Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Umuhimu wa Kupanda Mimea Nyumbani

Watafiti wanasema kwamba “maelfu ya wanafunzi wangefanikiwa zaidi katika mitihani iwapo mimea ingepandwa kuzunguka shule yao,” laripoti gazeti The Times la London. Profesa Derek Clements-Croome wa Chuo Kikuu cha Reading amegundua kwamba gesi ya kaboni dayoksaidi katika madarasa yaliyo na wanafunzi wengi kupita kiasi na ukosefu wa hewa ya kutosha ni mara tano zaidi ya kiwango kinachohitajika, hivyo kuwafanya wanafunzi wasiwe makini na kuzuia maendeleo yao. Yeye anaita hali hiyo ugonjwa unaosababishwa na mazingira ya darasani na kusema kwamba idadi ya wanafunzi darasani ni mara tano zaidi ya ile ya wafanyakazi ofisini, ambapo “ugonjwa unaosababishwa na mazingira ya nyumba” huathiri wafanyakazi na kazi. Ni mimea gani inayoweza kutumiwa kuboresha hali hiyo? Uchunguzi mmoja uliofanywa nchini Marekani ulionyesha kwamba mimea inayoitwa spider inaweza kusaidia sana. Mimea ya dragon, ivy, rubber, peace lily, na yucca inaweza kusafisha hewa pia. Mimea hiyo hupunguza kiwango cha kaboni dayoksaidi na kuigeuza kuwa oksijeni.

Kizazi “Kisicho na Ujuzi”

“Vijana Wamarekani hawana ujuzi wa kutosha,” lasema gazeti la New York la Daily News. “Asilimia 11 hawajui mahali Marekani ilipo” katika ramani ya dunia. “Nusu yao hawawezi kuonyesha mahali jiji la New York lilipo katika ramani ya Marekani.” Kuhusu nchi nyingine ambazo hutajwa mara nyingi katika habari, asilimia 13 pekee ndio wanaojua mahali Iraki au Iran ilipo, na asilimia 17 tu ndio wanaojua mahali Afghanistan ipo. Asilimia 71 tu ya vijana Wamarekani wenye umri kati ya miaka 18 hadi 24 ndio wanaoweza kuonyesha bahari kubwa zaidi duniani, yaani Bahari ya Pasifiki. Shirika la National Geographic lilifanya uchunguzi huo kwa kuwapatia vijana 3,250 kutoka Italia, Japan, Marekani, Mexico, Kanada, Sweden, Ufaransa, Uingereza, na Ujerumani maswali 56. Ingawa hakuna taifa lililopata alama ya “A,” ambayo ilihitaji angalau alama 42, Sweden ilikuwa ya kwanza na alama 40, ikifuatwa na Ujerumani na Italia na alama 38 kila moja. Marekani ilikuwa ya pili kutoka mwisho na alama 23, na kushinda Mexico pekee iliyokuwa na 21. Msimamizi wa Shirika la National Geographic, John Fahey, aliuliza hivi: “Ikiwa vijana wetu hawajui kusoma ramani wala matukio ya kila siku, watawezaje kuelewa masuala ya kijamii, ya kiuchumi, na ya kiasili yanayotukabili?”

Kuvuna Ulichopanda Baada ya Umri wa Miaka 40

“Matokeo ya mambo ambayo mtu alichagua na mazingira alimokaa huanza kuonekana wakati anapofikisha umri wa miaka 40, anapoanza kuzeeka.” Mkataa huo ulifikiwa katika mkutano wa afya ulioripotiwa na gazeti The Daily Telegraph la Sydney, Australia. Kulingana na Rocco Di Vincenzo, mtaalamu mkuu wa Hospitali ya Swinburne huko Victoria, “‘kasoro katika chembe za urithi’ au kasoro za viungo” haziathiri mtu baada ya umri wa miaka 40 ikilinganishwa na machaguo aliyofanya kuhusu afya yake kabla ya wakati huo. “Sasa tunajua kwamba afya ya mtu baada ya umri wa miaka 40 inategemea mambo ambayo amerithi na mambo ya kimazingira,” anasema Di Vincenzo. “Kulingana na Taasisi ya Kitaifa ya Uzee, asilimia 80 ya matatizo ya afya ya watu wazee hayasababishwi na uzee, bali yanasababishwa na kukosa utunzaji mzuri maishani mwote. Matokeo ya kukosa utunzaji mzuri huanza kuonekana baada ya umri wa miaka 40.”

