi unaharibu hewa na maji na kudhoofisha mifumo ya kinga ya wanyama na wanadamu.” Kisha anaongezea kauli ya Dakt. Epstein kwa kusema hivi: “Kwa kuwa wanadamu wameharibu mazingira, wamedhoofisha uwezo wa kiasili wa kukinza magonjwa na kutokeza hali zinazofanya viini viongezeke.”

Msukosuko wa kisiasa husababisha vita ambavyo huharibu mazingira na njia za usafiri zinazowasaidia watu kupata matibabu na chakula. Zaidi ya hilo, kituo cha Internet cha jumba fulani la makumbusho huko Marekani kinachoitwa Biobulletin kinasema hivi: “Kwa kawaida wakimbizi, walio dhaifu na wanaoteseka kwa sababu ya utapiamlo, huwekwa katika kambi zenye watu wengi mno na zenye uchafu mwingi, hivyo wao hukabili hatari ya kuambukizwa magonjwa.”

Matatizo ya kiuchumi huwalazimu watu kuhamia sehemu nyingine za nchi au nchi nyingine, na mara nyingi wao huhamia miji yenye watu wengi kupita kiasi. Kituo cha Biobulletin kinasema hivi: “Viini husitawi katika maeneo yenye watu wengi.” Idadi ya watu inapoongezeka sana, “mara nyingi miradi ya utunzaji wa afya hukwama, kama vile kuwaelimisha watu, kuwapa chakula bora, na kuwadunga sindano za chanjo.” Watu wanaposongamana sana, inakuwa vigumu kudumisha usafi kwa sababu ya kukosa maji na mifumo ya kuondoa maji machafu. Katika hali hizo, wadudu huongezeka na viini huenea. Hata hivyo, kama makala inayofuata inavyoonyesha, kungali na matumaini.

[Blabu katika ukurasa wa 11]

“Magonjwa mengi sugu yamezuka tena kwa sababu ya shughuli za wanadamu”

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 7]

Virusi vya West Nile Vyashambulia Marekani

Virusi vya West Nile, ambavyo huwapata wanadamu hasa wanapoumwa na mbu, viligunduliwa kwa mara ya kwanza huko Uganda mnamo mwaka wa 1937 na baadaye vikagunduliwa katika Mashariki ya Kati, Asia, Oceania, na Ulaya. Virusi hivyo viligunduliwa katika mabara ya Amerika mwaka wa 1999. Hata hivyo, tangu wakati huo imeripotiwa kwamba zaidi ya watu 3,000 wameambukizwa nchini Marekani na zaidi ya watu 200 wamekufa.

Ijapokuwa watu fulani huenda wakawa na dalili za ugonjwa huo, wengi hawajui kwamba wameambukizwa. Lakini wachache kati yao hupata magonjwa hatari kama vile ugonjwa wa kuvimba ubongo na homa ya uti wa mgongo. Kwa sasa hakuna chanjo wala tiba ya ugonjwa wa West Nile. Vituo vya Marekani vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa vinaonya kwamba watu wanaweza pia kuambukizwa virusi vya West Nile wanapopandikizwa viungo au wanapotiwa damu ya mtu aliye navyo. Shirika la habari la Reuters lilisema hivi katika mwaka wa 2002: “Kwa sasa hakuna njia ya kupima damu yenye virusi vya West Nile.”

[Hisani]

CDC/James D. Gathany

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 8, 9]

Jinsi Unavyoweza Kujikinga Madokezo Kadhaa

Waandishi wa Amkeni! walizungumza na wakazi wa maeneo yenye wadudu wengi na maeneo yanayokumbwa na magonjwa yanayoenezwa na wadudu ili kupata madokezo juu ya jinsi ya kudumisha afya bora. Huenda ukafaidika na mashauri yao.

Usafi Ndiyo Njia Bora ya Kujikinga

Dumisha usafi nyumbani

“Funika vyombo vyenye vyakula. Funika vyakula vilivyopikwa hadi vinapopakuliwa. Safisha sehemu zilizomwagikiwa na vyakula bila kukawia. Usiache vyombo vilale vikiwa vichafu wala usiweke takataka nje usiku ukikusudia kuzitupa asubuhi. Funika au ufukie takataka kwani wadudu na panya hutafuta chakula usiku. Pia, hata ikiwa nyumba ina sakafu ya udongo, ni vizuri kuilainisha kwa saruji kwani hilo litasaidia kuzuia wadudu wasiingie nyumbani na pia kudumisha usafi.”—Afrika.

