Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Je, Unahisi Maadili Yamezorota?

Je, Unahisi Maadili Yamezorota?

Je, Unahisi Maadili Yamezorota?

“NI TATIZO gani linalowaathiri watu wengi zaidi katika nchi hii?” Watu wengi walipoulizwa swali hilo huko Marekani, walisema kwamba kuzorota kwa maadili na kuvunjika kwa familia ndiyo matatizo makubwa yanayowahangaisha. Watu wengine pia wana maoni kama hayo.

Kwa mfano, gazeti la Paris International Herald Tribune lilisema hivi: “Inaonekana vijana wanatafuta jambo la kuwaunganisha, yaani, wanatafuta maadili yanayoweza kutumiwa kukomesha matatizo ambayo yanaenea ulimwenguni kama vile pupa, ubinafsi, na ukosefu wa ushirikiano katika jamii. . . . Jitihada hizo za kutafuta maadili ya kuongoza ulimwengu wote zinaonyesha kwamba hakuna maadili.”

Je, unafikiri kwamba serikali, viongozi wa ulimwengu, na wafanyabiashara mashuhuri wana maadili yanayoweza kutuletea wakati ujao wenye furaha na ulio salama zaidi? Je, unahisi pengo fulani unapoona matokeo ya kuzorota kwa maadili?

Huenda jambo moja linalokuhangaisha sana ni usalama wako. Je, unaishi mahali ambapo unaweza kuacha mlango wako ukiwa wazi na usiibiwe vitu? Je, wewe huhisi ukiwa salama unapotembea barabarani usiku? Hata ikiwa unaishi katika eneo ambalo halina vita, fujo za kikabila, au mapigano kati ya magenge, huenda bado unaogopa kushambuliwa, kunyang’anywa vitu kwa nguvu, kuvamiwa na wakora nyumbani, au kuibiwa vitu. Mambo hayo yanaweza kukufadhaisha na kusababisha pengo maishani mwako.

Huenda pia umeacha kuwatumaini watu kwa kadiri fulani. Labda katika maisha yako na kazini umekutana na watu wanaotaka kukuumiza ili wajifaidi, hata ikiwa watafaidika kidogo tu.

Serikali Zinapaswa Kuweka Mfano Mzuri

Katika historia yote, maadili ya watu yameathiriwa sana na maadili ya viongozi wanaowatawala. Calvin Coolidge alisema hivi kabla hajawa rais wa Marekani: “Watu husema kwamba kuna haki za kiasili, lakini ningependa mtu ajitokeze na aniambie wakati hususa ambapo haki zozote zimekuwapo au zimetambuliwa, isipokuwa tu iwe ni baada ya sheria kutungwa ili kuzitambulisha waziwazi na kuzilinda.”

Kwa hakika, serikali inayotawala—hata iwe ilitumia njia gani kuingia mamlakani—ndiyo inayoweza kuruhusu au kuzuia haki za wanadamu kama vile uhuru wa vyombo vya habari, uhuru wa kukusanyika, uhuru wa kidini, uhuru wa kusema hadharani, haki ya kutokamatwa au kusumbuliwa bila idhini, na kupata hukumu ya haki.

Abraham Lincoln alisema hivi kabla hajawa rais wa Marekani: “Kusudi kuu la serikali ni kuwafanyia watu mambo wanayotaka kufanya, lakini ambayo hawawezi kujifanyia, au ambayo hawawezi kuyafanya vizuri kwa uwezo wao wenyewe wakiwa mmoja-mmoja.” Serikali zinapojitahidi kutimiza makusudi hayo mazuri, watu huwatumaini viongozi.

Hata hivyo, watu leo hawawatumaini viongozi na badala yake wana shaka na wasiwasi kuwahusu. Uchunguzi mmoja uliofanywa huko Marekani uliripoti kwamba asilimia 68 ya wale waliohojiwa walisema kuwa matendo ya maafisa wa serikali yanaridhisha kwa kadiri au hayaridhishi kabisa. Katika nchi nyingi watu wameacha kuwaamini maafisa wa serikali kwa sababu ya kashfa nyingi za hongo na ufisadi. Hiyo ndiyo sababu watu wengi leo wanahisi kuna pengo fulani maishani mwao.

Mfano Mzuri wa Mfalme Solomoni

Mfano mmoja wa kale unaonyesha jinsi maadili ya watawala yanavyoweza kuwa na athari kubwa sana. Mfalme Solomoni alitawala yale makabila 12 ya Israeli kuanzia mwaka wa 1037 hadi 998 K.W.K. Mfalme Daudi, baba yake, alikuwa mmoja wa wafalme wazuri wa Israeli. Biblia inasema kwamba Daudi alipenda kweli na uadilifu na, zaidi ya yote, alikuwa na imani na usadikisho thabiti katika Mungu wake, Yehova. Daudi alimfunza Solomoni maadili hayohayo.

