Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Magonjwa Yanayoenezwa na Wadudu Yanaongezeka

Magonjwa Yanayoenezwa na Wadudu Yanaongezeka

Magonjwa Yanayoenezwa na Wadudu Yanaongezeka

NI WAKATI wa kulala huko Amerika Kusini. Mama mmoja anamlaza mtoto wake kitandani, anamfunika vizuri, na kumtakia usiku mwema. Lakini usiku huo mdudu mweusi mwenye urefu wa sentimeta tatu hivi ambaye huuma karibu na mdomo anatoka kwenye maficho yake katika dari la nyumba. Bila kujulikana, anamwangukia mtoto huyo usoni na kuuma ngozi yake nyororo kwa mdomo wake mrefu. Mdudu huyo ananyonya damu ya mtoto na kuacha kinyesi chake chenye vimelea. Akiwa angali usingizini, mtoto huyo anajikuna usoni na kueneza kinyesi hicho kwenye kidonda chote.

Kupitia kidonda hicho, mtoto huyo anaambukizwa maradhi ya Chagas. Baada ya juma moja hivi, anaugua homa na mwili wake unafura. Asipokufa, vimelea hivyo vinaweza kukaa mwilini mwake vikishambulia moyo, neva, na chembe zake. Huenda miaka 10 hadi 20 ikapita bila dalili zozote kuonekana. Hata hivyo, baadaye anaweza kupata vidonda katika mfumo wake wa kusaga chakula, kuathiriwa sehemu fulani ya ubongo, na hatimaye kufa kwa sababu ya moyo kushindwa kufanya kazi.

Hadithi hiyo ya kuwaziwa inaonyesha jinsi maradhi ya Chagas huambukizwa. Huko Amerika Kusini, mamilioni ya watu wamo katika hatari ya kuambukizwa maradhi hayo ambayo huua.

Wadudu Wanaoishi na Wanadamu

Kitabu Encyclopædia Britannica kinasema hivi: “Magonjwa mengi ya kuambukizwa husababishwa na viini ambavyo huenezwa na wadudu.” Neno “wadudu” hutumiwa kurejelea wale wenye miguu sita kama nzi, viroboto, mbu, chawa, na mbawakavu, na pia walio na miguu minane kama vile kupe na utitiri.

Wadudu wengi hawadhuru watu, na wengine ni muhimu sana. Bila wadudu fulani, mimea na miti mingi ambayo wanadamu na wanyama hutegemea kwa chakula haiwezi kuchavushwa na hivyo haiwezi kuzaa matunda. Wadudu wengine hugeuza takataka kuwa bidhaa zenye faida. Wadudu wengi hula mimea tu, na wengine hula wadudu wengine.

Ni kweli kwamba baadhi ya wadudu huudhi kwa sababu ya kuwauma watu na wanyama, au hawapendezi kwa kuwa wametapakaa kila mahali. Wengine huharibu mimea. Hata hivyo, wadudu fulani hueneza magonjwa na wengine husababisha kifo. Duane Gubler wa Vituo vya Marekani vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa alisema kwamba magonjwa yanayoenezwa na wadudu “yaliathiri na kuua watu wengi zaidi katika karne ya 17 hadi mwanzoni mwa karne ya 20 kuliko sababu nyingine zote zikijumlishwa pamoja.”

Leo, karibu mtu 1 kati ya watu 6 anaugua ugonjwa ambao umeenezwa na wadudu. Licha ya kusababisha mateso, inagharimu pesa nyingi kutibu magonjwa yanayoenezwa na wadudu hasa katika nchi zinazoendelea ambazo hazina uwezo mkubwa wa kifedha. Hata mlipuko mmoja wa ugonjwa unaweza kugharimu pesa nyingi sana. Kisa kimoja kama hicho kilichotokea magharibi mwa India mnamo mwaka wa 1994 kiligharimu nchi hiyo na nchi nyingine mamilioni ya pesa. Kulingana na Shirika la Afya Ulimwenguni, uchumi wa nchi maskini zaidi duniani hauwezi kusitawi mpaka magonjwa hayo yadhibitiwe.

Jinsi Wadudu Wanavyoambukiza Magonjwa

Wadudu huambukiza magonjwa kwa njia kuu mbili. Kwanza, wao hubeba viini hivyo nje ya miili yao. Kitabu Encyclopædia Britannica kinasema kwamba kama vile tu uchafu ulio chini ya viatu unavyoingizwa nyumbani, “ndivyo nzi wanavyoweza kubeba mamilioni ya viini miguuni mwao na kusababisha magonjwa.” Kwa mfano, nzi wanaweza kubeba uchafu kutoka chooni na kuutia kwenye chakula au kinywaji. Kupitia njia hiyo, wanadamu wanaweza kuambukizwa magonjwa hatari kama vile homa ya matumbo, kuhara damu, na kipindupindu. Nzi wanaweza pia kueneza mtoto wa jicho, ugonjwa unaowafanya watu wengi zaidi duniani wawe vipofu. Ugonjwa huo hupofusha kwa kuharibu sehemu inayofanana na kioo mbele ya jicho. Watu 500,000,000 duniani kote huugua ugonjwa huo.

Mende hukaa kwenye maeneo machafu, na inasemekana kwamba wao hubeba viini vya magonjwa juu ya miili yao. Isitoshe, wataalamu wanasema kwamba ongezeko la watu wanaougua pumu, hasa watoto, linasababishwa na mizio ya mende. Kwa mfano, siku nyingi Ashley, msichana mwenye umri wa miaka 15, hakuweza kupumua kwa sababu ya ugonjwa huo. Daktari alipokuwa akipima mapafu yake, mende alianguka kutoka kwenye shati lake na kutembea juu ya meza ya daktari.

