Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

“Mvua Hainyeshi Kamwe Huku Lima”

“Mvua Hainyeshi Kamwe Huku Lima”

“Mvua Hainyeshi Kamwe Huku Lima”

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI PERU

Ukitembelea nchi ya Peru, huenda utamsikia mtu akisema: “Mvua hainyeshi kamwe huku Lima,” jiji kuu la nchi hiyo. Huenda ukashuku taarifa hiyo kwa kuwa tayari unatetemeka kwa sababu ya upepo mkali wenye unyevu mwingi.

JIJI la Lima liko katika jangwa kubwa linaloanza kwenye Pwani ya Pasifiki ya Amerika Kusini. Hilo ni mojawapo ya maeneo yenye hali ya hewa ya ajabu. Eneo hilo kavu linaanza kwenye Jangwa la Sechura lililoko kaskazini kabisa mwa Peru hadi kwenye Jangwa la Atacama lililoko kaskazini mwa Chile.

Jangwa hilo la pwani liko kati ya Milima ya Andes iliyochongoka na Bahari ya Pasifiki yenye maji safi ya bluu. Ukiwa mbali, unaweza kudhani hakuna kitu kingine ila vilima vyenye miamba na mchanga wa aina mbalimbali za kahawia. Miamba mingi imemomonyoka na kuanguka chini ya vilima. Miamba hiyo husonga polepole hadi baharini. Wakati mwingine, miamba hiyo husukumwa na mitetemo ambayo hutokea mara nyingi katika eneo hilo.

Miamba hiyo inapofika ufuoni, mawimbi yenye nguvu ya Bahari ya Pasifiki huiponda-ponda pole kwa pole na kuwa mchanga. Kisha mchanga huo hurundamana na kufanyiza umbo la mwezi mwandamo. Katika sehemu fulani za jangwa hilo kubwa, mvua haijanyesha kwa muda wa miaka 20 na ndiyo sababu eneo hilo ni mojawapo ya maeneo makavu zaidi duniani. Lakini ni nini kinachofanya eneo hilo liwe kavu hivyo?

Upande Mmoja wa Milima ya Andes Haupati Mvua

Pepo zinazovuma kutoka mashariki hadi magharibi huchangia hali hiyo. Pepo hizo huinuliwa zinapogonga Milima mirefu ya Andes iliyochongoka. Pepo hizo zinapojaribu kuvuka milima hiyo, zinakuwa baridi, na mvuke ulio katika pepo hizo huganda. Kisha mvua hunyesha au theluji huanguka, hasa kwenye upande wa mashariki wa milima hiyo. Hivyo, milima hiyo huzuia mvua isinyeshe upande wa magharibi.

Isitoshe, Mkondo baridi wa Peru, au Mkondo wa Humboldt, unaotoka kwenye Ncha ya Kusini na vilevile upepo unaovuma kutoka Pasifiki Kusini hauna mvuke mwingi. Mambo hayo yote hufanya eneo hilo liwe jangwa kavu lisilokuwa na joto. Inashangaza kwamba ijapokuwa mvua ni haba, hewa huwa na unyevu mwingi sana, hasa wakati wa baridi kali, kuanzia Mei hadi Novemba. Unyevu huo hutoka wapi?

Ukungu wa Garúa

Wakati wa baridi kali, mawingu mazito hutanda karibu sana na pwani, na ukungu mzito, ambao Waperu huuita garúa, hutoka kwenye Bahari ya Pasifiki na kufunika eneo hilo. Wakati huo, jua linaweza kukosa kuonekana kwa miezi kadhaa na kusababisha baridi kali ambayo watu wengine husema kwamba ni hali ya hewa isiyopendeza hata kidogo. Ijapokuwa eneo hilo ni la kitropiki, halijoto katika jiji la Lima wakati wa baridi kali huwa kati ya nyuzi 16 na 18 Selsiasi. Wakati wa baridi kali, unyevu wa hewa unaweza kufikia asilimia 95 bila ya mvua kunyesha, na wenyeji wa Lima, wanaoitwa Limeños huvaa mavazi ya kujikinga na baridi hiyo kali. *

Manyunyu yanayonyesha wakati wa baridi kali hulowesha barabara za Lima na kuotesha mimea ya jangwani iliyo kwenye vilima virefu vya pwani. Makundi makubwa ya mbuzi, kondoo, na ng’ombe hufaidika kutokana na mimea hiyo inayositawi. Isitoshe, tangu mwanzoni mwa miaka ya 1990, wakaaji wa miji fulani katika jangwa hilo wamekuwa wakitumia nyavu kubwa za plastiki ili kukusanya maji ya ukungu kutoka kwenye mawingu yaliyojaa ukungu. Wao hutumia maji hayo kwa ajili ya kunywa na kunyunyizia mashamba.

Hata hivyo, maji hayo yanayotokana na ukungu na mawingu hayawezi kusitawisha mimea mwaka mzima. Kiasi chote cha maji kinachopatikana kila mwaka kutokana na mawingu huko Lima hakizidi milimeta 50, na maji mengi hutokana hasa na ukungu wa garúa. Basi, mimea ya kijani ambayo husitawi katika jangwa hilo la pwani ni ile inayopata maji kutoka kwenye vijito vinavyotiririka kutoka kwenye Milima ya Andes yenye theluji. Mtu anapotazama vijito hivyo kutoka angani, anaweza kudhani kwamba tepe za kijani zimetandikwa kwenye jangwa hilo.