Mungu Mweza-Yote alimtokea Solomoni katika ndoto na kumwambia: “Omba utakalo nikupe.” (2 Mambo ya Nyakati 1:7) Badala ya kuomba mali nyingi, utukufu, na ushindi wa kivita, Solomoni alionyesha maadili yake mema kwa kuomba moyo wa hekima, wa uelewevu, na mtiifu ili aweze kutawala taifa la Israeli vizuri.

Utawala wa Solomoni uliwaletea raia zake matokeo gani? Mungu alimbariki kwa kumpa hekima, utukufu, na utajiri maadamu aliendelea kufuata maadili ya kiroho ya taifa hilo. Vitu vilivyochimbuliwa vinathibitisha kwamba kulikuwa na ufanisi mwingi wakati wa utawala wa Solomoni. Kitabu The Archaeology of the Land of Israel kinasema: “Utajiri uliotoka pande zote na kuingia katika makao ya kifalme, na biashara iliyotia fora . . . zilileta maendeleo ya haraka ya kila aina.”

Naam, utawala mzuri wa Solomoni uliwaletea raia zake amani, usalama, na furaha. “Yuda na Israeli wakakaa salama, kila mtu chini ya mzabibu wake na chini ya mtini wake, tokea Dani mpaka Beer-sheba, siku zote za Sulemani.”—1 Wafalme 4:20, 25.

Mfano Mbaya wa Mfalme Solomoni

Hata hivyo, inasikitisha kwamba maadili ya Solomoni yalizorota kama vile maadili ya viongozi wengi wa leo. Biblia inasema hivi: “Akawa na wake mia saba binti za kifalme, na masuria mia tatu; nao wakeze wakamgeuza moyo. Maana ikawa, Sulemani alipokuwa mzee, wake zake wakamgeuza moyo wake, afuate miungu mingine, wala moyo wake haukuwa mkamilifu kwa BWANA, Mungu wake, kama moyo wa Daudi baba yake.”—1 Wafalme 11:3, 4.

Maadili ya Mfalme Solomoni yalipozorota, raia zake waliathiriwaje? Ijapokuwa alikuwa na uwezo mkubwa na hekima nyingi, Solomoni akawa mtawala mwonevu mwishoni-mwishoni mwa utawala wake. Uchumi wa taifa ulizorota sana kwa sababu ya matumizi mengi ya serikali yake. Wafanyakazi wake hawakuridhika. Wapinzani wa kisiasa wakampinga mfalme na wakapanga njama za kumpindua. Taifa likapoteza umoja. Inashangaza kwamba Solomoni mwenyewe ndiye aliyeandika hivi: “Wenye haki wakiwa na amri, watu hufurahi; bali mwovu atawalapo, watu huugua.”—Mithali 29:2.

Muda mfupi baada ya kifo cha Solomoni, msukosuko wa kisiasa na wasiwasi ulifanya taifa hilo ligawanyike na baadaye kukawa na magumu, mtengano, na hali zikazorota. Waisraeli walihisi pengo kubwa maishani mwao. Maadili ya serikali yao yalikuwa yamezorota, na ikaacha kuwajali. Tatizo kuu lilikuwa kwamba viongozi wao walimpuuza Yehova na sheria zake. Basi, taifa lote likaumia.

Watu Wengi Hawatumainiani Leo

Wakuu wengi katika serikali, biashara, na dini hawajali maadili yao. Hilo limewafanya watu wengi wahisi kuna pengo maishani mwao. Serikali na viongozi wanaendelea kushindwa kutatua matatizo ya msingi ya nchi zao.

Kwa mfano, wameshindwa kukomesha vita, kupunguza gharama zinazozidi kupanda za matibabu, au matokeo mabaya ya ulanguzi wa dawa za kulevya. Pia, elimu imeathiriwa. Serikali fulani-fulani hata huanzisha vituo vya kuchezea kamari. Vilevile, wafanyabiashara mashuhuri na viongozi wa dini wamehusika katika matendo ya kusikitisha ya ufisadi na upotovu wa maadili. Basi haishangazi kwamba watu wengi leo hawawatumaini viongozi.

Je, kweli inawezekana kwa serikali yoyote ile kulinda na kutegemeza haki na maadili ya wanadamu? Ndiyo, inawezekana. Makala ya mwisho itaeleza jinsi inavyowezekana.

[Blabu katika ukurasa wa 7]

Pupa, ubinafsi, na ukosefu wa ushirikiano katika jamii ni mambo yanayoenea ulimwenguni.’ —International Herald Tribune

[Picha katika ukurasa wa 8]

Mfalme Solomoni alipotii sheria za Mungu, aliwasaidia raia zake wawe na maadili mema