Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Tambili Ni Nazi Bora Zaidi

Tambili Ni Nazi Bora Zaidi

Tambili Ni Nazi Bora Zaidi

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI SRI LANKA

TAMBILI ni jina la Kisinhala la tunda la mnazi aina ya aurantiaca. Aina hiyo ya minazi huzaa vichala vya nazi kubwa za rangi nyangavu ya machungwa mwaka mzima, miaka sita hadi minane baada ya kupandwa. Hiyo ni minazi maridadi wee! Nazi za tambili zina urefu wa sentimeta 30 na uzito wa kilogramu moja na nusu. Minazi hiyo hukua kwa wingi kotekote katika kisiwa chenye joto cha Sri Lanka. Katika Kisinhala, tambili ni jina la nazi na pia la rangi yake nyangavu ya machungwa.

Kinywaji cha tambili kinapatikanaje? Nazi hutundwa kabla haijakomaa. Halafu upande wa juu wa nazi hiyo hukatwa na kutobolewa. Tambili inaweza kutoa karibu lita nzima ya maji. Maji hayo ni matamu na yenye lishe. Ni kawaida kwa watu wa Sri Lanka kuwapatia wageni wao waliochoka na wenye kiu maji ya tambili.

Unapotembelea kisiwa cha Sri Lanka, utaona vibanda vingi ambapo tambili zinauzwa kwa bei ya chini sana. Muuzaji hukata nazi hiyo upande wa juu kwa ustadi na kukuwekea mrija. Kisha unaweza kufurahia kinywaji bora, kinachoburudisha, na chenye lishe. Ukipenda kuiga wenyeji wa huku unaweza kunywa maji hayo moja kwa moja bila mrija, lakini ikiwa huna uzoefu mzuri huenda ukamwaga maji mengi kuliko yale utakayokunywa!

Faida za kiafya za tambili zinajulikana vizuri na watu wote wa Sri Lanka. Inasemekana kwamba maji ya tambili hupunguza joto mwilini na kutuliza tumbo. Maji hayo yana madini kadhaa, vyakula fulani vinavyoupatia mwili nguvu, protini kadhaa, mafuta, kalisi, vitamini C, fosforasi, na chuma. Maji hayo yenye madini huwasaidia watu waliochoka kwa kufanya kazi wakati wa jua kali, wanaosokotwa na tumbo, au wenye kipindupindu kuongeza maji mwilini. Kwa kawaida maji mengi ya kunywa huwa machafu, lakini tambili huwa na maji safi, yaliyohifadhiwa vizuri, na yenye lishe pia.

Ukitembelea pwani nzuri zenye joto na zenye mimea mingi za Sri Lanka, tuna hakika utafurahia umaridadi wa mnazi wa tambili unaorembesha bustani nyingi na pia maji yake yenye kuburudisha.