Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Mbwa-Mwitu Wavua Samaki

Kwa miaka mingi ilidhaniwa kwamba mbwa-mwitu hula wanyama wa nchi-kavu peke yake kama vile mbawala. Hata hivyo, kulingana na gazeti Vancouver Sun la Kanada, mbwa-mwitu wanaoishi katika misitu ya mvua iliyo kwenye pwani ya katikati ya British Columbia wameonekana wakila kome, chaza, na hata samoni, “20 kwa saa moja.” Wao humnyemelea samaki polepole, kisha “wao huruka ndani ya maji kwa miguu yote minne na kumshambulia ghafula bin vuu.” Wao hufanikiwa kumshika samaki mara 4 hivi kati ya kila mara 10 wanazojaribu. Hata hivyo, watafiti wanashangaa ni kwa nini mbwa-mwitu hula tu kichwa cha samoni. Mtafiti Chris Darimont anadokeza kwamba huenda kichwa cha samoni kina virutubisho fulani ambavyo mbwa-mwitu wanavipenda au huenda mwili wa samoni una vimelea hatari. Darimont anasema hivi: “Mbwa-mwitu hao wanaendelea kutushangaza. Hilo linanionyesha kwamba huenda kukawa na maajabu mengi yasiyojulikana katika misitu ya mvua.”

Vijana Wanazoezwa Kuwa Mabwana Wakubwa

“Watoto ndio wanaotawala nyumbani!” lasema gazeti Wprost la Poland, linalochapishwa kila juma. “Sisi hununua nguo za bei, vipodozi, na vifaa vya kisasa hasa kwa ajili yao. Katika familia zenye mapato ya kiwango cha chini na cha kadiri, asilimia 80 ya gharama zote huwa kwa ajili ya vijana.” Ikizungumzia utafiti uliofanywa na Małgorzata Rymkiewicz wa Chuo Kikuu cha Wazazi cha Warsaw, ripoti hiyo ilitaja baadhi ya tabia zinazoonyesha jinsi watoto wanavyotenda kama mabwana. Kwa mfano, badala ya kuwashukuru wazazi, “wao hudai mengi zaidi, hawaridhiki na wanachopata, ni wajeuri, [na] hawawajali wengine.” Rymkiewicz anasema: “Sisi hufanya makosa makubwa tukiwa wazazi kwani tunawaruhusu hata watoto wadogo kufanya lolote wanalotaka.” Shirika la Wanasaikolojia la Poland linaunga mkono maoni hayo kwa kusema hivi: “Kijana hutambua mipaka yake ikiwa aliwekewa mipaka alipokuwa na umri wa mwaka mmoja hadi minne. . . . Tukikubali manung’uniko yote na vitendo vyote vya ujeuri vya vijana, tutalea mabwana wakubwa.”

Mashirika ya Kuvunja Ndoa

Ripoti moja katika gazeti la IHT Asahi Shimbun la Tokyo inasema kwamba wenzi fulani wa ndoa huko Japan wanatafuta msaada kutoka kwa mashirika fulani ili yavunje ndoa zao. Ikiwa mume anataka kumtaliki mkewe na hana sababu halali za kumtaliki, basi anaweza kulilipa shirika la kuvunja ndoa ili limtume mwanamume mwenye sura nzuri akutane na mke wake “pasipo kutarajia” na kuanza uhusiano wa kimapenzi pamoja naye. Muda si muda, mke wake atakubali talaka. Mwanamume aliyekodiwa hutoweka akiisha kumaliza kazi hiyo. Mke akitaka kumtaliki mumewe, shirika hilo humtuma msichana mrembo ili amtongoze mumewe afanye uzinzi. Msichana mmoja mwenye umri wa miaka 24 anayefanya kazi hiyo anasema kwamba wanaume wengi anaokutana nao “hukubali mara moja. Mimi hufanikiwa kutongoza asilimia 85 hadi 90 [ya wanaume hao].” Gazeti hilo linasema kwamba msimamizi wa shirika moja kama hilo huwafuta wafanyakazi wanaoshindwa kufanikiwa mara 3 kati ya mara 5. “Ni lazima wafanikiwe,” yeye alisema. “Ni kazi.”

Kwa Nini Kuna Watoto wa Mitaani?

Gazeti O Estado de S. Paulo la Brazili linasema: “Ujeuri nyumbani ndilo jambo kuu linalowafanya watoto na vijana watoroke nyumbani na kuhamia mitaani.” Uchunguzi uliofanywa hivi karibuni kuhusu watoto 1,000 wa mitaani wanaotunzwa na Shirika la Watoto na Vijana Waliobalehe la Rio de Janeiro ulionyesha kwamba asilimia 39 ya watoto hao walidhulumiwa nyumbani au waliona wazazi wao wakipigana. Mwanasaikolojia Leni Schmitz alisema: “Watoto hao hutaka kuheshimiwa na wanafikiri kwamba watapata heshima hiyo wanapohamia mitaani.” Uchunguzi huo ulionyesha kwamba asilimia 34 ya watoto hao walihamia mitaani kufanya kazi za malipo ya chini au kuombaomba, asilimia 10 walifanya hivyo kwa kuathiriwa na dawa za kulevya, na asilimia 14 walisema kwamba walitaka tu kwenda huko. Watafiti wanasema kwamba mara nyingi sababu hiyo ya mwisho huficha sababu nyingine, kama vile kutendewa vibaya kingono nyumbani. Asilimia 71 hivi ya watoto hao huishi na watoto wengine mitaani, na wanawaona kama “watu wa familia, hata wanawaita ndugu, wajomba, baba, au mama,” asema Schmitz.

