Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Maji Ni Muhimu kwa Uhai

Maji Ni Muhimu kwa Uhai

Maji Ni Muhimu kwa Uhai

YESU alimweleza mwanamke mmoja Msamaria aliyekuwa akichota maji kuhusu maji yanayobubujika kuwapa watu uzima wa milele. (Yohana 4:14) Ijapokuwa hakuwa akizungumzia maji halisi, maji ni muhimu kwa uhai na ndicho kitu cha pili kilicho muhimu zaidi baada ya oksijeni. Mtu anaweza kuishi kwa majuma kadhaa bila kula chakula lakini hawezi kuishi kwa zaidi ya siku tano bila maji!

Maji yanafanyiza karibu robo tatu ya uzito wa mwili wetu. Kwa mfano, maji yamefanyiza asilimia 75 hadi 85 ya ubongo, na asilimia 70 ya misuli. Maji hufanya mambo mengi kama vile kumeng’enya na kupeleka chakula kwenye chembe. Maji huondoa sumu na uchafu mwingine mwilini, hulainisha viungo na utumbo mpana, na kusawazisha joto la mwili. Lakini je, unajua kwamba kunywa maji ya kutosha husaidia kupunguza uzito?

Kunywa Maji Upunguze Uzito

Kwanza kabisa, maji hayana kalori, mafuta, kolesteroli, na hayana sodiamu nyingi. Pili, maji hupunguza hamu ya kula. Tatu, maji husaidia kuvunjavunja mafuta yaliyohifadhiwa mwilini. Jinsi gani? Figo zinapokosa maji ya kutosha, haziwezi kufanya kazi vizuri. Hivyo, ini huanza kufanya kazi hiyo, lakini jambo hilo huzuia uwezo wake wa kuvunjavunja mafuta mwilini. Hivyo, mafuta hubaki mwilini na kumfanya mtu aongeze uzito. Hivyo, kama vile Dakt. Donald Robertson wa kituo fulani cha elimu ya lishe bora huko Scottsdale, Arizona, Marekani anavyosema, “kunywa maji ya kutosha husaidia kupunguza uzito. Iwapo watu ambao wanajaribu kupunguza uzito hawanywi maji ya kutosha, miili yao haitaweza kuvunjavunja mafuta kabisa.”

Ni kweli kwamba mara nyingi maji yanapobaki mwilini, hufanya uzito wa mwili uongezeke. Hivyo, watu wengi walio na tatizo hilo hudhani kwamba suluhisho ni kutokunywa maji mengi. Lakini sivyo ilivyo. Mwili usipopata maji ya kutosha utahifadhi maji yoyote yaliyosalia mwilini kwenye miguu na mikono. Kwa hiyo wataalamu wa elimu ya lishe wanapendekeza kwamba tunywe maji ya kutosha kwani mwili unayahitaji. Pia, kumbuka kwamba kadiri unavyokula chumvi ndivyo maji mengi zaidi yatakavyobaki mwilini ili kuiyeyusha.

Ongeza Maji Mwilini

Kila siku, sisi hupoteza kwa wastani lita mbili za maji kupitia ngozi, mapafu, matumbo, na figo. Kila siku sisi hupoteza karibu nusu lita ya maji tunapopumua. Tusipokunywa maji zaidi, maji yataisha mwilini. Dalili za kuishiwa maji mwilini ni kuumwa na kichwa, uchovu, maumivu ya misuli, mkojo wenye rangi, kutoweza kuvumilia joto, na kukauka mdomo na macho.

Basi, tunapaswa kunywa kiasi gani cha maji? Dakt. Howard Flaks, mtaalamu wa tatizo la kunenepa kupita kiasi, anasema hivi: “Kiasi cha chini kabisa ambacho mtu mwenye afya anahitaji kunywa ni lita mbili au lita mbili u nusu kwa siku. Unahitaji kunywa maji mengi zaidi ikiwa wewe hufanya mazoezi sana au unaishi katika eneo lenye joto. Watu waliozidi uzito wa kawaida wanapaswa kunywa robo lita zaidi ya maji kwa ajili ya kila kilogramu 10 za ziada za uzito wao.” Hata hivyo, siku hizi watu wengine wanasema kwamba inatosha kunywa maji wanapokuwa tu na kiu. Lakini huenda ikawa tayari umeishiwa maji unapoona kiu.

Je, inafaa kunywa vinywaji vingine badala ya maji? Ingawa si vibaya kunywa vinywaji vilivyotengenezwa kwa matunda na mboga na kisha vikaongezwa maji, bado vinywaji hivyo vina kalori. Pia, vinywaji vyenye sukari na maziwa mengi huufanya mwili uhitaji maji zaidi ili vitu hivyo vimeng’enywe. Isitoshe, kwa kadiri fulani vileo na vinywaji vyenye kafeini kama vile kahawa na chai humfanya mtu aende haja ndogo mara nyingi na hivyo kumlazimu anywe maji zaidi ili kurudisha maji yaliyopotea. Naam, hakuna kinywaji kingine kinachoweza kutimiza kazi muhimu ya maji. Basi, mbona usinywe glasi moja sasa?

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 12]

Jinsi Unavyoweza Kunywa Maji Mengi Zaidi

● Beba chupa ya maji.

● Unywe maji kila unapokula.

● Unywe maji kabla ya kufanya mazoezi, wakati unapoyafanya, na baada ya mazoezi.

● Saa za chai zinapofika, kunywa maji.

● Ili kuboresha ladha ya maji ya mfereji, ongeza maji ya limau au uyachuje.

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 12]

Photo: www.comstock.com