Safari ya Kupendeza Sana Baharini
Safari ya Kupendeza Sana Baharini
NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI NORWAY
KILA jioni, meli moja hung’oa nanga katika jiji la Bergen, kusini-magharibi mwa Norway, na kusafiri kilometa 4,500 hivi kuelekea kaskazini kwa siku 11. Meli hiyo hupitia visiwa vingi, milango na mikono ya bahari, majiji, miji, na vijiji katika pwani maridadi sana ya Norway yenye miamba-miamba.
Watu wengi huiona safari hiyo ya baharini kuwa maridadi zaidi ulimwenguni. Lakini safari hiyo pia ina manufaa mengine, kama vile kusafirisha mizigo, kupeleka barua, na kubeba abiria hadi mwisho wake huko Kirkenes, katika Mzingo wa Aktiki wa dunia.
Meli huwezaje kusafiri kwenye barafu, hasa katika majira ya baridi kali wakati ambapo meli haziwezi kusafiri katika sehemu nyingine za eneo hilo? Ni kwa sababu pwani ya Norway hupata maji moto ambayo huletwa na pepo kutoka Atlantiki Kaskazini na pepo zenye joto la kadiri kutoka magharibi. Pepo hizo husawazisha hali ya hewa nchini Norway na kufanya maji yake kuwa tofauti na maji mengine ya eneo hilo. Kwa hakika, maji ya bandari za Norway huwa hayagandi hata wakati wa baridi kali.
Njia Kuu ya Baharini Yaanzishwa
Mwishoni mwa karne ya 19, kulitokea uhitaji wa kuunganisha makazi ya pwani kwa barabara, reli, au bahari, na ikaamuliwa kwamba usafiri wa meli ndio ungefaa. Hata hivyo, wakati huo ilikuwa vigumu kusafiri baharini, kwa sababu hata ingawa bahari haikuganda, ilikuwa hatari kuisafiria usiku au wakati hali ya hewa ilipokuwa mbaya.
Hasa kutokana na ustadi na bidii ya nahodha Richard With, huduma za kawaida za meli zilianzishwa mnamo Julai 2, 1893. Siku hiyo, meli ya kwanza iling’oa nanga huko Trondheim, kuelekea Hammerfest, jiji lililoko mbali zaidi kaskazini huko Ulaya. Ijapokuwa watu fulani walifikiri kwamba mambo yangekwenda mrama, meli hiyo iliwasili salama salimini. Baadaye bandari 34 ziliongezwa kati ya Bergen na Kirkenes, majiji ambayo meli hizo huanzia na kumalizia safari. Wakazi wa pwani wameiita njia hiyo Njia Kuu Na. 1 kwa sababu ya umuhimu wake na mafanikio ambayo yametokana nayo.
Leo, Njia Kuu Na. 1 hutumiwa na meli 11 za kisasa ambazo huondoka kila baada ya saa 24. Lakini kutokana na kuboreshwa kwa reli na barabara za pwani, meli hizo zimetumiwa hasa kuwasafirisha watalii na jambo hilo linaonyeshwa na muundo wa meli hizo.
Mandhari Zenye Kuvutia
Njia hiyo imezungukwa na miamba, fuo na vitu vingine. Kwa hiyo, kwa zile siku 11, abiria hufurahia mandhari nzuri sana ya Norway, kama vile vijiji vyenye watu wenye urafiki vinavyozungukwa na malisho yenye majani mabichi, vijiji vya wavuvi, mito ya barafu, milango ya bahari, milima yenye vilele vya theluji, miamba ya bahari yenye ndege wengi sana, maporomoko ya maji, na hata nyangumi.
Isitoshe, abiria wanaweza kuondoka melini na kutazama mandhari meli inapotia nanga. Katika mji wa Molde, kwa mfano, wanaweza kutazama Milima ya Romsdal Alps yenye vilele 87 vyenye theluji. Huko Ålesund na Trondheim, abiria wanaweza hata kuondoka kwa muda fulani kutoka melini na kutalii barabara zilizozungukwa na nyumba zenye usanii wa kipekee wa huko. Katika miji mingine, abiria fulani hata hukodi magari na kujiunga na meli katika bandari inayofuata.
Inapopita mji wa Bodø na Mlango wa Bahari wa Vest, meli hupitia Visiwa vya Lofoten. Hilo ni eneo lenye visiwa vingi vyenye milima-milima na vijiji vingi vya wavuvi wenye urafiki na lina urefu wa kilometa 175. Visiwa fulani vya Lofoten vilivyo karibu zaidi na pwani vina matumbawe na miamba inayochomoza kutoka baharini, na wakati mwingine huwa na taa au ishara ya kuongozea meli. Visiwa hivyo pia ni makao ya ndege wengi wa baharini, kama vile shakwe, membe, somateria, puffin, muresi, mnandi, kittiwake wa Atlantiki, razor-bill, na wakati mwingine aina fulani ya koikoi. Ndege hao ni wengi sana.
Kila majira ya baridi kali, eneo la Lofoten hujaa watu wenye mashua za kuvua aina fulani ya chewa. Eneo hilo pia lina nyangumi wengi. Abiria hufurahi wee wanapowatazama kwa karibu samaki hao wakubwa mno wakiruka na kurusha manyunyu ya maji hewani!
