Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Mbuga ya Kitaifa ya Nairobi Ambapo Wanyama Wako Huru

Mbuga ya Kitaifa ya Nairobi Ambapo Wanyama Wako Huru

Mbuga ya Kitaifa ya Nairobi Ambapo Wanyama Wako Huru

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI KENYA

NI SAA 12 na nusu asubuhi. Jua linalochomoza upande wa mashariki linafanana na johari kubwa jekundu lenye kupendeza sana. Huku kukiwa kumepambazuka, miali ya jua inapenya madirisha ya majengo marefu na kufanyiza rangi maridadi ya manjano. Mwendo mfupi kutoka kwenye majengo hayo, kuna tukio halisi lenye kusisimua linaloendelea.

Kwa muda fulani, simba aliyejificha kwenye nyasi ndefu, amekuwa akimnyemelea swara anayelisha. Swara anatambua hatari na kutimua, na simba anamfuata unyounyo. Kukurukakara za mbio zinaanza. Akifaulu, simba atamnyafua mnyama huyo maskini.

Matukio kama hayo hurudiwa-rudiwa kila siku katika Mbuga ya Kitaifa ya Nairobi, iliyoko viungani mwa jiji kuu la Kenya, Nairobi. Wanyama katika mbuga hiyo huishi karibu na watu. Ndiyo sababu mnamo mwaka wa 1962, simba mmoja alionekana akizurura karibu na hoteli moja ya kifahari, labda akijaribu kunyakua makazi yake mapana ya zamani. Wanyama walikujaje kuishi karibu na wakazi wa jiji?

Mwanzo Wenye Matatizo Mengi

Haikuwa rahisi kuanzisha mbuga hiyo. Ilikuwa lazima kwanza kutatua matatizo fulani ili wanyama waweze kufurahia kuishi katika mbuga inayolindwa vizuri. Kabla ya karne ya 20, wanyama walizunguka-zunguka kwa uhuru katika eneo kubwa la Afrika Mashariki. Katika eneo hili, watu walikuwa na uhusiano mzuri na wanyama wa mwitu, wakilisha mifugo yao karibu nao. Wengine hata waliwaona wanyama hao kuwa mifugo wao wa kipekee!

Lakini, wawindaji waliojihami kwa bunduki walimiminika nchini, wengi wakiwa na nia ya kuwinda wanyama ili wapate tuzo nyingi iwezekanavyo. Mmoja wao alikuwa rais wa zamani wa Marekani, Theodore Roosevelt, aliyekuja Kenya katika mwaka wa 1909 kukusanya vitu vya kale ili kuviweka katika vyumba vya makumbusho. Akiwa na wachukuzi 600 na wawindaji wenye uzoefu, aliwaua wanyama zaidi ya 500 na kuzisafirisha ngozi zao nyumbani. Karibu na wakati huo, kulikuja mwindaji mwingine mashuhuri, Edward, Mwana-Mfalme wa Uingereza. Ziara za watu hao ziliimarisha safari za uwindaji wa wanyama wakubwa. Risasi zingeweza kwenda kasi na kulenga shabaha kuliko mishale iliyotumiwa zamani.

Reli ya kutoka Kenya hadi Uganda ilipokamilishwa, watu wengi zaidi walianza kuishi karibu na Nairobi, hivyo haikuwa rahisi kwa wanyama kutembea-tembea kila mahali. Uhuru wao ulikuwa unakaribia kutoweka.

Katika miaka ya 1930, watu fulani walianza kutetea wanyama hao. Mlinzi wa mbuga Archie Ritchie na mhasibu Mervyn Cowie, walikuwa miongoni mwa wateteaji hao. Walifanya mikutano na kuandika habari kwenye magazeti wakiisihi serikali ya wakoloni ianzishe mbuga ya kitaifa ambayo ingesaidia kukomesha au kupunguza mauaji ya wanyama ya kiholela. Serikali haikutaka kufanya hivyo. Haikuwa tayari kutumia eneo lililokuwa linawavutia wakazi wengi zaidi katika Afrika Mashariki, kwa minajili ya kutunzia wanyama na mimea.