Wadudu Ambao Hubeba Viini Mwilini

Wadudu wanaweza pia kubeba virusi, bakteria, au vimelea mwilini mwao, na kuvipitisha kwa wanadamu wanapouma au kwa njia nyinginezo. Ni wadudu wachache tu ambao hueneza magonjwa kwa wanadamu kwa njia hiyo. Kwa mfano, ingawa kuna maelfu ya aina za mbu, aina moja tu ya mbu anayeitwa Anopheles ndiye anayeeneza viini vya malaria. Ugonjwa huo huua watu wengi zaidi kati ya magonjwa yote ya kuambukizwa duniani (baada ya kifua kikuu).

Hata hivyo, aina nyingine za mbu hueneza magonjwa mengine mengi. Shirika la Afya Ulimwenguni laripoti hivi: “Kati ya wadudu wanaoeneza magonjwa, mbu ndio hatari zaidi kwa sababu wao hueneza malaria, kidingapopo, na homa ya manjano, magonjwa ambayo huua watu milioni kadhaa na kuwapata mamia ya mamilioni ya watu kila mwaka.” Angalau asilimia 40 ya watu duniani wamo katika hatari ya kuambukizwa malaria, na asilimia 40 hivi wamo katika hatari ya kupata ugonjwa wa kidingapopo. Katika sehemu nyingi, watu huambukizwa yote mawili.

Mbali na mbu, kuna wadudu wengine pia ambao hueneza magonjwa kupitia viini vilivyo ndani ya miili yao. Mbung’o hueneza viini vya protozoa ambavyo husababisha malale. Ugonjwa huo huwapata mamia ya maelfu ya watu na kufanya jamii nzima-nzima zihame na kuacha mashamba yao yenye rutuba. Wadudu wanaoitwa black flies hueneza upofu wa mtoni, na wamefanya watu wapatao 400,000 barani Afrika wawe vipofu. Wadudu wanaoitwa usubi hueneza protozoa ambao husababisha magonjwa fulani yanayolemaza, yanayoumbua sura, na mara nyingi kuua, na ambayo sasa yamewapata watu wengi wenye umri mbalimbali duniani kote. Kiroboto anayepatikana mahali pengi anaweza kueneza minyoo, uvimbe wa ubongo, ugonjwa wa tularemia, na hata tauni. Katika Zama za Kati (500 W.K. hadi 1500 W.K.), tauni ilisababisha vifo vya thuluthi moja ya watu au zaidi huko Ulaya katika kipindi cha miaka sita tu.

Chawa, utitiri, na kupe wanaweza kueneza magonjwa mbalimbali ya typhus na mengineyo. Kupe katika maeneo yenye joto la wastani wanaweza kueneza ugonjwa hatari wa Lyme unaopatikana sana huko Marekani na Ulaya. Uchunguzi uliofanywa nchini Sweden ulionyesha kwamba ndege wahamaji wanaweza kubeba kupe umbali wa maelfu ya kilometa, na huenda wakahama na magonjwa hadi maeneo mengine. Kitabu Britannica kinasema kwamba “kupe husafirisha viini vingi vya magonjwa kuliko wadudu wengine wote (isipokuwa mbu).” Kwa kweli, kupe wanaweza kusafirisha viini aina tatu vya magonjwa na kupitisha vyote wanapomuuma mtu mara moja tu!

Magonjwa Yalitoweka kwa Muda

Wanasayansi waligundua kwamba wadudu hueneza magonjwa katika mwaka wa 1877. Tangu wakati huo, kampeni kabambe zimefanywa ili kuzuia na kuua wadudu hao. Mnamo mwaka wa 1939, dawa ya kuua wadudu ya DDT iligunduliwa, na kufikia miaka ya 1960, magonjwa ambayo huenezwa na wadudu hayakuwa tena tisho kubwa kwa afya ya umma nje ya Afrika. Sasa badala ya kuzuia wadudu, jitihada ilifanywa kutibu magonjwa hayo haraka kwa kutumia dawa. Watu hawakuona haja ya kufanya utafiti kuhusu wadudu na makao yao. Dawa mpya ziligunduliwa, na ilidhaniwa kwamba wanasayansi wangegundua dawa ambayo ingeweza kutibu magonjwa yote bila madhara yoyote. Magonjwa ya kuambukizwa yalikuwa yametoweka. Lakini baada ya muda yalirudi. Makala ifuatayo itaonyesha kwa nini yalirudi.

[Blabu katika ukurasa wa 3]

Leo, mtu 1 kati ya watu 6 anaugua ugonjwa unaoenezwa na wadudu

[Picha katika ukurasa wa 3]

Mdudu ambaye huuma mdomoni

[Picha katika ukurasa wa 4]

Nzi hubeba viini vya magonjwa miguuni

[Picha katika ukurasa wa 5]

Wadudu wengi hubeba viini vya magonjwa ndani ya miili yao

Nzi anayeeneza upofu wa mtoni

Mbu hueneza malaria, kidingapopo, na homa ya manjano

Chawa wanaweza kueneza magonjwa ya “typhus”

Viroboto hueneza uvimbe wa ubongo na magonjwa mengineyo

Mbung’o hueneza malale

[Hisani]

WHO/TDR/LSTM

CDC/James D. Gathany

CDC/Dr. Dennis D. Juranek

CDC/Janice Carr

WHO/TDR/Fisher

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 4]

Clemson University - USDA Cooperative Extension Slide Series, www.insectimages.org