Wakati wa kiangazi, meli hutumia njia ya kuingia Mkono wa Bahari wa Troll. Njia ya kuingia katika mlango huo wa bahari ni nyembamba na ina miamba yenye miinuko mikali sana hivi kwamba unaweza kushika miamba iliyo kando ukinyoosha mkono wako. Nahodha hapaswi kupiga honi asije akafanya miamba iporomoke! Pia kuna milima yenye theluji kileleni yenye kuvutia sana hivi kwamba watu hufurahia kupiga picha eneo hilo.
Baada ya kupitia majiji mengine kadhaa na vijiji vya wavuvi, meli sasa huelekea upande wa mashariki, mahali ambapo wengi
wanapapenda sana. Kwa mfano, inapopita bandari ya Honningsvåg, abiria wanaweza kutembelea North Cape ambapo miamba huinuka kwa meta 300 kwenye kingo za Bahari ya Aktiki. Mandhari nzuri ajabu!Meli huwasili kwenye bandari ya mwisho ya Kirkenes iliyoko kaskazini, na kutia nanga kwa saa chache tu kabla ya kuanza safari yake ya kurudi Bergen. Safari ya kurudi kusini huwawezesha abiria kuona mandhari ambazo hawakuweza kutazama wakati walipokuwa wamelala katika safari ya kaskazini. Kwa mfano, katika Mzingo wa Aktiki, wanaweza kuona ukanda mrefu wa barafu wa Svartisen wenye ukubwa wa meta 370 za mraba. Kisha meli inapitia karibu na safu ya milima yenye kuvutia ya Seven Sisters, na Mlima Torghatten unaofanana na kofia yenye shimo katikati. Kati ya miji ya Måløy na Florø, meli hupita karibu na Mlima Hornelen wenye urefu wa meta 860, ambao una mwinuko mkali sana hivi kwamba nahodha hapaswi kupiga honi ili miamba isije ikaporomoka.
Nuru au Giza kwa Saa 24
Watalii wanaotumia barabara hiyo wakati wa kiangazi wanaweza kuona nuru kwa saa 24 katika safari nzima. Kwa kweli, sehemu kubwa ya Njia Kuu Na. 1 huwa katika “eneo ambalo jua huangaza hata usiku wa
manane,” kaskazini mwa Mzingo wa Aktiki. Jua huwaka usiku kucha katika majira hayo. Kwa mfano, huko North Cape, jua halitui kwa majuma 12 hivi!Hali huwa tofauti kabisa wakati wa baridi kali, yaani giza hufunika eneo hilo kwa muda mrefu. Lakini majira hayo huwa na umaridadi wake wakati anga, bahari, milima, na theluji zinapomulikwa na nuru hafifu ya jua ambalo halichomozi kabisa. Isitoshe, wakati huo wa baridi kali, anga hutokeza kivutio kizuri ajabu, yaani mianga ya kaskazini. Mianga hiyo hutokea wakati mawimbi ya jua yenye nishati yanapopenya angani na kutokeza mimweko yenye rangi ya kijani, manjano-kijani, na wakati mwingine mistari myekundu inayometameta, kuchezacheza na kujipindapinda.
Bila shaka, si lazima utumie meli ili ufurahie mandhari hizo za kupendeza. Unaweza kutembelea sehemu kubwa ya Norway kwa gari au gari-moshi kwani barabara na reli zimeenea kotekote nchini humu. Kwa wale ambao hawana pesa za kutosha, njia hizo za usafiri ni mwafaka. Hata hivyo, haidhuru njia unayochagua kutumia, jambo moja ni hakika—huwezi kuchoka kufurahia mandhari ya Norway yenye kupendeza sana ambayo hubadilika unaposafiri kila baada ya kilometa moja na majira baada ya majira.
[Ramani katika ukurasa wa 13]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
FINLAND
SWEDEN
NORWAY
OSLO
Njia ya baharini
▿ ▵ Bergen
▿ ▵ Florø
▿ ▵ Mȧløy
▿ ▵ Ȧlesund
▿ ▵ Molde
▿ ▵ Trondheim
MZINGO WA AKTIKI
Mnara wa ukumbusho kwenye Mzingo wa Aktiki
▿ ▵ Bodø
▿ ▵ Visiwa vya Lofoten
Mkono wa Bahari wa Troll
▿ ▵ Tromsø
▿ ▵ Hammerfest
▿ ▵ Honningsvȧg
▿ ▵ Kirkenes
[Hisani]
Based on map: Hurtigruten
[Picha katika ukurasa wa 15]
Mkono wa Bahari wa Troll uliozungukwa na milima mirefu
[Hisani]
TO-FOTO AS, Harstad
[Picha katika ukurasa wa 14]
Visiwa vya Lofoten vina ndege wengi wa baharini kama vile shakwe, muresi, na “puffin”
[Picha katika ukurasa wa 16]
Njia Kuu Na. 1 inaanzia Bergen
[Picha katika ukurasa wa 16]
Mnara wa ukumbusho kwenye Mzingo wa Aktiki
[Picha katika ukurasa wa 16]
Jua la usiku wa manane
[Hisani]
TO-FOTO AS, Harstad
[Picha katika ukurasa wa 16]
Milima ya Seven Sisters
[Hisani]
Per Eide
[Picha katika ukurasa wa 17]
Kijiji cha pwani katika majira ya baridi kali wakati wa usiku
[Picha katika ukurasa wa 17]
Mianga ya kaskazini
[Hisani]
© TO-FOTO AS, Harstad
[Picha katika ukurasa wa 17]
Safari inaishia Kirkenes
[Hisani]
Hallgeir Henriksen
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 13]
Nancy Bundt