Wamishonari Wamekuwa Wafadhili Badala ya Kuwa Wahubiri

“Wamishonari wengi wanampuuza Yesu.” Hivyo ndivyo gazeti La Stampa la Italia lilivyosema hivi karibuni. Badala ya kuhubiri kumhusu Kristo, inasemekana kwamba wao hutanguliza miradi ya kijamii ya kuondoa umaskini na kuteseka. Kulingana na kituo cha Internet cha Vatican City, kadinali Crescenzio Sepe, msimamizi wa Idara ya Kuhubiri Injili ya Vatikani, alisema hivi kuhusu wamishonari Wakatoliki: “Kishawishi kikubwa katika miaka ya karibuni . . . ni kupuuza agizo ambalo Kristo alitoa waziwazi na utume wa kiroho [kuwaelekea watu]. Jambo hilo limewafanya wamishonari fulani wazingatie tu kazi ya ufadhili, ambayo ingawa ni shughuli ya kijamii yenye faida, haipatani na mtazamo wa mitume unaoonyeshwa wazi katika Matendo ya Mitume.”

Hatari Nyingine za Sigara

Gazeti The Daily Telegraph la London linaripoti hivi: “Wanawake wanaovuta angalau sigara tatu kwa siku wanaongeza uwezekano wa kupatwa na ugonjwa wa moyo na kifo cha mapema kwa mara mbili.” Uchunguzi uliofanywa kwa miaka 20 kuhusu wanaume na wanawake 12,000 kutoka Denmark umeonyesha kwa mara ya kwanza kwamba hata kuvuta sigara chache tu kwa siku ni hatari. Hata wavutaji ambao hawavuti moshi hadi mapafuni wanakabili hatari kubwa zaidi. Amanda Sandford, msemaji wa Mradi Unaohusu Uvutaji wa Sigara na Afya, alisema kwamba mambo yaliyobainika katika uchunguzi huo yanaonyesha kuwa “wavutaji wanapaswa kuacha kuvuta sigara kabisa.” Katika uchunguzi mwingine, ulioripotiwa na gazeti The Times la London, madaktari wa Taasisi ya Tiba Katika Chuo Kikuu cha Athens waligundua kwamba wanaume wanaokuwa karibu na wavutaji wa sigara kwa dakika 30 kila siku (hiyo inakadiriwa kuwa sawa na kuvuta sigara moja) wanakabili hatari kubwa zaidi ya kupata ugonjwa wa moyo kwa asilimia 47, na wanawake wanakabili hatari kubwa zaidi ya kuupata kwa asilimia 56.

Fuo Maalumu za Sili Wanaoangamia

Tangu mwaka wa 1996, sili-watawa wa Mediterania wamekuwa kati ya wanyama kumi walio katika hatari kubwa ya kutoweka, laripoti Shirika la Kimataifa la Kuhifadhi Viumbe na Mali za Asili. Bado kuna kati ya sili 400 na 600 wa aina hiyo baharini. Idadi yao ilipungua waliposhambuliwa na wawindaji na kuuawa kimakosa na wavuvi. Baadaye, kwa sababu ya utalii na maendeleo, makao yao yaliharibiwa, lasema gazeti El País la Hispania. Hivyo, sili hao wakajificha mapangoni. Lakini wakati wa dhoruba, watoto wa sili hunaswa katika mapango hayo kwa sababu ya mawimbi yenye nguvu. Sasa serikali za Hispania na Mauritania zinashirikiana ili kutenga fuo maalumu karibu na mapango na majabali ya Cabo Blanco kwenye Pwani ya Atlantiki ya Sahara Magharibi. Eneo hilo lina sili-watawa 150, na hilo ndilo kundi kubwa zaidi la sili. Inadhaniwa kwamba wanadamu hawataweza kuwadhuru sana viumbe hao.

Pesa za Plastiki

Mnamo Oktoba 2002, Mexico ilianza kutumia pesa za plastiki kama nchi nyingine kadhaa. Pole kwa pole pesa za plastiki zinachukua mahali pa pesa zilizotengenezwa kwa karatasi. Kulingana na gazeti El Universal, tayari pesa za plastiki zinatumiwa huko Australia, Brazili, New Zealand, na Rumania. Gazeti hilo linaripoti kwamba Wachina ndio walioanza kutengeneza pesa za karatasi, lakini Waaustralia ndio waliounda plastiki ambayo inatumiwa kutengeneza pesa hizo mpya. Pesa za plastiki zina faida mbalimbali. Zaidi ya kuwa safi, pesa hizo “hudumu mara nne zaidi ya pesa za karatasi, hazichakai haraka, . . . ni vigumu kutengeneza za bandia, na zinaweza kutengenezwa upya zinapochakaa.”