Jitihada ya kuwatunza wanyama ilipata pigo jingine wakati wa Vita ya Pili ya Ulimwengu, wanajeshi walipofanya mazoezi katika eneo hilo na kuliharibu. Bila shaka wanyama pia waliathiriwa na vita hiyo. Kwa kuwa waliwazoea wanajeshi, wanyama waliacha kuogopa watu, hivyo kukawa na uwezekano mkubwa kwamba wangewala watu. Ili kuepusha jambo hilo, wanyama kadhaa waliuawa, kutia ndani simba wa kike aliyeitwa Lulu pamoja na kundi lake maridadi la simba.

Hata hivyo, serikali ilibadili nia. Matatizo mengi yalitatuliwa na watunzaji wa wanyama wakafikia shabaha yao. Hatimaye, baada ya kipindi kirefu chenye magumu, Mbuga ya Kitaifa ya Nairobi ilianzishwa. Gavana wa koloni la Kenya, Bwana Philip Mitchell, aliiidhinisha rasmi mnamo Desemba 16, 1946, nayo ikawa mbuga ya kwanza ya kitaifa katika Afrika Mashariki.

Bustani ya Wageni

Mbuga ya Kitaifa ya Nairobi ni ndogo inapolinganishwa na mbuga nyingine za Afrika Mashariki. Inakadiriwa kuwa na ukubwa wa kilometa 117 za mraba na lango lake kuu liko umbali usiozidi kilometa kumi kutoka katikati mwa jiji la Nairobi. Hata hivyo, umaarufu wake unatokana na saizi yake ndogo. Huwezi kupata mandhari nzuri ya mbuga kama hiyo katika sehemu nyingi duniani ambapo mtu anaweza kutazama wanyama huku jiji la Nairobi likionekana kwa mbali.

Kwa kuwa mbuga hiyo si kubwa, unaweza kuwaona wanyama wengi wakubwa wakiwa pamoja, isipokuwa tembo. Hiyo ni tofauti na mbuga nyingine kubwa. Kuna aina 100 za wanyama na zaidi ya aina 400 za ndege. Mbuga hiyo iko karibu na mahali ambapo ndege hupitia zinapotaka kutua katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Nairobi.

Mgeni anaweza kutoka kwenye hoteli ya starehe, asafiri karibu na majengo maridadi, na kuwasili katika mbuga hiyo yenye nyanda za kale, vichaka, na misitu. Huko kuna simba na wanyama wengine wawindaji. Huwezi kusahau mandhari hiyo, ambapo wanyama hufukuza mawindo yao huku majengo marefu yanayometameta yakiwa nyuma.

Mbuga hiyo ina wanyama wengi kama vile nyati, chui, duma, twiga, tumbili, mamia ya paa, na kifaru mweusi aliye katika hatari ya kuangamia. Wengi wa wanyama hao ni wakazi wa kudumu wa mbuga hiyo. Katika majira ya kiangazi ya Februari hadi Machi na Agosti hadi Septemba, wanyama wengi wahamaji, kama vile nyumbu, huonekana karibu na vidimbwi vingi vilivyoko katika mbuga hiyo.

Kwenye vidimbwi fulani, vinavyoitwa kwa kufaa vidimbwi vya viboko, makundi ya viboko hushinda majini siku nzima, na kutoka nje ya maji wakati wa usiku kulisha. Karibu na vidimbwi hivyo, kuna vijia vya miguu ambavyo mtu anaweza kutembelea. Hata hivyo unapaswa kutahadhari: Matembezi hayo yanaweza kuwa hatari kwani mamba wanaweza kuwa wamestarehe ukingoni mwa vidimbwi fulani na huenda wageni wasiwaone! Kwa hiyo, ili kuepuka kuwa kitoweo chao, inafaa utembee pamoja na walinzi wa mbuga waliozoezwa.

