Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Barcelo Jiji Lenye Sanaa na Mitindo ya Kuvutia

Barcelo Jiji Lenye Sanaa na Mitindo ya Kuvutia

Barcelo Jiji Lenye Sanaa na Mitindo ya Kuvutia

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI HISPANIA

HEBU wazia kwamba unatembea katika nyumba kubwa ya sanaa. Kuna sanaa iliyotandazwa ambayo inavuta uangalifu na fikira zako mara moja. Kila mahali unaona maumbo, miundo, na rangi nyingi maridadi. Hata hivyo, sanaa hiyo yenye kustaajabisha haipatikani katika jengo au jumba fulani la kifalme. Jiji la Barcelona lenyewe ndilo lenye sanaa hiyo, hasa sehemu iitwayo Quadrat d’Or, * (Eneo la Kidhahabu). Sanaa ya jiji hilo si michoro wala michongo, bali ni majengo. Wageni wanaweza kuona mitindo na mapambo mbalimbali yenye kustaajabisha.

Labda jiji la Barcelona, ambalo liko kwenye Pwani ya Mediterania ya kaskazini-mashariki ya Hispania, ndilo linalofanana zaidi na majiji ya Ulaya, likiwa umbali wa kilometa 160 tu kutoka kusini mwa mpaka wa Ufaransa. Kwa miaka 100 iliyopita, limepata umaarufu kutokana na majengo yake na mitindo yake ya kisanaa.

Ijapokuwa lilishindwa mara kadhaa na Waroma, Wavisigothi, Wamoori, na Wafranka, Barcelona lilisitawi na kuwa kitovu cha biashara. Kufikia karne ya 14, jiji hilo lilikuwa jiji muhimu zaidi katika Hispania na bandari ya Mediterania. Majengo ya Kigothi na kanisa kuu, ambayo leo ndiyo majengo makuu katikati ya jiji, ni ya karne ya 14. Majengo ya Kigothi (1), yaliyoundwa kwa njia tata na ya hali ya juu yanaonyesha ukwasi na utajiri ambao Barcelona ilikuwa nao katika karne hiyo.

Katika karne ya 16, Hispania ilielekeza fikira zake kwenye makoloni yake yaliyokuwa Magharibi, kwa kuwa ilipata faida kubwa zaidi za kibiashara huko. Lakini kwa sababu ya maendeleo ya kiuchumi ya karne ya 19, Barcelona likawa jiji la Hispania lenye kutokeza la biashara ya nguo, nalo likaanza kusitawi tena.

Jiji Jipya Laanzishwa

Ukuzi wa haraka-haraka wa karne ya 19 ulililetea jiji hilo matatizo na vilevile utajiri. Idadi ya watu wa Barcelona iliongezeka sana kuanzia katikati ya karne ya 19, lakini ni sehemu ndogo tu ya jiji iliyokuwa imeendelea. Jambo fulani lilihitaji kufanywa ili kutatua tatizo la msongamano wa watu. Mhandisi wa ujenzi Ildefons Cerdà alipewa kazi ya kuchora ramani ili kufanya jiji hilo na eneo linalozunguka liwe na maendeleo.

Ramani ya Cerdà iliyochorwa mwaka wa 1859, iliitwa L’Eixample, au upanuzi, na hilo ndilo jina la eneo hilo la jiji. Kulingana na ramani yake, barabara zenye miti kandokando zingepakana na majengo yenye umbo la mraba. Barcelona lingekuwa jiji jipya lenye mazingira ambayo yangechangia afya bora.

Jiji lilianza kukua haraka kulingana na ramani ya Cerdà. Majengo yote yalijengwa kwa njia ya kipekee na kwa mitindo mbalimbali hivi kwamba wageni wanaotembelea huko leo wanaweza kuona umaridadi wake. Pia barabara zenye kuvutia ziliundwa. Katika kitabu chake Barcelona, Robert Hughes asema kwamba L’Eixample ‘ni mojawapo ya maeneo ya jiji yenye kupendeza zaidi huko Ulaya kwa sababu ya majengo yake.’

Utajiri wa Barcelona ulifanya jiji hilo liteuliwe kuandaa Maonyesho ya Ulimwenguni Pote yaliyofanywa mwaka wa 1888. Lango linaloitwa Arc de Triomf (2) (Lango la Ushindi), lililo karibu na katikati ya jiji, lilijengwa kuadhimisha tukio hilo muhimu. Hata hivyo, mnara huo wa ukumbusho pia huonyesha maendeleo ya sanaa ambayo yamefanya Barcelona kuwa miongoni mwa majiji ya pekee ulimwenguni.

Sanaa Mpya Iliyorembesha Jiji

Mwanzoni mwa karne ya 20, Sanaa Mpya—mtindo wa urembeshaji wa sanaa unaofanywa kwa maumbo ya kiasili—ilianza kuenea kotekote katika Ulaya na Marekani. * Barcelona lilikuwa na utajiri, lilikuwa na ramani ya majengo ya kurembesha jiji, na wasanifu wa ujenzi walikuwa na hamu ya kufanya kazi hiyo. Hivyo, Sanaa Mpya ikalipatia jiji umbo lake lisilo na kifani. Antoni Gaudí (1852-1926) ndiye aliyekuwa bingwa wa aina hii mpya ya sanaa, na kazi zake zaonekana wazi katika jiji la Barcelona.