Kukabiliana na Ukame

Ili kukabiliana na hali hiyo ya ukame, wenyeji wa kale wa Peru, kama vile Wachimu na Wamochica, walitengeneza mifumo tata ya kunyunyiza maji mashambani. Mbinu hiyo ya kilimo ilikuwa kama ile iliyotumiwa na Wamisri wa kale, na ilitegemeza makabila mengi yaliyokuwa yamestaarabika. Wenyeji wa Peru walitumia matofali yaliyochomwa kujenga miji mikubwa yenye mahekalu ya piramidi, kuta kubwa, na hifadhi mbalimbali. Kwa sababu ya ukosefu wa mvua, magofu ya majengo hayo yamedumu hadi leo hii. Hivyo, wachimbaji wa vitu vya kale wamegundua vitu vinavyoonyesha jinsi maisha yalivyokuwa huko Peru kabla ya mwaka wa 1500 W.K. Hadi leo hii, wenyeji wa maeneo mengi ya pwani bado wanategemea mifereji na mitaro iliyochimbwa maelfu ya miaka iliyopita.

Udongo wa jangwa hilo una rutuba sana katika sehemu zenye maji, na wenyeji wa kale wa eneo hilo walijua jambo hilo. Miradi ya kilimo cha kunyunyizia maji mashamba kwenye pwani ya Peru huandaa maji ya kutosha ili kuzalisha mazao kama vile pamba, mpunga, mahindi, miwa, mizabibu, mizeituni, mboga ya asparaga, na mboga nyingine na matunda mengine. Kwa sasa, zaidi ya nusu ya wale wakaaji milioni 27 wa Peru huishi kwenye eneo la pwani.

Mvua Inaponyesha

Hata hivyo, nyakati nyingine mvua hunyesha kwenye sehemu fulani za jangwa hilo, na pia katika jiji la Lima. Kila baada ya miaka michache, Mkondo baridi wa Peru hutokeza maji yenye joto. Maji hayo hutoka magharibi mwa Bahari ya Pasifiki. Tukio hilo huitwa El Niño, nalo huonyesha kwamba mvua iko karibu. Mvua kubwa ya El Niño ilinyesha hasa katika mwaka wa 1925, 1983, na 1997/1998. Ama kwa hakika, wakaaji wa jangwa hilo, ambao hawajazoea kupata mvua hata kidogo, huwa hawajajitayarishia mvua hiyo kubwa na mafuriko yanayosababishwa nayo.

Kwa mfano, jiji la Ica huko Peru, lilikumbwa na mafuriko katika mwaka wa 1998. Mto Ica ulifurika na maji hayo yakasambaa katika sehemu nyingi za jiji hilo na kufagia nyumba za matofali. Maeneo mengine ya jangwa hilo yalifaidika kutokana na maji hayo na mimea ikasitawi. Mvua ya El Niño ya hivi karibuni ilifanya maua maridadi na mimea ya kijani isitawi katika Jangwa la Sechura, na hilo linatukumbusha ahadi ya Mungu kwamba siku moja ‘jangwa litachanua maua kama waridi.’ (Isaya 35:1) Mvua hiyo kubwa ilifanyiza pia ziwa kubwa katikati ya jangwa hilo. Inakadiriwa kwamba ziwa hilo lina urefu wa kilometa 300 na upana wa kilometa 40. Magazeti yaliliita ziwa hilo La Niña.

Ama kwa hakika, jangwa la pwani ya Peru ni mojawapo ya maajabu mengi yaliyopo duniani. Ijapokuwa mvua hainyeshi mara nyingi huku, kupitia kilimo cha kunyunyiza maji mashambani na kwa kutumia maji vizuri, mamilioni ya watu wanafurahia kuishi katika eneo hilo kavu.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 11 Katika majira ya kiangazi wakati halijoto zinapofika nyuzi 20 au 27 Selsiasi, wenyeji wa Lima hawahitaji tena kuvaa mavazi mazito bali wakati huo wao hujifurahisha kwenye fuo zao nyingi.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 27]

UTAJIRI KUTOKA KWA MBOLEA

Kwa maelfu ya miaka, mamilioni ya ndege wamekuwa wakila dagaa walio katika bahari iliyo kwenye pwani ya magharibi ya Peru. Kwa sababu ya uhaba wa mvua katika eneo hilo, kinyesi cha ndege hao kilirundamana sana kwa miaka mingi kwenye visiwa vya pwani na hata kikafikia urefu wa meta 30! Kabla ya Wahispania kuwasili huko, ilionwa kwamba kinyesi hicho kingekuwa mbolea nzuri na wakakiita guano, jina ambalo ni la Kihindi cha Kikuechua. Mwishoni mwa miaka ya 1800, mbolea hiyo ilikuwa ikiuzwa sana katika nchi za nje hadi wakati ambapo mbolea za kemikali zilipoanza kutumiwa. Kufikia wakati huo, marundo ya kinyesi yalikuwa yamekwisha. Mbolea ya guano inayotumiwa leo hutokana na kinyesi kinachoachwa na ndege hao kwa sasa.

[Ramani katika ukurasa wa 24]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

Lima

[Picha katika ukurasa wa 25]

Pwani ya Pasifiki iliyoko kusini mwa Lima

[Hisani]

© Yann Arthus-Bertrand/CORBIS

[Picha katika ukurasa wa 25]

Jangwa la Sechura lililoko kwenye pwani ya Peru

[Picha katika ukurasa wa 26]

Nyavu za kukusanya ukungu huko Mejía, Peru

Mitaro ya maji iliyochimbwa na Wainka bado inatumiwa huko Ollantaytambo, Peru

[Hisani]

▲ © Jeremy Horner/CORBIS; inset: Courtesy of the charity FogQuest; www.fogquest.org

[Picha katika ukurasa wa 26]

Mvua kubwa za El Niño zilisababisha mafuriko makubwa huko Ica, Peru, mnamo Januari 30, 1998

[Hisani]

AP Photo/Martin Mejia