Pia kuna ndege wanaojulikana sana. Kuna mbuni mwenye urefu wa meta mbili, ambaye ni mkubwa zaidi kati ya ndege wote wanaojulikana. Tumbusi mwenye sifa mbaya anaweza kuonekana angani akitafuta mawindo. Ndege huyo asiyependeza ana fungu muhimu katika kusafisha mbuga, kwani yeye hula mizoga ya wanyama inayoweza kutokeza bakteria ambao ni hatari kwa wanyama wengine.

Pindi kwa pindi, unaweza kumwona ndege aitwaye karani. Ana manyoya marefu nyuma ya masikio. Manyoya hayo yanafanana na yale yaliyotumiwa zamani na makarani kuandikia. Ndege huyo huwa na shughuli nyingi kwelikweli. Ndege wengine wanaopatikana huko ni mshingi, taji, saddle-bill na yangeyange.

Ingawa mbuga hiyo ni ndogo, ina namna nyingi za uhai. Katika upande wa magharibi, karibu asilimia 6 ya eneo la mbuga lina msitu, ambao hupokea milimeta 700 hadi 1,100 za mvua kwa mwaka. Eneo hilo lina miti mingi kama vile Cape chestnut, na croton iliyo maridadi. Pia kuna nyanda, mabonde, na milima katika eneo kubwa la kusini na mashariki, ambazo hupokea mvua ya milimeta 500 hadi 700. Nyasi ya red oat, aina fulani ya tende, miti ya arrow poison, na aina kadhaa za migunga hulifanya eneo hilo kuwa savana halisi.

Pia kuna miamba mikubwa ambayo imeinuka kutoka kwenye bonde hadi urefu wa meta 100. Si kazi rahisi kuipanda angaa kwa wale ambao wangependa kujaribu!

Mbuga Imo Hatarini

Matatizo yote ya kuhifadhi wanyama huletwa na wanadamu. Mbuga ya Kitaifa ya Nairobi huenda ikatoweka kwa sababu ya miradi ya ‘maendeleo.’ Makazi ya watu katika jiji la Nairobi ambayo yalifanya mbuga hiyo ianzishwe na hivyo kupata sifa ya ulimwengu mzima yanazidi kupanuka na kuwaachia wanyama nafasi ndogo sana. Watu zaidi na zaidi wanapoendelea kuhamia jijini, kunakuwa na uhitaji mkubwa zaidi wa mashamba na wanyama hawawezi kujitetea. Maji machafu yanayotoka katika viwanda vilivyo karibu, yanatishia uhai wa wanyama na mimea katika mbuga.

Jambo jingine linalotishia mbuga hiyo ni ukosefu wa nafasi ambayo wanyama fulani wanaohama hupitia. Eneo kubwa la mbuga limezingirwa ili kuwazuia wanyama wasiingie jijini. Shughuli nyingi za kilimo katika upande wa kusini wa mbuga zinazidi kusonga njia inayoelekea kwenye mbuga. Iwapo itabidi njia hiyo ifungwe kabisa, hilo litaleta matokeo mabaya. Wanyama wanaohama mbugani kutafuta malisho huenda wasiweze kurudi tena! Ili kuokoa njia hiyo ya wanyama, Shirika la Huduma za Wanyama la Kenya, lenye daraka kuu la kulinda wanyama, limepata idhini ya kukodi eneo linalopakana na mbuga hiyo. Licha ya matatizo mengi, Mbuga ya Kitaifa ya Nairobi huendelea kuwavutia maelfu ya wageni kila mwaka wanaopenda kuona mandhari yake yenye kupendeza.

[Picha katika ukurasa wa 24]

Twiga

[Picha katika ukurasa wa 25]

Chui

[Picha katika ukurasa wa 26]

Kundi la Kongoti

[Picha katika ukurasa wa 26]

Mamba

[Picha katika ukurasa wa 26]

Simba

[Picha katika ukurasa wa 26]

Taji

[Picha katika ukurasa wa 26]

Kifaru mweusi

[Picha katika ukurasa wa 26]

Mbuni