“Hifadhi matunda au vitu vyovyote vinavyowavutia wadudu nje ya nyumba. Weka mifugo yako kama vile mbuzi, nguruwe, na kuku nje ya nyumba. Funika vyoo vilivyo nje ya nyumba. Funika mbolea ya samadi udongoni bila kukawia au uifunike kwa chokaa ili kuzuia nzi. Hata ikiwa majirani hawafanyi mambo hayo, unaweza kuwawekea mfano mzuri kwa kupunguza idadi ya wadudu.”—Amerika Kusini.

[Picha]

Mtu asipofunika vyakula au takataka ni kana kwamba anawaalika wadudu wale naye

Usafi wa mwili

“Sabuni si bei ghali, kwa hiyo nawa mikono mara nyingi na ufue nguo mara nyingi, hasa baada ya kuwasalimu watu au kuwagusa wanyama. Usiguse mizoga ya wanyama. Epuka kushika-shika mdomo, pua, na macho. Nguo zinapasa kufuliwa kwa ukawaida hata ikiwa zinaonekana kuwa safi. Marashi fulani huwavutia wadudu, kwa hiyo epuka sabuni zenye marashi.”—Afrika.

Njia za Kujikinga

Haribu maeneo ambapo mbu huzaana

Funika tangi za maji na beseni za kufulia nguo. Haribu vyombo vyote vya kutekea maji ambavyo havina vifuniko. Usiache maji katika vyombo vya kuwekea maua. Mbu wanaweza kutaga mayai katika maji ya kidimbwi ambayo hayajasonga kwa muda wa siku nne.—Kusini-Mashariki mwa Asia.

Jikinge na wadudu

Epuka kuwa nje wakati wadudu wengi wanapoanza kutokea na uepuke pia sehemu zote zenye wadudu. Jua hutua mapema katika maeneo ya kitropiki, kwa hiyo shughuli nyingi hufanywa usiku wakati wadudu wanapokuwa watendaji zaidi. Wakati magonjwa yanapozuka, ni rahisi kuambukizwa ikiwa utaketi na kulala nje.—Afrika.

[Picha]

Mtu anapolala nje katika maeneo yenye mbu wengi ni kana kwamba anawaalika wamtafune

Vaa mavazi yanayofunika mwili vizuri, hasa unapotembea msituni. Jipake dawa ya kufukuza wadudu ngozini na kwenye mavazi yako na ufuate maagizo yaliyoonyeshwa. Baada ya kutembea nje, angalia ikiwa wewe au watoto wako mna kupe. Wasafishe wanyama wako ili wasiwe na wadudu na uwatunze ifaavyo.—Amerika Kaskazini.

Epuka kuwa karibu na mifugo mara nyingi kwani unaweza kuambukizwa ugonjwa ukiumwa na wadudu waliowauma mifugo hao.—Asia ya Kati.

Washiriki wote wa familia wanapaswa kutumia vyandarua, hasa vyandarua vilivyotiwa dawa ya kuwafukuza wadudu. Weka nyavu dirishani, na uzitengeneze zinapoharibika. Ziba nyufa zilizo pembeni mwa paa la nyumba ambapo wadudu wanaweza kuingia. Njia hizo za kujikinga zinagharimu kiasi fulani cha pesa, lakini unaweza kupoteza pesa nyingi sana ikiwa utalazimika kumpeleka mtoto hospitalini au mtu anayetegemewa katika familia anapougua.—Afrika.

[Picha]

Vyandarua vilivyotiwa dawa za kuwafukuza wadudu havigharimu pesa nyingi kama matibabu

Wazuie wadudu wasijifiche mahali popote nyumbani mwako. Piga lipu ukutani na kwenye dari, na uzibe nyufa na mashimo. Ikiwa nyumba imeezekwa kwa nyasi, funika dari hilo kwa kitambaa cha kuwazuia wadudu. Ondoa vitu vilivyorundamana kama vile marundo ya karatasi, marundo ya nguo, au picha nyingi zilizowekwa ukutani, kwani huko ndiko wadudu hujificha.—Amerika Kusini.