Sanaa za Gaudí zilizo bora zaidi, nyingi zikiwa zimeorodheshwa katika majengo ya Mirathi ya Ulimwengu, zinapatikana Barcelona. Mfano mmoja wenye kutokeza ni Casa Milà (3), au La Pedrera, lililo kwenye Passeig de Gràcia karibu na katikati ya jiji. Kuta za jengo hilo haziko wima. Ni kana kwamba sehemu ya mbele ya jengo hilo imechongwa kwenye miamba. Kingo zilizochongwa kwa chuma cha mfuo zinazofanana na fungu la majani na mikwamba zimepamba sehemu ya nje. Upande wa ndani, kuna dari zilizopinda na nguzo zenye maumbo ya pekee.

Kielelezo kingine cha kazi zenye kuongoza za Gaudí ni jengo linaloitwa Casa Batlló (4), lililo pia kwenye Passeig de Gràcia. Kuanzia mwaka wa 1904 hadi 1906, Gaudí aliliunda upya jengo lililokuwa limemilikiwa na Josep Batlló i Casanovas, mfanyabiashara tajiri. Msanifu huyo alibuni nyumba nzuri ajabu. Paa lake lenye mabonde-mabonde lamkumbusha mtu uti wa mgongo wa mnyama dinosau, na vigae vyake ni kama magamba ya samaki. Nyumba hiyo ni ya pekee sana.

Labda mojawapo ya vielelezo vyenye kutokeza zaidi vya ubuni wa Gaudí ni kazi yake bora zaidi ambayo hakuimaliza, yaani kanisa Sagrada Familia (5). Minara minne upande wa mbele kaskazini hufanana na nta iliyoganda na kujipindapinda ambayo imetiririka kandokando ya mishumaa minne mirefu. Kwa kuwa minara hiyo ni mirefu sana kuliko majengo yote yanayoizunguka, imekuwa alama ya kimataifa ya Barcelona.

Pia yenye kustaajabisha ni bustani inayoitwa Parc Güell (6). Hiyo ni bustani iliyobuniwa na Gaudí iliyo kwenye kilima magharibi mwa jiji. Kuna michongo na nguzo zilizojipinda, picha zenye rangi mbalimbali, majengo ya kipekee na mabomba ya kutolea moshi ambayo yamezungukwa na bustani nzuri. Jengo jingine ambalo lavutia macho kwa sababu ya muundo wake na rangi yake ni Palau de la Música Catalana (7) (Jumba la Muziki) lililobuniwa na Domènech i Montaner, aliyeishi wakati mmoja na Gaudí.

Kati ya Milima na Bahari

Mahali ambapo Barcelona ipo, na pia urithi wake wa kisanifu, hulipatia jiji hilo sifa ya pekee. Milima ya Collserola inalizunguka jiji hilo upande wa magharibi na Bahari ya Mediterania yapakana nalo upande wa mashariki. Bahari hiyo ndiyo imechangia utajiri wa Barcelona na kuifanya iwe bandari kuu ya kibiashara ya Hispania. Haishangazi kwamba kuna sanamu ya kuchongwa ya Christopher Columbus (8) akielekeza kidole baharini karibu na bandari.

Kwa kuwa jiji hilo limezingirwa na milima na bahari, linapata hali ya hewa ya wastani ambayo inafaa kwa matembezi. Mwaka mzima, barabara hujaa watu kuanzia asubuhi na mapema hadi jioni kabisa. Mikahawa ya barabarani iko katika karibu kila pembe, ikimshawishi mpita-njia kwa harufu ya kahawa chungu au nafasi ya kuonja chakula cha wenyeji. Masoko ya chakula, kama vile Boquería lililo kwenye barabara inayoitwa La Rambla iliyojaa miti kandokando, huuza kila aina ya matunda, mboga, au samaki.

Hata hivyo, hutakuwa umekamilisha safari yako ya Barcelona bila kutembea kwenye kilima kinachoitwa Montjuïc, kilicho karibu na bahari. Wakiwa Montjuïc, wageni wanaweza kutazama vizuri majumba ya makumbusho, ya sanaa, na kuona jiji na Bahari ya Mediterania vizuri sana. Pia majengo makubwa yaliyotumiwa kwa ajili ya Michezo ya Olimpiki ya mwaka wa 1992 yanapatikana huko Montjuïc. Mashahidi wa Yehova wanapanga kwenda Barcelona kwa ajili ya kusanyiko la kimataifa kuanzia Julai 31 hadi Agosti 3. Kusanyiko hilo litahitaji kufanyiwa kwenye uwanja wa mchezo wa kandanda, Camp Nou ili kutoshea wakusanyikaji wote.

Ijapokuwa Barcelona ina matatizo yake kama vile tu majiji mengine makubwa, ni kawaida kwa wageni kufurahia unamna-namna wake wa Mediterania. Iwe ni vibanda vya maua na mikahawa ya La Rambla, barabara nyembamba na uzuri wa kale wa Mtaa wa Gothi, au usanifu wa jiji wenye kuduwaza, mtu hawezi kusahau kamwe sanaa na mitindo yenye kuvutia ya rangi mbalimbali ya Barcelona.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 3 Jina hilo ni la Kikatalani, ambayo ndiyo lugha kuu huko Barcelona na eneo jirani la Catalonia. Lugha yenyewe inatokana na Kilatini na inahusiana na Kihispania na Kifaransa. Watu wengi jijini huongea Kihispania na Kikatalani.

^ fu. 13 Mtindo huo wa sanaa wajulikana huko Hispania kuwa Modernismo.

[Ramani katika ukurasa wa 14]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

Barcelona

Madrid

Seville

[Picha katika ukurasa wa 16]

Mabomba ya kutolea moshi ya Casa Milà

[Hisani]

Godo-Foto

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 15]

Top photos: Godo-Foto

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 17]

Sandra Baker/Index Stock Photography

Godo-Foto