Watoto Huwa Wazoefu wa Sigara Haraka

“Watoto wanaweza kuwa wazoefu wa tumbaku siku chache tu baada ya kuanza kuvuta sigara na hata wanaweza kuwa wazoefu kutokana na sigara ya kwanza,” unasema uchunguzi mmoja uliochapishwa katika gazeti la London, The Guardian. “Kati ya vijana 332 waliowahi kujaribu kuvuta sigara hata mara moja, asilimia 40 walisema waliona dalili za uzoefu. Kati ya 237 ambao walivuta moshi wa sigara hadi mapafuni, asilimia 53 waliona dalili za uzoefu.” Utafiti huo wa miezi 30, ulioongozwa na Dakt. Joseph DiFranza wa Taasisi ya Tiba ya Chuo Kikuu cha Massachusetts, Marekani, ulichunguza karibu wanafunzi 700, waliokuwa na umri wa miaka 12 na 13 mwanzoni mwa uchunguzi. “Kabla ya uchunguzi huo ilidhaniwa kwamba ilichukua miaka miwili kwa vijana kuwa wazoefu wa tumbaku, na kwamba walihitaji kuvuta sigara kila siku, angalau nusu pakiti kwa siku,” asema DiFranza. “Baadhi ya vijana hao walianza kuwa wazoefu baada ya kuvuta sigara kwa siku chache. . . . Nafikiri kwamba mara nyingi mtu huwa mzoefu anapovuta sigara ya kwanza.” DiFranza anaamini kwamba vijana huwa wazoefu haraka kwa sababu bongo zao bado zinakua. “Ningependa vijana wafahamu kwamba hawawezi kujaribu kuvuta sigara na waepuke kuwa wazoefu. Huwezi kuvuta sigara bila kupatwa na matokeo mabaya,” anasema. “Tunahitaji kuwasadikisha vijana kwamba kujaribu kuvuta hata sigara moja kunaweza kuwafanya wawe wazoefu katika maisha yao yote.”

Habari Mpya Kuhusu “Njozi” za Wanaougua Kifafa

Kulingana na shirika la habari za kisayansi la Ujerumani Bild der Wissenschaft-Online, wataalamu wa mfumo wa neva huko Uswisi walitumia vyuma vilivyopitishwa nguvu za umeme kuchunguza kinachosababisha wanawake wapate mipapatiko ya kifafa. Bila kukusudia, jambo hilo lilimfanya mgonjwa aone njozi. Wakati kiungo fulani cha tabaka la nje la upande wa kulia wa ubongo kilipoguswa, mwanamke huyo alisema kwamba aliona ni kana kwamba alitenganishwa na mwili wake na akautazama akiwa juu. Inadhaniwa kiungo hicho huunganisha picha za mambo tunayotazama na hisi zinazoonyesha mahali mwili ulipo. Shirika la Bild der Wissenschaft linasema kwamba “msisimuko unaosababishwa na umeme ulikatiza muungano huo, na hivyo mgonjwa akahisi akiwa nje ya mwili wake.” Njozi hizo “zimefanya watu wafikiri tena na tena kwamba nafsi inaweza kutenganishwa na mwili.”

Rosari Imeboreshwa

“Kwa miaka 500, Wakatoliki washupavu wamekuwa wakitumia rosari kukariri sala kama vile Baba Yetu na Salamu Maria kwa kusudi la kumsaidia mtu akumbuke matukio au ‘mafumbo’ 15 katika maisha ya Yesu na ya mama yake,” laripoti gazeti Newsweek. “Katika [Oktoba] mwaka jana, Papa John Paul wa Pili aliandika barua ya utume ambapo aliongeza duru ya nne ya rosari,” inayohusu huduma ya Yesu tangu alipobatizwa hadi Mlo wa Jioni. “Kusudi la papa ni kufanya sala hiyo ‘anayopenda sana’ ivutie, kwa sababu umaarufu wake umepungua tangu Mkutano wa Pili wa Vatikani,” gazeti hilo linaongeza kusema. “Papa anakusudia kuifanya sala hiyo ambayo hutumiwa na Wakatoliki pekee imkazie Kristo zaidi kuliko Maria, kwani Maria huonwa kuwa muhimu zaidi katika rosari.” Papa alisema inatarajiwa jambo hilo litawafanya Wakatoliki wawe na zoea la kutafakari, “kwani Ukristo unaathiriwa na njia ya kutafakari ya dini za Mashariki.”

Wanatarajia Mengi Kupita Kiasi

“Ndoa nyingi nchini Ujerumani hukosa kufanikiwa kwa sababu ya matumaini mengi kupita kiasi,” lasema gazeti Die Welt. Kulingana na Profesa Wassilios Fthenakis, anayechunguza maisha ya familia, “watu hutamani kupendwa sana na kuwa na furaha nyingi katika ndoa yao.” Hata hivyo, alisema kwamba haifai kutarajia msisimuko huo udumu kwa miaka mingi. Kwa kuwa sasa watu wanahangaikia furaha yao na kufikia miradi yao binafsi, wenzi wa ndoa hawako tayari kushirikiana ili kutatua matatizo. Mtaalamu mwingine wa maisha ya familia alisema hivi: “Leo msisimuko unapoisha, watu hawafanyi jitihada yoyote ya kuzungumza na kutatua matatizo ili kuokoa ndoa yao.” Kwa wastani, ndoa nchini Ujerumani zinadumu kwa miaka 12 hivi siku hizi.