Watu wengine hudhani kwamba wadudu na panya ni wageni waheshimiwa. La hasha, wao si wageni! Usiwakaribishe kamwe. Tumia dawa za kuwafukuza na za kuwaua wadudu, lakini usisahau kufuata maagizo yaliyoonyeshwa. Tumia mitego ya nzi na vifaa vya kuwaua nzi. Uwe mbunifu: Mwanamke mmoja alitumia kitambaa kutengeneza mfuko, kisha akajaza mchanga katika mfuko huo na akauweka chini ya mlango ili kuwazuia wadudu wasiingie ndani ya nyumba.—Afrika.

[Picha]

Wadudu si wageni waheshimiwa. Wafukuze!

Njia za kuzuia magonjwa

Imarisha mfumo wako wa kinga kwa kula vizuri, kupumzika vya kutosha, na kufanya mazoezi. Jitahidi kupunguza mfadhaiko.—Afrika.

Wasafiri: Jitahidini kupata habari za karibuni kuhusu visababishi vya magonjwa yanayoenezwa na wadudu. Habari hizo zinaweza kupatikana kwenye idara za afya na vituo vya Internet vya serikali. Kabla ya kusafiri, tumia dawa za kuzuia magonjwa ambayo hupatikana mahali unaposafiri.

Ukihisi U Mgonjwa

Mwone daktari haraka

Magonjwa mengi yanaweza kutibiwa iwapo yanagunduliwa mapema.

Hakikisha ugonjwa wako umetambuliwa kwa usahihi

Waone madaktari wanaotibu magonjwa yanayoambukizwa na wadudu na ikiwa umetembelea maeneo ya kitropiki mwone daktari anayetibu magonjwa yanayopatikana huko. Mweleze daktari dalili zako zote na maeneo yote ambayo umesafiri, hata sehemu ulizozitembelea zamani. Tumia dawa ikiwa lazima, na umalize vidonge vyote.

[Picha]

Magonjwa yanayoenezwa na wadudu yanaweza kufanana na magonjwa mengine. Mweleze daktari sehemu zote ulizozitembelea

[Hisani]

Globe: Mountain High Maps® Copyright © 1997 Digital Wisdom, Inc.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 10]

Je, Wadudu Hueneza Virusi vya UKIMWI?

Baada ya kufanya utafiti kwa zaidi ya miaka kumi, wataalamu wa wadudu na wanasayansi wa kitiba hawajapata uthibitisho wowote unaoonyesha kwamba mbu au wadudu wengine hueneza virusi vya HIV vinavyosababisha UKIMWI.

Kwa mfano, mdomo wa mbu si kama sindano, kwani hauna njia moja tu ya kupitisha damu. Badala yake, mbu hufyonza damu kupitia njia moja na huondoa mate kupitia njia nyingine. Kisha, kulingana na Thomas Damasso, mtaalamu wa virusi vya UKIMWI anayefanya kazi katika Kikosi cha Utunzaji wa Afya cha Wilaya katika mji wa Mongu, Zambia, mfumo wa mbu wa kumeng’enya chakula huvunja-vunja damu na kuharibu virusi hivyo. Virusi vya UKIMWI havipatikani katika kinyesi cha wadudu. Tofauti na vimelea vya malaria, virusi vya UKIMWI haviingii katika tezi za mate za mbu.

Mtu huambukizwa virusi vya UKIMWI anapopata damu nyingi yenye virusi hivyo. Mbu hawezi kumwambukiza mtu virusi hivyo kwani damu inayobaki mdomoni mwake ni kidogo sana, hata ikiwa amemuuma baada tu ya kumuuma mtu mwingine mwenye UKIMWI. Wataalamu wanasema kwamba hata ukimgonga mbu aliye na damu nyingi yenye virusi vya UKIMWI juu ya kidonda, hutaambukizwa virusi hivyo.

[Hisani]

CDC/James D. Gathany

[Picha katika ukurasa wa 7]

Kupe wanaoishi kwenye miili ya mbawala (picha kubwa kulia) wanawaambukiza wanadamu ugonjwa wa Lyme

Kushoto hadi kulia: kupe wa kike aliyekomaa, wa kiume aliyekomaa, na mtoto wa kupe, wote wana ukubwa wa kawaida

[Hisani]

All ticks: CDC

[Picha katika ukurasa wa 10, 11]

Mafuriko, uchafu, na uhamaji huchangia kuenea kwa magonjwa yanayosambazwa na wadudu

[Hisani]

FOTO UNACIONES (from U.S. Army)